KWA AJILI YENU WANANGU, NITAMWAGA DAMU
Sehemu: 01
Mtunzi: Sultan Uwezo
Whatsapp: +255743204194
Anga la jiji la Windhoek nchini Namibia limechafuka kwa wingu zito lililopelekea jiji zima kulivaa giza japo ilikuwa ni mchana wa saa sita,lakini tayari nuru ilikuwa imeporwa haki yake ya utawala. Lakini pamoja na hali hii ya hewa kuwa si shwari lakini bado pilika za hapa na pale ziliendelea japo asilimia kubwa ya wana Windhoek wasiokuwa wafanyabiashara na wafanyakazi walikuwa bize kupishana kwenye vyombo vya usafiri kuwahi majumbani mwao baada ya kupata mahitaji kwani tayari matone ya mvua yalishaanza kuiadhibu ardhi huku ngurumo na radi nazo zikiendelea kutoa vitisho kwa wakazi wa mji huu. Lakini pamoja na vurugu zote za mvua iliyokuwa ikinyesha kwa nguvu muda huu na kupelekea mifereji ya maji barabarani kufurika maji kama mito na kusababisha mitaa kufurika maji hali ilikuwa ni tofauti kwa mwanamke mmoja ambaye alikuwa akiendelea kukata mitaa huku akiwa hana wasiwasi wowote kwa mvua iliyokuwa ikimnyeshea. Japo alikuwa akitetemeka kutokana na mvua pamoja baridi kali iliyokuwa ikipuliza muda huu lakini wala hakurudi nyuma yeye alisonga mbele na kuna wakati aligeuka kurudi alikotoka na kukamata mwelekeo mwingine hii ilionesha wazi hakuwa mwenyeji maeneo haya. Mavazi aliyovaa, nywele zake na muonekano wako viliwafanya hata watu wa mitaa aliyopita wakiwa kwenye vibaraza vyao kupuuzia kumpa msaada kwa kuhisi ni miongoni mwa vichaa walio ndani ya mji huo. Aliendelea na matembezi yake huku mikono ikiwa kichwani kama mtu aliyepatwa na mkasa fulani ambao umeichukua furaha yake.
"Hata inyeshe mwaka mzima lazima nifike nyumbani haijalishi hata kidogo."
Alijisemesha mwanamke huyu muda huu ambao mvua ilianza kupunguza kasi yake ya kunyesha.
"Ahaaa ulifikiri nitakuogopa kwa kishindo chako? Thubutuu, na mwisho wa mchezo umesalimu amri mwenyewe mvua mimi si kama hao waoga waliokukimbia na kuacha shughuli zao huku wengine wakiacha bidhaa zao zikipokea adhabu yako."
Aliongea maneno hayo akiingia ndani ya soko la mboga mboga na matunda huku akiisogelea meza moja iliyokuwa imesheheni matunda mbalimbali kama vile machungwa, maembe, mapera, mananasi, nazi na ndizi. Baada ya kuifikia meza hii alinyosha mkono wake kutaka kuchukua embe lakini kabla halifikia embe lile alikatishwa na sauti kutoka kwenye magunia yaliyorundikwa kwenye banda lililokuwa na hiyo meza.
"Wewe chizi acha utani na biashara za watu ohooo, mchana wa leo umeshaharibiwa na mvua hii na wewe umekuja kutia nuksi hapa, hebu ondoka bwana kabla sijakukata masikio yako."
Mwanamke huyu alimtazama mwanaume huyo aliyekuwa akiongea maneno hayo kwa muda kisha akamjibu.
" Samahani kijana wangu mimi si chizi kama unavyodhani nina akili zangu timamu kabisa sema tu haya ni matokeo ya maisha yangu ya nyuma na kama hutojali naomba msaada wako kwani nina njaa sana kijana wangu."
"Kwani umepatwa nini mpaka kuwa kwenye hiyo hali mama yangu?"
Mfanyabiashara huyu alimuuliza baada ya kumuona mama huyu akiongea kwa hisia kali ziliambatana na machozi.
"Mwanangu historia yangu si muhimu kwako kwa sasa ila tu naomba msaada wa chochote kile niweze kupunguza njaa."
Kijana yule alimtazama mama huyu baada ya kujibiwa vile, akaona isiwe shida akainama chini na kuchukua chakula alichokuwa amekinunua muda mfupi kabla ya mvua kunyesha na kumpa mama huyu lakini baada ya kuinuka akiwa na sahani yenye chakula alipigwa na butwaa kwani hakuweza kumuona mama yule. Aliangaza macho yake vibanda vya jirani lakini hakuweza kumuona akaweka chini chakula kile kisha akaruka meza yake na kuanza kumtafuta maeneo jirani na hapo lakini hakumuona. Wakati akiwa amekata tamaa na kuamua kurejea gengeni kwake mara akasikia sauti za kundi kubwa la watu.
"Kamata mwizi huyooo, piga mwizi huyooo, jamani mwizi huyooo......" Alirudi nyuma hatua kadhaa na kuuchungulia uchochoro ule ambao sauti zilitokea huko, hakuweza kuamini baada ya kumuona mwanamke yule yule akikimbia kujaribu kuokoa maisha yake kutoka kwa kundi lile ambalo halikuwa mbali naye. Akaona nafasi pekee ni kwenda kumsaidia mama huyu.
"Jamani eee msimfanye chochote mama huyo naamini si mwizi ndugu zangu."
Aliongea hayo baada ya kulikuta kundi likiwa tayari limemkamata mama yule na kuanza kumpiga pasipo kumpa nafasi ya kujieleza.
"Unasemaje wewe Hamza, siyo mwizi kivipi ilhali sisi ndiyo tumemfuma akiiba chakula kwa mama Nyeki."
Kijana mmoja aliyekuwa na kipande cha nondo akiwa anatiririkwa na jasho jingi aliongea hayo kwa ghadhabu ya juu akiwa amemgeukia Hamza.
"Si maanishi hivyo jamaa yangu, huyu mama alifika gengeni kwangu na kutaka kuiba hivyo hivyo na nikamfokea lakini aliniomba msamaha na kunieleza kwa ufupi kuwa yeye si mwizi alifanya vile ili kutaka kupunguza njaa aliyonayo nikamuonea huruma nikaona nichukue chakula nilichokuwa nataka kula nilipoinuka tu sikumuona bila shaka alikimbia baada ya kuona nimeinama chini akajua nachukua kitu cha kumpigia."
Hamza alihitimisha maelezo yake.
" Acha maneno yako Hamza, kwa unataka kutuambia nini?"
Mama Nyeki akiwa na mwiko mkononi huku mkono mwingine ukifuta jasho alimtolea macho Hamza na kumuuliza.
" Mama Nyeki naomba nilipe kwa kile alichokufanyia mama huyu lakini aachwe huru asiuawe."
Aliubeba mzigo wa mama huyo kwani alijua nini kingefuata kwa mama huyo baada ya kukamatwa, kwani sheria ya eneo hilo ni kwamba mtu akikamatwa anaiba au anavunja sehemu ili aibe adhabu yake ni kifo.
" Kwa hiyo uko tayari kumlipia huyu chizi siyo? "
Mama Nyeki alimuuliza Hamza swali hilo huku akinyoosha mkono kwa wale vijana kuwataka wasitishe zoezi la kumpiga mama huyo.
"Niko tayari mama Nyeki kwani kesho yangu siifahamu na hii ni leo yangu ambayo naifahamu mpaka sasa."
"Okay sawa nipe shilingi elfu hamsini keshi hapa hapa bila maelezo tofauti na hapo tunamalizia zoezi lililobakia."
Mama Nyeki alimtaka Hamza kumlipa kiasi hicho cha fedha na si vinginevyo. Basi Hamza alitoa burungutu la noti mfukoni na kuchomoa kiasi kilichotajwa na mama Nyeki na kumkabidhi.
" Muacheni chizi huyo chetu kiko tayari tuondokeni."
Mama Nyeki aliwaamuru vijana wale ambao walijitokeza kumsaidia kumnasa mwizi wake kumuacha na kuondoka zao na kumuacha Hamza aliyekuwa kamsogelea mama huyo kumpatia msaada wa kumuinua kutoka eneo lile lililokuwa na matope ambayo yalimbadilisha muonekano ndani ya muda mfupi na kumfanya aonekane kituko zaidi mara baada ya kutapakaa matope mwili mzima.
"Asante kijana wangu kwa msaada wako na ninaomba unisamehe kwa kukuingiza hasara."
Mama huyu alimwambia Hamza aliyekuwa akimuinua kutoka pale chini alipokuwa.
"Wala usijali mama yangu, naomba jitahidi uinuke ukapatiwe huduma ya kwanza."
"Mungu atakulipa kwa ulilomfanyia mtu usiyemfahamu."
Mama huyu aliongea hayo kisha akainama kulia tena na muda huyu Hamza alikuwa amemshika mkono akimkongoja kutoka hapo walipokuwa na kulifuata eneo la wazi kwani walikuwa uchochoroni.
JE, UNAFIKIRI MWANAMKE HUYU NI NANI NA KATOKEA WAPI NA ANAELEKEA WAPI?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA
sultanuwezotz.blogspot.com