HADITHI: NITAKUUA MWENYEWE


 NITAKUUA MWENYEWE 

Sehemu : 01

Mtunzi: Sultan Uwezo

Whatsapp +255743204194  

sultanuwezotz.blogspot.com 


   Robinson aliamka asubuhi na mapema kuelekea shambani akiwaacha wazazi wake wakiwa bado wamelala, lengo likiwa kwenda kumalizia kieneo kidogo ambacho walikibakiza kulima kwenye shamba lao la mihogo.

   Alichukua panga lake na jembe lake begani na kuianza safari ya Kuelekea shambani.

Kutoka nyumbani mpaka shambani kwao kulikuwa na kama kilometa kumi hivi na eneo hili lilionekana kuwa na rutuba kiasi chake na walilitegemea tofauti na eneo la upande wa milimani lilikuwa na kokoto nyingi sana hivyo halikuwa rafiki kwa kilimo.

        Eneo la mzee Kaaya halikuwa kubwa sana ni kama viplot vitatu tu.

Alipofika shambani alianza moja kwa moja kulima eneo lile, ilipotimia saa nne asubuhi jua lilikuwa kali hivyo kumfanya aache kulima na Kuelekea bondeni ambako kulikuwa na kijito kidogo lakini kilichotiririsha maji mwaka mzima.

Alivua nguo zake na kuanza kuoga kwa kuogelea kwenye kisehemu ambacho maji hujikusanya na kuwa kama kibwawa hivi, aliogelea na alipomaliza alivaa nguo zake na kuondoka zake lakini akiwa njiani aliamua Kupitia kwenye migomba ili akatafute ndizi zilizoiva walau atulize njaa ambayo tayari ilikuwa imeanza kuchukua nafasi.

     Aliizunguka migomba yote lakini hakukuwa na dalili yoyote ya uwepo hata wa chembe moja ya ndizi, alijilaumu sana.

"Ona sasa migomba yote hii inakosaje ndizi?"

Baada kujiridhisha kuwa hakukuwa na ndizi aliondoka zake kurudi shambani.

"Kwa njaa hii sijui nitafanikisha kumaliza eneo lililobaki." Alijisemea mwenyewe.

   Mungu ni mwema alimaliza kulima kisehemu kile na kuchukua zana zake na kurejea nyumbani.

"Habari yako kaka!"

Ilikuwa ni salamu iliyomshtua Robinson akiwa njiani kurudi nyumbani. Aligeuka na kumuangalia aliyetoa salamu hiyo.

Alikutana na sura ya mtoto wa kike mrembo mwenye wingi wa tabasamu usoni.

Robinson aliangaza huku na kule kujua dada huyu katokea wapi na kama ni nyuma yake mbona alipokuwa anaingia kwenye barabara hiyo hakuona mtu.

"Kaka vipi nimekusalimia mbona hujibu?" Mrembo huyo aliuliza baada ya kuona Robinson hajibu salamu yake.

Na swali hili lilimtoa mawazoni.

"Salama dada, samahani kwa kuchelewa kujibu salamu yako nadhani ni uchovu tu." Alitetea.

"OK, naitwa Jackline." Mrembo huyu alijitambulisha.

"Naitwa Robinson."

"Nafurahi kukufahamu Robby."

"Siyo Robby, naitwa Robinson dada."

"Aah ok Robinson."

"Samahani Robinson naomba msaada wako, Gari langu limenizimia pale bondeni nimetoka mjini nilikuwa naelekea kijijini kwa mzee Fikirini na kabla sijafika mafuta yameniishia."

"Du pole sana, nakusaidiaje dada yangu?"

"Naomba msaada wa mafuta kijijini."

"Ni mbali sana kutoka hapa mpaka kijijini,lakini ngoja nijaribu."

"Asante sana kaka yangu, ngoja nikupe hela ila kidumu utaomba huko huko."

"Bila shaka, so wewe unabaki huku huku?"

"Inabidi nibaki mpaka utakaporudi ila utanikuta ndani ya gari."

"OK, basi ngoja niwahi."

Robinson alikimbia haraka kufuata mafuta ya gari la mgeni wake. Alishika vizuri panga na jembe ili visiweze kumkwaza kwa mbio zake. Aliwaza sana juu ya yule binti,

"Inakuwaje mrembo kama yule anatembea porini peke anajiamini nini? "

Ndani ya muda mfupi alikuwa nyumbani kwao akiweka zana zake za kazi na kisha kuingia kwenye kichumba cha kutunzia vyombo na kuchukua kidumu cha lita 5 na kutoka mbio.

"Robinson, Robinson." Mama yake aliita baada ya kumuona yuko juu juu na ghafla akitoka na kidumu. Lakini alikuwa kuchelewa kwani tayari alikuwa akikata kona ya mtaa wa tatu.

"Sijui anaharakia wapi mtoto huyu chakula chenyewe hajala." Aliwaza mama yake.

Alifika na kumuomba muuza petroli pale vibandani ampimie ya lita 5 kwani anaharaka sana.

"Samahani kaka nifanyie haraka niwahi ninasafari ya mbali." Aliongea Robinson.

"OK, dakika chache tu mdogo wangu."

Baada ya kulipa na kuridishiwa chenji yake alichukua dumu lile na kuanza kuondoka kwa kasi yake Kuelekea kule porini. Japo jua lilikuwa kali halikumzuia kutembea haraka ili kumuwahi mgeni wake akiamini binti kama yule kukaa porini kwa muda mrefu ni hatari.

Alifika na kumkuta Jackline akiwa kalala fofofo akiwa kalaza kiti cha mbele lakini kioo akiwa kakishusha.

"Jackline, Jackline, Jackline."

 Alimuamsha kwa dakika kadhaa ndipo aliposhtuka kutoka usingizini.

"Niache Siyo mimi, siyo mimi."

"Siyo wewe nini Jackline?"

"Oogh sorry Robby, nilikuwa naota ndoto ya ajabu sana. Umeenda haraka sana ee mara hii au siyo mbali."

Jackline alijibu kwa swali.

"Sema njia yenyewe nimeizoea sana."

"Aisee, uko fasta sana Robinson."

Baada ya kuweka mafuta aliiwasha gari ikawaka, Jackline alifurahi sana kuona gari imekubali kusonga mbele.

"Robinson panda twende zetu hapa imepona."

Aliongea Jackline.

Robinson alipanda gari hiyo aina ya Honda na safari Kuelekea kijijini ilianza.

"Unatelemkia wapi Robinson." Aliuliza Jackline.

"Kwenye ile nyumba ya yenye bati kuu kuu."

"Ndo kwenu pale ee."

"Hapana, nyuma ya ile nyumba."

"Ok, nitafika nipafahamu."

"Karibu sana dada Jackline."

"Usijali."

Gari ilisogea taratibu kabisa na ikaacha Njia na kuelekea chini ya mti mkubwa wa mwarobaini uliokuwa nje ya nyumba yenye bati kuu kuu na kupaki. Jackline aliteremka kwa madaha na Kuelekea upande ule wa kushoto na kumfungulia Robinson mlango si unajua tena "MASHIKORO MAGHENI" kisha akalock milango na kumfuata Robinson.

"Twende zetu Robby." Aliongea Jackline.

"Njia ni huku kwenye hiki kiuchochoro."

"Ok."

Walitembea Kuelekea kwenye kiuchochoro hicho huku Robinson akiongoza njia.

Jackline aliwaacha watu wa mtaani hapo kuacha kazi zao na kumkodolea macho Robinson na mgeni wake huku wakimkazia macho zaidi Jackline kutokana na mavazi ambayo aliyavaa.

"We mama umemuona yule dada."

"Jamani jamani, sasa ndiyo nguo gani zile yaani suruwale imembana vile akitaka kuivua anafanyaje mwe." Aliongea mama huyu aliyepigwa butwaa.

"Hivi hata chooni anaendaga kweli maana kule nyuma nako kaaa!" Alichombeza mama mwingine aliyekuwa akitokea kuchota maji.

"We mama Joi hivi huyu binti ndiyo mke wa Robinson?" Aliuliza Mama muuza nyanya.

"Atambe na umaskini alionao atamuoa nani, mtoto wa mama Mashaka mwenyewe alimshinda kwenye uchumba tu baada ya kutajiwa ng'ombe watatu sembuse huyu mkanyaga lami?" Alijibu mama Joyce.

Robinson na mgeni wake walikata mtaa na hatimaye kufika nyumbani kwa kina Robinson.

" Karibu sana Jackline hapa ndo nyumbani."

"Ooh Asante Robinson ni pazuri." Alijibu Jackline.

Robinson aliingia ndani na kutoka na kiti kidogo cha miguu mitatu maarufu kama KIGODA na kumkabidhi mgeni wake, kisha kuingia tena ndani.

"Mama, mama!"

"Rabeka mwanangu, hivi ulikuwa unakimbilia wapi muda ule nakuita."

"Shikamoo mama."

"Marhaba, jibu swali langu kwanza."

"Mama nitakujibu tu lakini kwa muda huu njoo huku nje kuna mgeni."

"Katokea wapi?"

"Utajua hapo hapo nje."

Walitoka nje na kumkuta mgeni ambaye alionekana ni mgeni kijijini hapo.

"Mama Shikamoo." Alisalimia Jackline.

"Marahaba mwanangu, karibu kwetuu."

"Asante mama."

"Mama, huyu ni Jackline anatokea mjini kaja hapa kijijini kwetu na huyu ndie aliniomba nije huku kumnunulia mafuta ya petrol kwa ajili ya Gari lake ambalo liliishiwa."

"Aaa karibu sana mwanangu."

"Asante mama."

"Robinson au ndiye mkwe wangu nini maana nyinyi vijana mhh."

"Hapana mama nilikutana naye tu kule shambani."

Baada ya kutambulishana huko Jackline aliomba aende kwani bado anakasafari kidogo kwani alikuwa akielekea mwisho wa kijiji.

"Mama naomba mniruhusu niende, maana bado nina kasafari kidogo."

"Si usubiri baba yako aje umsalimie na umfahamu?"

"Wakati mwingine mama yangu nitamuona tu." Aliongea huku akiingiza mkono ndani ya pochi yake na kutoa noti tatu za elfu kumi. Na kumkabidhi mama Robinson.

"Asante Sana mwanangu Mungu akubaliki weweee."

"Kidogo mama."

"Karibu sana dada Jackline."

"Usijali Robinson."

Baada ya hapo walimsindikiza mgeni wao mpaka kwenye gari lake na kufungua mlango na kuingia ndani. Aliwasha gari na kulisogeza barabarani na kulipaki na kumwita Robinson.

"Hii ni namba yangu ya simu tusipoonana utanitafuta kwa mawasiliano. Na hii itakusaidia kwa mishe za hapa na pale."

"Asante sana nashukuru!"

Kisha gari liliondolewa kwa kasi na kutokomea. Huku nyuma Robinson hakuamini alichokiona mkononi mwake kwani alikuwa na kitita cha shillingi elfu sabini. Mama Robinson alimfuata mtoto wake na kumwambia kitu hiki.


ALIMWAMBIA NINI MTOTO WAKE, NA JACKLINE ANAELEKEA WAPI?

UNGANA NAMI KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


            



Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post