NITAKUUA MWENYEWE
Sehemu : 02
sultanuwezotz.blogspot.com
Mzee Fikirini alifurahi sana kumuona binti yake Jackline tena ambaye waliachana kwa kipindi cha miaka ishirini na tano.
Jackline ni mtoto wa kaka yake mzee Fikirini ambaye alijulikana kwa jina la Joachim. Joachim na mke wake walifariki muda mrefu sana katika ajali ya gari ambayo ilitokea katika mlima Sekenke mkoani Singida walipokuwa katika ziara ya mapumziko katika kisiwa cha Ukerewe na katika ajali hiyo alinusurika binti yao wa pekee Jackline, ambaye baada ya taratibu zote kufuatwa alikabidhiwa mzee Fikirini kipindi hicho Jackline alikuwa na umri wa mwaka mmoja tu.
Kutokana na urafiki uliopitiliza baina ya mzee Joachim na mzee Jonathan Ubao. Ilibidi mzee Jonathan Ubao amuombe Jackline kutoka kwa mzee Fikirini ili akaishi naye nyumbani kwake mkoani Tabora ikiwa ni pamoja na kumpatia mahitaji yake ya muhimu kama vile Elimu kama asante yake kwa rafiki yake Joachim kwa msaada ambao alimsaidia kipindi alichokuwa amefirisika.
Mzee Joachim alimsaidia kiasi cha shilingi milioni nne ili imsaidie kumrudisha kwenye mstari, na hapo ndipo alipoamua kufanya biashara ya mazao hasa mchele ambapo alikuwa akinunua mpunga kutoka wilaya za Nzega na Igunga na kisha kukoboa na mchele kuusafirisha mpaka mkoani Singida ambako aliwauzia wafanyabiashara kutoka Arusha na Zanzibar kwa bei ya jumla. Biashara hii ilimfanya kuwa maarufu ndani ya miaka miwili, kwani kwa kipindi hicho cha miaka miwili tayari alikuwa na mtaji uliofikia milioni 30 kwa kipindi hicho na kumfanya kuwa na mashine yake ya kukoboa mpunga mkoani Singida.
Hii ilimrudisha kwa rafiki yake Joachim na kumshukuru kwa msaada wake na hakusita kumfahamisha maendeleo ya biashara zake.
Miaka kadhaa baadaye alisikitishwa na taarifa ambazo zilimfikia juu ya ajali mbaya ya rafiki yake. Ilimuuma sana Mr. Jonathan kutokana na maisha ambayo waliyapitia yeye na rafiki yake na mpaka kufikia hatua ya Kupokea msaada wa shilingi milioni nne kama mtaji na sasa alikuwa milionea.
Hivyo jukumu lake baada ya kukamilisha shughuli za mazishi ya mzee Joachim na mkewe ikabidi achukue jukumu la kumlea Jackline na kumsomesha mpaka pale atakapofikia. Na hilo ndilo alilifanya kwa Moyo wake wote.
Na leo hii binti huyu alikuwa kwenye ardhi ya baba yake mdogo mzee Fikirini pale kijijini Lupa Wilayani Chunya ambako mzee huyu alijishughulisha na kilimo cha mihogo, ndizi, mahindi pamoja na zao la Tumbaku ambalo kwa wakati huu wakulima walilazimika kutumia mtaji na hii iliwafanya wengi washindwe kulimudu zao hili na kuegemea kwenye mazao mengine na kuwaacha wakina Fikirini wakipambana na zao hilo kwa Kupitia migongo ya wakulima wakubwa pale kijijini.
"Hivi ni wewe mwanangu Jackline kweli?" Aliuliza mzee Fikirini.
"Baba ni mimi ndiye, kwani vipi?"
Alijibu Jackline.
"Yaani bado siamini kama ni wewe maana ni muda mrefu sana."
"Ni kweli kabisa baba lakini ramani uliyokuwa umenielekeza kuanzia pale madukani haikunisumbua sana japo nilipokuwa nimekaribia maeneo yale ya Kaea kwa chini kabla ya kuvuka daraja lile dogo mafuta yaliniishia, lakini nimshukuru sana yule kijana anaitwa Robinson alinisaidia sana."
"Aaa yule kijana nampenda sana kwa tabia yake, ni mtulivu, mwelewa, asiye na majivuno kama wenzake waliopo mtaani hapa. Kwanza bidii yake shambani wee acha tu mzee Kaaya kalamba dume."
Maneno yale ya mzee Fikirini yalipenya vilivyo masikioni mwa Jackline na kumfanya afikirie kuendelea kumfuatilia zaidi huyu Robinson. Mbali na hayo lakini Jackline alimsimulia baba yake safari nzima ya kimasomo pale Tabora mpaka mkoani Tanga na kisha nchini Afrika Kusini.
Kifupi baada ya kumaliza shule ya msingi alijiunga na Sekondari ya Nanga iliyoko Wilayani Igunga na baadaye kujiunga na Sekondari ya juu ya Umoja iliyo karibu kama kilometa kadhaa kutoka Kijiji cha Ndala-Nzega kwa elimu ya kidato cha tano na Sita.
Kwa kuwa shule ile ya Umoja ni ya kidini iliweza kuwadhamini wanafunzi ambao walifanya vizuri kwenye mitihani ya mwisho kidato cha Sita na Jackline akiwemo kwa elimu ya juu ya Chuo Kikuu na hapo ndipo Jackline alipata nafasi ya kuingia ndani ya Chuo Kikuu cha Soweto nchini Afrika ya Kusini.
"Kwa hiyo huko Afrika ya Kusini uliwahi kuonana na Mandela mwanangu." mzee Fikirini Aliuliza.
"Halafu na wewe baba bwana, kwani wewe mpaka umefika umri huo ni raisi gani wa Tanzania umewahi kuonana nae?"
"Mhh, tuachane na stori hizo za Mandela, maisha yalikuwaje kuanzia kwa mzee Jonathan mpaka Chuoni Afrika ya Kusini?"
"Kwanza kabla ya yote mama na wadogo zangu wako wapi baba, maana toka nimefika sijawaona."
"Mama yako yuko msibani sehemu moja umeipita inaitwa Bitimanyanga kuna rafiki yake alihamia huko miaka kadhaa nyuma ndo ambaye kafariki juzi baada ya kupigwa na radi akiwa shambani kwenye Matumbaku yetu haya, na mdogo wako Shamimu anasoma kidato cha tatu hapa hapa Lupa Sekondari na kaka yako Athuman anaishi jijini Mbeya akifanya biashara ya mitumba huko."
Wakati baba na mwana wakiendelea na mazungumzo baada ya kuachana kwa muda mrefu wakati huo wakiwa Wilayani Manyoni kabla ya mzee huyo kuhamishia makazi yake kijijini hapo. Alifika Shamimu kutoka shule na ndipo mzee Fikirini alipomtambulisha kwa Jackline na baada ya utambulisho huo Jackline na Shamimu walikumbatiana kwa furaha.
****
"Baba Robinson yaani Leo mwanetu katuletea neema hapa acha kabisa yaani toto tulizaaa."
"Mbona sikuelewi mke wangu kuna nini tena kuhusiana na hiyo neema?"
"Leo nikiwa nawaza hili na hili juu ya nini tutapika jioni hii, mara Robinson huyo kaongozana na mgeni wake, mgeni mwenyewe toto, toto kweli baba Robinson sijui walikitana wapi huko mimi nikajua ni mkwe wangu kumbe la hasha ni mtoto wa mzee wa kule juu uwanja wa ndege kwa mzee Fikirini."
"Mzee Fikirini, mtoto gani mbona huyu Shamimu bado anasoma hapa hapa Lupa ni nani huyo?"
"Mhh, we Robinson yule binti uliyekuja nae jina lake nani?"
"Anaitwa Jackline mama."
"Basi huyo ni mgeni wao tu kutoka mjini huko." Aliongea mzee Kaaya.
"Inawezekana lakini yote kwa yote mume wangu alichotufanyia yule binti acha tu mimi minoti, mwanao minoti yaani wiki hii ni mwendo wa kunikia msosi wa maana."
"Pendeni vya bure na mwanao angalieni mtaolewa ooh." Maneno ya mzee Kaaya.
"Yule si mwanamke? atatuoaje mimi na mwanangu labda mwanao Robinson. Na mwanangu ukifanikiwa kuwa na yule binti Hatareee tutanuka minoti na mihogo atabaki analima baba yako sisi wengine tunabadili magari tu."
"Wee nani alime mihogo peke yake na mimi si nitahama kutoka komoni mpaka bia."
Hizo zilikuwa ni tambo za Hawa wazazi wa Robinson iwapo angebahatika kuoana na Jackline na hatujui iwapo hilo litatokea kwenye hizi familia mbili.
****
Shamimu alikuwa na furaha kubwa wikendi hii baada ya dada yake kumbeba ndani ya gari yake na Kuelekea mjini Makongolosi kwa ajili ya kwenda kufanya manunuzi, wakiwa sheli ya mafuta wanajaza mafuta akatokea Robinson akiwa na rafiki yake kuja kununua petrol ya bodaboda ya rafiki huyo Awadh tayari kwa safari Kuelekea Mpirani Isangawana.
"Robby."
Robinson aligeuka kuangalia sauti ilitokea wapi lakini alipoangalia pembeni akawa ameifahamu ile gari, akakumbuka siku moja iliyopita gari ile aliipanda. Akiwa bado anaendelea kuishangaa ndipo mlango wa gari ile ulifunguliwa na msichana aliyechanua vilivyo akashuka na kuwafuata pale walipokuwa wamesimama.
"Mambo Robby!"
"Poa Jackline, hivi hapa nilikuwa naangalia anayeniita ni nani?"
"Ni mimi bwana."
"OK, kutana na rafiki yangu Awadh."
"Mambo Awadh, na ninafurahi kukufahamu."
"Awadh, huyu ni rafiki yangu anaitwa Jackline nimekutana naye jana kule Kaea baada ya gari yake kukata Wese."
"OK, Jackline karibu sana Lupa."
"Nishafika Awadh."
"Wapi sasa Jackline muda huu."
"Na ndo maana nimekufuata nilipokuona hapa, naelekea Makongolosi niko na mdogo wangu Shamimu lakini Njia yeye anadai haifahamu vizuri unaonaje ukaungana nasi kwenye hii safari utupe kampani!" Aliomba Jackline.
"Mbona sisi tun.......!"
"Mbona nini si umsindikize Jackline bwana kwani kule unakwenda kucheza wewe, mpira tuachie sisi Robby." Awadh alimkatisha Robinson.
Hakuwa na jinsi zaidi ya kumkubalia Jackline ombi lake lakini kwa sharti la kwenda kwanza nyumbani kwao akaombe ruhusa. Hilo halikuwa Shida sana kwa Jackline alikubali
na kuingia kwenye usukani na kugeuza gari Kuelekea maeneo ya misheni ya Lupa kwa nyuma ambako ndiyo nyumbani kwa kina Robinson.
Kutokana na hili Awadh Ilibidi aondoke peke yake Kuelekea mpirani.
"Sijaamini kama baba anaweza kuniruhusu kirahisi rahisi namna ile maana wazazi wangu ni watata balaa." Aliongea Robinson.
"Wanakupenda na ndiyo maana wanakuchunga sana, na hii imekufanya kuwa kivutio kwa kila mzazi pale kijijini."
"Kivutio namna gani Jack."
"Si ni upole na utulivu ulionao bwana. Kila mzazi anakusifia kwa hilo."
"Sasa ushaanza kuwa muongo, wewe umefika jana tu umeyajuaje haya?"
"Tukiwa njiani tukitokea nyumbani kuna sehemu ina kiduka tukiwa pale niliwasikia wazee fulani wakikujadili."
"Hata mimi niliwasikia dada, halafu wao wanadhani wewe dada ni mke wa Robinson." Aliongeza Shamimu.
"Mhhh." Robinson aliguna tu.
"Vipi Robby mbona unaguna kwani uongo mimi siyo mke wako?"
"Nitaanzia wapi mtoto wa mzee Kaaya na umaskini wetu."
"Usiseme hivyo Robby huwezi jua Mungu kaandaa nini mbele yako."
Safari iliendelea kuwa nzuri ndani ya hii gari ambayo tayari ilikuwa inaichungulia Makongolosi na safari ilikuwa fupi kutokana na utani wa hapa na pale na hapa ndipo Jackline alipogundua kuwa Robinson ni muongeaji sana.
Na kimoyomoyo akajisemea mwenyewe.
"Lazima nitampata tu Robinson."
Safari yao ikaishia nje ya geti la Hotel maarufu mjini Makongolosi inayojulikana kama PM HOTEL na kupaki gari nje ya hotel hiyo na kutelemka.
Waliposhuka aliwaongoza Robinson na Shamimu Kuelekea ndani ya hotel hiyo kutokana na ugeni uliokuwa umejionesha mbele yake. Wakaongoza mpaka kwenye moja ya mwamvuli na kukaa.
Mhudumu mmoja wa hotel hiyo aliwafuata wateja wake.
"Habari zenu, naitwa Magreth ni Mhudumu ndani ya hotel hii. Karibuni niwahudumie." Aliongea hayo na kuonesha kitambulisho chake kisha akawakabidhi menyu.
"Ok, tunashukuru kwa utambulisho wako ngoja tuipitie menyu hii kisha tutakuita dada eee." Jackline alimjibu.
Wakati hayo yote yakiendelea upande wa Robinson na Shamimu ilikuwa ni giza totoro hawakujua chochote kilichokuwa kikiendelea pale.
"Hii karatasi ina huduma zote zinazopatikana hapa kuanzia Chakula mpaka kulala, hivyo kila mmoja aangalie kinachomfaa kuweka tumboni."
Aliongea Jackline akimkabidhi Robinson ile menyu.
"Vitu vya wazungu hivi mimi sijavizoea hata kidogo, mimi naomba waniletee Wali maharage." Alijibu Robinson.
" Dada si uagize tu chochote kinachotufaa hapa badala ya haya makaratasi. "
Majibu ya Shamimu yaliwafanya wote waangue kicheko.
" Ni kweli kabisa Shamimu." Alijazia Robinson.
"Acheni hizo nyie chagueni vyakula ohh." Jackline aliongea akisimama na kumfuata Magreth.
Huku nyuma Shamimu na Robinson waliendelea kuchekana kutokana na kushindwa kuagiza vyakula walivyoambiwa waagize.
"Mbona hata wewe umechemka bwana usinishushue hapa." Shamimu alimwambia Robinson.
"Mimi hata Sekondari sijagusa ni kweli nina kaushamba, sasa wewe mwenzangu msomi kabisa." Alisema Robinson.
"Bwana ee kwenye misosi hakuna cha usomi wala nini, wote hollaaaaa."
"Ila dogo tumetia aibu balaa." Aliongea Robinson.
"Bwana eee." Maneno ya Shamimu.
"Halafu nimekumbuka, hebu weka namba yako ya simu hapa kwenye kimeo changu." Aliongea Robinson.
"Mambo ya namba yameanza hapa Mhhh usiharibu hali ya hewa Robby."
"Usihofu ni kwa ajili ya kuchati tu."
"Maana nikimuangalia dada ni kama tayari kakufia kifuani tayari."
"Acha hizo amekuambia?"
"Dalili zinaonekana tu."
Shamimu alirudisha simu haraka baada ya kumuona dada yake anarejea kuungana nao pale mezani.
Muda mfupi Magreth alifika akiwa na kuku watatu waliookwa vizuri na chupa kubwa ya soda aina ya koka kola. Hali ile iliwaacha macho kodo Robinson na Shamimu.
" Mbona mnashangaa si mlinipa kazi, kazi kwenu kuendeleza umafya kwenye hao kuku."
Aliongea Jackline.
"Kwa kweli, umetuweza na sisi ngoja tukuoneshe kazi ya mdomo." Aliweka utani Shamimu.
"Jamani baada ya kula tutaelekea kule madukani kila mmoja akang'ae kimjini mjini mnasemaje?"
Aliuliza Jackline.
"Si la kuuliza hilo dada." Alijibu Shamimu.
"Mimi mtanikuta hapa hapa naangalia televisheni." Aliongea Robinson.
"Kwa ajili ya nini, utanikwaza Robby.Hii safari tuko wangapi?"
"Robinson acha kumkwaza dada ndo nini sasa si ungebaki Lupa." Aliongea Shamimu kuonesha nae kutofurahishwa na kauli ya Robinson.
"Naombeni mnisamehe kama nimewakwaza jamani."
"Ok, ila siyo vizuri kujitenga tenga wakati tumekuja Pamoja."
Aliongea Jackline akionekana kukubali kumsamehe Robinson.
Waliendelea kukishambulia Chakula kile huku Robinson akiwa anawachekesha pale mezani.
"Niwe mkweli tu, toka kuzaliwa kwangu mwenzenu sikuwahi kula mkuku mzima kama leo da Asante sana mgeni kwa kuja."
Wote waliangua kicheko mpaka kupelekea Shamimu kupaliwa na soda iliyohama njia na kutokea puani.
"Robinson utasababisha Matatizo hapa bwana aaa." Aliongea Jackline.
"Hata yeye Shamimu kashindwa kuongea tu ni mwenzangu tu na ndiyo maana kakutwa na tukio hilo."
Aliongeza Robinson.
Kauli ile ya Robinson ilimkwaza sana Shamimu na kuondoka kwa hasira akitoka nje ya hotel.
"Unaona sasa maneno yako Robinson."
"Naomba mnisamehe jamani ilikuwa ni utani tu na sikujua kama nitamkwaza mtu." Alijitetea Robinson.
Aliinuka Robinson na kumfukuzia Shamimu kule nje na kumkuta akiwa katulia kwenye viunga vya nje. Alimsogelea na kumuomba msamaha.
*******
"Pole na yote mke wangu kuanzia msibani na njiani pia." Aliongea Mzee Fikirini
"Asante sana mume wangu, namshukuru Mungu tumesafiri salama mpaka kufika salama." Alijibu mama Shamimu.
"Ni jambo la kumshukuru Mungu mke wangu."
"Ni kweli kabisa."
Mzee Fikirini alimsimulia mke wake ujio wa mtoto wa marehemu kaka yake Jackline. Na kueleza namna alivyokuwa mkubwa.
"Unasema kweli mume wangu kuwa Jackline kaja??"
"Amini sasa kaja na mimi nilishikwa na mshangao kama wewe mke wangu."
"Kama ndoto Vile jamani."
"Kafika hapa na gari lake mizawadi kibao iko jikoni huko yaani ndani ya muda mfupi tumekuwa wengine kabisa."
"Kaja na gari?"
"Basi ana mihela huyo Jackline ee."
"Unashangaa gari wakati mwenzako alikuwa anaishi Afrika ya Kusini wee."
"Haa, ndio kile kipindi ulichokuwa humpati kwenye simu na kwanini mzee Jonathan alikuficha."
"Tuache hayo kikubwa amerudi nyumbani."
"Yuko wapi sasa."
"Wameelekea Makongolosi na mdogo wake kuna vitu amefuatilia huko sijui vitu gani hivyo."
"Waangalie wasijeibiwa gari lao."
"Hawawezi bwana."
Mama Shamimu aliingia jikoni kwa ajili ya maandalizi ya Chakula cha jioni. Alipofika huko jikoni vitu alivyokutana navyo hakuamini macho yake kwani baada ya kukuta mchele, Viazi, Ndizi, sukari, Chumvi, mafuta ya kupikia na vingine vingi.
" We baba Shamimu mavitu yooote haya si tutafungua duka sisi."
"Unashangaa hivyo njoo uchukue begi lako la manguo."
Alipokabidhiwa lile begi la nguo alipigwa na mshangao kwa alichokutana nacho ndani yake maana kulikuwa na kila aina ya nguo ya mwanamke kuanzia za ndani na hata nyingine nyingi kama Vile vitenge, kanga na Waksi za kutosha hakika ilikuwa furaha ndani ya nyumba hii.
Tukutane katika sehemu ifuatayo kujua kilichotokea. Komenti yako ni muhimu sana ndugu Msomaji.