NITAKUUA MWENYEWE
Sehemu: 07
sultanuwezotz.blogspot.com
Jackline na Robinson wako ndani ya msitu mnene wa San Antonio ulioko nchini Brazil. Msitu huu unapakana na Ufukwe wa Marigezh kwenye mji wa Belem.
Imekuwaje waingie Brazil haraka kiasi hiki badala ya kuelekea Afrika Kusini kama walivyokubaliana na mwenyeji wao.
Safari hii ilikuja ghafla mara baada ya kupata taarifa kuwa kuna mtu ameuawa kwa kuchomwa moto katika msitu wa manyanya ndani ya Makongolosi.
Na inasemekana pikipiki Pamoja nyaraka nyingine zilikamatwa na kuhifadhiwa kituoni kwao.
Ndani ya nyaraka hizo kulikutwa picha za Jackline, mzee Fikirini na vitambulisho vya jambazi huyo aitwaye Surambaya.
Hivyo jeshi hilo la polisi lilipanga kuwatafuta watu hawa popote pale ili kupata maelezo ni kwa namna gani picha zao zimekutwa kwenye fuko la mtuhumiwa. Taarifa zilisambaa kila kona ya maeneo yale na hivyo zilimfikia baba mzazi wa Robinson mzee Kaaya ambaye moja kwa moja aliwataarifu wakina Jackline na Robinson.
Jackline alimuomba mzee Kaaya aende polisi kuripoti na ikiwezekana amuunganishe na mkuu wa kituo ili aweze kujua ikoje hiyo taarifa mpaka picha zao kukutwa kwenye begi la marehemu. Na kweli alifika pale na kupata maelezo ya kutosha juu ya tukio lilivyotokea na ndipo mzee Kaaya naye akatoa maelezo yake kwa namna anavyoijua stori hiyo na kisha akamuunganisha na Jackline ambaye muda huo alikuwa mkoani Dodoma.
Jackline aliweza kuelezea kila kitu kuanzia vifo vya wazazi wake na namna walivyodhulumiwa mali zao na mzee Jonathan Ubao na kutoa hisia zake kuwa huyu mzee anahusika na hili.
Hivyo kuahidiwa kuwa jeshi la polisi litakuwa bega kwa bega naye katika kuhakikisha mzee Jonathan anapatikana kutokana na kuangalia namba ya mwisho iliyowasiliana na marehemu ilikuwa ni ya Jonathan ambaye baada ya kufanya mawasiliano na mamlaka ya mawasiliano kuikagua namba ile inaonekana ipo ndani ya nchi na wala si nje ya nchi bali anapatikana Kanda ya Ziwa. Hivyo baada ya kuhakikishiwa na jeshi la polisi kuwa mtuhumiwa atatiwa mikononi muda si mrefu lakini Jackline alifanya mawasiliano na Simbozya kumueleza kilichotokea na hivyo Simbozya akafanya mawasiliano na Santana juu ya mkasa wa rafiki yake akashauri wamfuate Brazil ndani ya siku hizi tano ili mchakato ufanyike mapema kama ujuavyo jeshi la polisi linaweza lisiifanye kazi yake ipasavyo hivyo ilikuwa ni bora wajiandae ili kumkabili adui yao. Hivyo moja kwa moja wakakubaliana kuwa badala ya kwenda Afrika ya Kusini ni bora waunganishe safari kuelekea Brazil na kisha Simbozya naye ataungana nao huko huko.
Na mwenyeji wao bwana Santana anaishi ndani ya mji huu wa Belem ambako anafanya shughuli zake mbalimbali, pamoja na shughuli hizo lakini pia Santana hukodiwa na Matajiri wakubwa wa eneo hilo katika shughuli zao fichivu mbele ya serikali.
"Mnaionaje hali ya hewa hapa Belem?" Aliuliza Santana.
"Si mbaya sana kwani inafanana na hali ya hewa ya nchini kwetu Tanzania." Alijibu Jackline.
"Naomba mpango wako ili niufanyie kazi usiku wa leo ili ikiwezekana kesho tuanze na program fupi fupi katika kuiweka miili Sawa."
Jackline alitoa laptop yake na kumkabidhi Santana na alipoipokea aliifungua na kuanza kuangalia baadhi ya vitu ambavyo vitamsaidia katika kuanza mazoezi yao.
" OK, iko vizuri sana nadhani itakuwa kazi ndogo sana kwa upande wako labda kwa Robbie ndo itachukua muda mrefu kidogo kwa kuwa yeye bado kabisa Hana kitu."
"Tutashukuru sana Santana kwani nina hasira sana na mzee Jonathan Ubao."
"Ondoa shaka hili limekwisha labda kama kuna jingine Jack?"
"Hakuna."
"Ila mawasiliano yenu namaanisha simu zenu hazitakuwa hewani ndani ya mwezi mzima mpaka tumalize programu na hivyo mtanikabidhi kesho OK."
"Brother kwanini?" Aliuliza Robinson.
"Robinson utaelewa maana baadaye na si kwa sasa." Alijibu Santana.
Baada ya maongezi hayo Santana aliwachukua wageni wake na kuwapeleka kwenye jumba ambalo wataishi kwa kipindi chote ambacho watakuwepo nchini Brazil.
Jumba hili lilikuwa ni zuri na la kuvutia sana lakini kilichomshangaza Jackline na kumuacha na mshangao Robinson ni juu ya jumba hilo kujengwa katika ya msitu huu wa Caratonsa karibu zaidi na mto wa Rio Amazonas.
"Kaka Santana ilikuwaje mjengo wa kifahari Kama huu ukajengwa msituni huku na si mjini?" Aliuliza Robinson.
"Brazil ni miongoni mwa nchi ambazo biashara ya madawa ya kulevya inafanyika sana na kushika kasi duniani japo haiongelewi sana. Na hili jumba lilijengwa na bilionea maarufu kwenye biashara ya madawa ya kulevya NduguTuyilagezi mwenye asili ya Bara la Afrika nchini Burundi."
"Haaa, yaani karibu na nyumbani kwetu Tanzania, alipenya vipi na kufika huku kufanya biashara hii?" Aliuliza Jackline.
"Familia yake yaani wazazi wake ndo walikimbilia huku mwanzoni mwa miaka ya 1886 na hivyo tunaweza kusema ni mwenyeji wa huku."
"Yuko wapi sasa huyu bilionea Tuyilagezi?" Aliuliza Robinson.
"Kwa leo pumzikeni kisha kesho nitawapeleka kwenye jengo lile pale juu ya kilima kwa ajili ya kutambua vizuri bilionea huyu au mnasemaje?"
"Bila shaka kaka Santana." Alijibu Jackline.
Baada ya kuwakabidhi sehemu ya kupumzika wenyeji wake aliondoka na kuelekea mtoni Rio Amazonas kwa ajili ya kuendelea na shughuli yake ya uvuvi.
Huyu Santana katika historia yake ni miongoni mwa wanajeshi walioacha kazi yake na kuamua kuwekeza katika shughuli ya uvuvi kama kivuli cha kazi lakini akiwa ni mfanya biashara wa madawa ya kulevya lakini yeye akiifanya kwa kificho sana.
*****
Taarifa zake kuonekana kwenye magazeti karibia yote nchini Tanzania zilimtisha sana kwani wakati anaamua kufanya umafya huu hakutegemea kama hili lingetokea. Hii ilikuja baada ya vitambulisho vyake, picha zake na business card yake kukutwa kwenye begi la Surambaya na hivyo ikawa ni rahisi kwa waandishi wa habari kuzichapisha mbele ya magazeti yao huku gazeti mojawapo kuwa na kichwa hiki kilichokolezwa kwa maandishi meusi..."PICHA ZA BILIONEA JONATHAN ZAKUTWA KWENYE BEGI LA JAMBAZI SUGU NCHINI, JE NI MIONGONI MWA WAFADHILI WA MAGENGE YA UJAMBAZI?"
"Mume wangu utakuwa mgeni wa nani katika hili?"
"Yaani hapa mke wangu kichwa hakifanyi kazi na sijui nifanye nini da Surambaya Surambaya umeniachia msala mimi." Alilalamika mzee Jonathan.
"Mimi nadhani tulia lala nadhani mpaka kufikia kesho utakuwa umepata jibu Mume wangu."
"Ni kweli mke wangu lakini tayari picha na jina viko gazetini jamani."
Mara simu yake mke wa mzee Jonathan iliita na Mama huyu aliipokea simu hii baada ya kugundua ni shoga yake Shufaa wa Nzega.
"Mhhh, wa kwanza huyu hapa! Halloo."
"Halloo shoga yangu wa ukweli, pole na majukumu."
"Asante wangu, lete stori uko pande zipi?"
"Nipo tu nyumbani naangalia TV hapa, lakini kuna taarifa kutoka mkoani Mbeya inamhusu shemeji kulikoni?"
"Mimi sijaiona hiyo ni taarifa mbaya au nzuri?"
"Mhhh, washa TV uone lakini hata kwenye magazeti ya leo zimesambaa sana na ndiyo habari ya mjini."
"Basi ngoja niangalie kama nitaiwahi, Mume wangu nini kimemkuta jamani?"
"Haya shoga mimi nikuache, ila mwambie Shem kama Zina ukweli ateleze mapema."
HAYA SASA UHONDO NDIYO HUO.
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA
#SULTANUWEZO