NITAKUUA MWENYEWE
Sehemu: 08
sultanuwezotz.blogspot.com
Katikati ya usiku wa manane Robinson alishtushwa na sauti za watu waliokuwa wakisikika nyuma ya chumba walicholala. Aliamka na kuelekea kwenye dirisha lile la nyuma ili abaini ni wakina nani.Alipolifikia alilifungua kidogo na kuchungulia kule chini, kwa mbali aliona watu wanne wakibishana Jambo fulani. Na kwa kuwa ilikuwa ni usiku na mwanga wa taa za jengo lile haukuwafikia vizuri hivyo ikawa ni tatizo kuona vizuri.
Robinson alianza kupata hofu baada ya kuona kuna muda walikuwa wakimulika taa zao usawa chumba chao.
Alirudi mpaka kitandani na kumuamsha Jackline aliyekuwa kalala fofofo hajui kinachoendelea duniani zaidi ya ndoto tamu aliyokuwa akiiota muda huo.
"Jack, Jack, Jack."
"Mhhhh."
"Amka baby haraka uone."
"Niache nilale bwanaa..."
"Baby amka bwana uone kule nje kuna sintofahamu." Aliendelea kumuamsha huku akimvuta.
Jackline alijivuta vuta kivivu kutoka pale kitandani huku akimlaumu mpenzi wake kwa kumkatisha ndoto yake. Robinson hakujali hizo lawama zake aliendelea kumvuta mpaka dirishani na kumfunulia pazia kidogo na kumtaka aangalie nje.
"Angalia kule nje unaona nini?"
"Ni kama kuna watu hivi."
"Endelea kuwafuatilia wanafanya nini pale."
"Robinson, tumekwisha wale si watu wazuri kwetu inavyoonesha wanataka kutuvamia maana naona wanaoneshana huku na wanamulika mulika huku pia."
"Baby, inamaana ndio mwisho wetu umefika? Tunafia ugenini bila hata miili yetu kuonwa na wazazi, ndugu jamaa na marafiki? Mungu wangu."
Robinson alianza kulia kwa kwikwi kwani taswira ya wazazi wake ilimjia kichwani na kuwaona walivyokuwa wakihangaika bila msaada wowote na yeye ndiyo alikuwa mkombozi wao na sasa alijiona mfu ndani ya ardhi ya ugenini, kilimuuma sana.
"Robinson acha kulia kama mtoto, wewe ni mwanaume shupavu mbele ya mtoto wa kike na tena mrembo simama na tuchukue hatua."
Maneno yale ya Jackline yalimtoa kwenye mawazo ambayo yaliuteka mfumo mzima wa fahamu na ghafla alijiona yeye ndiye kidume mle ndani na mwenye nguvu hivyo alisimama na kuanza kuvaa nguo zake na katika muda Jackline alikuwa tayari kajiandaa alikuwa akimngoja Robinson na alirudi pale dirishani kuchungulia nje tena.
"Kunja hilo blanket kwa urefu liwe jembamba, na kisha chukua hilo shuka na funika juu yake na kwa juu huo mto uweke tengeneza kama kichwa kisha funika shuka hilo jingine."
Robinson alifanya kama alivyoagizwa na Jackline na baada ya kumaliza alimwambia aangalie kama kapatia.
" Baby cheki kama nimepatia."
"Umepatia, lakini nilisahau huoni kama hapo kalala mtu mmoja, hilo blanket jingine fanya kama hilo kisha shuka lililobaki funika miili yote miwili."
Na baada ya maelekezo yale kutoka kwa Jackline, Robinson akafanya kama alivyoambiwa.
"Waoo, umepatia baby." Jackline aliongea kwa sauti ya chini huku akiwa mwilini mwa Robinson kwani alimrukia na kumaliza na bonge la kisss."
Robinson alibaki katoa tu mimacho akimshangaa Jackline ambaye alionekana mwenye furaha ilhali nje kulikuwa na Hatari.Na mwisho akajistukia baada ya kuona Jackline kamkazia macho.
" Asante sana baby." Alijikuta maneno yenye umombo ndani yake yakimtoka.
"Nifuate." Jackline alitoa amri.
Walitoka na kuubana mlango na kisha waliongoza mpaka kwenye sebule ya nyumba ile na kumwambia Robinson alale nyuma ya sofa kubwa lililo upande wa kushoto wa sebule ile. Robinson alifanya kama alivyoagizwa, Jackline aliondoka na kulifuata dirisha la pale sebuleni na kuchungulia kule nyuma tena.
Baada ya kuangalia kwa muda pale dirishani aliondoka haraka na kuelekea nyuma ya kabati na kujificha nyuma yake.
Ndani ya dakika chache walisikia kitasa cha mlango kikichezewa na kunyongwanyongwa.
Huwezi amini Robinson aliyekuwa nyuma ya sofa gimba lilikuwa linagonga na kurudi. Akiwa bado kautolea mlango ule uliokuwa ukichezewa ghafla ulifunguka na kuwafanya wale watu wenye nia ovu kuingia na moja kwa moja kuongoza mpaka kwenye kile chumba
Na walipofika pale mlangoni hawakuwa na la kusubiri zaidi ya mmoja wao kuupiga teke na mlango na ukakubali wakajaa ndani.
"Paaaaaaaa, pa pa papaaaaaaa." Milio ya risasi kutoka chumbani kule ilisikika.
Ghafla wale jamaa Walitoka na kukimbia kuelekea nje pasipo hata kurudisha mlango.
Tendo lile liliwashangaza Jackline na Robinson kwani hawakujua nini maana ya tendo lile na kwanini waliongoza chumbani kwao.
Jackline ambaye alionekana ni jasiri kuliko Robinson alinyata na kuufuata mlango na kutoka nje, lakini alirudi na kumfuata Robinson.
Alipofika pale nyuma ya sofa alichokikuta kilimshangaza sana kwani Robinson alikuwa keshazimia muda mrefu.
"Roby don't do that, utani wako si nzuri bwana hebu amka tuondoke."
Lakini Robinson hakuonesha dalili yoyote ya kushtuka na hapo Jackline akajua tukio lile limemshtua mpenzi wake na kupelekea kuzimia.
Alimfanyia huduma ya kwanza kwa muda wa takribani dakika ishirini na ndipo aliamka.
" Nimekufa tayari?"
Lilikuwa ni swali la kwanza la Robinson baada ya kuamka.
"Haujafa bado, na hauwezi kufa na kama ungekuwa umekufa ungeongea wewe?"
Jackline alimjibu huku akimuinua na kicheko kama chote kwa alichokingea Robinson.
"Baby tuondoke hawa jamaa watarudi tena."
"La msingi kaoge kisha badilisha hizo nguo kisha tuondoke."
Baada ya kauli ile ya Jackline, Robinson alipojikagua akagundua gimba lilikuwa limetua kwenye jinsi yake na kusababisha harufu mbaya mle ndani. Alijisikia aibu sana na akaongoza ndani haraka, na haikuchukua muda mrefu akarejea pale sebuleni.
" Pole sana mpenzi wangu, najua hali hii ni kwasababu ya ugeni wako kwenye matukio kama haya."
"Ni kweli kabisa, toka nizaliwe sijawahi sikia mlio wa risasi zaidi ya kwenye video."
"Kwa sasa utazoea tu, mwenzako tayari nina uzoefu na misukosuko kama hii."
Hesabu zikaanza kupigwa kwamba wakitoka wataelekea wapi wakati huko nje wao bado ni wageni kabisa. Lakini kilichowachanganya ni nani yuko nyuma ya mchezo huu mchafu,au ni Majambazi lakini kwanini wameongoza chumbani kwao moja kwa moja na kushambulia na kisha kuondoka? Hawakupata majibu ya maswali yao.
"Mbona hapa kama sielewi elewi hivi?"
Robinson aliuliza.
"Si wewe tu hata mimi mpenzi hili tukio limenichanganya sana kwani sifahamu ni nani anatufanyia mchezo huu."
"Mpenzi naweza kukuuliza swali dogo?"
"Uko huru mpenzi niulize tu."
"Hivi huyu mwenyeji wetu unamfahamu kwa undani kabisa?"
"Ngoja kwanza."
Jackline alifungua mlango na kutoka nje na baada ya dakika chache alirejea tena.
"Nilihisi kama kuna minyato ya mtu hivi lakini ni salama, kiukweli simfahamu hata kidogo nimemwamini tu kwa kuwa yuko karibu na mshikaji wangu yule msauzi."
"Hauoni kama tumekifuata kifo chetu wenyewe huku? Badala ya kuja kujifunza namna ya kukabiliana na adui yetu tumejaa wazima wazima kwenye mdomo wa Mamba."
Robinson aliongea hayo akiingia kwenye chumba ambacho walilala.
"Haa ile plani imefanya kazi yake mpenzi, huwezi amini risasi zote zimeishia kwenye mablanketi watu tuliyoyatengeneza."
"Hiyo nilijua tu, kwani siku zote wavamizi hufanya kazi kulingana na akili zao zilivyowatuma hivyo hawakuweza kujiridhisha kama waliowamiminia ni walengwa au la?"
"Hisia zangu zinanituma wanaweza kurudi kuhakikisha kama kazi imekamilika ili malipo yafanywe kama walikodiwa na katika hili nina hofu na mwenyeji wetu Santana."
"Siwezi kukupinga katika hili mpenzi kwani hata mimi akili yangu inaniambia hivyo hivyo, hebu tufanye tuondoke huko nje akili itatukaa sawa."
Walifungua mlango taratibu na kutoka kwa kunyata, kama walivyokubaliana kuwa wakifika nje itafahamika ni wapi waelekee.
JE, NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
#SULTANUWEZO