IMETOSHA MAMA MKWE - 06 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


IMETOSHA MAMA MKWE - 06

sultanuwezotz.blogspot.com 


Mama Fabiana aliachana na mizigo na kunifuata pale nilipokuwa nikilia.

"Unalia nini tena mwanangu?"

Aliniuliza baada ya kunifikia.

"Hamna kitu mama."

Nilimjibu.

"Hamna kitu tena? Mbona kilio." Aliniuliza kwa mshangao.

"Nilikudanganya mama yangu naomba unisaidie." Nilimjibu.

"Kivipi ulinidanganya Herieth?"

Aliniuliza huku akinifuta machozi.

"Kifupi sifahamu niendako japo nakufahamu nilikotoka inaniuma sana mama yangu." Nilimjibu na kuendelea kulia.

"Si uliniambia kuwa unakuja kwa baba yako?" Aliniuliza.

"Ni kweli kabisa mama lakini hakukuwa na ukweli wowote katika hilo mama yangu." Nilimjibu mama Fabiana.

"Kivipi binti yangu?" Aliniuliza. Lakini badala ya kumjibu niliishiwa nguvu na kuanza kulia kwani hili liliniletea ganzi la mwili, mama Fabiana alipoona hivyo akajua kuwa atajaza watu pale stendi ambao tayari walishaanza kujongea eneo hilo na kuhofia kusababisha mtafaruku ambao asingeweza kuuhimili katikati ya watu hivyo akanivuta mpaka kwenye Bajaj ambayo ilikuwa imefika baada ya kuiita kwa ishara kisha tukaingia ndani yake.

"Pakia hiyo mizigo yote." Mama Fabiana alimuelekeza dereva Bajaj ambaye alikuwa akiiweka vizuri pembeni.

"Sawa mama." Alijibu na kushuka kuifuata.

"Samahani mama yangu hujanilipa nauli ya mizigo." Alikuja kondakta wa basi ambalo tulikuja nalo kutoka Iringa.

"Mamaaa nisamehe bure kijana wangu ni kupitiwa tu haikuwa makusudi." Mama Fabiana alimjibu huku akiifungua pochi yake kutoa hela.

"Naomba basi usaidiane na kijana huyo wa Bajaj kupakia mizigo hiyo kwenye hii Bajaj tafadhali kijana wangu." Akiwa anaendelea kutafuta hela ndogo ndogo ndani ya pochi yake alimuomba kondakta huyo amsaidie kuiingiza mizigo ndani ya Bajaj. Lakini kondakta inaonekana hakufurahishwa na ombi la mama Fabiana kutokana na kumtazama kwa muda akiwa kaikunja sura yake na kisha alimfuata dereva Bajaj na kusaidiana kupakia haraka mizigo ambayo ilikuwa mingi kidogo na baada ya kumaliza dereva aliingia kwenye Bajaj na yule kondakta alimfuata mama Fabiana ambaye alimkabidhi hela yake.

"Mama usinifanyie hivyo basi yaani mizigo yote hiyo unilipe kiasi hiki kiduchu cha fedha?"

Aliuliza mara baada ya kuona kapunjwa hivi.

"Siyo hivyo kijana wangu sina hela nyingine zaidi ya hiyo nisaidie tu."

Mama Fabiana alimjibu na kumsisitiza kuwa amsaidie kwa kiasi hicho.

"Siyo hivyo mama yangu kama ulijua una kiasi kidogo si ungeniambia kule kule kabla hatujaondoka?" Kondakta alimlalamikia mama Fabiana.

"Nisamehe mwanangu kwa hilo lakini naomba unielewe mama yako." Mama Fabiana alimjibu kondakta huyo kwa upole zaidi kiasi kwamba hakuwa na jinsi kondakta wa watu zaidi ya kuondoka na kutuacha.

"Sawa mama yangu lakini hiyo siyo poa kabisa heshimu kazi za watu."

Aliondoka akijilalamisha mwenyewe kiasi kwamba mama Fabiana hakupendezwa na ile hali ikabidi ashuke amfuate yule kondakta.

"Mama achana naye hizo ni lugha za kawaida kabisa kwa sisi tushindao juani na kama huamini nenda kamalizane naye kisha uone kama hatakushushia dongo jingine lolote."

Dereva alipoona mama Fabiana akishuka kutoka kwenye Bajaj akaona amshauri kulingana na ayajuavyo mazingira ya stendi tofauti na mama Fabiana ambaye inawezekana akawa si mwenyeji wa mazingira kama yale na kweli mama Fabiana alimuelewa kijana huyu wa Bajaj na hatimaye kurejea ndani ya Bajaj na kuketi.

"Uelekeo wapi mama yangu?" Dereva Bajaj alimuuliza mama Fabiana ambaye muda huo alikuwa akinifunika sweta lake huku yeye akitumia kitenge kujifunika.

"Tunakwenda mitaa ya Bwawani." Alimjibu akijitengeneza vizuri katika kukiweka sawa kitenge mwilini mwake.

"Sawa mama."

Dereva Bajaj alimjibu.

"Herieth punguza mawazo ninaamini kila kitu kinakwenda sawa na bila shaka utajisikia ni wa tofauti kabisa." Aliniambia mama Fabiana.

"Nashukuru mama yangu Mungu akusimamie kwa kila hatua yako ya utafutaji." Nilimjibu huku macho yangu yakiwa nje ya Bajaj kuushangaa mji huu wa mzee JAH PEOPLE namna ulivyojengeka na usipoambiwa kuwa ni halmashauri ya mji mdogo unaweza kujikuta ukiuita kwa jina kubwa zaidi.

" Yatakwisha baada ya kufika nyumbani." Alinijibu tena mama Fabiana na muda huo alikuwa akimpa ishara dereva Bajaj ya kukata kona ya kuingia mtaa wa nyuma kutoka barabarani.

"Kwenye lile geti jeusi utasimama kijana wangu." Alimuelekeza.

"Sawa mama." Alimjibu.

Na kama ndoto vile hatimaye tulifika nje ya lile geti ambalo lilikuwa limeipamba nyumba ya mama Fabiana ambayo ilikuwa ni ya kisasa kabisa kwa namna tu ilivyokuwa ikionekana kwa nje.

"Nashukuru sana kijana wangu."

Mama Fabiana alimshukuru sana kijana huyo wa Bajaj akiwa anampa hela yake huku mimi nikimsaidia kuipokea mizigo aliyokuwa akiitoa kwenye Bajaj.

Baada ya kukamilisha kushusha mizigo Bajaj iliondoka na kisha mama Fabiana aligonga geti huku akichungulia ndani bila shaka ilikuwa ni kuona kama kuna mtu karibu.

"Herieth hapa ndiyo nyumbani kwangu na bila shaka utapafurahia pia na wewe."

Mama Fabiana alinijulisha.

"Ni pazuri sana." Nilimjibu huku macho yangu yakiwa huku na kule kuyazoea mazingira si unajua tena ukiwa ugenini tahadhari ni muhimu.

"Una mambo wewe umepajuaje kama ni pazuri wakati bado hujaingia ndani."

Alinijibu na hapo hapo mlango ulifunguliwa na kisha kijana mmoja alitoka ndani.

"Waoo mama yangu mwenyewe karibu sana na pole kwa safari."

Kijana huyo alifurahi mara baada ya kukutana na mama Fabiana pale nje.

"Asante mwanangu habari ya siku?"

Mama Fabiana alimjibu kijana huyo.

"Ni nzuri mama." Alijibiwa na kijana huyo ambaye macho yalikuwa kwangu bila shaka alikuwa akinifurahisha kama kuna sehemu aliwahi kuniona kabla lakini mama Fabiana aliweza kuliona hilo.

"Kenedy mwanangu, huyu anaitwa Herieth ni ndugu yako pia najua hujawahi kumuona lakini utamjua baada ya kueleweshwa baadaye."

Mama Fabiana alimjulisha Kenedy aliyekuwa akiikusanya mizigo karibu zaidi na mlango.

"Okay sawa mama nashukuru kumfahamu."

Kenedy alimjibu huku macho yakiwa kwangu.

"Herieth mwanangu huyu ni kaka yako anaitwa Kenedy ni nani hapa kwangu utamjua baadaye lakini kwa sasa itoshe hivyo." Mama Fabiana alinitambulisha huku akimpa ishara Kenedy kuanza kuingiza mizigo ndani. Alichukua mkoba wake na kuniongoza ndani huku Kenedy akibebelea mizigo. Tulitembea mpaka kwenye mlango wa kuingia ndani mama akavua viatu vyake aina ya raba na kunikaribisha ndani na mimi ikabidi nivue visendo vyangu vilivyokuwa vimekula vumbi la kutosha. Wakati huo Kenedy alikuwa akibebelea mizigo na kuiingiza mlango wa pili bila shaka ilikuwa ni jikoni au stoo. Baada ya kuingia ndani niliketi kochini huku macho yangu yakiwa kwenye utalii wa nyumba hii ambayo ilikuwa ni ya kuvutia sana kwa namna ilivyokuwa imejengwa.

"Herieth mwanangu karibu sana hapa ndiyo kwangu jisikie nyumbani kabisa shaka ondoa." Akiwa na glasi ya maji mkononi alinikaribisha mama Fabiana huku naye akiketi kochini.

"Nashukuru sana mama yangu nimekaribia." Nilimjibu huku macho yangu yakiendelea na utalii ambao safari hii ulitua kwenye skrini kubwa iliyokuwa pale sebuleni na kusetiwa ukutani na kuifanya kuvutia vilivyo.

"Sasa utatakiwa kupata maji ya kuoga kisha tutapata chakula kabla mwili haujapata kupoa."

Mama Fabiana aliniambia.

"Nashukuru mama yangu, nitaoga baadaye kidogo." Nilimjibu mama Fabiana lakini kitu kilichonishangaza ni baada ya kumwambia vile niliona akitoa tabasamu huku macho yake yakiwa usawa wa kichwa changu.

"Mwanangu laiti kama ungejiona ulivyo kichwani wala usingekataa kwenda kuoga na kama huamini hilo kifuate kioo kile pale ukajitazame mwenyewe." Alinielekeza kule kioo kilipokuwa na mimi sikuwa na hiana zaidi ya kuifuata kilipokuwa na baada ya kukifikia sikuamini macho yangu baada ya kukutana kituko kwenye kioo.

" Kwa hiyo nimesafiri safari nzima kutoka Iringa mpaka Makambako nikiwa kwenye hali hii?"

Nilijikuta nikiwaza kwa sauti kiasi kwamba mama alijikuta akiangua kicheko na kisha kujibu japo halikuwa sikulenga kumuuliza yeye.

"Umesafiri hivyo hivyo mwanangu na sikutaka kukushtua katika hilo japo tayari nilianza kupata wasiwasi juu yako." Alinijibu.

"Kivipi mama?" Nilimuuliza.

"Kaoge kwanza kisha tule baada ya hapo hadithi za hapa na pale zitaendelea tu."  Alinijibu kisha akaingia chumbani kwake huku na mimi nikiingia kwenye chumba ambacho nilielekezwa huko.

Nilioga na baada ya kumaliza mama Fabiana alikuja na kunipatia nguo ya kubadili ambayo ilikuwa ni kitenge nilijifunga na kutoka.

"Nifuate huku Herieth."  Mama Fabiana alinitaka nimfuate alikokuwa akienda. Nilimfuata mpaka kwenye mlango mmoja kati ya milango ya vyumba vya nyumba ile na kisha aliufungua na kunikaribisha ndani yake. Tuliingia ndani kilikuwa ni chumba kizuri sana kikiwa na kitanda kikubwa chenye ukubwa wa kutosha huku pembeni kukiwa na kimeza chenye kioo juu yake huku pale mezani kukiwa na mafuta ya aina tofauti tofauti kifupi kulikuwa na kila aina ya kipodozi pale juu. Hakika ilipendeza sana na kunivutia mtoto wa watu. Nikiwa nimeikodolea macho ile meza ndipo mama aliponishtua.

"Herieth hiki ni chumba ambacho utakitumia kwa kipindi chote hiki ambacho utaishi hapa, sawa?"

Alinielekeza mama Fabiana huku akilifuata kabati la nguo ambalo lilikuwa pembeni yake.

"Sawa mama nashukuru." Nilimjibu huku nikiwa siamini kama nitakuwa nikiegesha mbavu zangu pale.

"Na humu kuna nguo za kutosha ambazo utachagua zinazokutosha na kuendelea kuzivaa." Alizidi kunikabidhi kila kilichokuwa mle chumbani na mimi nikijiuliza ni vitu vya nani mpaka vikose mtumiaji.

"Sawa mama nashukuru, sijui hata nikwambiaje lakini Mungu atakulipa mama yangu." Nilimjibu huku nikimfuata alipokuwa kasimama akiwa kafungua kabati na kutoa moja ya gauni ambalo alikuwa akinikabidhi.

"Wala usijali katika hilo kwanza vaa hili kwanza naona linaendana na mwili wako na utaangalia mafuta ya kukufaa utapaka kisha utanikuta sebuleni." Alimaliza kunielekeza kisha akatoka na kuondoka zake na kuniacha mle chumbani nikishusha pumzi ndefu nikiwa siamini kinachotokea kwangu tena kutoka kwa mtu niliyekutana naye tu njiani hanijui hata jina langu lakini kanikubali hivyo hivyo kitu hicho kilinifanya kuyakumbuka yote niliyofanyiwa nyumbani na baba yangu na mpaka kutimua mbio hapo machozi yalianza kunitoka mfululizo. Lakini mara mlango uligongwa, hapo nilifuta machozi haraka kwa kutumia upande wa kitenge ambacho nilikuwa nimekiweka kando kidogo na kubaki kama nilivyo si unajua tena mambo ya kujiachia mwenyewe chumbani. Mgongaji hakuacha aliendelea kugonga na hapo ilibidi nijifunge kitenge na kujifuta vizuri machozi ili nisishtukiwe kisha nikauendea mlango kuufungua.


NINI KITATOKEA NDANI YA NYUMBA HII?


MDAU TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUPATE KUJUA MAJIBU YA SWALI LETU.


       #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post