IMETOSHA MAMA MKWE - 07 (Mtunzi: Sultan Uwezo)


 IMETOSHA MAMA MKWE  - 07

sultanuwezotz.blogspot.com 


Macho yangu yalikutana na ya mama baada ya kuufungua mlango.

"Hebu niletee simu yangu nimeisahau hapo 'dressing table' sijui nilikuwa nawaza nini?" Aliniagiza kumchukulia simu yake hivyo sikuwa na la kusubiri nilirudi ndani na kuifuata simu ambayo niliikuta pale aliponielekeza na nilikuja nayo moja kwa moja na kumkabidhi mama Fabiana ambaye aliichukua na kutaka kuondoka lakini alisita kidogo na kunigeukia.

"Herieth hebu jitahidi basi fanya haraka haraka chakula kiko tayari unasubiriwa wewe tu."

"Sawa mama nakuja sasa hivi." Nilimjibu na kurejea ndani na kuurudisha mlango kisha nilifanya haraka kubadili nguo na kisha kupaka mafuta ya lotion aina ya 'Angle Smooth' yaliyokuwa pale 'dressing table' ambapo baada ya kumaliza kupaka nilijikagua kwenye kioo na kisha nilichana nywele zangu na kisha nilitoka nje ili kuungana na wenyeji wangu kwa ajili ya chakula cha mchana.

"Waoo my sweet, umependeza sana yaani kama vile ulipimwa wewe." Mama Fabiana alinisifia nilipofika sebuleni.

"Asante mama." Nilimshukuru mama Fabiana.

Chakula kilikuwa tayari mezani ambapo alikuja msichana mmoja ambaye sikumuona hapo kabla na kuweka sawa meza na kisha kutukaribisha.

"Karibuni chakula." Alitukaribisha msichana huyo ambaye alionekana mwenye tabasamu muda wote kitu ambacho nilimuonea wivu kwani kwa upande wangu mambo yalikuwa ni tofauti kutokana na dunia kuwa kinyume nami kwa yale ambayo yalinitokea.

"Herieth nawa kwa chakula." Mama Fabiana alinishtua kutoka kwenye dimbwi la mawazo yaliyokuwa yamenichota ghafla.

"Nashukuru mama." Nilimjibu mama na kuanza kunawa tayari kwa kuanza kula.

"Na wewe Noela kaa kwanza hapa nikutambulishe kwa mgeni." Mama Fabiana alimwita msichana ambaye jina lake ni Noela kutokana na vile alivyoitwa na alirudi na kukaa kitini.

"Abee mama." Aliitika.

"Herieth huyu ni binti yangu aitwaye Noela Kibiki si binti wa kumzaa hapana ni mfanyakazi wangu humu ndani huku wakisaidiana Kenedy Liganga ambaye yeye kazi zake ndani ya nyumba hii ni maua kule nje pamoja na geti. Na wewe Noela huyu ni mwanangu pia anaitwa Herieth atakuwa nasi hapa kwa siku kadhaa kabla ya kuondoka." Alimaliza kutambulisha japo maneno yake ya mwisho yalinitonesha donda langu kwani mimi sikuwa tayari kuondoka hapo kwa muda huo kutokana na mazingira niliyokutana nayo pale kwake sasa yeye atasemaje kwa siku chache kisha nitaondoka.

" Nashukuru kukufahamu Herieth karibu sana ndugu yangu Makambako." Noela alinikaribisha huku tabasamu lake likiendelea kuchanua usoni kwake.

"Asante sana Noela nimefika." Nilimjibu huku nikiinuka kupakua chakula.

"Hivyo hakikisheni kuwa mnashirikiana kwa kila kitu kama ndugu pasipo kuwa na malumbano, sawa wanangu?"  Mama Fabiana alimalizia na kisha kumruhusu Noela kuondoka kuendelea na shughuli nyingine kule jikoni na sisi tukaanza kula chakula. Lakini wakati nikianza kula chakula taswira ya mama ilinijia mbele yangu ikiwa na huzuni sana huku akinitaka kurudi nyumbani. Hali hiyo ilinishtua kidogo kwa haraka sana nikaondosha macho yangu pale ukutani na kuelekeza macho yangu kwenye chakula lakini hali ile ilishuhudiwa na mama Fabiana japo mimi sikumuona kama kaniona.

"Herieth unaweza nini mbona kama umeshikwa na hofu hivi?"

Mama Fabiana aliniuliza baada ya kuishuhudia hali ile.

"Hakuna kitu mama." Hakuna kitu mama niko sawa kabisa.

"Hapana Herieth najua una jambo tena si dogo japo unanificha hebu kula unieleze kila kitu huwezi jua labda naweza kukusaidia." Sikuweza kumjibu chochote zaidi ya kumtazama tu kisha kutingisha kichwa kuonesha kuwa nimemuelewa kwa kile alichokiongea. Hivyo tuliendelea kula chakula huku kila mmoja akiwa kakiinamia chakula chake pasipo kuruhusu maongezi kupenya katikati yetu. Alianza mama kushiba na mimi baada ya muda nilifuatia.

"Ongeza chakula Herieth." Alinitaka kuongeza chakula.

"Nashukuru sana mama nimeshiba." Nilimjibu huku nikiinuka kutoa vyombo ili kuvipeleka jikoni. Lakini mama Fabiana alinitaka kuviacha pale pale mezani na kisha kumuita Noela ambaye alikuja na kuvitoa kisha kusafisha meza na kuitandika kama ilivyokuwa.

"Herieth wewe leo ni mgeni hizi kazi utakutana nazo kuanzia kesho."

Aliniambia huku macho yake yakiwa kwenye simu ambayo alikuwa kaishika muda huo.

"Sawa mama nashukuru." Nilimjibu.

"Vizuri, sasa nafikiri unakumbuka nilichokuambia muda mfupi uliopita ni kitu gani kilichopelekea wewe kuondoka nyumbani." Alinitaka nimsimulie kilichonikuta sikuwa na jinsi ilibidi nianze kumsimulia japo nilikuwa na hofu kwamba anaweza kunifukuza kwake lakini nifanyaje sikuwa na jinsi ilibidi nianze.

" Mama kama ambavyo nilikudokeza hapo awali kuwa nilikudanganya si uongo ni kweli kabisa mama, mimi jina langu siyo Herieth bali naitwa Christina Thobias Masenga ni mwenyeji wa Ilula Iringa nikiwa nimezaliwa mwaka 1990 katika Hospitali ya mkoa Iringa na kisha kuanza darasa la kwanza mwaka 1995 na hatimaye kuhitimu darasa la saba mnamo mwaka 2001 pale pale Ilula kwenye moja ya shule za msingi na kwa kuwa Mungu alinijalia uwezo darasani sikushtuka pale nilipoletewa taarifa za kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Sekondari moja ambayo jina lake nalificha kapuni lakini haiko mbali sana Ilula. Wazazi wangu walifurahi sana kwa kitendo cha mimi mtoto wao kuwa miongoni mwa wanafunzi waliochaguliwa mwaka huo na hatimaye nilifanyiwa sherehe fupi ambayo kwangu naiona kama iliniletea nuksi ambayo natembea nayo mpaka sasa." Simulizi yangu ilionekana kumvutia sana mama Fabiana ambaye alitoka pale alipokuwa kaketi na kukaa karibu yangu ili aweze kunisikia vizuri.

" Jamani pole Christina wangu." Alinipa pole huku akinifuta machozi ambayo yalianza kutoka bila kuomba ruhusa yangu.

"Asante mama yangu japo naona kama vile bado zigo limenielemea kichwani." Nilimjibu nikikaa sawa.

"Umesema baba yako ni mzee Thobias Masenga na mama jina lake anaitwa nani? Na kwanini unasema sherehe uliyofanyiwa ilikuletea nuksi?" Alinipiga maswali mawili mfululizo.

"Mama yangu anaitwa Lidia Simon Ludenye ambaye naye ni mzaliwa wa pale pale Iringa na kuhusu siku ile niliyofanyiwa ile sherehe kuiona kama iliniletea nuksi ni baada ya kwenda kuanza masomo yangu ya kidato cha kwanza. Niliyaanza nikiwa nimewapa ahadi tele wazazi wangu ya kufanya vizuri katika hatua hiyo na hatimaye kusonga hatua inayofuata lakini kumbe nilijidanganya mwenyewe kwani wakati nikipanga hayo kumbe shetani naye alikuwa pembeni yangu akicheka mwenyewe kwa kuisemea kesho nisiyoijua kwani baada ya kuwa pale nilianza masomo yangu kwa kasi ya ajabu kutokana na kufanya vizuri huku jina langu likiwa midomoni mwa kila mwanafunzi. Kama ujuavyo mama yangu ngoma ikilia sana hupasuka na ndivyo ilivyonitokea mimi kwani kabla nilikuwa kipenzi cha kila mwanafunzi pale shuleni na walimu pia lakini huwezi amini jambo la dakika moja tu lilibadili mfumo mzima wa maisha yangu." Nilitulia kidogo nikamimina maji kwenye glasi na kunywa maana japo kulikuwa na baridi muda ule lakini kwangu jasho lilikuwa la kutosha.

" Jambo gani hilo Christina? " Aliniuliza mama Fabiana.

" Nikiwa kinara kitaaluma darasani kwangu kwa upande wa wasichana nilikutana na kinara mwenzangu aliyeitwa Meshack Witonga ambaye mbali na kuwa msaada mkubwa kwangu kwenye upande wa taaluma lakini ndiye aliyenishawishi kufanya naye mapenzi japo nilikuwa bado mdogo, nilijaribu kukataa kwa vile nilivyoweza lakini alizidisha ushawishi wake kwenye hilo akitumia kila aina ya mbinu na ahadi tele na hatimaye siku moja tukiwa tunajisomea kwenye moja ya ofisi za serikali ya wanafunzi ndipo aliponilazimisha kufanya tendo hilo ambalo lilibadili kila kitu katika maisha yangu na mpaka hivi sasa naishi kama digidigi porini mara hapa mara kule."

"Christina mbona kiumri bado mdogo sana japo Mungu kakujaalia mwili ilikuwaje ukaruhusu jambo hilo kutokea? Na nini kilikutokea?"

Mama Fabiana aliendelea na maswali yake ambayo yalikuwa msumari kwangu.

"Kutakuwa na nini mama yangu zaidi ya kupata mimba iliyopelekea kufukuzwa shule, ni inawezekana nimefanya kosa nakubali lakini kinachoniumiza mama yangu ni kitendo cha mkuu wa shule pamoja na baba yangu kutonipa nafasi ya kunisikiliza hilo linaniuma sana. Kwani baada ya kufukuzwa na kufika nyumbani baba alichukua jukumu la kutaka kuniadhibu kwa kumtia aibu japo mama yangu alitaka wanipe nafasi ya kunisikiliza mwisho wa siku hata yeye alikutana na kichapo ndipo nilipoamua kutimua mbio usiku ule ule kujinusuru na kichapo ambacho nilihisi kingepelekea kifo changu."

Nilitulia kidogo kufuta machozi.

" Noelaa, Noela... " Mama Fabiana alimwita Noela.

" Abee mama." Aliitikia kutoka jikoni.

" Hebu tuchemshie maziwa maana siyo kwa baridi hii." Alimuagiza.

" Sawa mama." Noela alimjibu na kurudi jikoni.

" Simulizi yako inahuzunisha sana Christina kwa umri wako sikutegemea kukutana simulizi yenye kusisimua kama hii, eenh na huyo Meshack yeye yuko wapi? "

Aliniuliza swali ambalo lilinifanya niikumbuke siku ile nikiwa natoka na mizigo yangu kuelekea stendi huku yeye akiwa ndani ya gari la kaka yake na kuondoka zao, niliumia sana kusema kweli basi tu.

" Na yeye alifukuzwa shule kama mimi tu japo mwenzangu inaonekana kwao mambo safi kwani alifuatwa na kaka zake ambao waliondoka naye bila hata kunipa nafasi ya kuongea naye hata kidogo na kutuacha tukiwa tumewatolea macho tu hivyo sifahamu hata aliko kwa sasa."

Nilimjibu.

" Hakukwambia kwao ni wapi?"  Aliniuliza tena.

" Hapana hakuwahi kuniambia mama yangu." Nilianza kulia tena kitendo kilichomfanya mama Fabiana kuanza kunituliza kwani inawezekana hadithi ile ilimsikitisha sana.

" Mama niache nilie tu maana nimewakosea wazazi wangu kwa hilo nakiri lakini na wao walitimiza majukumu yao ya kunipa elimu hii ambayo sikuifahamu vizuri?" Swali hili nilijikuta likinitoka tu kinywani japo lilionekana kumshtua mama Fabiana ambaye aliniangalia kwa muda akatikisa kichwa kunisikitikia na kisha aliinuka kuelekea kwenye chumba ambacho aliniambia nitakuwa nakitumia kwa kipindi chote nitakachokuwa pale kwake.


JE, NI NINI KITAENDELEA? USIKAE MBALI NA KOMPYUTA YAKO, SIMU YAKO KUSUBIRI YAJAYO.


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


            #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post