IMETOSHA MAMA MKWE - 08 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


IMETOSHA MAMA MKWE - 08

sultanuwezotz.blogspot.com 


Baada ya dakika kadhaa alirejea akiwa sweta ambalo alinikabidhi nilivae maana baridi ilikuwa kali sana, nililipokea na kulivaa kisha alisogea karibu yangu na kuketi. Kwa kumtazama tu alionekana kuwa na maswali mengi sana juu yangu.

"Christina unawapenda wazazi wako?" Aliniuliza swali ambalo sikulitarajia muda huo. Ilinichukua muda kidogo kulijibu swali hilo maana sikujua analenga nini kuniuliza.

"Ndiyo nawapenda." Nilimjibu.

"Vizuri sana mwanangu, unajua nini siku zote mzazi hakosei hata iweje hivyo nikiyachekecha haya yote yaliyokutokea napata jibu kuwa hasira ziliwatawala hasa baba yako. Yote ni kwa sababu alikuwa amewekeza malengo yake kwako." Alinieleza mama Fabiana.

"Kivipi aliwekeza malengo yake kwangu?" Nilimuuliza baada kuona sijaelewa vizuri alimaanisha nini.

"Ni hivi alipanda kukusomesha ili baadaye uje uwasaidie watakapokuwa hawana nguvu za kujitafutia mkate wao hivyo kutokana na kilichotokea kilimpandisha hasira baba yako." Alinifafanulia.

"Mama naomba nikuombe kitu." Nilikwambia hivyo mara baada ya kuona maelezo yake ni kama vile anataka kunirudisha nyumbani kitu ambacho sikuwa tayari kuona linatokea.

"Ruksa." Alinijibu kwa mkato.

"Naomba niishi hapa kwako kwa kipindi hiki chote mpaka pale ambapo nitaridhia kurudi nyumbani." Nilimweleza mama Fabiana.

"Wala usijali katika hilo mwanangu lakini jambo moja tu ambalo ni la muhimu sana kwa usalama wako na mimi pia hata kwa kiumbe kilicho tumboni mwako." Alinishtua kidogo.

"Lipi hilo mama?" Nilimuuliza.

"Kuwajulisha wazazi wako wajue kuwa haujapotea uko hapa...." Kabla hajaendelea nilimkatisha.

"Hapana mama siyo kwa sasa, wataambiwa tu muda ukifika ila si kwa sasa." Nilimwambia.

"Sawa mwanangu lakini kumbuka kuwa huko wako kukutafuta kila kona na baada ya kukukosa watakwenda kutoa taarifa Polisi ambao wataanza kukusaka kila kona na mwisho wa siku watakukuta hapa unafikiri nini kitatokea kwangu?" Maelezo ya mama Fabiana yaliniingia vilivyo na kujikuta kuwa naweza kumsababishia matatizo kwa swala ambalo linaweza kutatuliwa hivyo ilibidi nikubaliane naye.

" Nimekuelewa mama kwa hiyo unataka nirudi nyumbani?" Nilimuuliza.

" Hapana sijamaanisha hivyo Christina kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni wewe kunitajia namba ya simu ya baba au mama niipige kisha wewe ndiyo uongee nao ili kuwatoa hofu." Hilo nilikubaliana naye nikamtajia namba ya mama na baada ya kuipiga ilipatikana na sekunde sifuri ilipokelewa.

" Nani anaongea?" Mama yangu aliniuliza baada ya kuipokea simu. Nilivuta pumzi kwanza kabla ya kuongea chochote huku mama Fabiana akinipa ishara ya kuongea kisha niliongea.

"Mama ni mimi mwanao." Nilimjibu.

"Wewe mtoto uko wapi lakini mbona unatuweka roho juu kiasi hicho?" Aliniuliza baada ya kujitambulisha.

"Niko mbali sana mama yangu sehemu ambayo hamuwezi kuniona kikubwa eleweni kuwa mwanenu ni mzima wa afya kabisa sina tatizo lolote." Kisha nikaikata simu ile na kumrejeshea simu mama Fabiana.

"Umefanya nini sasa Christina? Ulitakiwa kumweleza uko wapi hujui hapo ndiyo umemchanganya kabisa." Mama Fabiana alinifokea kwa kile nilichokifanya japo kwa upande wangu nilihisi niko sahihi. Lakini akiwa anaendelea kuniambia yale niliyoyakosea mara simu yake iliita na aliichukua na kuiangalia kisha akaniangalia mimi na kuipokea.

" Habari yako, mimi ni msamaria mwema tu ambaye nilimuokota mwanao kwenye mazingira ambayo hayakuwa mazuri hata kidogo maana huko angeweza hata kubakwa lakini Mungu saidia yuko salama kabisa na ninachokuombeni tulieni niendelee kumbembeleza kidogo kidogo maana hataki kabisa kurudi nyumbani." Baada ya kuongea hayo alikata simu na kuiweka pembeni.

"Si umeona Christina haya mambo si rahisi kama unavyofikiria wewe lakini usijali nitalikabili hilo. Kunywa maziwa kabla hayajapoa." Alipomaliza kunieleza hayo aliinuka na kuelekea chumbani kwake na baada ya muda alirejea akiwa na albamu ya picha mkononi na kuketi.

" Hebu sogea hapa nikuoneshe kitu mwanangu." Nilisogea kutaka kujua anataka kunionesha kitu gani kutoka kwenye hiyo albamu yake.

"Unaziona hizi picha hapa." Aliniuliza.

"Naziona." Nilimjibu.

"Huyo aliyekaa juu ya mabomba ni marehemu mume wangu aliyefariki miaka minne iliyopita kwa ajali ya gari akiwa anatoka kwenye majukumu yake ya kikazi mkoani Njombe. Alikuwa ni fundi mkuu wa Mamlaka ya Maji hapa Makambako wakiwa wanarudi kutoka Njombe maeneo ya Mtwango gari lao liliacha njia na kupinduka, sababu kubwa ya ajali hiyo ilikuwa ni ukungu ambao ulitanda sana siku hiyo na kumfanya dereva ambaye alikuwa kalewa kiasi kutoiona barabara vizuri. Nakumbuka sana mume wangu kipenzi mzee Jordan Hangai" Alianza kulia mara baada ya kueleza hayo kitu ambacho kilinifanya nigeuke kuwa mnyamazishi wake japo dakika kadhaa yeye ndiye alikuwa mnyamazishi wangu.

" Pole sana mama yangu kwa hili ambalo sikuwa nalifahamu." Nilimnyamazisha alitulia akajifuta machozi kwa upande wa kanga yake kisha akaendelea kufunua ile albamu yake na baada ya kufika kwenye picha fulani hivi alitulia kidogo.

"Huyu ni mwanangu anaitwa Fabiana ndiye mtoto wangu wa pekee, jicho langu la pekee na taswira yangu nampenda sana sijui ni kwa sababu kafanana sana na marehemu baba yake yaani sijui." Alimuelezea mtoto wake aitwaye Fabiana.

"Yuko wapi mbona hapa nyumbani hatujamkuta?" Nilimuuliza juu ya huyo mwanaye.

"Anasoma, kwa sasa yuko chuo kikuu cha ardhi mkoani Dodoma mwaka wa pili kwa majaliwa ya Mola mwakani anavaa Joho na ndiye mwenye kile chumba ulichofikia wewe." Alinieleza.

"Mungu amsaidie afikie ndoto zake siyo kama sisi wakina kalala wapi tulioishia kufukuzwa majumbani mwetu kwa ujinga wetu." Nilianza kutokwa na machozi kutokana na kile nilichokiongea kilinifikisha mbali sana.

"Wala usijali mwanangu kwani hata wewe bado una nafasi ya kuzifikia ndoto zako baada ya kujifungua."

Alinituliza mama Fabiana.

"Najua haiwezekani kabisa hapa unaniliwaza tu." Nilianza kulia tena.

"Christina naomba unisikilize vizuri wewe bado mdogo miaka chini ya kumi na tano bado sana unaweza kujifungua na kisha ukamuacha mwanao na kwenda kuendelea na masomo ya Sekondari katika shule za kulipia au kwenye taasisi na hatimaye kuziishi ndoto zako." Alipomaliza kuongea hayo nilimgeukia na kumuangalia vizuri.

" Si umeona sasa mama shule za kulipia unafikiri ni nani ambaye ataweza kuufanya huu upuuzi hasa ukizingatia nimeshawakatisha tamaa najua hilo haliwezekani hata kidogo." Alinisogeza miguuni mwake.

"Kikubwa ukiwa na nia ya kutaka kusoma hata mimi naweza kukulipia ada ili uzifikie ndoto zako."

Maneno yake yaliniinua kutoka pale kwenye miguu yake na kukaa vizuri.

"Kweli unaweza kufanya hivyo kwangu mama?" Nilimuuliza.

"Kwanini nisiweze kuna kipi cha kunishinda hapo kikubwa uwe tayari tu." Aliniambia.

"Mimi niko tayari mama yangu." Nilimhakikishia katika hilo mama Fabiana.

"Vizuri sasa ngoja nitoke kidogo nakuja ukichoka utakwenda kulala." Aliniambia akiinuka na kisha alitoka nje na kurudisha mlango.

Baada ya kutoka tu Noela alikuja pale sebuleni nilipokuwa na kunikuta nikiendelea kuangalia picha mbalimbali zilizokuwa kwenye albamu ile ambayo aliniachia.

" Kumbe siyo ndugu yako? " Noela aliniuliza.

"Kwanini unauliza hivyo?" Na mimi nilimrudishia swali.

"Nimeyasikia maongezi yenu yote kuanzia mwanzo mpaka mwisho." Alinijibu Noela.

"Hii dada Noela kwa hiyo mwili wako ulikuwa jikoni masikio yako yote yalikuwa sebuleni kama antena kusikiliza yasiyo kuhusu." Nilimzodoa.

"Tuachane na hayo mdogo wangu ila tu una bahati ya kuongea vizuri hivi na Bi Matrida?" Aliniambia.

"Kivipi?" Nilimuuliza.

"Bi Matrida ni mkali sana hasa kwa mtu anayekwenda kinyume naye lakini ukiendana naye utafaidi sana." Alinijibu Noela ambaye naye alisogea karibu kuziangalia picha. Tukiwa tunaendelea kuangalia picha pale sebuleni mara mlango uligongwa.

"Ni nani tena huyo?" Noela aliuliza huku akiinuka kuufuata na baada ya kuufungua kumbe alikuwa ni Kenedy.

"Kulikoni tena na wewe?" Alimuuliza swali akiwa pale pale mlangoni kaushikilia mlango.

"Noela unakuaje hivyo ina maana mimi siruhusiwi kuingia ndani?" Kenedy alimuuliza dada Noela.

"Siyo hivyo ila nashangaa maana siyo kawaida yako kuacha geti mida kama hii." Alimjibu.

"Hebu achana na mawazo hayo potofu nimeambiwa na mama nije nichukue maziwa." Ilibidi amwambie kile kilichomleta pale.

"OK nilijua umeijia mambo yako ya kijinga." Noela alimuacha na maneno ambayo yalinishtua kidogo. Kisha alimuacha na kuelekea jikoni kumchukulia maziwa.

"Karibu sana mgeni wetu jisikie nyumbani." Kennedy alinikaribisha baada ya kuingia sebuleni.

"Asante sana nimeshakaribia tayari." Nilimjibu na wakati huo huo dada Noela alifika na kumkabidhi glasi ya maziwa kisha Kennedy aliipokea na kuondoka zake na kutuacha.

"Unajua nini Kennedy anakuaga na utani sana na ndiyo maana mama huwa hataki yeye kuacha geti na kuja kucheza ndani." Dada Noela aliongea hayo baada ya kuona nimeng'amua kitu baina yao.

"Dada Noela una mambo wewe sasa mtu mzima kama yule anachezaje ndani?" Nilimuuliza swali ambalo lilimfanya ajing'ateng'ate kabla ya kulijibu.

"Hebu tuachane na mambo ya Kennedy tuendelee kuangalia picha bwana." Alinijibu kisha tuliendelea kuangalia picha zile na baada ya kuona macho yameanza kukosa nguvu nilimuaga na kwenda zangu kulala na kumuacha pale pale sebuleni.


NINI KITATOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA MKASA HUU.


          #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post