IMETOSHA MAMA MKWE - 09 (Mtunzi: Sultan Uwezo)


 IMETOSHA MAMA MKWE  - 09

sultanuwezotz.blogspot.com 


Maisha ndani ya mji wa Makambako wenyewe wakiuita mji wa Jah People yalisonga na siku wiki hata miezi pia ilikatika huku nikiwa mikononi mwa mama yangu mlezi mama Fabiana. Aliyabeba mazuri yangu pamoja na mabaya yangu pasipo kuchukua maamuzi magumu juu yangu zaidi ya kunishauri. Kiukweli maisha niliyafurahia sana mpaka kuna muda nilijisahau na kujikuta nikimuingiza mama Fabiana kwenye kundi la ndugu zangu kutokana na vile tulivyokuwa tunaishi kizuri zaidi hata baada ya mtoto wake Fabiana kurejea likizo alinipokea kama ndugu yake na wala hakuchukia kwa mimi kukitumia kitanda na vitu vyake zaidi aliendelea kunitia moyo.

Siku moja nikiwa njiani natoka sokoni na Noela tulipishana na Bajaj moja ya rangi ya blue ambayo ilikuwa kasi ikielekea tunakokwenda sisi lakini kilichonishtua ni mtu mmoja ambaye alituchungulia kwa kutoa kichwa nje, nilimfananisha na mama japo haikuwa kwa asilimia mia moja lakini mpaka mapigo ya moyo yalinidunda.

"Mbona yule mama alituchungulia vile akianguka sasa?" Noela aliuliza baada ya kumshuhudia mtu yule aliyetuchungulia.

"Atakuwa na yake tu si unajua tena mjini hapa." Nilimjibu japo mimi mwenyewe nilipatwa na mshtuko juu yake.

Hivyo tulijivuta mpaka nyumbani lakini kitu cha kushangaza ile Bajaj ilikuwa ndiyo inaacha mazingira ya nyumbani hivyo tulimfuata Kennedy na kumuuliza ni ugeni gani uliowasili.

" Kaka Kennedy hiyo Bajaj tuliyopishana nayo hapo njiani imemleta nani?"  Nilimuuliza.

"Mmhh hapana simfahamu lakini anaonekana kufahamiana vizuri na mama." Alinijibu.

"Acha maswali twende zetu ndani bwana mama Fabiana hutembelewa na wageni wengi sana." Noela aliniambia huku akinishika mkono.

Basi tuliachana na mlinzi wetu Kennedy pale getini na kuingia ndani na baada ya kufika tu kwenye lango la kuingilia sebuleni sikuamini macho yangu baada ya kukutana uso kwa uso na mama yangu mzazi haki Mungu sikuamini kabisa nilijikuta nikiishiwa nguvu mwilini sikujua ni mchezo gani alioucheza Bi Matilda kwenye hili sikuona sababu ya kusalia pale niliishika njia kuelekea chumbani.

"Christina, wee Christina kwamba hujatuona hapa sebuleni au?" Bi Matilda aliniita lakini sikutaka kumsikiliza niliongeza mwendo. Niliingia chumbani na kuufunga mlango kwa komeo kabisa kwani nilijua mwisho wa furaha yangu umewadia na mimi sikuwa tayari kuipoteza furaha yangu.

" Tina, Tina mwanangu hebu fungua mlango kwanza najua umechukia kwa kile ulichokiona lakini hebu fungua mlango nikueleze kila kitu kumhusu mama yako mpaka akawa hapa." Mama Fabiana (Bi Matilda) aliendelea kulisisitiza jambo hilo ambalo mimi kama Christina sikuwa tayari kulisikia hata kidogo hivyo nilijifunika blanketi wenyewe wanasema gubi gubi. Baada ya kuita kwa muda mrefu bila mafanikio yoyote aliondoka kurudi sebuleni na mimi nilipoona mlango umeachwa kugongwa niliamka na kuketi kitako kufikiria mama kafuata nini hapa au ndiyo kanifuata mimi. Anataka nirudi nyumbani? Nilijiuliza maswali mengi sana ambayo hayakuwa na majibu niliinuka pale kitandani mpaka kwenye kioo pale 'dressing table' na kujitazama kwa muda kisha nikajiapia.

"Kwa sasa siwezi kurudi nyumbani hata kwa Katapila na kama Bi Matilda kanichoka niko tayari kwenda kulala mtaani na wale watoto wanaoitwa 'Walala Singe' na baada ya kufikia hapo niliinuka na kuuendea mlango nikaufungua na kutoka mpaka sebuleni ambapo nilimkuta mama yangu mzazi akiwa kajiachia akiangalia televisheni.

"Mwanangu mbona umenuna hivyo au hujafurahishwa na ujio wangu?" Mama aliniuliza baada ya kuniona nimefika na kukaa bila kuongea chochote.

"Wala sijachukua ila kuna uwezekano nikayachukia au kuyafurahia yale yaliyokuleta hapa." Nilimjibu mama.

"Bila shaka utayafurahia tu sina uhakika kama utayachukia mwanangu." Mama Fabiana Bi Matilda alinijibu akija taratibu akitokea jikoni na glasi mbili za juisi.

"Ni kweli kabisa Bi Matilda mwambie inawezekana anajua kuwa niko hapa labda kumfuata yeye kumbe lililonileta ni jingine kabisa." Mama alidakia huku akipokea glasi ya juisi kutoka kwa Bi Matilda.

"Christina nakuomba usimchukie mama yako kama ni mtu anayetakiwa kuchukiwa ni mimi na si mwingine mwanangu, mimi ndiye niliyemwambia aje baada kuona miezi inakimbia na siku zako zimesogea nikaona niombe usaidizi kutoka kwa mama yako na si hivyo tu bali kwenye kila hatua yako ya malezi ya mimba nilimjulisha hivyo usifikiri kuwa kaja akiwa hajui hali yako kwa ujumla ilikuwaje na ikoje anafahamu kila kitu mwanangu."  Maelezo marefu ya mama Fabiana yalinifanya niwe mpole kwani sikujua lolote kwenye hilo mimi akili yangu yote nilijua mama kanifuata.

" Kwanza kabisa naomba nikuhakikishie mama yangu mlezi kuwa wewe siwezi kukuhukumu hata siku moja nakumbuka ulikonitoa mpaka ulikonifikisha hivyo nitakuwa mtovu wa nidhamu iwapo nitafanya hivyo pili naomba nimkaribishe mama yangu hapa niko tayari kupokea huduma yake yoyote ile isipokuwa moja tu ya kunikutanisha na baba yangu kwa namna yoyote ile." Nilipomaliza kuongea hayo tu mama alinifuata na kunikumbatia kwa furaha kubwa.

" Mwanangu siko tayari kuipoteza furaha yako iliyodumu kwa miezi kadhaa hata kidogo bali niko hapa kuhakikisha kuwa unajifungua salama kabisa."

Alinieleza hayo mama yangu akiwa kanikumbatia. Hakika ilikuwa ni furaha pale sebuleni kwa wakati ule kila mmoja akiwa na furaha isiyo na kifani.

" Unajua nini mama Tina?"  Bi Matilda alimuuliza mama swali.

" Naam Bi Matilda."  Mama alimjibu.

" Mwanao ana akili sana sema alichokutana nacho ni mitihani tu ya dunia." Alinielezea mama Fabiana.

"Namfahamu sana mwanangu kwenye hilo na ndiyo maana hata hili lilipotokea nilihitaji sana kumsikia mwenyewe lakini ndiyo hivyo tena baba yake alipandwa na gadhabu kiasi cha kumfanya Tina kutoroka jambo ambalo hata yeye hana amani kwa sasa hata chembe baada ya kubaini kuwa alifanya makosa yaliyopelekea mtoto kuondoka lakini yote kwa yote Mungu ni mwema." Mama alieleza kile ambacho kilikuwa moyoni mwake.

" Ni kweli kabisa lakini nikuhakikishie kuwa pamoja na yote mwanenu baada ya kujifungua atarudi shule kuendelea na masomo kwani mpaka hivi tunavyoongea anahudhuria masomo yake jioni kwenye kituo kimoja hapo mjini na nina imani hataathirika na chochote kile kwani wale aliowaacha shuleni atamaliza nao kidato cha nne au yeye atatangulia." Mama Fabiana alimwambia mama kile ninachokifanya kwa wakati wote niliokuwa pale kwake kiasi cha mama kushangazwa kwani hakutarajia kusikia kitu kama hicho.

" Hilo linawezekana kweli ndugu yangu?" Mama aliuliza kwa mshangao.

" Kwanini nikudanganye hilo litawezekana vizuri tu kwani iwapo atajiunga na vituo vya miaka miwili kwa masomo ya kidato cha kwanza mpaka nne atatangulia kuhitimu kwa maana yeye atautumia mwaka ujao na ule mwingine wakati wenzake wakiwa kidato cha tatu lakini yeye ndiye ataamua." Mama Fabiana alifafanua kauli yake.

" Mmh yaani sijui hata niseme nini katika hili ulilolifanya kwa mwanangu lakini niseme tu nakushukuru sana na kwa sasa wewe ni zaidi ya ndugu." Mama alimshukuru Bi Matilda.

" Wala usijali Christina kwangu kawa mtoto wangu kwa namna nilivyoishi naye kwa kipindi hiki namfahamu vizuri akiwa na furaha anakuwaje na hata akiwa na hasira anakuwaje." Bi Matilda alimuondoa hofu mama juu yangu.

Mazungumzo ya hapa na pale yaliendelea pale sebuleni mara baada ya kila kitu kuwa sawa na mimi nikaona niwaache na kuelekea jikoni kuungana na dada Noela kuandaa chakula. Niliingia kule na kumkuta akiwa ndiyo anajiondoa mlangoni na ungo wa mchele mara baada ya kuniona.

"Kama kawaida yako dada hupitwi na kitu hatari wewe." Nilimwambia baada ya kuingia.

"Niache bwana wewe laha ya ubuyu uumung'unye mwenyewe na si umung'unyuliwe na mtu." Alinijibu akikaa.

"Pamoja na yote lakini mwenzangu umezidi hee si kwa umbea huo." Nilimpa za uso.

"Wacha tu niwe mumbea mwenzangu labda siku nikifika huko Mbeya ndiyo naweza kuiacha hii tabia maana wanasema dawa ya moto ni moto na kwa kuwa mimi napenda umbea inawezekana nikifika Mbeya nitaachana nao." Yaani Noela hata aibu hana hata kidogo na mbaya zaidi hata tone la aibu hana sasa hofu yangu ni itakuwaje siku akiolewa na umbea wake huo si ataachika mara moja kwani hatakuwa tayari kuukosa umbea hata kama mume yuko kitandani.

" Huna lolote hebu lete huo ungo nikusaidie kuchambua mchele na wewe endelea na umbea wako si unalipa." Nilikwambia nikiamini atashushuka lakini wapi mtu mwenyewe dada Noela yaani ni kiboko yao.

"Ila nikwambie kitu mdogo wangu?" Alianza mambo yake.

"Hukomi tu dada Noela?" Nilimuuliza swali.

"Wacha niendelee kupunguza magonjwa bwana wewee, yaani wewe na mama yako ama mnafanana utafikiri mapacha? Jamani!"

"Sasa hapo ajabu iko wapi kwa mama kufanana na mtoto wake? Au ulitaka nifanane nani au jirani?" Nilimuuliza.

"Umesema wewe na si mimi mbona mimi nimefanana na baba yangu wala si mama." Alinijibu.

"Cheki sasa toto la kike kufanana na baba hapa sishangai mfanano bali navuta picha huyo baba yako naye ni mzee wa ubuyu kama wewe?" Nilimuuliza swali la maudhi kidogo ambalo lilimpandisha hasira.

"Weeee ishia hapo hapo tuongee mengine yote tutaniane vyovyote vile lakini usiwaingize wazazi wangu na tena iwe mwisho." Katika kuishi kwangu kote na dada Noela sikuwahi kumshuhudia akiwa kachukia kwani hata alivyonifikia na kunipiga roba ya shingo sikumuona nilishtuka mtu yuko mbele yangu kanitolea macho.

" Hee kumbe na wewe unachukiaga dada Noela?" Nilimuuliza.

" Ndiyo sasa mnafanya hapo?"

Lilikuwa ni swali ambalo lilitufanya wote tuishiwe pozi huku dada Noela akiniachia na kuuchukua mchele haraka.


NI NANI HUYO KATUFUMA?



TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA KUMJUA LAKINI UNAWEZA KUBASHIRI.


       #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post