IMETOSHA MAMA MKWE - 10 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


IMETOSHA MAMA MKWE - 10

sultanuwezotz.blogspot.com 


Tuliishiwa pozi kwa pamoja maana tulikuwa tumejiachia wenyewe kama vile tuko kwenye makazi yetu tawaliwa. Kutetemeka kwa Noela kulipelekea mchele wote kumwagika na kubaki kaushikilia ungo uliokuwa na vipunje kadhaa vya mchele, tukio hilo ndiyo liliivuruga kabisaa akili ya Noela kwani alijikuta akiinuka na kumfuata Bi Matilda pale mlangoni.

"Naomba usipandishe hasira zangu bure Noela nafikiri si mgeni kwangu, ondoka miguuni kwangu haraka." Bi Matilda aliongea kwa hasira na kusogea pembeni na kumuacha Noela akiwa kaisujudia sakafu. Hali ile iliniogopesha sana mimi kwani sikuwahi kuiona sura ya Bi Matilda hata mara moja ikiwa kwenye hali ile hivyo nilitetemeka sana nikijua baada ya Noela ni zamu yangu.

"Christina !!" Aliniita baada ya kunitazama.

"Abeee mama." Niliitikia kwa hofu.

"Hujihurumii na hali yako siyo au unafikiri umebeba manguo tumboni mwako?" Aliongea maneno makali juu yangu kiasi cha kuniogopesha.

"Hapana mama ni bahati mbaya tu imetokea dada Noela kazidisha michezo yake kiasi cha kufikia pale ulipotukuta lakini tunaomba msamaha wako halitojirudia hili tena." Nilimsogelea Bi Matilda karibu na kumuomba msamaha kwa kile tulichokifanya ambacho ni uhakika kingepelekea matatizo kwangu bila kujua si unajua utoto tena. Pamoja na niliyomweleza mama Bi Matilda huwezi amini hakuweza kunijibu chochote alichokifanya aliinama kuniinua.

"Unayajutia uliyoyaongea kweli?" Aliniuliza akiwa kanikazia macho. Kwa hofu nilimjibu kwa ishara ya kutingisha kichwa kuashiria kukubali kuwa najutia hilo.

"Sijakuelewa Tina." Alinitega nikajua shida yake ni kuisikia sauti yangu yenye wingi wa uoga.

"Najutia mama yangu tena sana nahisi hata dada Noela kajuta kupitiliza na ndiyo maana yuko hapo chini mpaka sasa akitiririkwa na machozi ya majuto." Maneno yangu yalipenya vilivyo kwenye vifereji vya masikio ya mama Bi Matilda na baada ya kuyachanganua alikuja na jibu ambalo liliamsha tabasamu lenye wingi wa furaha nyusoni mwetu wote pale jikoni.

" Kwa kuwa ni kosa lenu la kwanza lenye wingi wa utoto ndani yake nawasamehe kwenye hili wanangu endeleeni na kazi ila nisingependa kuwaona pamoja humu jikoni hivyo Tina elekea chumbani kwako kajiandae tunaelekea mjini."  Mama alihitimisha na kutoka zake huku nyuma tulikumbatiana na dada Noela kwa ushindi tulioupata mbele ya Bi Matilda ambaye alikuwa anakwenda kufanya maamuzi magumu.

" Umeona kilichotokea?" Nilimuuliza dada Noela.

" Nimeona mwenzangu lakini wewe ndiyo chanzo mdogo wangu kwa sababu usingeingia huku jikoni haya yote wala yasingetokea." Noela aliongea hayo akiniachia.

"Endelea kunilaumulaumu hapa nikurudie mikono mitupu hapa bila zawadi yoyote." Nilimchimba utani.

"Hee mdogo wangu hutaniwi na weweee hebu wahi mama asije rudi hapa moto ukawaka upya bure." Kauli ya dada Noela ilinifanya nitoke mbio kuelekea chumbani maana kwa kilichotokea sikuwa tayari kumpandisha mama Fabiana mashetani ya nchi jirani ambayo yakikupanda tu kitu cha kwanza kukuomba ni 'chips mguso' niliingia chumbani na kufanya usafi wa mwili wangu pale bafuni na baada ya kumaliza nilitoka chumbani nikiwa najifuta maji mwilini si unajua mambo ya peke yako chumbani hujali kitu hivyo nilijiachia mwenyewe. Lakini ile kugeuka tu nyuma macho yangu yalikutana na mama ambaye hata sikujua kaingia muda gani chumbani mwangu, weee kilichofuata ilikuwa ni kutaka kukata kona kurejea bafuni lakini kabla sijafanya hivyo niliteleza na kuanguka. 

"Christinaaaaaaaaa.........." Ni maneno ya mwisho ya mama yangu niliyoyasikia kabla ya kupoteza fahamu kabisa.


"Mmh hapa ni wapi tena?" Lilikuwa ni swali lililopita kichwani kwangu mara baada ya kupata fahamu. Kilikuwa ni chumba kizuri kilichovutia kukiangalia kutokana na muonekano wake lakini kitu cha utofauti ni vitu vilivyokuwa ndani yake na hivyo ndiyo vilinifanya nipate uoga.

" Umeamka mwanangu?" Lilikuwa ni swali kutoka kwa mama yangu baada ya kuingia ndani aliloniuliza japo jibu lilikuwa mbele yake labda alihisi macho yake yanamdanganya.

"Mama niko wapi hapa? Na nimefuata nini hapa mama yangu?" Nilimuuliza mama yangu aliyenifuata na kuketi karibu yangu pale kitandani nilipokuwa nimelala.

"Mwanangu Christina hapa ni hospitali tulikukimbiza hapa jana mara baada ya kudondoka pale chumbani."  Aliniambia mama yangu huku akiwa ananishikashika nywele zangu taratibu kwa sauti ya upole kama siyo yule ninayemjua vizuri.

"Mwanangu kapona mama?" Nilimuuliza tena swali nikiwa nimeupeleka mkono wangu wa kulia tumboni. Lakini mama yangu baada ya kusikia swali langu aliachia tabasamu pana huku akikaa vizuri pale kitandani.

"Ashukuriwe Mola mwanangu mwanao ni mzima kabisa wa afya na kwa maelezo ya daktari baada ya vipimo ni siku kama siyo masaa unakwenda kukumbatiana na mwanao." Maelezo ya mama yangu yalitaka kuniinua kitandani lakini mama alinizuia na kunirejesha kitandani.

"Mwanangu bado hali yako haijakaa sawa unataka kufanya nini tena?"  Mama alinituliza.

"Taarifa yako imenitia kiwewe mama yangu kwanini nisichanganyikiwe?" Nikiwa mwenye tabasamu tele usoni nilimjibu mama.

"Sasa mwanangu hiyo tu inakuchanganya hivyo nikikupa ya pili si ndiyo utatoka na kuanza kupiga makelele makoridoni." Mama aliniambia.

"Kuna nyingine tena?" Nilitokwa na swali jingine lakini tofauti na matarajio yangu jibu lilikuja kutoka kwa mtu mwingine.

"Lipo mwanangu, ndiyo lipo." Hakuwa mwingine bali alikuwa ni Bi Matilda ambaye aliingia akiwa kaongozana na dada Noela.

"Mmhh mama nawe umesikia nini?" Nilimuuliza Bi Matilda mara baada ya kuketi kitandani karibu na mama.

"Kila kitu nimekisikia nikiwa mlangoni nikaona niwakatishe kwanza, lakini nikuulize swali mwanangu?" Bi Matilda aliniuliza.

"Niulize tu mama japo najisikia njaa." Sikutaka kusubiri maana niliona soga zimezidi wakati mwenzao nikutia kitu chochote tumboni kwa muda.

"Noela fanya haraka basi mbona pole pole hivyo nilishakwambia jifunze kuwa shapu shauri yako utaachwa ukiwa bado unapenda ohohh." Wanajuana hawa kwani maneno ya mama Bi Matilda yalimfanya Noela atabasamu bila kuongea chochote huku akiendelea kuandaa chakula.

" Mama bwana muache dada Noela umesema unataka kuniuliza swali niulize sasa." Nilimwambia.

" Katika huo ujauzito wako ungependelea kujifungua mtoto gani?" Swali la mama yangu mlezi liliniduwaza kidogo.

"Mtoto gani tena?" Nilimuuliza.

"Ndiyo." Aliitikia.

"Mama au umesahau kuwa uliniambia mimi ni mama kijacho?" Nilimuuliza.

"Nakumbuka mwanangu." Alinijibu.

"Sasa iweje mama yangu wa ukweli mama kijacho akachagua jinsi ya mtoto?" Nilimuuliza swali ambalo lilimfanya asogee na kunikumbatia.

"Kweli umekuwa binti yangu unazungumza kama mtu mzima?"  Mama yangu mzazi aliongea hayo huku akijifuta machozi yake kwa upande wa kanga.

Hali ile ilimfanya Bi Matilda amchukue mama na kutoka naye nje na kutuacha na mcharuko wangu dada Noela.

"Ilikuwaje na wewe mpaka ukaanguka? Bahati yako sikuwepo ningekushindilia mingumi ya mtumbo wako huu kwanza ushike adabu ndiyo ningeita msaada." Dada Noela aliniuliza kiutani huku akinikumbatia kwa furaha yaani nalipenda hili lidada mcharuko sema ndiyo hivyo ukiligusa kwenye vidonda vyake linakubadilikia muda huo huo.

" Ningekuacha? Ungejuta mwenyewe kunijua."  Nilimjibu huku nikimpigapiga kisogoni.

"Nini tena ninyi?"  Lilikuwa ni swali kutoka kwa Bi Matilda ambaye alituuliza mara baada ya kuingia ndani na kutukuta tukiwa tumekumbatiana. Haraka sana dada Noela alijitoa kwangu na kutoka kuinuka ili aondoke lakini mimi nilimzuia asifanye hivyo. 

"Mama Noela kaja kunipa pole tu wala si vurugu zake kama za siku ile." Nilimjibu mama Bi Matilda ambaye alitoa ishara ya kunielewa kwa kunipa dole. 

"Sasa inuka ule maana muda wa kuona wagonjwa unakaribia tusije ondoka na wewe ukashindwa kula kwa kuwa uko peke yako." Mama alinitaka nile chakula ambacho tayari kilishaandaliwa na dada Noela.

"Kwa hiyo mama mtaondoka na kuniacha peke yangu hapa Hospitali?" Ilibidi niulize maana ni kama nilisikia vibaya yaani nilale peke yangu pale Hospitali. 

"Ndiyo binti ni utaratibu wa Hospitali hii hawaruhusu watu wengine kulala hapa zaidi ya mgonjwa mwenyewe lakini usijali nesi anayekuhudumia ni rafiki yangu hivyo atahakikisha kila kitu kinakwenda vizuri." Majibu ya Bi Matilda yalinifanya nikose hata hamu ya chakula kwani nilitamani kama walivyo walale nami pale kitandani lakini ndiyo hivyo tena. Wakiwa wanajiandaa kutoka mara mlango uligongwa. 


JE NINI KITAENDELEA? 


USIKOSE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA KUJUA NINI KILIENDELEA. 


        #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post