IMETOSHA MAMA MKWE - 18 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


IMETOSHA MAMA MKWE - 18

sultanuwezotz.blogspot.com 


"Ndiyo dada yangu mmefika wapi?" Bi Matilda alimuuliza mama mara baada ya kupokea simu.

Sikuweza kusikia mama aliongea nini lakini nilimsikia Bi Matilda akimjibu mama.

"Nisamehe bure ndugu yangu simu yangu niliitoa mlio kutokana na sehemu ambayo nilikuwa na baada ya kutoka ndipo nikaona miss calls zako, nisamehe bure mko wapi lakini?" Aliuliza na baada ya kupewa majibu kutoka upande wa pili mara alikata simu na kunitazama.

" Wazazi wako wameshafika stendi hivi ninavyoongea na wewe wanajiandaa kuelekea nyumbani hivyo tufanye haraka tuwawahi." Alinieleza akiiweka simu yake kwenye pochi yake.

"Afadhali maana siyo kwa kuwamisi kule." Nilimjibu mama Fabiana huku tukiingia kwenye taxi ambayo tuliisimamisha.

"Tunaelekea eneo la misheni sijui tukuchangie kiasi gani?" Mama Fabiana alimuuliza dereva Taxi yule.

"Kwa mwingine sawa lakini kwako mama yangu siwezi fanya hivyo nitakupelekeni bure kabisa." Majibu ya dereva taxi yule yalimfanya mama Fabiana amtazame vizuri ili kuona kama anamfahamu.

"Mbona unanitazama hivyo mama yangu kwamba hunitambui au?" Aliuliza baada ya kuona mama Fabiana anamtazama zaidi usoni.

"Ni kweli kijana wangu inawezekana nimekusahau lakini sura yako ni ngeni kabisa kwangu." Mama Fabiana aliona asijifunge akaongea ukweli wake juu ya kijana huyo ambaye alikuwa na furaha muda wote nyuma ya usukani.

"Inawezekana umenisahau kweli maana ni muda mrefu sana toka kuonana mara ya mwisho, mimi naitwa Ruben Kaijo ni mtoto wa....." Alipofika hapo tu mama Fabiana alimkumbuka kwani alimkatisha mara moja.

"Ishia hapo hapo Ruben Kaijo, mtoto wa Afisa Uhusiano Shirika la reli Tazara Kituo cha Makambako si ndiyo?" Alimuuliza kwa bashasha la aina yake.

"Ndiye mimi mama." Ruben alimjibu.

"Jamani kweli miaka inakwenda kasi sana yaani Ruben umekua namna hii hata ingekuwaje nisingeweza kukukumbuka hata chembe maana mlihama Makambako ukiwa na miaka kumi kama sikosei." Mama Fabiana aliongea hayo akiitoa simu yake.

"Ni kweli kabisa mama nilikuwa mdogo sana na sasa nina miaka ishirini na tano." Alimjibu mama Fabiana huku akiendelea kuendesha gari yake taratibu huku macho yake yakiwa ndani ya miwani angavu ambayo haikumtatiza kuiona barabara vizuri.

"Enhh kwa sasa mnaishi wapi? Maana nakumbuka mlipohama mlielekea mkoani Morogoro." Mama Fabiana alimuuliza.

"Morogoro hatukukaa muda mrefu sana tukahamishiwa Dar es Salaam huko mzee wangu alifanya kazi kwa miaka saba tu akapata matatizo kazini ambayo yalipelekea kusimamishwa kazi na kupisha uchunguzi ambao hatujui uliishia wapi kwani baadaye alipata matatizo ya moyo ambayo miaka miwili baadaye alifariki. Hatukuwa na chaguo jingine zaidi ya kuliacha jiji la Dar es Salaam na kurudi Mbeya si unajua tena mama ni mzaliwa wa kule na tayari mzee alikuwa amefanya uwekezaji kidogo..." Alipofika hapo alipunguza mwendo akatoa kitambaa kisha akaitoa miwani yake na kujifuta machozi na kisha akairudisha miwani sehemu yake.

" Oohh jamani, poleni sana kumbe mzee Kaijo alishafariki muda mrefu?" Alimpa pole huku akimtupia swali jingine.

" Asante mama tulishapoa na maisha yanaendelea kama kawaida kwa sasa mimi naishi mkoani Mbeya sehemu moja inaitwa Forest mpya nikiwa msimamizi mkuu wa kampuni ya Uzalishaji Kuku na Chakula  iitwayo 'Kaijo Kuku Bora Co. Ltd' ambayo iko eneo la Viwanda Kabwe huku mama yeye akiishi Forest ya zamani na mdogo wetu wa mwisho." Ruben alitoa maelezo ambayo yalimfanya mama Fabiana kushangaa sana, japo alitamani kuendelea na maswali aliona akatishe lakini akamuomba namba yake ya simu na ya mama yake ambapo Ruben alichomoa kadi kwenye dashboard ambayo ilikuwa na mawasiliano na kumkabidhi.

"Hizo zote zinapatikana." Alimweleza mama Fabiana.

"Nashukuru sana kijana wangu nilitamani tuendeleze maongezi haya mazuri lakini ndiyo hivyo ninawawahi wageni wangu hivyo kwa kuwa nimepata namba hizi najua tutaongea kwa kirefu zaidi." Mama Fabiana alimshukuru kwa kumkabidhi mawasiliano yake na kisha alimuelekeza kwa kutushushia.

" Hapana mama nielekeze nyumbani niwakimbize mara moja kisha niendelee na safari yangu sina haraka sana." Ruben alimjibu hivyo mama Fabiana. Hivyo ilibidi amuelekeze barabara ya kuelekea nyumbani na tatizo Ruben alikanyaga mafuta mpaka barabara ielekeayo misheni mtaa wa Bwawani ambako ndiyo makazi yetu.

"Dada nakaribia kufika, nipe dakika sifuri." Mama Fabiana aliongea na mama kwenye simu ikiwa ni hofu ya mama baada ya kuona hatufiki haya yote yamesababishwa na usafiri wa taxi huu ambao tuliuchukua siku zote tumezoea usafiri wa Bajaj.

"Makambako imebadilika sana mama siyo kama zamani yaani mgeni akiambiwa hapa ni makao makuu mkoa fulani lazima akubali kumbe ni mji fulani fulani ambao umebaniwa sana na kuwa wilaya." Ruben alibadilisha mada baada ya kuona mama Fabiana anajitetea kwenye simu.

" Mmhh lakini tayari ni halmashauri ya mji mdogo wa kibiashara ukiwa tayari umejizolea umaarufu ndani ya nchi na nje ya nje." Mama Fabiana alimjibu Ruben aliyekuwa akiiacha barabara inayoelekea Hospitali ya mji na kushika barabara ya kuelekea misheni.

"Huku naelekea wapi mama?" Ruben alimuuliza mama Fabiana baada ya kuifikia barabara inayoelekea ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania.

"Ifuate hiyo barabara iliyo mbele yako nyoosha mpaka kwenye vile vibanda pale mbele kisha utakunja kulia kwako utaiona nyumba kubwa yenye gari bovu nje." Mama alimuelekeza naye akaifuata kama alivyoelekezwa.

"Sawa mama." Ruben aliitikia na kisha kuongoza. Na haikuchukua muda mrefu sana tukawa nje ya geti.

"Bila shaka ndiyo hapa?" Ruben aliuliza akipaki gari kando ya geti.

"Bila shaka ndiyo hapa hapa mwanangu tunashukuru sana kwa msaada wako haya karibu ndani upate japo maji ya kunywa." Mama Fabiana alimkaribisha ndani Ruben.

"Mama nashukuru sana, kikubwa nimeshapafahamu nyumbani nitakapokuwa narudi kutoka Dar es Salaam nitapitia hapa." Ruben alimjibu.

"Haya mwanangu ni wewe tu kikubwa umepafahamu nyumbani karibu sana na ukiishia mitini tu namba umenipa nitakiwasha." Mama alimjibu Ruben aliyekuwa akiingia kwenye gari.

"Wala usijali mama niamini tu." Ruben alimjibu kisha akapandisha kioo huku mama akimpungia mkono wa kumuaga.

"Haya wenye ndugu wanaomiliki magari." Nilimuanza mama Fabiana tukiwa getini kumsubiri Kennedy atufungulie.

"Mhh nawe umeanza maneno mengi yasiyofanana na umri wako hebu tuingie zetu ndani." Mama alinijibu tukiingia ndani kupitia lango dogo mara baada ya dada Noela kutufungulia.

"Na Kennedy je?" Mama Fabiana alimuuliza dada Noela aliyetufungulia mlango.

"Kennedy kaenda mjini kufuata vitu maana jikoni vilipungua kabisa na ukizingatia wageni walishawasili muda mrefu." Dada Noela alimjibu mama huku mimi nikifunga mlango.

"Okay sawa si wako ndani wageni wetu." Mama Fabiana aliuliza.

"Ndiyo." Alimjibu.

Tuliingia ndani na kuwakuta wakiwa wametulizana sebuleni wakiangalia televisheni huku mama akiwa kampakata mjukuu wake.


"Waoo wageni hao jamani." Mama Fabiana alianza kwa kuwakaribisha wageni wake.

"Wageni wapi sisi tulishakuwa wenyeji muda mrefu sana na mjukuu wetu mikononi." Baba alimjibu mama Fabiana kabla mama hajaongea chochote.

"Na kweli kama uonavyo mwenyewe hapa." Mama naye alidakia.

"Thobias mwenyewe katulia tuli hata kuhisi kama mama yake nimerudi hakuna kaa." Niliongea huku nikimshikashika mwanangu.

"Enhh mama Christina mnaendeleaje na pole kwa majukumu tuliyokuachia." Baba alimsalimu mama Fabiana akiwa na shauku ya kutaka kujua tunaendeleaje.

"Kiukweli......." Mama Fabiana alianza kujibu lakini alishindwa kuendelea kwani nilimkatisha.

"Baba kiukweli sina cha kumlipa mama yangu huyu kwani nikifikiria tulivyokutana na tunavyoishi Mungu ndiye anayejua." Niliwaeleza wazazi wangu na kuanza kububujikwa na machozi ikiwa ni kama hasira kwani ni ndugu gani ambaye angeweza kuchukua maamuzi kama haya.

" Tina nyamaza bwana si unakumbuka namna ambavyo tuliongea haya japo najua bado unaumia, Ni kweli haya yanatokea lakini niamini kwa sasa mimi ni mmoja wa ndugu zako hata Fabiana kaniambia kuwa baada ya kumaliza masomo yake huko chuo safari ya kwanza mtakayoifanya ni kuelekea Iringa." Mama Fabiana alininyamazisha.

" Waoo itakuwa nzuri sana hii na sisi kwa mikono miwili tunawakaribisha." Baba alifurahi sana na kuahidi kuwa tayari katika hili aliloliongea mama Fabiana.

" Ni kweli tuko tayari kwani kule ni nyumbani kwao pia na hii itakuza uhusiano wetu zaidi." Mama naye alichangia hilo na kila mmoja mle ndani alifurahi.

" Shikamoo mama." Kennedy alifika na kumsalimia mama Fabiana akiwa na mafurushi mkononi.

"Kennedy, Kennedy kwani unafukuzwa? Mafurushi tele mkononi si uyatue kwanza kisha uje kutusalimu sisi hatuondoki tupo tu." Maneno ya mama Fabiana yalimfanya Kenny aondoke pale sebuleni na kuelekea jikoni kuifikisha mizigo aliyokuwa kaibeba. Lakini baada ya kuifikisha hakurudi tena pale sebuleni badala yake alitoka zake nje bila kugeuka nyuma.

" Yaani Kennedy hapo ndiyo tayari kachukia na akiwa kwenye hali hiyo huwa hapendi kuwa karibu na mtu yeyote yule." Mama Fabiana aliongea mara baada ya kumuona Kennedy akitoka nje. Lakini wakati akiongea hayo mara Kennedy alirudi tena.

"Mama kuna wageni wako huku nje." Kennedy alimtaarifu mama Fabiana kisha akatoka zake nje.

"Si mmemuona alivyo." Mama Fabiana aliongea akijizoazoa kutoka nje kuwaangalia hao wageni waliofika na kutaka kukutana na Bi Matilda.


JE NINI KITAENDELEA? NA HAO WAGENI NI WAKINA NANI? 


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUPATE KUJUA. 


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post