MTOTO MALATWE - 09
sultanuwezotz.blogspot.com
Kila mmoja alichangamkia chakula chake huku Malatwe akionekana kufurahia zaidi maana vitu kama hivi kwake inaweza kuwa ndoto kwani hakuwahi kuota kama kuna siku anaweza kuyaishi maisha haya lakini chini ya familia hii ya mwalimu Vincent imewezekana.
" Malatwe kama hujashiba agiza kingine." Bi Priscilla alimwambia.
" Hapana mama inatosha isije kuwa shida njiani."
" Kwani tatizo liko wapi? Tuna usafiri wetu wenyewe tumbo likitibuka tunapaki pembeni unafanya yako kisha tunaendelea na safari." Mwalimu Vincent alimtania Malatwe.
" Asante nimeshiba baba." Malatwe alimjibu akiinuka kufuata viatu.
" Kwa sasa nafurahi kuona Malatwe akiwa kwenye furaha yake, namuombea kwa Mungu azidi kuwa na furaha hii hii na pia asije badilika." Bi Priscilla alimwambia mume wake.
" Kwangu mimi hii ni kama zawadi, mke wangu kumsaidia mwenye uhitaji ni sadaka kwa Mungu hivyo namshukuru kwa hili." Mwalimu Vincent aliongea akitoa waleti mfukoni na hii ilikuja baada ya mhudumu wa mgahawa huu kusubiri malipo ya huduma. Baada ya kulipa alivipokea viatu vyake kutoka Malatwe akavivaa kisha aliinuka na kumfuata mng'arisha viatu kwa ajili ya kumlipa.
" Shukrani sana kaka." Aliyemng'arishia viatu alimshukuru sana mwalimu Vincent kwa alichokifanya.
" Brother, mimi ndiyo nikushukuru wewe kwa huduma nzuri uliyoifanya kwangu."
" Pamoja kaka."
" Okay." Mwalimu Vincent alimshukuru na kurudi walipokuwa wakina Malatwe kisha aliwaambia ni muda wa kuondoka, baada ya kuingia kwenye gari mwalimu aliiangalia 'gage' ya mafuta ili kujua kama yanatosha na alipoona yameshuka kidogo aliona wapitie sheli moja ya 'camel' iliyoko upande wa kushoto kama unaelekea Makambako karibu na kabisa na mlima Nyoka walikatisha na kuingia kituoni hapo.
" Habari kaka,niweke ya shilingi ngapi?" Mhudumu wa kituo hicho alifika na kumsalimu kisha kuuliza aweke ya kiasi gani.
" Niwekee ya shilingi elfu hamsini na tano." Alimjibu akibonyeza kitufe kilicho kwenye dashboard na baada ya kufunguka alitoa noti tano za shilingi elfu kumi kumi kisha akamgeukia mke wake.
" Sorry, niongeze elfu tano nijazie hapa." Mwalimu Vincent alimwambia mke wake. Na Bi Priscilla hakujibu chochote zaidi aliufungua mkoba wake na kutoa kiasi hicho na kumkabidhi ambapo aliziunganisha na kumkabidhi mhudumu aliyemfanyia huduma kisha aliwasha gari kutaka kuondoka lakini kuna mtu alikuja na kugonga kioo cha mlango wa upande wa kwa dereva, na bila ajizi aliufungua ili kumsikiliza mtu huyo.
" Sorry brother kuna vichwa vitatu hapa vinadropu Makambako na vina shilingi elfu kumi na nane." Alikuwa mpiga debe ambaye aliwafukuzia na kuwaombea nafasi abiria aliokuwa nao.
" Kwa maana kila mmoja shilingi elfu sita?" Mwalimu Vincent alimuuliza.
" Ndiyo bosi."
" Waambie waongeze walau ifike shilingi elfu ishirini na moja."
" Wamenikabidhi elfu ishirini kaka na mimi nimejisevia elfu mbili si unajua tena mjini pagumu akili ya ziada inatakiwa." Alijitetea mpiga debe huyu ambao kwa sasa ni maarufu kwa jina la 'Maafisa Usafirishaji' na hii ilikuja mara baada ya serikali kuwataka waondoke kutoka kero zao za kuwabughudhi abiria.
" Waambie waingie tuwahi." Mwalimu aliwataka waingie safari ianze maana aliona kama mpiga debe huyu anamcheleweshea muda wake.
" Habarini jamani." Mmoja kati ya wale abiria alisalimia akikaa vizuri.
" Nzuri tu." Bi Priscilla aliyekuwa bize kumnyonyesha alimjibu. Na wakati huo mwalimu alikuwa anaangalia nyuma yake kama kuna usalama ili aingie barabarani na kuendelea na safari.
Baada ya saa moja na nusu walishaingia Igawa mji mkongwe na wenye historia kubwa ndani ya mkoa wa Mbeya na wilaya ya Mbalali kwa ujumla. Historia ya mji huu ni kwenye upande wa biashara ndogondogo za kuuza bidhaa barabarani hasa kwenye magari. Na biashara ambayo iliupaisha mji huu ni biashara ya karanga na siyo karanga unazozijua wewe, karanga ya Igawa ilikuwa ni ile ambayo ni ya kuchemsha iwe kiangazi, iwe masika Igawa karanga utazipata kuhusu zinalimwa kila wakati mimi na wewe hatuna majibu ila majibu ilikuwa unayapata pale utakaponunua hizo karanga. Vile vile mahindi ya kuchemshwa yaliongeza umaarufu wa mji huu ambapo nayo yalikuwa yakipatikana muda wote japo ukiyanunua hasa kiangazi utaifaidi shoo yake mahindi ni makavu ila yamelowekwa kisha kuchemshwa na kuwauzia wasafiri wapitao mjini hapo. Hata walipofika wakina Malatwe walipokelewa na wafanyabiashara hawa kiasi cha mwalimu Vincent kupaki gari pembeni na kuruhusu watu wake wanunue karanga au mahindi wakati huo yeye alishuka na kwenda kwenye duka moja la bidhaa mchanganyiko hapo alinunua vocha pamoja maji makubwa matatu na kuja nayo kwenye gari na kumkabidhi Malatwe ambaye aliyahifadhi pembeni yake.
"Samahani wazee kwa kuwachelewesha." Mwalimu aliwaomba msamaha abiria wake.
"Hapana kijana uko vizuri tu na hatuko nje ya muda mpaka muda huu." Abiria mmoja wao alimjibu mwalimu Vincent.
"Nashukuru sana ndugu zangu." Aliongea akifunga mkanda na kisha safari ilianza kuutafuta mpaka wa Mbeya na Njombe, sehemu ambayo inatumiwa na askari wa usalama barabarani pamoja na baadhi wa uhamiaji kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa. Kama ilivyo ada walipofika tu sehemu hii walikutana na mkono wa askari mkakamavu mwanamke ambaye hakuongea chochote zaidi ya kuonesha sehemu ya kupaki gari lao kisha akaendelea kuyasimamisha mengine.
"Kumekucha nao hawa huko kwingine kote tumepita vizuri bila pingamizi hebu muone alivyonuna." Bi Priscilla alionekana kukasirishwa na kitendo cha kusimamishwa.
" Hapana dada usiseme hivyo au kulaumu kumbuka na yeye yuko kibaruani kama wafanyakazi au wafanyabiashara wengine hivyo kumlaumu ni kutaka watoto wake wakose mkate wao wa kila siku." Mmoja wa abiria aliona amueleweshe Bi Priscilla kutokana na maneno yake aliyoyaongea.
" Hata kama ndugu yangu wamezidi sana hawa watu yaani walishaweka kitega uchumi barabarani." Hakuelewa kitu zaidi ya kuzidi kulaumu tu bila sababu.
" Habari yenu." Aliwasabahi askari wa kiume aliyefika na kuchungulia kupitia dirishani.
"Salama tu Afande." Bi Priscilla alijibu haraka haraka.
" Naona umempakata mjomba hapo." Alimtania Bi Priscilla.
" Kajichokea tu hapa na safari mwenyewe."
" Aisee anaitwa nani mjomba wangu?" Askari huyo aliuliza akiendelea kuzungusha macho kukagua abiria walio ndani ya gari hilo.
" Anaitwa Lilian." Bi Priscilla alimjibu.
" Waoo ana jina zuri sana mwanao hongera." Askari huyo alimsifia.
" Vipi injinia wangu, una leseni?" Alimgeukia dereva ambaye ni mwalimu Vincent.
" Hii hapa kaka." Alimjibu akimuonesha ilipo pale juu ilipokuwa inaning'inia.
" Vizuri, jamani niwatakie safari njema na mfike salama lakini pia dereva kuwa makini barabarani kama unavyoona hali ya ukungu ilivyo uendako." Alimtahadharisha.
" Asante kaka nitakuwa makini." Mwalimu Vincent alimjibu na kuondoka.
" Si umeona dada hawana tatizo kama umetimiza kila kitu kwenye chombo chako cha usafiri." Yule abiria alimgeukia tena Bi Priscilla kutokana na yale ambayo aliyaongea juu ya hawa Askari wa Usalama barabarani.
" Hakuna lolote sema tu nyota yake na ya kwangu zimeendana bila hivyo angekiwasha tu." Majibu yake yalimfanya mume wake kuingilia kati.
" Kuna kitu ambacho watu wengi hawakifahamu kuhusu hawa Askari, uwepo wao barabarani ni msaada mkubwa sana kwetu nakumbuka mwaka fulani pale 'Inyara Pipe Line' kuna basi lilisimamishwa na hawa hawa askari lakini kabla hajaongea chochote alisikia cheche za moto zikilia kutoka chini ya hilo basi ikabidi ainame kuangalia huwezi amini alikutana na moto karibia na tairi la nyuma haraka sana aliinuka na kuwaambia washuke. Mbele ya kifo acha kabisa kuna wengine walipitia madirishani na ndani ya dakika kadhaa mara baada ya wote kushuka lile basi liliteketea pale pale je asingekuwa yule Askari ingekuwaje?" Mwalimu Vincent aliuliza baada ya simulizi yake.
" Na ndiyo maana kaka nasema hawa watu ni muhimu sana kwetu ila tunawaona wabaya kutokana na makosa yetu yaliyojazana kwenye vyombo vyetu vya usafiri." Abiria huyo alichangia.
" Na kingine sisi ndiyo ambao tunachochea hizi rushwa kutokana na haraka zetu na makosa yetu, kwani wao ndiyo hutulazimisha kutoa kitu kidogo? " Aliuliza mwalimu.
" Hakuna kabisa." Abiria mwingine alidakia.
" Haya basi mmeshinda punguzeni kelele mtoto asije amka bure." Bi Priscilla aliona asingizie mtoto mara baada ya kuona hoja yake imegonga mwamba.
" Si useme umeshindwa mke wangu?" Mwalimu Vincent alimtania mke wake. Lakini Bi Priscilla alimuangalia kwa jicho kali bila hata kujibu chochote kile na mwalimu alijua tafsiri yake ni nini ilibidi atulie zake kwenye usukani asije sababisha ajali. Malatwe yeye mpaka muda huo alikuwa kalala usingizi wa mkoromo na hakuwa na habari ni wapi wamefika.
"Samahani ndugu zangu mnashukia kituo gani?" Mwalimu aliwauliza abiria wake wakiwa ndiyo wanausogelea mji wa Makambako.
" Kama mnaingia mjini tunashukia stendi ya zamani."
" Msijali tunaingia huko huko." Aliwajibu. Na baada ya kufika karibu na stendi ya zamani alisimamisha gari ili kuruhusu wao kushuka na baada ya kushuka walishukuru sana kisha waliagana.
" Tutapumzika hapa Makambako kisha kesho alfajiri tutaendelea na safari yetu unaonaje mke wangu?" Mr Vincent alimuuliza mke wake Bi Priscilla.
" Hatuna haraka mume wangu wacha tulale hapa kesho nayo ni siku tutaendelea na safari, kwanza kwangu itakuwa vizuri kuuvinjari mji huu ambao mara zote nimekuwa nikipita tu halafu nasikia hata Hotel na Guests za hapa hazina gharama sijui ni kweli?"
" Hata ingekuwa gharama mke wangu ndiyo matumizi ya pesa hayo hebu muamshe huyo mlugaluga kulala gani huko?"
" Hapana tutamuamsha tukifika hotelini muache amalizie usingizi wake baridi likimpiga vizuri ataisoma namba." Bi Priscilla alimjibu mume wake ambaye muda huo alikuwa akiingia ndani ya Hotel ya Durban.
" Tumefika, mlete Lilian wewe saidiana na Malatwe kuchukua mabegi."
" Sawa." Alimjibu akimkabidhi mtoto.
" Mhh hii nguo nyepesi sana kwa baridi hili la alasiri asije pata tatizo."
" Nilizobeba ni nyepesi sikuwa na wazo la kwamba tungelala hapa, inabidi tukamnunulie baadaye kidogo baada ya kupumzisha." Bi Priscilla alimjibu mume wake aliyekuwa kaanza kuvuta hatua kuelekea mapokezi.
" Karibuni Durban Hotel kwa huduma bora kabisa." Mhudumu wa Hotel hiyo aliwachangamkia.
" Asante tumefika, tunahitaji 'family rooms' "
" Mmepata karibuni."
" Asante dada." Bi Priscilla alijibu. Mhudumu huyu alitoka na kuwapeleka viliko hivyo vyumba ambavyo aliamini vitakuwa rafiki kwa wateja wake. Na baada ya kuwafikisha kwenye hivyo vyumba walifurahia sana na hawakutaka kwenda kwenye vingine.
" Tumefika dada hivi vinatosha." Aliwaambia Bi Priscilla.
" Karibuni, kwa huduma nyinginezo simu zinafanya kazi tupigieni." Mhudumu huyo aliwakaribisha na kisha alitoka kupisha wateja wake.
" Malatwe, wewe chumba chako hicho hapo." Mwalimu Vincent alimwambia Malatwe ambaye aliketi sebuleni akiwa kachoka maana hajawahi kusafiri iwe safari fupi au ndefu hivyo kwake hii ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza kusafiri.
" Kwa hiyo hapa ni kwa nani?" Malatwe aliona aulize. Swali lile lilimfanya Bi Priscilla kuangua kicheko maana hakulitarajia.
" Halafu Malatwe usinivunje mbavu zangu mimi Mungu wangu, hapa ni Hotelini siyo kwa mtu kila mmoja anaruhusiwa kulala ni hela yake tu." Majibu yale hayakumuingia Malatwe.
" Mbona kwa tulivyojifunza shuleni ni kwamba hoteli ni sehemu ambayo watu wananunua chakula tu na sehemu za watu kulala zinaitwa Guesti sasa wewe unasemaje hapa ni Hotelini?" Swali lile lilimfanya Bi Priscilla aishiwe pozi na kujikuta kiherehere kimemwisha akamtazama mume wake bila shaka alihitaji usaidizi zaidi.
JE NI NINI KITATOKEA KATIKA KITIMUTIMU HIKI?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUPATE KUJUA KITAKACHOTOKEA KWA FAMILIA HII ALIYOINGIA MALATWE.
#SULTANUWEZO