MTOTO MALATWE - 17 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


MTOTO MALATWE - 17

sultanuwezotz.blogspot.com 


Malatwe alirudi nyumbani mbio baada ya kuagana na kikongwe ambaye walikubaliana kuonana siku inayofuata. Malatwe alikuwa anakimbia huku masikio yake yakiwa hewani kusikiliza kama anaweza kusikia chochote kutoka kwa shemeji yake Bi Judith. Akiwa anavutana na kisogo chake pamoja na miguu yake huku mgongo ukiwa ndiyo muamuzi kuhakikisha viungo hivi havikutani. Mungu saidia aliwasili nyumbani na kuufuata mlango wa mianzi ambao tunaweza kusema ndiyo geti lakini akiwa anachomoa mtwangio kwenye waya ili geti lifunguliwe mara mwanga wa pikipiki ulimmulika machoni na kujikuta anaishiwa pozi asijue afanye lipi, alifungue geti au atulie kwanza kusubiri ataambiwa nini.

" Mbona umepigwa butwaa kulikoni Malatwe?" Naboti alimuuliza Malatwe. Lakini badala ya kujibu swali aliangaza macho yake kule alikotokea na kumfanya Naboti kupatwa na wasiwasi.

" Umefanya tukio gani huko ulikotoka mbona macho juu juu?" Alimuuliza akimfuata baada ya kuipaki pikipiki vizuri.

" Hakuna kitu kaka sijafanya chochote kile, kwani umefika muda gani?" Alijikuta akiuliza swali badala ya kutoa majibu sahihi kwa kaka yake wa kufikia. Ilibidi amfuate mpaka pale aliposimama Malatwe na kumtandika kibao cha shavu kilichomfanya apepesuke na kwenda chini, alimfuata tena pale chini na kumuinua kisha akamtandika tena kibao ambacho kilimfanya ayumbe na kwenda kuegemea fensi ya mianzi na kwa tukio lile lilimfanya aachane naye kwanza na kuifuata njia aliyoitumia Malatwe kuja na kumuacha akilia.

" Kaka Naboti yaani unanipiga bila kosa lolote? Au mimi ni mbwa wa getini kwako?" Malatwe aliendelea kulia huku akitokwa na maneno hayo ambayo bila shaka hayakumfikia Naboti ambaye alikuwa keshapotelea gizani japo kulikuwa na kimwezi kwa mbali. Aliinuka na kuifuata geti ambalo alilifungua na kuingia ndani na kuongoza chumbani kwake. Na ndani ya dakika kama kumi na sita hivi alimshuhudia Bi Judith kupitia dirishani akiingia ndani kwa kunyata.

" Shemeji kulikoni? Umechomwa miba mbona unatembea hivyo?" Alimuuliza kupitia pale pale dirishani. Lakini Bi Judith hakumjibu chochote zaidi ya kupitiliza jikoni ambako hakukaa sana alitoka na kuingia chumbani kwa Malatwe.

" Kaka yako yuko wapi mbona pikipiki iko pale nje?"

" Sifahamu chochote mimi." Malatwe alimjibu.

" Unataka kuniambia kuwa hamjaonana?" Judith alimuuliza tena swali ambalo Malatwe hakulijibu zaidi ya kurudi kwenye kirago chake na kujilaza.

" Unalala na chakula je?"

" Chakula? Wewe si ulisema kuwa hakuna chochote mpaka kaka arudi?"

" Ulikuwa utani ule na wewe ina maana uliliweka akilini?"

" Mmh mimi nitakula kesho muda huu nimeshiba." Malatwe alimjibu.

" Umekula wapi mbona jiko limepoa?"

" Nilikwenda kule vibandani nikakutana na rafiki yangu niliyefahamiana kilabuni akaninunulia mihogo hivyo niko sawa." Judith hakutaka kuendelea kujibishana na Malatwe alitoka nje ambako uso kwa uso na mume wake akiingiza pikipiki ndani.

" Na wewe ulikuwa wapi?" Ni swali alilokutana nalo kabla hajaipanda ngazi kuingia ndani kwao.

" Mimi?"

" Kwani naongea na nani hapa au unajitoa fahamu?"

" Nauliza kwa sababu ni swali ambalo sijalielewa linalenga nini, mimi sijaondoka hapa nyumbani toka ulipotuacha muda ule." Judith alimjibu bila wasiwasi.

" Una uhakika na jibu lako?" Mume wake alimuuliza.

" Kivipi? Au unataka nikudanganye."

" Okay samahani mke wangu naomba tusiende huko nilitaka kupata uhakika tu, na vipi kuhusu Malatwe?"

" Malatwe kalala muda mrefu tu humo chumbani mwake alipomaliza kula tu huyo kulala." Majibu ya mke wake yalimpa mashaka Naboti akajikuta anaufunga mlango mdomo wake na kuiingiza pikipiki huku mke wake akiingia ndani. Baada ya kuipaki pale anapoiwekaga pikipiki yake aliingia chumbani kwa Malatwe na kumkuta kajilaza alijaribu kumuamsha lakini Malatwe alitulia kimya bila kumjibu chochote huku akiingiza kukoroma. Hilo lilimfanya Naboti aachane naye na kutoka nje na kuingia chumbani kwake na kumkuta mke wake akiwa anajiandaa kwenda bafuni maana alikuwa kwenye kitenge cha kuongea na mkononi akiwa na kipande cha sabuni.

" Naona meza imenuna sijui leo wengine hatuli?" Naboti aliuliza.

" Kwani mkeo hakukupikia? Au yeye kazi yake ni kukinga tu mikono kupokea hela ambazo sisi wengine kazi yetu ni kuzitafuta na yeye akizifaidi bila jasho." Alimjibu.

" Unasemaje weweeee?"

" Umesikia au unataka nikupandishe hasira." Alimjibu akitoka nje.

" Unakwenda wapi rudi hapa kwanza." Alimshika mkono na kumzuia asitoke nje.

" Hebu niachie nikaoge huko." Alimjibu akijivuta mikononi mwa mume wake.

" Nitakuachia iwapo utaniambia ni kwanini hujaniwekea chakula na huyo unayesema nampelekea hela ulinitongozea wewe?"

" Kama siyo kweli mbona unaendelea kulishadadia basi ni kweli." Naboti alipandwa na hasira akamkamata kichwa mke wake kwa nguvu na kumgongesha mlangoni.

" Nitakuua mwanaharamu hebu kaniandalie chakula haraka kabla sijapandisha mashetani yangu."

" Nasema hivi jikoni siendi hapiki chakula mtu hapa unanitishia mashetani yako mimi si uyapandishe ili uniue vizuri ili nafsi yako isuuzike mshenzi wewe usiye na haya." Alimjibu akiwa amejitoa mikononi na kutoka mbio nje.

" Rudi haraka kabla sijakufanya kitu kibaya wewe."

" Nani arudi? Pambana na nyumba yako si hiyo hapo unafikiri mimi sina wazazi? Unafikiri mimi sina wazazi?" Alimjibu akiwa nje ya geti sijui alikuwa anakwenda wapi usiku ule. Wakati hayo yakitokea Malatwe alikuwa dirishani akishuhudia kila kitu kilichokuwa kinaendelea kwa wenyeji wake lakini alipomuona tu Naboti akitoka alirudi kulala ili kama anakuja kwake amkute akikoroma tena na kama alivyowaza ndivyo ilivyokuwa kwani Naboti aliingia kwake na kuanza kumuamsha kwa kumtingisha, alibana pumzi kama kalala usingizi lakini mwisho wa siku alishindwa kuvumilia vurugu za Naboti kwa alivyokuwa akimfanyia ikabidi aamke tu.

"Nataka uniambie leo mlikuwa wapi na mke wangu? Haiwezekani nikute geti limefungwa kwa nje mwingine aniambie kuwa hajaondoka alikuwa ndani wakati si kawaida yake na wewe umekuja uliponiona tu ukapigwa butwaa kuna nini mnachonificha?" Naboti alimuuliza Malatwe akiwa kamkunja kama vile anataka kumtundika mtini. Lakini Malatwe hakuweza kumjibu chochote alibakia kimya. 

" Nauliza tena Malatwe kuna nini katikati yenu? Na mlikuwa wapi siku ya leo?" 

" Kwa hiyo kaka unataka kusemaje?" Malatwe alimuuliza akiwa kaachiwa sweta lake. 

" Nasemaje? Ina maana hujasikia swali au?" Aliinuka na kutoka nje na kumuacha Malatwe akiitingisha shingo yake kuona kama iko sawa maana kabali ilikuwa bab'kubwa. 

" Hii sehemu nimeivamia si salama kwangu na sijui kwanini niliangukia mikononi mwao? Najihisi nina mkosi kwanini kila ninakokwenda nakutana na vikwazo? Bora ningebaki zangu kwa mwalimu Vincent ilikuwa burudani sana bila chuki." Malatwe alijiwazia akiwa kabakia peke yake mle ndani baada ya Naboti kutoka. 

" Ingekuwa siyo kukutana na yule bibi walahi ningeondoka usiku huu huu lakini acha niisubiri hiyo kesho mpaka nionane na yule bibi nijue kuna kipi kipya ndipo nifanye maamuzi yangu haiwezekani mavurugu kila kukicha maisha gani haya. Halafu sijui kama walishaondoka kwenda Singida au bado wako Makambako?" Alijiuliza.

Kulikucha Malatwe akaamka na kuchukua maji kwenye kata na kuzunguka nayo nyuma ya nyumba ambako alikata kimti ambacho alikitafuna na kuanza kuswaki meno yake taratibu.

" Kweli siku zinakwenda mbio sana jamani nilianzia kwenye miswaki ya miti kisha nikaja kwenye miswaki ya dukani huku dawa ikiwa juu yake lakini kama ndoto vile nimerudi kule kule nilikoanzia hii inaashiria nini? Maana kama ni grafu imeshuka ghafla ilikokuwa imeanzia duu." Alikuwa akiwaza wakati ananawa. Mara alisikia mlio wa pikipiki ukitoka ndani na alipochungulia alimuona Naboti akitoka kasi.

" Mwanajeshi anakwenda vitani tena sijui alikutana na tutusa lake? Au ndiyo kalala pole pole nini?" Malatwe alijisemea akitupa mswaki na kurudi ndani. Hakutaka kuchelewa hata kidogo aliweka ile kata chini na kutoka mbio kuelekea kwa bibi aliyewekeana miadi. Kwa bahati nzuri hakuweza kupotea njia alifika mpaka kwa Bibi Mpinge na kugonga mlango.

" Bibi hodi!, Hodi bibi!" Alipiga.

" Karibu nani asubuhi yote hii?"

" Ni mimi mjukuu wako wa jana usiku." Malatwe alimjibu.

" Asante bibi ndiyo nimekuja hivyo."

" Bibi, bibi hebu niite bibi Mpinge sawa?"

" Sawa bibi Mpinge nashukuru kukufahamu mimi naitwa Malatwe." Malatwe alimjibu.

" Karibu ndani mjukuu wangu." Malatwe alikaribishwa ndani na kuingia kilikuwa kijumba chenye giza kwa sababu kilikuwa hakina madirisha ya kutosha zaidi ya vile vidogo na vilivyoshindiliwa matambala na hivyo kumfanya kuwasha kuwasha kibatari muda wote.

" Bibi mbona nyumba yako ina giza kiasi hiki hakuna madirisha tuyafungue?" Malatwe alimuuliza.

" Madirisha ya nini kwani mimi nahitaji kuwaangalia wapita njia mpaka niwe na hayo madirisha?"

" Simaanishi hivyo bibi ni kwa ajili ya kupunguza hili giza."

" Wewe fuata kilichokuleta haya mengine ni maisha yangu mimi na si ya mtu mwingine umenielewa?"

" Sawa bibi naomba unisamehe nimeijia suala letu la jana." Malatwe alimtaka radhi. Aliletewa kigoda na kumkabidhi Malatwe kisha akaingia jikoni ambako alitoka na kibakuli chenye viazi vya kuchomwa na kukiweka chini kisha akamkaribisha.


JE NI NINI KITAENDELEA KWA MALATWE?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


#SULTANUWEZO 

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post