MUUAJI MWENYE BARAKOA - 08
sultanuwezotz.blogspot.com
"Ndiyo mzee wangu na si majanga tu bali ni tetemeko na hofu juu yake na hapa ninapoongea na wewe sijui kama kesho nitaiona." Mchungaji aliendelea kumpa presha mzee Kitesa.
"Hebu acha kupindisha maneno kuwa wazi Mchungaji." Mzee Kitesa alimtaka Mchungaji Rodney kueleza kinachomkabili pasipo kumficha.
"Mzee wangu hivi karibuni nimekuwa nikitishiwa maisha na mtu nisiyemfahamu na tayari keshaua waumini wangu zaidi ya watatu kama hilo halitoshi alihusika na kumteka Bwana fedha wetu Bartholomew ikiwa ni pamoja na kupora kiasi chote cha fedha kilichotumwa na Taasisi rafiki kutoka Ng'ambo na kama haitoshi leo hii mke wangu na mlinzi sijawakuta hapa nyumbani nimekutana na ujumbe tu wa vitisho juu yangu." Mchungaji Rodney alimsimulia mzee Kitesa kila kitu ya yaliyotokea.
" Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa mkeo pamoja na mlinzi wako wametekwa au kuuawa?"
" Naweza kusema ndiyo au hapana labda niisubiri simu yao kwanza maana wameniambia nisifanye chochote japo nimekwenda kinyume nao sijui itakuwaje baada ya mazungumzo haya." Mchungaji alimjibu.
" Mtegemee Mungu kwa kila jambo maana yeye ndiye mleta majibu, hebu kata simu kwanza kuna mtu nataka kuongea naye nafikiri kesho asubuhi tuwasiliane kijana wangu." Mzee Kitesa alimtia moyo Mchungaji Rodney na kisha Mchungaji alifanya kama alivyoambiwa, alichukua begi lake dogo lililokuwa kwenye kiti kisha aliifuata 'Main switch' na kuzima umeme kwa nyumba nzima na kuondoka zake kwa miguu akiyaacha magari mle ndani.
***
Baada ya safari ndefu hatimaye mama Mchungaji Bi Catherine, Seynabou na Adoyee waliwasili ndani mji wa Saint Louis ulioko kaskazini magharibi mwa Pwani ya Senegal na moja kwa moja walifikia kwenye jumba fulani hivi chakavu kwa muonekano wa nje lakini kwa ndani kulikuwa tofauti kabisa kwani kulisheheni kila kitu cha thamani kinachopatikana kwenye majengo mengine ya kifahari. Jengo hili linalokadiliwa kujengwa miaka ya 1897 na lilikuwa likitumiwa na wavuvi wa kifaransa mpaka pale walipoamua kulitelekeza na kurejea kwao baada ya kutokea mapigano kati ya wavuvi wa Kifaransa pamoja na wavuvi wazawa ambao waliamini kuwa wavuvi hawa wageni walipoka ajira zao na kuwafanya kuwa watumwa wao mpaka pale walipoamua kushikamana pamoja na kuwasambaratisha mnamo mwaka 1932 ambapo jengo hili lilikuja kuchukuliwa na serikali ambayo iliwakabidhi watoa tiba za asili ambao wanaendelea kulitumia mpaka sasa lakini likiwa chini ya Tabibu maarufu na tishio wa Tiba za asili kwa ukanda wote wa Jangwa la Sahara Mzee Malick Bolenge.
"Kabla hamjafanya chochote wajukuu zangu naweni nyuso zenu kwa maji yaliyo kwenye hivyo vyungu." Ilikuwa ni sauti ya mzee Malick Bolenge akiwapa maagizo wageni wake walioingia mahali pale mida ya usiku wa saa nne.
"Tayari babu." Catherine alimjibu baada ya kufanya kama alivyowaagiza.
"Vizuri sasa acheni hapo mizigo yenu kisha nifuateni."
"Sawa babu." Catherine aliyekuwa mwenyeji wa maeneo yale alimjibu mzee Malick Bolenge. Walimfuata mpaka ndani na wakati haya yote yanafanyika Adoyee alionekana kuogopa sana tofauti na Seynabou aliyekuwa mtulivu muda wote akifuatilia maagizo yalivyokuwa yakitaka wafanye.
"Kuna baridi kali sana dada Catherine." Seynabou alimwambia Catherine baada ya kuanza kuonja baridi lililokuwa likipuliza kama vile limefunguliwa sehemu kwa makusudi.
"Hali hii ni ya kawaida sana kwa eneo hili ukizingatia kuwa tuko kwenye ncha ya mto senegal pamoja na uso wa bahari ya Atlantiki hivyo kulifanya kuwa na hali ya kipekee zaidi, japo kuna majira hali hubadilika na kuwa ya joto sana." Catherine alimjibu Seynabou.
" Karibuni sana wageni wangu nimewasubiri sana toka uliponijulisha kuwa uko njiani." Mzee Malick Bolenge aliwakaribisha sebuleni na kuwataka waketi vitini.
" Pole sana mzee wangu lakini si unajua mapito yetu yalikuwa ni ya kusubiri giza tu jua likichomoza tu ilikuwa ni lazima tulikwepe kwa kuingia kwenye mapango."
" Poleni sana kikubwa mmefika salama mengine ni changamoto tu."
"Ni kweli kabisa mzee wangu." Catherine alimjibu mzee Malick.
Baada ya Catherine kueleza kilichompeleka pale kwake mzee Malick Bolenge aliwataka waoge ili kupata nguvu wakati chakula kikiandaliwa kwa ajili yao. Huyu mzee Malick Bolenge ni kaka wa marehemu mama yake Catherine japo yeye kulingana na shughuli zake uganga alitengana na ndugu zake kufuata maagizo ya mizimu. Kila kitu kilipokuwa tayari ikiwa ni pamoja na chakula mzee Malick Bolenge alipata wasaa wa kuzungumza na Catherine.
"Mhh kulikoni mwanangu mwenyewe?" Alianza.
"Mjomba kilichonileta hapa nyumbani ni kutaka kuweka mambo yangu sawa." Catherine alimwambia Mjomba wake.
"Lakini nikikuangalia wewe na watu ulioongozana nao nahisi kuna tatizo hivi?"
"Ni kweli kuna tatizo lakini wacha niwaoneshe sehemu za kulala wageni wangu maana wamechoka sana." Catherine aliona ampotezee kwanza mzee Malick Bolenge.
"Okay sawa fanya hivyo." Alimjibu. Catherine aliinuka na kutoka kuelekea walikokuwa wakina Adoyee.
"Poleni kwa kunisubiri."
"Tulijua ndiyo tunalala hapa hapa kama unavyomuona Adoyee hapo anakoroma tu kama gari lililotumika kwenye vita ya kwanza ya dunia." Seynabou alimjibu.
"Hapana bwana si unajua tena ni muda mrefu sijakutana na mjomba wangu lakini kila kitu kiko sawa hebu muamshe nikamuoneshe malalo yake." Seynabou alimuamsha Adoyee kisha akapelekwa kwenye chumba ambacho kiliandaliwa kwa ajili yake na baada ya kumuonesha alirudi na kumuambia Seynabou amfuate. Waliingia kwenye chumba kilichokuwa karibu zaidi na sebule.
" Karibu mdogo wangu hapa ndiyo tutalala mimi na wewe." Catherine alimwambia Seynabou.
"Asante dada." Alimjibu akijitupa kitandani.
"Lakini kuna jambo tunatakiwa tutete usiku huu huu ili ikiwezekana kesho tuanze utekelezaji."
"Lipi hilo dada?" Seynabou alimuuliza.
"Kama tulivyoongea huko nyuma mimi na wewe ni wahanga wa Mchungaji Rodney pamoja na kundi lake na kilichonifurahisha zaidi ni kuwa tayari kulipa kisasi."
"Kuhusu hilo niko tayari hata muda huu haiwezekani mama yangu apotee katika mazingira yenye utata kama yale huku baba yangu hata sura yake tu siikumbuki, inauma sana." Seynabou aliongea ya moyoni huku machozi yakimtoka.
"Seynabou inaonekana una mengi ambayo bado hujaniambia, ina maana huyu mzee Alioune hakuwa baba yako?" Catherine aliuliza.
"Dada naomba tulale kisha siku ya kesho tuitumie kujuana zaidi."
"Bila shaka, kumbe weka mambo sawa wacha nikamuage mjomba ananisubiri bandani mwake."
"Sawa dada." Seynabou alimjibu na Catherine alitoka.
Hakumkuta mzee Malick Bolenge pale alipomuacha hivyo alirejea chumbani kwa ajili ya kuutafuta usingizi ukizingatia kuwa ana siku kama tatu hajapata usingizi wa kutosha kutokana na heka heka za hapa na pale. Akiwa chumbani kwao kabla ya kulala aliichukua laptop yake na kuiwasha ili kuangalia kinachoendelea kwa mume wake Mchungaji Rodney kwa kutumia App maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya kufuatilia nyendo za Mchungaji huyu na hata kama asipokuwa hewani akiiunganisha tu na mtandao kila kitu kitaingia kuanzia jumbe alizotuma na kupokea Mchungaji pia simu alizopiga na kupokea zitakuwa zimerekodiwa hivyo kazi yake itakuwa na kusikiliza na kusoma, kama alivyokuwa ametegemea ndivyo ilivyokuwa kwani alipoifungua tu aliweza kuuona ujumbe ambao alimwambia kijana wake Jumbe amtumie baada ya kuusoma alitabasamu kisha akakifungua kisanduku cha sauti na kuanza kuyasikiliza mazungumzo yote yaliyofanywa kati ya Mchungaji na mzee Kitesa. Hapa ilibidi achunguze kiunganishi cha namba hii ili kujua mtu huyu ni kutoka nchi gani na ndipo alipoikuta ni +255 hapo hapo akaichukua simu yake na kufungua 'app' ya 'codes' za nchi mbalimbali ili kuibaini.
"Tanzania? Inapatikana kanda gani ya Afrika? Na kwanini alimpigia mtu huyu?" Catherine alijiuliza akiifungua 'Google map'.
"Baba Mchungaji kwa sasa wewe ni kivuli changu huwezi kunikwepa hata kidogo." Catherine aliongea huku akiurusha mkono wake mmoja juu kama ishara ya ushindi. Aliifunga laptop yake na kuiweka kwenye begi lake kisha akampigia simu Jumbe muda huo huo hakutaka kusubiri mpaka kesho.
" Naam Bosi." Jumbe aliitika baada ya kupokea simu.
" Ni hivi Jumbe, huyu panya kaanza kufanya mawasiliano na mtu kutoka nchi inayoitwa Tanzania bila shaka kuna jambo hapa."
"Tunafanyaje bosi?" Jumbe alimuuliza.
"Najua mpaka kesho nitakuwa nimepata jibu, kingine naomba wale vijana ambao nilikwambia kuwa nina mashaka nao waulie mbali kabla hawajauza ramani yetu kisha miili yao hakikisha inakwenda kutupwa nje ya Kanisa la JESUS OUR KING la Mchungaji Rodney na baada ya hapo wewe na wenzako mtaondoka eneo hilo kuelekea sehemu nitakayowaelekeza."
"Kama ulivyoagiza bosi nitafanya." Jumbe alimjibu Catherine ambaye alikata simu na kujilaza.
JE NI NINI KITATOKEA KATIKA KITIMUTIMU HIKI?
TAFADHALI UNGANA NAMI KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUJUE NINI KILICHOJIRI KATIKA SONGOMBINGO HILI.
#SULTANUWEZO