MUUAJI MWENYE BARAKOA - 09 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


MUUAJI MWENYE BARAKOA - 09

sultanuwezotz.blogspot.com 


****


Baada ya dakika kadhaa aliwasili Kanisani kwake akitumia usafiri wa Bajaj ambao aliukodi na baada ya kumlipa mwenye Bajaj hiyo alichukua mkoba wake na kuelekea getini ambako alibonyeza kengele.

"Nani?" Mlinzi aliuliza.

"Fungua geti Davis."

Alipoisikia sauti hiyo mlinzi huyo haraka sana alifungua geti dogo na kuchungulia nje.

"Karibu baba Mchungaji." Alimkaribisha.

"Asante Davis, habari ya kazi?"

"Ni nzuri tu bosi vipi kwema utokako maana sioni gari hapa nje." Davis alimuuliza Mchungaji ambaye kwa muda huo alihisi maswali yale yanamchelewesha tu.

"Usiwe na wasiwasi Davis kila kitu kiko sawa nimekuja hapa kuna kazi maalum na sitapenda kupokea mgeni muda huu mpaka kesho, sawa!" Alimwambia akimpiga begani.

"Nimekuelewa Mchungaji, halafu mzee Lusoka alikuja hapa kama masaa kadhaa nyuma akakuuliza."

"Ukamwambiaje?" Mchungaji alimuuliza baada ya kulisikia jina hilo.

"Nilimwambia haujafika akaondoka." Davis alimjibu.

"Vizuri endelea na kazi yako fanya kama nilivyokueleza."

"Sawa Mchungaji." Davis alimjibu na wakati huo Mchungaji aliachana na mlinzi huyo na kuelekea ofisini.

"Nilikuonya usifanye chochote kile lakini naona umevuka mipaka mpaka nchi ya Tanzania, unafikiri utaondoka mbele ya macho yangu yenye uwezo wa kuangalia kila kona ya Dunia? Nafikiri ndani ya masaa machache utakipata kilichowapata Catherine pamoja Adoyee mlinzi wako." Ulikuwa ni ujumbe ambao uliingia kwenye simu ya Mchungaji wakati akiketi kitandani kwenye chumba kilicho ndani ya ofisi yake. Alipousoma ujumbe ule aliishusha pumzi ndefu kama vile aliutua mzigo mzito mgongoni mwake. Na baada ya kutafakari kwa muda ikabidi aipige ile namba iliyotuma ujumbe ule ili aweze kumtambua adui yake ambaye kila kukicha ni vitisho tu. Maajabu aliyokutana nayo Mchungaji kiasi cha kumfanya kutabasamu na halikuwa la furaha bali la hasira kutokana na namba ile kutopatikana na ilikuwa ni namba mficho hivyo ikawa ni ngumu kumpata.

"Ni nani huyu ambaye kila hatua yangu yuko nyuma yangu?" Mchungaji Rodney alijiuliza. Na katika kuwaza zaidi akaijiwa na wazo la kumpigia simu mzee Lusoka ambaye mchana walikwaruzana, hivyo aliipiga namba ya mzee huyo lakini wakati inaita alitupa macho yake kwenye saa ya ukutani ndipo aliposhangaa kuona ni saa nane usiku haraka sana akakata simu na kuizima kabisa.

"Ndiyo nimefanya nini usiku wote huu kwenye majumba ya watu na masimu." Aliwaza haya akiwa analivuta blanket.

Kulikucha japo hali ya hewa haikuwa nzuri sana kutokana na mvua iliyokuwa ikinyesha kiasi cha kusababisha utokaji kuwa mgumu kuelekea makazini. Kwa upande wa wakulima kwao ilikuwa ni furaha kubwa hasa ukizingatia mvua ilikuwa ina muda mrefu haijanyesha hivyo muda huu kila mmoja alikuwa shambani kwake wa kupanda alikuwa akipanda na wale wa kulima ilikuwa hivyo hivyo ilmradi tu siku isiende bure.

Wakati hayo yakienda hivyo nje ya geti la kanisa kulikuwa na mtu ambaye alikuwa akigonga geti kama vile ana ugomvi nalo na wala hakujali mvua hii iliyokuwa ikiendelea kunyesha. Kelele za geti hili zilimuamsha Mchungaji kule ndani na kuchungulia nje kupitia dirishani ambapo alikuwa kasimama akiangalia kuna nini.

"Hivi huyu Davis kakumbwa na nini yaani hayo makelele hayasikii?" Mchungaji alijiuliza akiendelea kuchungulia pale dirishani, lakini kijasho kilimshuka baada ya kumuona Davis akilifungua geti na kabla hajachungulia nje kulikoni alimshuhudia Davis akisukumwa na kuanguka chini na hapo hapo aliingia mama fulani ambaye anamfahamu vizuri kutoka nyumba kama ya nne hivi.

"Mhh huyu si mama Sharon?" Mchungaji alijiuliza.

"Mchungaji, Mchungajiiiiii kama uko ndani naomba utoke huku nje kuna tatizooo......" Mama Sharon alisikika kiasi cha kumshtua Mchungaji.

"Tatizoooo? Tatizo gani hilo?" Alijiuliza akitoka kumsikiliza mama Sharon.

"Enheeee afadhali nimekuona baba Mchungaji njoo uone huku nje." Mama Sharon aliongea akimkamata mkono Mchungaji na kuanza kumvuta kuelekea nje. Mlinzi baada ya kuona kitendo kile cha kuvutwa bosi wake akainuka kutoka pale chini na kuwafuata nyuma.

"Mama Sharon kuna nini naona unanipelekesha tu bila kuongea chochote kwani kuna nini dada yangu?" Mchungaji Rodney aliona aulize tu ili ajue kuna nini.

"Utajua huku huku baba Mchungaji." Mama Sharon alimjibu kwa kifupi. Baada ya kufika nyuma ya ukuta wa kanisa palipo na dampo la taka Mchungaji hakuamini macho yake kwa alichokutana nacho.

"Hicho ndicho nilitaka kukuonesha baba Mchungaji, nimeikuta miili hiyo mitatu kama inavyoonekana hapo wakati nimekuja kutupa taka." Mama Sharon alitoa ufafanuzi kuhusu ile miili ya marehemu iliyokutwa pale jalalani ikiwa ndani ya fuko moja la nailoni angavu.

" Ni nani kafanya mauaji haya na kuja kuitelekeza hapa?" Mchungaji alijiuliza wakati mama Sharon akiondoka eneo lile.

"Mchungaji ni wakina nani hawa?" Davis alimuuliza Mchungaji wakati akiipekua simu yake.

"Wala sifahamu chochote wacha nitoe taarifa Polisi wao ndiyo watajua kipi ni kipi." Mchungaji alimjibu mlinzi huku simu ikiwa tayari sikioni.

"Ndiyo Afande ni hapa kwenye Jalala letu la taka." Baada ya kutoa maelezo hayo Mchungaji alitulia kidogo kusikiliza na ndipo alihitimisha kwa kumjibu.

"Nawasubiri Afande bila shaka."

Alipoitoa simu sikioni macho yake yalibaki kwenye kioo.

"Kama ambavyo nilikujulisha jana kuwa ifikapo leo nitakupa maelekezo nadhani kuna ujumbe umeupokea hapo ufanyie kazi lakini jua kwamba taarifa hizi zikifika kwenye vyombo vya sheria utatujua." Ulisema ujumbe huo. Alipomaliza tu kuusoma ujumbe huo alimwita Davis kwa ishara ya mkono.

" Naam Bosi." Aliitika mlinzi.

" Utabakia hapa mpaka pale Askari watakapofika kuchukua hii miili."

"Sawa bosi." Davis alimjibu. Mchungaji aliondoka pale jalalani na kuelekea ofisini kwake.

"Hapa usalama wangu ni kutoroka tu." Alijisemesha Mchungaji.



#SULTANUWEZO 

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post