MUUAJI MWENYE BARAKOA - 10 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


MUUAJI MWENYE BARAKOA - 10

sultanuwezotz.blogspot.com 


***


Catherine aliamka asubuhi na mapema na kutoka nje ya lile jengo akiwa kavalia mavazi yake ya michezo bila shaka alikuwa akielekea kufanya mazoezi ufukweni. Akijua kuwa amewahi sana kufika mazoezini alistaajabu kumkuta Adoyee akiwa sambamba na mzee Malick Bolenge wakiwa wamelowa kwa jasho.

"Ndiyo kusema wameamka usiku sana?" Catherine alijiuliza mwenyewe.

"Kumbe na wewe ni muumini wa mazoezi ee hatukuona sababu ya kuwaamsha tulihisi mtakuwa mmechoka sana." Mzee Malick Bolenge alimuuliza.

"Sawa tu Mjomba mmeshinda." Catherine alimjibu mjomba wake huku akimpita kwa spidi ndogo ya mbio.

"Usichukie mjomba, ukifanya hivyo asubuhi yangu itaanza vibaya."

"Wala hajakusikia." Adoyee alimwambia mzee Malick Bolenge aliyekuwa kaelekeza macho yake kwenye uelekeo wa Catherine.

"Kasikia sana ila tu kaamua kukaa kimya na hii ndiyo ilikuwa tabia ya mama yake hajaacha kitu. Achana naye wacha mimi nikaoge kuna sehemu natakiwa kuelekea."

"Sawa mzee." Adoyee alimjibu. Wakati huo huo alikuja Seynabou na kuungana na Catherine ambaye mwili wake ulikuwa umeshapata moto. Walifanya mazoezi yao kwa muda wa masaa mawili hivi kisha Seynabou na Catherine wakaona waingie kuogelea huku Adoyee akiwaacha na kurudi nyumbani.

"Madam nikuulize swali?" Seynabou alimuuliza Catherine.

"Uliza tu mdogo wangu."

"Hivi unafahamu kuogelea?" Alimuuliza.

"Kiukweli Seynabou mimi siyo fundi sana wa kuyakata maji lakini kiasi chake vipi kuhusu wewe?" Alimjibu na kumgeuzia swali naye.

"Mimi tena? Hapa ni maji marefu madam naweza kuogelea hapa mpaka ng'ambo ya bahari." Alimjibu na kuanza kucheka na bila shaka alijua amedanganya.

"Nahisi baridi ishakuanza mdogo tuondoke maana si kwa kamba uliyonifunga yaani wewe uyakate maji haya ya bahari mpaka ng'ambo kweli? Hebu tuondoke zetu huyo Shetani wako wa uongo asijetokea bure hapa ukazidi kunipiga vitasa vya uongo bure."

"Huamini au nianze?" Seynabou alimjibu.

"Hapana bwana mimi sina nguvu za kumbeba mtu aliyeshiba vikombe vya majichumvi." Majibu ya Catherine yaliwafanya waanze kucheka na wakati huo walikuwa wakikimbia taratibu kurejea nyumbani.

"Bosi kifungua kinywa kiko tayari mezani." Adoyee alimpa taarifa hiyo Catherine.

"Mhh mapema hivi, ni nani kaiandaa?" Seynabou alishangaa.

"Seynabou mbona washangaa nimeiandaa mwenyewe hapa au kuna ubaya?" Adoyee alimjibu.

"Haujakosea hata kidogo Adoyee tunashukuru, ngoja tujiweke sawa kwanza kisha tujumuike mezani." Catherine alimjibu.

"Sawa bosi." Adoyee aliitika na kurudi sebuleni. Catherine alipoingia chumbani kitu cha kwanza kikawa ni kuiwasha simu yake pamoja na laptop kama utaratibu wake ulivyo kila siku.

"Maskini!" Aliongea kwa sauti mara baada ya kukutana meseji nyingi za Jumbe zilizomkosa hewani. 

"Kuna nini Madam?" Seynabou aliuliza.

"Si kubwa sana mdogo wangu ni Jumbe kapiga simu nyingi sana wakati simu ikiwa 'off' sijui kuna nini?" Alimjibu huku akiipiga namba ya Jumbe.

"Naam Bosi." Jumbe aliitika baada ya kupokea simu.

"Kwema Jumbe."

"Huku ni kwema bosi kwa kuwa ile shughuli nimeimaliza masaa kadhaa nyuma na muda huu tuko ndani ya msitu mmoja hapa tunapumzika kidogo kabla ya kuendelea na safari."

"Poleni sana, na wale washirika wetu umeongea nao juu ya kuyafuata magari yao?" Aliuliza.

"Muda mrefu sana na hivi tunavyoongea inawezekana hata 'plate numbers' washazibadilisha." Jumbe alimjibu.

"Vizuri, sasa ndani ya saa moja hivi nitakuwa hapo kuwachukua."

"Hapana bosi usihangaike sisi tutafika tu kuna mzee mmoja tumekutana naye hapa ana gari lake aina 'land lover' kakubali kutupa lifti na yeye katuomba tumsaidie kupakia magunia ya viazi mviringo alivyokuja kununua huku porini ambako ni wazalishaji wa zao hilo." Jumbe alimtoa hofu Catherine.

" Sawa Jumbe lakini kuweni makini msimuamini kila mtu mbele ya macho yenu." Aliwatahadharisha.

" Nimekuelewa mkuu wangu." Jumbe alimjibu. Catherine aliikata simu na kuiweka kitandani kisha macho yake yakahamia kwenye 'special app' na kufungua kisanduku cha simu ambazo ziliingia kwa Mchungaji haikuchukua muda kuondoka kwani alikutana na simu chache zisizo na maana hivyo akafungua kisanduku cha ujumbe mfupi nako hakupata anachokihitaji hapo aliondoka kwenye 'app' hiyo na kuingia kwenye 'unknown call' akaingiza namba ya Mchungaji na kuipiga.

"Shiiiit......!" Alijisemesha.

Seynabou aligeuka kumtazama bosi wake alitamani kuuliza kitu lakini aliona wacha akae kimya.

"Hauwezi kunikimbia mimi Rodney subiri uone." Catherine aliongea akiizima laptop.

"Vipi wewe tayari?" Alimuuliza Seynabou.

"Hapa nakusubiri wewe tu." Seynabou alimjibu.

"Okay wacha nifanye haraka mdogo wangu." Alimjibu akiinuka pale kitandani. Baada ya kuulainisha mwili wake kwa mafuta na vipodozi mbalimbali kama ilivyo kawaida kwa Wanawake na kutupia tracksuit yake ya rangi ya blue alitoka mle chumbani akiwa sambamba na Seynabou ambaye muda wote alikuwa kama mlinzi wake kwani hakubanduka mpaka pale Catherine alipokamilisha yale aliyokuwa akiyafanya.

"Adoyee mfuate Mjombe tushiriki pamoja kifungua kinywa." Catherine alimwambia Adoyee ambaye alikuwa bize kwenye simu yake.

"Bosi, mjomba kaondoka kasema amepata dharura kasema atarejea baadaye kidogo kuna mtu anakwenda kuonana naye."

"Mbona kaondoka kimya kimya hivyo?"

"Hakutaka kuwasumbueni na ndiyo maana akaniachia maagizo mimi." Adoyee alimjibu.

"Okay basi tufungue kinywa kisha tufanye moja ya shughuli iliyotuleta hapa Saint Louis."

"Sawa bosi." Adoyee alijibu.

"Seynabou umesikia nilichosema? Maana naona macho yamefia kwenye simu." Alimgeukia Seynabou.

"Macho ndiyo yalikuwa kwenye simu lakini kila kitu nimekisikia dada." Seynabou alimjibu.

Walijisevia kifungua kinywa na kuanza kupata huku mazungumzo ya hapa na pale yakiendelea na kwa kuziangalia nyuso zao walionekana kuwa furaha sana utafikiri wameishi pamoja muda mrefu.

" Bosi hivi unafikiri mchezo tuliomfanyia baba Mchungaji hautashtukiwa kweli?" Adoyee alimuuliza Catherine.

"Jamani si tumalize kwanza kula angalia sasa tunatemeana mate." Seynabou alimwambia Adoyee ambaye wakati akiongea alitokwa na vimate.

"Umeshinda basi siongei tena mimi." Adoyee alimjibu na kuinuka kisha akaondoka pale sebuleni.

"Kwa hiyo ndiyo kusema umezira au?" Catherine alimuuliza lakini hakupata jibu lolote kutoka kwa Adoyee.

"Seynabou umeshamkwaza mwenzako sasa." Catherine alimwambia Seynabou.

"Namshangaa sana anakuwa na vitabia vya kike kike sasa kilichomfanya azile hapo ni kipi kama siyo umama huo?"

"Mtajuana wenyewe bwana wacha mimi nijaze tumbo kwanza." Catherine aliongea akiongeza vipande vya nanasi kwenye sahani yake. Lakini wakati akichukua kipande kimoja cha nanasi simu ya mezani iliita ambayo toka wafike hapo wamekuwa wakiitumia kufanya mawasiliano na wakina Jumbe ambao wako njiani kuungana nao hapo Saint Louis hivyo kumfanya Catherine amwambie Seynabou akaipokee,naye akafanya kama alivyoelekezwa na bosi wake.

"Naongea na nani tafadhali?" Seynabou aliuliza baada ya kuuinua mkonge wa simu na kuiweka sikioni.

"Hapa ni ndani ya kijiji cha Omuega vijana wako tumewateka hivyo kama utakuwa tayari kuwapata wakiwa hai fuata masharti yetu." Upande wa pili uliongea kitu ambacho kilimfanya Seynabou asite kidogo kuongea chochote mpaka pale alipoweka kiganja chake kwenye simu na kuwasiliana kwanza na bosi wake juu ya kilichotokea.

" Unahitaji kitu gani kutoka kwetu?" Catherine aliingilia mazungumzo baada ya kuona ishara anazompa Seynabou haelewi.

"Simu itakayokuja muda si mrefu itakuwa na maelezo ambayo utatakiwa kuyafanyia kazi ndani ya saa moja kinyume na hapo hutotusahau maishani mwako." Kisha simu ilikatwa.

"Buushiiiiit ndiyo nini sasa au Jumbe kanichezea mchezo?" Catherine alipiga kelele.

"Kwanini afanye hivyo bosi wanaweza kuwa wametekwa kweli." Seynabou alipingana na kile alichoongea Catherine.

"Hapana mdogo wangu kuna kitu hakiko sawa hapa nilimwambia Jumbe tukawafuate lakini akakataa sasa yako wapi kama siyo kuunguza picha huku?"

"Tunahitaji kiasi cha paundi milioni moja ndipo tuwaachie na ukiwa tayari tujulishe mchana kupitia link hiyo hapo chini ili tukujulishe mahali kwa kuziweka." Upande wa pili uliongea baada ya Catherine kuipokea simu kwa mara ya pili.

"Paundi milioni moja?" Catherine aliuliza akiwa kaushika mdomo wake.

"Nimemaliza kazi kwako."Upande wa pili ulikata simu.

" Huu ni mchezo nimeamini haiwezekani nasema haiwezekaniiii!!!!!!!" Catherine alipiga kelele huku akiuachia mkonge wa simu kitu kilichomtoa chumbani kwake Adoyee kuja kuangalia kulikoni.

" Nini kimetokea bosi?" Adoyee aliuliza.

" Hivi mnafikiri zaidi ya shilingi bilioni tatu nitazipata wapi kwa muda huu?"Catherine aliuliza akijitupa kitini.

" Ni nani anahitaji kiasi hicho cha fedha?" Adoyee alimuuliza bosi wake.

" Kuwa mpole basi Adoyee huoni bosi hayuko sawa?" Seynabou alimuuliza Adoyee ambaye hakujua kinachoendelea sebuleni pale. Catherine alitoka nje ambako alizunguka nje ya nyumba huko alitulia kwa muda macho yakiwa baharini kuangalia muonekano bahari na shughuli mbalimbali zilizokuwa ziliendelea na bila kufanya vile ilikuwa ni kuutafuta utulivu juu ya kilichotokea dakika chache zilizopita. Akiwa pale nje alipata wazo la kumpigia simu mjomba wake mzee Malick Bolenge kutaka kumjulisha kilichotokea. Aliitoa simu yake mfukoni na kuitafuta namba ya mjomba wake kisha alimpigia.

"Nimetoka mara moja Mjomba wangu kuna sehemu nimekuja mara moja kuonana na mtu mmoja muhimu sana." Mzee Malick alianza baada ya kuipokea simu ya Catherine.

"Mjomba bwana sijakupigia kwa ajili ya hilo!" Catherine alimjibu.

"Kuna nini tena?" Mzee Malick Bolenge akamuuliza baada ya kubaini kajichanganya.

"Wageni wangu wametekwa na watekaji wanahitaji kiasi cha paundi milioni moja..."

"Paundi milioni? Zote hizo? Mjomba tutazitoa wapi sasa?" Mzee Malick Bolenge alimuuliza maswali mfululizo.

"Na ndiyo maana nimekupigia simu ili tushauriane na wanazihitaji fedha hizo leo hii hii Mjomba." Catherine alifafanua.

"Pole Mjomba suala hili si dogo hata kidogo."

"Asante Mjomba wangu." Catherine alimjibu.

"Hebu jiandaeni muda huu mje kwenye Hotel moja iitwayo TRAVIS MARK HOTEL." Mzee Malick alimwambia Catherine.

"Iko mji gani hiyo hotel Mjomba?" Catherine aliuliza.

"Iko nje kidogo ya mji huu wa Saint Louis tumieni gari ya kukodi mkimuelekeza tu dereva atawafikisha." Mzee Malick Bolenge alimuelekeza Catherine.

"Nimekuelewa Mjomba, tunakuja sasa hivi." Catherine alimjibu na kukata simu kwani hakutaka hata kusubiri neno lolote kutoka kwa Mjomba wake kisha alirudi ndani akiwa na furaha kiasi tofauti na mwanzo.

"Adoyee, Seynabou jiandaeni tunatoka mara moja." Aliwaambia akiingia chumbani.

Wakina Seynabou walishindwa hata kumuuliza chochote kwani alikuwa juu juu.

"Umemuelewa bosi Seynabou?" Adoyee alimuuliza Seynabou.

"Wala sijamuelewa maana namshangaa karejea akiwa na tabasamu usoni." Seynabou alimjibu.

"Mhh nenda kajiandae tusije mkwaza bosi wetu." Adoyee alimwambia Seynabou akiingia chumbani kwake.

"Mimi sina cha kubadili hivi hivi imetosha ninyi kajiandaeni nawasubiri." Seynabou alimjibu Adoyee. Ndani ya dakika kama kumi hivi Catherine alitoka akiwa ndani ya gauni refu jekundu huku mtandio mweupe ukikifunika kichwa na macho hakuyaacha hivi hivi aliyavisha miwani mikubwa myeusi mguuni akiwa kavalia raba nyeusi zenye soli nyembamba hakika alipendeza sana.

"Mhh umependeza sana bosi wangu wacha nikupokee mkoba kwa ulivyopendeza mkoba haukufai hata kidogo." Seynabou alimsifia Catherine ambaye hakumjibu kitu zaidi ya kutabasamu na kumkabidhi mkoba wake.

"Adoyee unavaa mavazi gani hayo muda wote huu?" Catherine alimtania.

"Niko tayari Madam." Alimjibu akitoka. Kisha walitoka mpaka nje ambako waliisimamisha taxi iliyokuwa ikipita.

"Samahani kaka tunaelekea TRAVIS MARK HOTEL kiasi gani?" Catherine aliuliza.

"Samahani dada hii siyo taxi lakini naweza kuwasaidia tu maana na mimi naelekea huko huko." Dereva yule aliongea akishuka kuwafungulia milango.

"Tunashukuru sana kaka kwa msaada wako." Catherine alimjibu akipanda siti ya mbele.

"Ingieni waungwana tuondoke." Dereva aliwaambia wakina Adoyee waliokuwa bado hawajapanda kwenye gari.

"Ubarikiwe kaka." Seynabou alimshukuru dereva huyu aliyejitolea kuwasaidia mpaka TRAVIS MARK HOTEL ambayo kwa hapa Saint Louis ndiyo hotel ya kifahari na ambayo hutembelewa na watu wa Mataifa mbalimbali.

"Msaada nilioutoa dada yangu kila mmoja angeweza kuufanya tu hivyo naombeni msinishukuru sana kiasi cha kupitiliza ndugu zangu." Dereva huyu aliwaambia wakina Catherine.

"Haya bwana tumeelewa." Catherine alimjibu huku akiiangalia simu yake.

" Ninyi ni wenyeji wa jiji hili?" Dereva aliwauliza.

" Mmhh ndiyo sisi ni wenyeji japo shughuli zetu huwa tunazifanyia nje ya nchi." Alijibu Catherine huku macho yake yakimkagua vizuri dereva huyu.

" Waoo kumbe na ninyi ni kama mimi tu."

"Kivipi?" Catherine alimuuliza.

"Naitwa Gidion Michael ni mfanyabiashara maarufu hapa nchini Senegal lakini makazi yangu yakiwa nchini Morocco na hapa mjini kwenu nimetua jana tu na nimefikia TRAVIS MARK HOTEL hivyo kukutana nanyi ni bonge la kampani. Kama hamtojali ningependa kuungana nanyi ukizingatia leo pale kuna Bonge la Show kutoka kwa Msanii mmoja maarufu sana kutoka nchini Tanzania anaitwa Diamond Platnumz." Gidion alijitambulisha kwa kirefu.

" Wee kaka acha uongo Mungu anakuona wewe, huyo Diamond unayemzungumzia ni yupi? Huyu huyu ninayemfahamu mimi au kuna mwingine?" Seynabou hakukubaliana na maneno ya Gidion.

" Dada yangu elewa kuna Diamond Platnumz mmoja tu Barani Afrika kama huamini tulia tukifika ndiyo unihukumu mambo yakiwa tofauti." Gidion alimjibu.

" Labda ngoja tufike." Seynabou alikubali kwa shingo upande.

" Kwani wewe Seynabou huyo sijui Platnumz unamfahamu?" Catherine alimuuliza Seynabou.

" Simfahamu kwa kumuona 'live' bali huwa namuona kwenye Televisheni tu." Seynabou alimjibu.

"Basi leo ndiyo siku yako ya kumuona macho kwa macho Nyota kutoka Afrika Mashariki." Gidion alikandamizia zaidi na muda wote huo Adoyee alikuwa bize na muziki 'earphones' zikiwa masikioni hasikii chochote kile kinachoendelea.


BILA SHAKA TUMESAFIRI PAMOJA MSOMAJI WANGU BILA TATIZO LOLOTE WALA KIKWAZO KUTOKEA, JE NI NINI KITATOKEA HUKO TRAVIS MARK HOTEL? 


UNGANA NAMI KATIKA SEHEMU INAYOFUATA UPATE KUJUA NI NANI MASTER PLAN WAKO.


#SULTANUWEZO 

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post