MUUAJI MWENYE BARAKOA - 11(Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


MUUAJI MWENYE BARAKOA - 11

sultanuwezotz.blogspot.com 


"Tumeshafika tayari hapa ndiyo TRAVIS MARK HOTEL." Gidion Michael aliwaambia wakina Catherine.

"Oohh kumbe ndiyo hapa eee?" Catherine aliuliza.

"Ndiyo dada." Gidion alimjibu Catherine akipaki gari lake ndani ya maegesho ya Hotel ya TRAVIS MARK HOTEL.

"Tunashukuru sana kwa msaada wako na Mungu akubariki." Catherine alimshukuru Gidion.

"Usijali dada yangu kwa sasa ninyi ni zangu na hii hapa ni kadi yangu yenye mawasiliano yote." Gidion alimkabidhi kadi Catherine ambaye ni alishashuka chini macho yakiwa kwa watu wanaoingia na kutoka ndani ya Hotel hiyo.

"Okay Gidion tutawasiliana, tungependa kuambatana nawe lakini kuna mtu tumekuja kumuona hapa." Catherine alimjibu akiwapa ishara wakina Adoyee wamfuate.

"Bila shaka ndugu zangu." Gidion alimjibu Catherine akiziweka sawa 'site mirror' za gari lake huku wakina Catherine wakipanda ngazi kuelekea ndani ya Hoteli.

"Mjomba ndiyo tunaingia hapa Hotelini." Catherine alimwambia mjomba wake baada ya kumpigia simu na kuipokea.

"Mkifika hapo mapokezi msiondoke nakuja sasa hivi." Mzee Malick Bolenge alimuelekeza Catherine.

"Ndiyo tuko hapa mapokezi." Catherine alimjibu mjomba wake.

"Dakika sifuri niko hapo mjomba wangu." Mzee Malick alimjibu na kukata simu. Hata dakika nne hazikuisha mzee Malick Bolenge alifika pale mapokezi na kukutana nao.

"Nifuateni huku." Mzee Malick aliwaambia wakina Catherine wamfuate na baada ya kuingia kwenye chumba kimoja ambacho kiko ghorofa ya tatu mzee Malick aliwaeleza kitu ambacho Catherine hakukitarajia hata chembe na kisha alitaka kujua zaidi ya kutekwa kwa wakina Jumbe.

"Catherine hii ni Hotel yangu japo wengi hawajui hicho na hii ndiyo ofisi yangu ambayo huwa naitumia kufanya mambo yangu mengi ya kibiashara lakini nikiwa kama mteja na..."

"Subiri kwanza Mjomba unataka kusema hili Hotel ni lako au umeamua tu kunipandisha presha?" Catherine alimuuliza mjomba wake.

"Mjomba, Mjomba hivi toka lini nikakudanganya? Hii ni Hotel yetu na labda tu nikwambie hii ni moja ya vitega uchumi vyangu lukuki vilivyo hapa nchini Senegal kwa muda huu tuachane na hili kwanza tuzungumzie uliloniambia." Mzee Malick Bolenge alimjibu Catherine huku akiiweka simu sikioni.

" Njoo ofisini kwangu mara moja." Aliongea na simu kisha akaikata na kumgeukia Catherine.

" Ndiyo Mjomba nakusikiliza."

"Kama nilivyokuambia Mjomba watu wangu wametekwa huko porini na watekaji wanataka paundi milioni moja na wanazihitaji leo hii hii mchana hapa kichwa kinaniuma Mjomba sijui nitazitoa wapi hizo hela kwa masaa machache hivi." Catherine alimweleza Mjomba wake kila kitu juu ya kilichotokea.

" Mhh ilikuwaje mpaka wakatekwa?" Mzee Malick alimuuliza Catherine.

" Yaani Mjomba sijui nikujibu vipi swali lako maana hata mimi naumiza kichwa hivyo hivyo."

" Naam Bosi." Alikuja mmoja wa wahudumu wa ile Hotel.

"Wahudumie wageni wangu hapa." Mzee Malick aliagiza.

"Karibuni niwahudumie tafadhali."

"Mimi nitakula baadaye niombe maji tu ya baridi." Catherine alimjibu.

"Mimi naomba Wali mkavu ulioungwa nazi pamoja na juisi ya nanasi." Adoyee aliagiza menyu yake.

"Kwa upande wangu mimi niletee kuku nusu na Coca Cola ya baridi usisahau na pilipili eee."

"Vinakuja mara moja." Mhudumu alijibu na kuondoka.

Baada ya mhudumu wa Hotel kuondoka Catherine alimgeukia mjomba wake.

"Wewe ni kiboko yaani mjengo kama huu hakuna anayejua? Au nilibaki mimi tu kujua?" Alimuuliza.

"Tena una bahati Mjomba hakuna anayejua zaidi yako na rafiki zako hawa mpaka nimefanya hivi mjue nimewaamini sana hivyo hakikisheni kila mlichokisikia hapa kinabaki hapa hapa." Mzee Malick alitoa tahadhari.

"Kuhusu hilo ondoa shaka Mjomba wangu na kuwahusu hawa nikutoe wasiwasi hawana tabia za kimbea ni watu makini sana." Catherine alimuondoa wasiwasi mjomba wake juu ya kuvuja kwa siri zake.

"Okay nimekuelewa mjomba wangu sasa juu ya hili la watekaji naomba nikuahidi kuwa vijana wako wote tutawaokoa na hao watekaji hawataambulia hata shilingi mbovu."

"Kweli Mjomba?" Catherine alimuuliza Mjomba.

"Kweli ndiyo au hauamini?"

"Nakuamini mjomba na ndiyo maana niko hapa."

Mhudumu alikuja akiwa menyu yote aliyoagizwa na wakina Seynabou.

"Karibuni mfurahie huduma zetu kutoka hapa TRAVIS MARK HOTEL ambapo siku zote tunasema 'Tuko Tayari kukuhudumia mteja wetu' muda wowote."

" Tunashukuru sana dada." Alimjibu Adoyee kwa niaba ya wenzake. 

" Rachel utaniletea Kande zangu kama ziko tayari." 

" Sawa bosi." Mhudumu alijibu na kutoka zake. 

" Namba yao kama uliikamata wapigie ukiwaambia kuwa uko tayari kutoa kiasi hicho cha fedha ili tujue plani yao ni ipi." 

"Walinitajia ninayo hapa wacha niwapigie." Catherine alimjibu huku akiinuka na kuelekea dirishani simu ikiwa tayari sikioni. Lakini wakati akiwa anaisikilizia simu ipokelewe upande wa pili Catherine kuna kitu aliweza kukiona kule chini akamwita Mjomba wake na kumuonesha kitu. 

" Yule mtu pale chini ni nani? Na unaweza ukawa unamfahamu?" Alimuuliza. 

"Nani Gidion? Kwa nchi hii ya Senegal ni nani asiyemjua huyo kwa utajiri alionao?" Mzee Malick alimjibu. 

"Ana hela ndefu eee?" Catherine alimuuliza tena.

"Hebu ongea na hao kwanza huyo mwingine huko chini achana naye muda ni mali." Mzee Malick alimsisitiza baada ya kuona Catherine anataka kuchanganya masuala.

"Sawa Mjomba lakini huyu mtu nina mashaka naye sana unajua nini?" Catherine alimuuliza Mjomba wake.

"Hata mimi nina mashaka naye pia si unakumbuka alituambia kuwa ndani ya Hotel hii kutakuwa na Onesho kubwa la Muziki kutoka kwa msanii maarufu ambaye kila nchi ingejivunia kuwa naye lakini toka tumeingia humu hotelini hata shangwe lenyewe sijalisikia." Seynabou aliongeza baada ya kusogea pale dirishani na kumuona Gidion.

" Kuna onesho hapa? Onesho gani hilo na ni la msanii gani huyo?" Mzee Malick Bolenge aliuliza baada ya kupata habari ambayo si ya kweli ukizingatia Hotel yake haijawahi kujishughulisha na maonesho ya aina yoyote ile toka ainunue Hotel hiyo kutoka kwa mfanyabiashara maarufu kutoka nchini Kenya aitwaye Onyango Keuthi ambaye alifanya hivyo baada ya kufilisika na kuamua kurejea nchini kwao kujipanga na kuanza upya.

"Ndiyo, na alisema kuwa ni la Mwanamuziki aitwaye Diamond Platnumz kutoka nchini Tanzania sasa ukiwa kama mmiliki wa Hotel hii mbona unashangaa?" Catherine alimuuliza Mjomba wake.

"Mjomba nashangaa ndiyo sababu hii Hotel kama mlivyoiona wenyewe haijawahi kufanya shughuli hizo labda huko mbeleni lakini siyo kwa sasa. Adoyee nenda kule chini kwa kupitia mlango wa nyuma ambao mhudumu wa mapokezi atakuonesha mfuatilie Gidion tujue anatafuta nini halafu na wewe Mjomba watu wako wanasemaje?"

" Kiukweli hawapokei simu labda watapiga wenyewe wacha tuwasubiri kidogo."

"Hakuna haja ya kusubiri wacha tucheze nao mchezo mzuri ambao hawatausahau maishani mwao, nifuateni huku." Mzee Malick aliwaambia wamfuate huku Adoyee akiwa tayari nje ya Hotel akimfuatilia Gidion ambaye alikuwa bize akiongea na simu huku mkononi akiwa na chupa kubwa ya maji. Waliingia mpaka kwenye chumba ambacho kilikuwa na Kompyuta nyingi sana huku vijana wawili waliowakuta mle wakiwa bize nazo inawezekana hawa walikuwa wataalam wa hizo Kompyuta.

"Vijana wangu kwanza poleni na kazi, itafuteni namba fulani kwenye 'Mark finder' mara moja." Mzee Malick alitoa maagizo akiketi kwenye kiti ambacho kilionekana dhahiri huwa hakikaliwi na yeyote zaidi yake kwa namna kilivyokuwa tofauti na vingine.

"Tunaiomba hiyo namba mkuu." Mmoja wa wale vijana aliiomba.

"Catherine wapatie ile ya maumbwa pori."

"Sawa Mjomba." Catherine alimjibu akimsogelea huyo kijana ili amkabidhi hiyo namba.


***


"Samahani binti." Mchungaji alimuita mhudumu wa ndege aliyekuwa akipita karibu yake.

"Karibu Bosi kwa huduma." Mhudumu huyo alimkaribisha.

"Naomba uniletee juisi ya limao tafadhali." Mchungaji aliagiza.

"Umeipata Bosi wangu si unajua kwetu mteja ni Mfalme japo hana Miliki." Mhudumu alimjibu akielekea kufuata.

"Hii ni kali ya mwaka yaani leo hii nakwenda kuishi ugenini? Kisa huyu muuaji muoga asiyejitokeza hadharani?" Mchungaji alijisemesha mwenyewe na muda huo ndege hiyo ilikuwa juu ya anga la nchi ya mzee Magufuli, kiongozi aliyejipatia Umaarufu hivi karibuni baada ya kufanya maamuzi magumu ya kuwataka Watanzania kuendelea na shughuli za uzalishaji Mali pasipo kuliogopa gonjwa hatari la COVID-19 linalo isumbua dunia baada ya kuua mamilioni ya watu. Akiwa anasubiri juisi yake aliyomuagiza mhudumu wa ndege mara kuna ujumbe ukaingia kwenye simu yake, hivyo akaufungua na kuusoma.

"Mchungaji Rodney unatafutwa na jeshi la Ulinzi la hapa Senegal kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya watu kadhaa ambao asilimia kubwa ni waumini wa kanisa lako la JESUS OUR KING. Kwa kukukumbusha tu nafikiri unawakumbuka wafuatao; Kijana wako Bartholomew, mama Jennifer mke wa Otago Mathew, Askari wa Doria mpaka wa Casamance, vijana wawili waliouawa huko Casamance mmoja akiwa ni 'Inspector' wa Jeshi la Polisi na kama haitoshi kuna watu wawili hawajulikani walipo mpaka sasa ambao ni Mama Mchungaji 'Catherine' na mlinzi wenu 'Adoyee' na hujaripoti kituo chochote cha Polisi pia kuna tetesi za kuuawa kwa rafiki yako Mganga wa Tiba za Asili mzee Alioune huku mtoto wake hajulikani aliko mpaka sasa, matukio haya yote yanaunganishwa pamoja kutokana na kupotea na kuuawa kwa Waumini wako miaka zaidi ya kumi na mbili iliyopita. Na vipi kuhusu miili ya vijana watatu iliyokutwa Kanisani kwako ni nani anayehusika?


KULIKONI TANZANIA TENA MCHUNGAJI RODNEY? JE UNAFIKIRI UJUMBE HUO UMETUMWA NA NANI?


TUKUTANE NDANI YA SEHEMU YA KUMI NA MOJA YA KIGONGO HIKI CHA MUUAJI MWENYE BARAKOA TUPATE MAJIBU YA MASWALI YETU.


#SULTANUWEZO 

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post