MUUAJI MWENYE BARAKOA - 12 (Mtunzi: Sultan Uwezo)


MUUAJI MWENYE BARAKOA - 12

sultanuwezotz.blogspot.com 


Ni ujumbe ulioingia kwenye simu yake na kumfanya Mchungaji kutokwa na jasho mfululizo huku macho yakirudia mara mbili mbili kuusoma ujumbe huo. Na hata alipokuja yule mhudumu kumletea juisi aliyoagiza hakuweza kumuona hata kidogo.

" Karibu mheshimiwa." Alikaribishwa.

"Unasemaje?" Aliuliza kwa kufoka.

"Nimekuletea juisi yako bosi." Yule mhudumu alijibu.

"Oohh sorry binti, nashukuru sana." Alimjibu akiichukua ile glasi na kuikata yote kisha akairudisha ile glasi kwenye trei, tukio lile lilimshangaza sana yule mhudumu.

"Unanidai shilingi ngapi?" Alimuuliza.

"Hapana hiyo ni moja ya huduma zetu ndani ya SERENGETI AIRWAYS." Mhudumu alimjibu huku akiwa bado anamshangaa Mchungaji Rodney.

"Okay kazi njema." Mchungaji alimuondoa kijanja mhudumu.

"Asante, lakini ni kama kuna tatizo hivi, naweza kukusaidia?" Alimuuliza kabla ya kuondoka.

"Nikiwa na tatizo nitakuiteni binti sawa?" Mchungaji alimjibu.

"Sawa Bosi." Mhudumu alimjibu na kuondoka.

"Ni nani aliyeutuma ujumbe huu Mungu wangu mbona majanga yananiandana kiasi hiki?" Mchungaji alijiuliza maswali huku akijitahidi kulitafuta jina la mtuma 'Email' hiyo ambayo haikuwa na jina wala anuani ya mtumaji.

"Abiria wetu awali ya yote nipende kumshukuru Mungu mwingi wa Rehema kwa kutufikisha salama na pili niwashukuru ninyi Wafalme wetu kwa kulichagua Shirika letu la SERENGETI AIRWAYS kuwa chombo chenu cha Usafiri. Tunashukuru sana na Karibuni tena wakati mwingine. NAWAOMBENI FUNGENI MIKANDA NDEGE INAJIANDAA KUSHUKA, ASANTENI." Ilikuwa ni sauti Nyororo ya Mhudumu wa kike wa ndege hiyo ndiyo iliyomtoa Mchungaji kutoka kwenye lindi la mawazo.

" Shabashi!! Ndiyo kusema tumeshawasili jijini Dar Es Salaam - Tanzania?" Alijiuliza Mchungaji.

" Ndiyo tumeshafika tayari." Bibi aliyekuwa karibu yake alimjibu.

"Hee ina maana nimeongea kwa sauti mpaka huyu bibi anijibu." Alijiuliza Mchungaji baada ya kuona bibi aliyekuwa siti ya jirani yake akimjibu wakati yeye hakumbuki kama aliongea kwa sauti. Baada ya ndege kusimama alimshukuru Mungu wake kwa kumfikisha salama safari yake kisha aliungana na abiria wenzake kushuka. Alipochukua mizigo yake alitoka eneo lile la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere akivuta begi lake huku macho yake yakiwa huku na kule kuona kama anaweza kumuona mwenyeji wake Daktari Sylvester Kitesa lakini hakuweza kumuona hivyo akaendelea kuvuta begi lake mpaka pale alipoweza kumuona mtu akimpungia mkono, alimtazama kwa muda mtu huyo aliyekuwa mbali kidogo na alipokuwa yeye hivyo aliona isiwe shida akaitoa simu yake na kumpigia.

"Vuka ng'ambo ya pili hapa ninapokupungia mkono Mchungaji." Daktari Sylvester Kitesa alimwelekeza baada ya kupokea simu.

"Sawa mzee."Mchungaji alimjibu huku akiangalia huku na kule kabla ya kuvuka na kama bahati vile alimuona akiwa karibu zaidi na gari aina ya Prado 2500LX ya mwaka 2020. Hivyo alivuka haraka huku sura yake ikiwa imepambwa na tabasamu na hii ni baada ya kumuona mwenyeji wake.

"Karibu Tanzania kijana wangu." Daktari Sylvester Kitesa alimkaribisha Mchungaji Rodney akimpokea begi.

"Nashukuru sana mzee wangu, nafurahi kuwa ndani ya nchi yenye historia ya kipekee duniani." Mchungaji alimjibu.

"Hii ndiyo nchi ya mzee wetu mpendwa rafiki wa wanyonge lakini pia mwenye hofu ya Mungu Mheshimiwa John Pombe Magufuli." Mzee Kitesa aliendelea kumtamanisha Mchungaji Rodney.

"Najiona niko Ulimwengu mwingine kabisa mzee wangu, yaani huko nyumbani mpaka kwenye Ndege nikiwa nakuja huku pua zetu na midomo ni mwendo wa Barakoa tu lakini cha ajabu toka nashuka kwenye Ndege mpaka hapa tulipo sijamuona mtu yeyote akiwa na Barakoa kaivaa. Ninachojiuliza hii Tanzania iko Ulimwengu gani maana nchi zote zilizo Duniani zinapambana na gonjwa hili la Covid-19 huku maelfu kwa maelfu wakiendelea kupoteza maisha."

" Kwanza kabisa niwape pole kwa yanayoendelea nchini kwenu katika kufanikisha mapambano dhidi ya Covid-19 pia na yote yaliyoikumba familia yako pamoja na Kanisa kwa ujumla wake." Daktari Sylvester Kitesa alimpa pole.

"Hatujapoa mzee wangu vita vinaendelea lakini yote kwa yote tumemkabidhi Mwenyezi Mungu." Mchungaji Rodney alimjibu. Mazungumzo yalikuwa yakiendelea kati yao huku gari likiwa linakata mitaa kutoka nje ya uwanja wa Ndege. Walipofika nje ya jengo moja refu hivi lililokuwa limeandikwa TROPICANA PLAZA mzee Kitesa alisimamisha gari kisha akamgeukia Mchungaji Rodney. "Sasa kijana wangu nisubiri mara moja nimchukue Mchungaji Tumaini Kalulanzi humu ndani." Mchungaji Rodney aliliangalia jengo hilo lililokuwa na ghorofa kama kumi na tatu kisha akamjibu Daktari Sylvester Kitesa.

"Sawa mzee wangu."

Macho ya Mchungaji Rodney yalikuwa kwa Daktari Sylvester Kitesa aliyekuwa akipanda ngazi kuelekea ndani ya jengo hilo. Akiwa kwenye tafakari mara simu yake iliita akaichukua na kuipokea.

"Bwana Yesu asifiwe Mchungaji." Upande wa pili wa simu ulianza na salamu.

"Amina mzee Lusoka, kwema huko?" Mchungaji alimjibu na kumuuliza.

"Kwema? Yaani unauliza kabisa Mchungaji wangu kana kwamba hujui kilichotokea huku?" Aliuliza mzee Lusoka.

"Mzee wangu unafahamu vizuri ninavyokuheshimu na si hivyo tu bali kwa umoja wetu tumefanya mengi sana lakini siku za hivi karibuni umekuwa kikwazo kwangu kwa hilo sipendi kabisa, ninachokitaka kwa sasa ni amani tu na si vinginevyo." Mchungaji alimfungukia mzee Lusoka 

" Mchungaji samahani sijakupigia simu kwa ajili ya hilo." Mzee Lusoka alimkatisha.

" Enhh nakusikiliza." Mchungaji aliongea.

"Inspekta wa Jeshi la Polisi akiwa kaongozana na viongozi wengine wa Kiserikali akiwemo Mwenyekiti wa Mtaa huu wamefika kwa mahojiano juu ya tukio la miili iliyokutwa jalalani kwetu hivyo wameniomba nikuite maana Inspekta kakupigia simu mara kadhaa haupatikani." Mzee Lusoka alimjibu kwa kutoa taarifa hiyo.

" Si muwaambie kuwa hata sisi tumeikuta hapo hapo!!" Mchungaji Rodney alimjibu kisha aliikata simu na kuizima kabisa.

" Wanautani na mimi hawa yaani nijitokeze kwa suala kama hili naumwa? Na hata ningekuwa mzima bado nisingekwenda huko." Mchungaji alijisemesha mwenyewe. Na muda huo huo mzee Kitesa akiwa na Mchungaji Tumaini Kalulanzi walifika na kuingia garini.

"Tulikutelekeza Mchungaji?" Mzee Sylvester Kitesa alimuuliza akikaa vizuri kitini.

"Hapana baba."

"Bwana Yesu asifiwe Mtumishi." Mchungaji Tumaini Kalulanzi alimsalimu Mchungaji Rodney.

"Amina kiongozi, poleni na Majukumu." Mchungaji Rodney alimjibu.

Baada ya hapo waliondoka huku nyuma ya usukani akiwa Mchungaji Tumaini Kalulanzi ambaye naye ni Mchungaji wa Kanisa hilo la JESUS OUR KING mkoani Morogoro. Na hata hilo gari ni mali yake Daktari Kitesa alilitumia tu mara baada ya Mchungaji Rodney kumtaarifu kuwa yuko ndani ya Tanzania hivyo aliona aazime.

"Mchungaji tulikuwa na kikao cha kazi ndani ya jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kutanua huduma nchini Tanzania. Ni baada ya kuona mikoa ambayo tumeifikia inafanya vizuri hivyo tukaona tuyafanyie kazi maombi ya Wasikilizaji wetu ambao wameomba tufikishe huduma mikoani mwao." Mzee Kitesa alimfafanulia.

" Ina maana mahubiri yenu huyatoa kwa njia ya redio?" Mchungaji Rodney aliuliza.

" Ndiyo na si hivyo tu tuliamua kuitumia mitandao ya kijamii kufikisha huduma zetu ikiwa ni pamoja na mtandao wa Facebook, Twitter, YouTube bila kusahau Instagram ambako kuna kundi kubwa la vijana na kwa kupitia hizo 'platforms' tumeweza kufanya vizuri na ndiyo maana tulikuwa jijini Dar es Salaam ndani ya Ukumbi wa TROPICANA PLAZA." Daktari Sylvester Kitesa alimjibu.

" Hongereni sana kwa hilo natamani hata kwetu lingefanyika hili."

" Hamjachelewa muda bado mnao kikubwa ni mikakati tu Mchungaji." Mchungaji Tumaini Kalulanzi aliongeza.

" Tutakuwa Morogoro kwa muda wa siku mbili kisha tutaelekea jijini Mbeya." Daktari Sylvester Kitesa alimwambia Mchungaji ambaye mawazo yalimsonga mara baada ya kupokea ujumbe wa Mwenyekiti wa Bodi kanisani kwake Dr Brown Lutasya uliosomeka kama ifuatavyo : " Mchungaji unasubiriwa hapa na viongozi kutoka Serikalini wanataka kuongea na wewe juu ya mauaji yasiyoisha hapa Kanisani. Hivyo fanya haraka kiongozi." Ujumbe huu uliingia mara baada ya kuiwasha simu yake ambayo aliizima muda mfupi uliopita.


JE NI NINI KITATOKEA KATIKA KITIMUTIMU HIKI?


TAFADHALI UNGANA NAMI KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUJUE NINI KILICHOJIRI.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post