MUUAJI MWENYE BARAKOA - 13
sultanuwezotz.blogspot.com
"Hili balaa mbona naandamwa na mikosi kiasi hiki lakini? Kwamba niwaambie ukweli kuwa nimeondoka nchini? Hapana hiyo ni ngumu kwangu." Mchungaji Rodney aliendelea kuwaza wakati wenyeji wake wakijadili yale waliyoazimia kikaoni. Safari iliendelea na muda huo walikuwa wakikaribia kuingia mkoani Morogoro.
" Mtumishi unaouona mbele ni mkoa wetu wa Morogoro ambao una historia kubwa sana ndani ya bara letu la Afrika." Mchungaji Tumaini Kalulanzi alimuonesha mgeni wao aliyekuwa ndani ya dimbwi la mawazo.
"Panaonekana pazuri sana." Mchungaji Rodney alimjibu.
"Ni mji mzuri kwa siku hizi mbili utauona uzuri wake wewe mwenyewe."
"Nitashukuru sana kaka." Mchungaji alimjibu. Na muda huo walikuwa wakiingia ndani ya jengo lililoko ndani ya Kanisa kubwa lenye maandishi makubwa yaliyoandikwa JESUS OUR KING (JOK) na gari lilikwenda na kusimama sehemu ambayo ina magari mengine mawili madogo na kusimama.
" Karibuni sana Viongozi." Mchungaji Tumaini Kalulanzi aliwakaribisha wageni wake.
"Tunashukuru sana Mtumishi." Mzee Sylvester Kitesa alimjibu huku akimpa ishara ya kuteremka Mchungaji Rodney. Walishuka na kulakiwa na mama Mchungaji Bi Silvia Kalulanzi.
"Karibuni sana."
"Asante shemeji." Mchungaji Rodney alimjibu macho yakiwa kwenye mazingira.
"Kaka hongera sana kwa kunogesha mazingira yako ya Kanisa na nyumbani pia." Hakuacha kumsifia mwenyeji wake.
"Nashukuru sana ndugu yangu si unajua tena majukumu yetu?" Alimjibu. Na wakati huo huo mzee Sylvester Kitesa alikuwa akiongea na simu.
***
Mmoja wa wale vijana alipoichukua ile namba alikwenda kuiingiza kwenye system na kufanya kama bosi wao mzee Malick alivyowaelekeza. Lakini wakati yule kijana akianza kutafuta eneo inakopatikana hiyo namba mara simu yake ilipata ujumbe mfupi uliomfanya yule kijana aukague hasa baada ya kuliona jina la mtumaji. "NI VIJANA WETU HIVYO TAFUTA UONGO WENYE MATUMAINI KWAO." Alipomaliza kuusoma alimgeukia mzee Malick Bolenge na kumpiga ukope kisha akaiweka mfukoni simu yake na kuendelea na shughuli ambayo alishaianza huku ikiwa ni nyepesi zaidi hasa baada ya kupewa muongozo na bosi wake. Wakati huo Catherine alikuwa bize kwenye simu akiwa hana wasiwasi na wenyeji wake ukizingatia mzee Malick Bolenge ni mjomba wake wa damu na si wa mkopo. Na baada ya kumaliza kile ambacho alikuwa akikifanya alimfuata Mjomba wake alipokuwa kaketi kisha naye alivuta kiti kilichokuwa karibu na kuketi.
"Mjomba tunaweza kuongea?" Catherine alimuuliza mjomba wake.
"Bila shaka tunaweza." Mzee Malick alimjibu.
"Nashukuru mjomba wangu, unajua nini hatujapata muda wa kuongea maana toka tumefika ni pilika tu." Catherine alimwambia mjomba wake.
"Ni kweli kabisa lakini bado tuna muda wa kufanya hivyo mjomba wangu." Alimjibu
"Haswaa...." Lakini kabla hajaendelea kuna ujumbe uliingia kwenye simu yake na kuusoma.
"Huyu Gidion si wa kawaida kwani ni kama kashtukia hivi, kaondoka haraka." Alipomaliza kuusoma alimjibu.
"Kama umemuona jaribu kumfuatilia mpaka tumfahamu ni nani." Alipoutuma aliiweka mfukoni simu yake na kusogea karibu na Mjomba wake.
"Unafuatiliwa mpige chenga huyo Kima kisha mvizie na kumkausha damu yake." Mzee Malick akiwa bize kumalizia kuandika ujumbe wake hakumuona Catherine aliyefika na kuusoma ujumbe ule uliompa mashaka na baada ya kubaini hajaonwa na mjomba wake alirudi nyuma kidogo kisha akainuka na kumfuata kijana aliyemkabishi ile namba.
" Kaka yangu kuna uwezekano wa kubaini eneo walipo?" Alimuuliza.
"Mpaka sasa sijapata signo yoyote ile labda wacha niendelee kuitafuta." Kijana huyo alimjibu. Majibu ya kijana huyu yalimpa mashaka kidogo kiasi cha kuanza kumtilia mashaka mjomba wake.
"Ok sawa jitahidi mdogo wangu ni muhimu sana." Catherine alimjibu.
"Mjomba nakuja mara moja." Catherine alimwambia mjomba wake baada ya kumkuta akiwa katulia akichezea vidole vyake.
"Sawa mjomba." Mzee Malick alimjibu. Hivyo Catherine aliinuka na kuondoka kuelekea viliko vyoo vya ile ofisi ambako aliingia na alipoufunga mlango vizuri aliitoa simu yake na kwenda sehemu ya ujumbe mfupi huko alimuandikia 'text' Adoyee.
"Geuka haraka sana hali si shwari achana naye huyo rudi tuangalie namna ya kujinasua mtegoni." Hakutaka kusubiri majibu aliifuata koki ya bomba la maji na kuyafungulia kwa nguvu huku mkono ukiwa kwenye hayo maji ya baridi.
" Inawezekana huu mchezo ni wa mjomba ee? Na ndiyo maana asubuhi tu mtu katuacha nyumbani kumbe alikuwa na lake jambo, nitamnasa tu we ngoja tu." Catherine alijiuliza maswali yaliyomchanganya kichwa baada ya kubaini kuwa anaishi na mtu mwenye nia ovu juu yao. Kabla hajatoka mle chooni alimpigia Seynabou simu ili kumpa tahadhari.
" Uko wapi wewe?" Catherine alimuuliza Seynabou.
" Naongea na simu hapa nje vipi nije?" Alimuuliza.
"Naomba unisikilize mdogo wangu, huku ndani si shwari hivyo usirudi wasiliana na Adoyee mjue namna ya kujinasua mtegoni mimi kwa sasa nimenasa sijui kama nitatoka salama kwenye huu mtego." Wakati Seynabou akitaka kumuuliza swali Catherine alishakata simu baada ya kuhisi minyatio nje ya choo, aliizima simu na kuiweka kwenye mfuko wa ndani ya tracksuit yake badala ya kwenye kipochi chake kisha akaufungua mlango na kutoka nje ambapo moja kwa moja alirudi na kumkuta Mjomba wake akiwa anajadiliana jambo na vijana wake, Hivyo hakutaka kuwaingilia alivuta kiti na kuketi huku masikio akiwa kayategesha kiaina kunasa wanachoteta pale lakini hakuweza kusikia chochote.
"Mjomba uko poa?" Mzee Malick alimuuliza Catherine.
"Niko sawa kabisa Mjomba kwanini umeuliza hivyo?" Catherine aliuliza.
"Nimeona umechukua muda mrefu chooni nikapata wasiwasi kidogo." Alimjibu.
"Hapana Mjomba wangu mazingira ya kule yalinifanya niweze kufanya mambo yangu mengine kwa utulivu kabisa si unajua tena wanasema mazingira mazuri ya chooni humfanya mtu kupata utulivu wa akili ambao hupelekea kuanza kupanga mikakati bila shaka yoyote." Catherine alimjibu mjomba wake.
" Hilo hata mimi niliwahi kulisikia lakini bado sijaukubali hata kidogo." Mjomba wake aliongeza.
" Mimi ni shuhuda mzuri katika hili kwani mambo yangu mengi yamefanyika katika mazingira haya ya maliwatoni na matokeo chanya nimeyaona." Catherine aliitetea hoja yake akiinuka kuwafuata vijana aliowakabidhi ile namba.
" Vipi hamjafanikiwa bado?" Aliwauliza.
" Tumefanikiwa kunasa sehemu ambayo mpigaji alikuwa kama saa moja na nusu lililopita, angalia hapa kwenye doti hii ya kijani." Kijana yule alimjibu.
"Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa wanaweza kuwa karibu na hili eneo?" Catherine alimuuliza swali kijana huyu huku akiwa makini kumfuatilia machoni kama ana kiashiria chochote cha hatari.
"Nahisi hivyo dada japo sina uhakika maana signo imepotea kabisa." Alimjibu.
"Na ninachoweza kushauri hapa ni kulifuatilia eneo hili maana sina uhakika kama wameondoka haraka hivyo ikiwa hawajui kama tunawaguatilia huku." Kijana mwingine alichangia wazo lake.
"Ngoja niwasiliane na Mjomba kwanza tujue la kufanya." Catherine alimjibu akimfuata mjomba wake aliyekuwa akiongea na mmoja wa wafanyakazi wa ile Hotel.
"Samahani Mjomba hii ndiyo mida yenye ya kuwasiliana na watekaji tunafanyaje?" Catherine aliwakatisha na kuuliza swali.
"Si umeiona ile signo ya saa moja nyuma?" Mzee Malick alimuuliza.
"Nimeiona."
"Nimeshaagiza dereva alete gari yangu ya kazi ili tuelekee huko maana ni eneo la kilometa zaidi ya arobaini na saba kama zilivyoonekana kwenye king'amuzi chetu." Mzee Malick alimjibu.
"Sawa Mjomba lakini tunakwenda kufanya nini ilhali sina kiasi cha fedha wanachokitaka hao watekaji." Catherine alikubaliana naye lakini akaonesha shaka yake.
"Ondoa shaka mjomba hao watekaji hawataamini kwani tunakwenda kuwakomboa mateka bila kutoa hata kumi moja, cha kufanya waambie vijana wako wajiandae kwa safari." Mzee Malick alimpa jibu ambalo lilimfanya atabasamu, si kwamba alilifurahia hili bali alikuwa akimhadaa mjomba wake asimshtukie kwenye mpango wake alioupanga. Baada ya majadiliano mzee Malick Bolenge alimwambia Catherine amsubiri nje ili amalizie maongezi na mfanyakazi wake ndipo waianze safari, Catherine alikubali na kutoka nje ya ile ofisi ya mjomba wake kuwaacha wamalizie mipango yao lakini pale nje alikutana na mazingira ambayo yalimfanya ahisi hatari kwani walikuwa ni vijana watatu waliokuwa wamevalia miwani ya rangi nyeusi huku t-shirt zao zikiwa za rangi ya blue zenye maandishi meupe yaliyosomeka 'SULTAN UWEZO' suruali zao za jinsi zikiwa nyeusi na chini wakiwa ndani ya buti nyeusi zenye asili ya Marekani. Watu hawa wenye miili iliyojengeka vizuri kimazoezi walikuwa karibu zaidi na mlango wa ofisi ya mjomba wake.
"Ohooo mambo yamekuwa mambo hapa, nisipokuwa makini nalamba mchanga." Catherine aliwaza akiwatazama watu wale. Wakati bado anaendelea kuwashangaa watu wale pale nje Mjomba wake alitoka na kumtaka waondoke.
"Sawa mjomba." Catherine alimjibu mjomba wake huku macho yakiwa kwa wale vijana.
JE UNAFIKIRI NINI KINAKWENDA KUTOKEA?
KAA KARIBU NAMI TUENDELEE KUIFUATILIA HADITHI HII MPAKA MWISHO.
#SULTANUWEZO