MUUAJI MWENYE BARAKOA - 14 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


MUUAJI MWENYE BARAKOA - 14

sultanuwezotz.blogspot.com 


Walitoka na kuingia kwenye gari aina ya Nissan Patrol 'box board' lililokuwa likiwasubiri nje. Catherine aliendelea kupata woga kwani ndani ya gari pia kulikuwa na vijana wengine wawili pamoja na wale waliopanda idadi yao ikiwa ni tano ukiongeza mzee Malick na Catherine jumla wakawa watu saba huku mmoja kati yao akiwa dereva. Hapa ndipo alipoamini kuwa usalama wake ni mdogo sana alimtazama mjomba wake mzee Malick Bolenge katika ya mbele alikuwa bize akichati na simu tu kitu ambacho kilimfanya ashushe pumzi ndefu, alipotuliza akili kidogo akapata wazo la kuwatumia ujumbe wakina Adoyee akaingiza mkono kwenye kipochi chake aitoe.

"Sista mbona tunaminyana bila utaratibu?" Mmoja wa wale vijana aliyekuwa amekaa karibu na Catherine alimuuliza huku akivua miwani yake.

"Braza tuheshimiane basi maneno gani hayo unaongea? Tumeminyana vipi hapa wakati hapa niko kutoa simu?" Catherine alimuuliza kijana huyo akiwa kamkazia macho usoni kama vile kamfumania hivi.

"Unajua nini? Mimi huwa sibishani na watu wa jinsi yako ebooo!!!" Kijana alimjibu huku akimsindikiza kwa kibao kikali cha shavuni kilichopelekea Catherine kumuangukia miguuni kijana wa upande wa pili.

"Aaaghh...! Kaka nimekukosea nini mpaka unipige kibao kikali kiasi hiki?" Catherine alimuuliza akiinuka huku mkono ukilishika lile shavu kuona kama liko sawa.

"Unataka kuijua sababu siyo?" Yule kijana aliyekuwa kajazia kuliko wengine wote mle garini alimuuliza. 

"Ndiyo nataka wewe unaona ulichokifanya kiko sahihi? Mjomba mbona huyu kijana wako ni korofi kiasi hiki?" Catherine alimjibu kisha akaona amtupie swali Mjomba wake ambaye muda wote huo alikuwa bize na simu kama vile hakuona wala kusikia kilichokuwa kikiendelea nyuma yake. 

" Majura hujui kama huyo ni Mjomba wangu? Kwanini unakosa adabu hivyo?" Mzee Malick alimjibu kijana huyo aliyemwita kwa jina la Majura, lakini kitu cha ajabu kijana huyo ambaye ni kama alizamilia jambo kwa Catherine ni kama vile aliambiwa ongeza tena kwani kilichotokea alimvuta na kumpiga kichwa cha usoni na kumpasua eneo la juu ya jicho hali iliyopelekea kuanza kuvuja damu nyingi.

"Mjomba mbona kijana wako anataka kuniua? Nimemkosea ni......" Kabla hajamalizia kuongea alipoteza fahamu na kumuangukia kijana wa upande wa pili. Hapo hapo Majura alitoa kitambaa cheupe kwenye kibegi chake kisha akachukua kichupa kidogo mfuko wa pembeni wa kibegi hicho na kukifungua, dawa iliyokuwa nyeusi hivi ya maji maji aliimwagia kwenye kile kitambaa na kumfunga usoni mpaka puani Catherine kisha akamuegesha kitini. 

" 'Well done ma boy' kazi nzuri sana msimuache hivyo hivyo mfungeni kamba za mikono na miguu." Mzee Malick alimpongeza Majura kwa kitendo alichokifanya kwa Catherine. 

"Lakini bosi huyu si mtoto wako, kwa ninavyojua mimi mtoto wa dada yako ni mtoto wako pia kulikoni kwako?" Kijana mwingine aliyekuwa kiti cha nyuma kabisa alimuuliza mzee Malick. 

"Wayaki tulia kijana wangu kwenye hili halikuhusu hata kidogo nimelianza mwenyewe nitalimaliza mwenyewe au tayari rangi ya mtoto imekuingia kwenye mishipa ya damu? Maana ninyi vijana msione vichaka tu tayari." Mzee Malick alimjibu Wayaki. 

"Aaahh bosi maneno gani hayo tena mimi sikuwa na maana hiyo hata kidogo nilitaka kujua tu." Wayaki alimjibu bosi wake baada ya kuona anaingiza maneno ya utani lakini yakiwa na maana fulani. Wakiwa wamekolea kwenye mazungumzo gari lilikuwa likiacha barabara kuu na kuingia barabara ya vumbi ambayo ilikuwa ni chakavu na ikionesha hakuna magari ambayo huingia kule mara kwa mara. Na baada ya mwendo kama wa kilometa saba hivi waliwasili kwenye eneo lililokuwa na mashamba lakini yakiwa ni kama vile ya mtu mmoja kwa sababu hakukuwa na mashamba mengine jirani zaidi ya lile lililokuwa limeizunguka nyumba ambayo bati lake lilikuwa limechoka kiasi. Mpaka wakati huo Catherine hakuwa akijua chochote kilichokuwa kikiendelea kwani alikuwa bado kazimia.

"Mshusheni huyo mwanaharamu na mpelekeni waliko wenzake." Mzee Malick aliongea akishuka garini na kuelekea ndani. Catherine alishushwa na Majura alimbeba peke yake na kumpeleka kwenye chumba cha giza kilicho ndani ya ile nyumba kama mzee Malick Bolenge alivyoagiza. Lakini wakati hayo yakiendelea pale, nje kidogo ya lile shamba kulikuwa na watu waliokuwa wakifuatilia kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Na hakuna hata mmoja miongoni mwa watu wa mzee Malick aliyeweza kushtukia hilo na watu hao hawakuwa wengine zaidi ya Seynabou mtoto wa marehemu mzee Alioune aliyekuwa mganga wa Mchungaji Rodney akiwa sambamba na kijana wa Kichad ambaye historia yake kidogo siyo nzuri kutokana na maisha aliyoishi huko nyuma kabla ya kukutana na Mchungaji Rodney pamoja na mke wake Bi Catherine ambapo baada ya kumfanyia darasa maalum la Saikolojia ambalo lilimsaidia kwa kiasi kikubwa na hapo ndipo alipopewa kazi ya ulinzi nyumbani kwa Mchungaji Rodney. Hawakuwa peke yao bali walikuwa na kijana mmoja mwenye asili ya Kiarabu aitwaye Awadh na huyu ndiye aliyekuwa akilifukuzia gari la wakina Majura na hii ni baada ya kupewa ujumbe na Catherine walitafuta msaada wa haraka kuhakikisha wanamuokoa bosi wao na hapo ndipo walipokutanishwa na kijana huyo ambaye ni fundi Bajaj na Pikipiki, baada ya kuwafukuzia na kuhakikisha sehemu walipoingia waliamua kutafuta njia ya kuwafikisha pale bila kuonekana. Ndani ya nyumba ile mzee Malick Bolenge na kundi lake walikuwa kwenye mazungumzo huku Jumbe na wenzake wakiwa hawaamini macho yao kumuona bosi wao kwenye hali ile ya kutojitambua.

"Hivi kaka Jumbe tutatoka salama hapa kweli ikiwa tuliyekuwa tunamtegemea kaletwa akiwa hajitambui kiasi hiki sijui kafa au mzima?....." Kabla hajamaliza kuongea kauli yake Jumbe alimtandika kibao yule kijana.

"Unaongea nini wewe? Hivi unafikiri ni muda wa kuongelea hayo?" Jumbe alimuuliza.

"Nisamehe kaka nimetokwa tu na maneno haya." Kijana huyo alimjibu.

"Okay nimekuelewa, kitu cha msingi hapa ni kuangalia tunajinasuaje kwenye mtego huu tulioingia bila kutarajia." Jumbe aliwaambia wenzake huku akimuangalia Catherine aliyekuwa chini hajitambui.

"Mhh mmhh mhhh...." Catherine alizinduka lakini akili haikuwa sawa ni kama alikuwa akiota hivi.

"Haa haa kaka Jumbe bosi Catherine kazinduka!!" Aliongea kijana mwingine aliyekuwa kimya muda wote wakati Jumbe akifokeana na mwenzake.

"Mathew na Soud nisikilizeni vizuri wadogo zangu, sisi ndiyo tuliosalia hapa ngomeni si mnamkumbuka yule mzee aliyetekwa pamoja nasi namna alivyouawa bila huruma? Na sasa tegemeo letu liko hapa pamoja nasi hivyo tukilaza akili tumekwisha." Jumbe aliwaambia wenzake.

" Mjomba, mjomba mbona unamuangalia tu huyu kijana? Au umeridhika na ninavyofanyi.... " Kabla hajamaliza alishtuka na kuanza kuangalia huku na kule mle ndani.

" Nimefikaje hapa na ninyi ni wakina nani?" Catherine aliwauliza wakina Jumbe.

"Sisi ni wakina nani?" Jumbe alimuuliza.

"Mhh wewe ni...."

"Mimi ni Jumbe au umenisahau?" Alimuuliza.

"Ndiyo kusema nimetekwa? Jumbe hebu niambie hapa nimefikaje?" Catherine aliuliza baada ya akili yake kuanza kukaa sawa na kuwatambua vijana wake.

"Tusipochukua tahadhari mapema bosi wetu hawa watu wanakwenda kutuulia mbali." Matthew aliongea akijivuta mbali na Jumbe.

"Nisikilizeni vijana wangu, mtengeneza hii filamu nimemfahamu tayari lakini msiwe na mashaka tunatoka salama kikubwa mimi nitaendelea kujifanya bado sijazinduka ili kuvuta muda mnanielewa?" Catherine aliwaambia wakina Jumbe na wakati huo huo mlango ulianza kufunguliwa, Catherine alijilaza vile vile kama awali.

" Toka nje ninyi, fanya haraka!!" Mmoja wa vijana wa mzee Malick aliwaambia wakina Jumbe ambao bila kubisha waliinuka na kuongoza nje na kumuacha Catherine pale chini huku yule kijana akiinama kumuangalia Catherine kama kuna dalili zozote za matumaini na baada ya kubaini hakuna aliinuka na kutoka nje na kuufunga mlango ambapo alikwenda mpaka walipokuwa wakina Jumbe na kuanza kuwasurubisha kwa mijeredi.

"Hapa mtaongea tu hata mjidai ni mabubu kiasi gani, najua mnaelewa ni wapi ulikotunzwa mzigo." Mzee Malick aliwaka kama Mbogo huku akiwatandika yeye mwenyewe.

"Kwanza kwanini nitoe mijasho ilhali vijana wangu mpo hebu walainisheni mbwa koko hawa mpaka waongee walikohifadhi mzigo." Mzee Malick aliwaamrisha wakina Wayaki kuwashughulikia vilivyo wakina Jumbe ambao walikuwa wamefungwa kwenye mti.

"Sawa bosi." Walijibu.

"Mkuu nakuhakikishia sisi hatujui huo mzigo uko wapi na wala hatuujui hata ulivyo." Jumbe alijitetea mbele ya sura ya mzee Malick iliyokuwa imefura kwa hasira.

"Unasemaje weweeee? Unathubutuje kuongea na mimi maneno ya kichawi kiasi hicho? Na kwanza eleweni kuwa mimi siyo bosi wenu au mnanifananisha na huyo Pimbi wenu?" Mzee Malick alimwambia Jumbe kisha alimtemea mate usoni na kuondoka zake.

"Wewe mshenzi umeona ulivyomuudhi bosi? Sasa leo mtatutambua vizuri." Kijana mmoja aliongea hayo na kuanza kuwatandika mijeledi bila mpangilio hakuangalia ni wapi awapige au wapi awaache yeye alikuwa akiwashushia mijeledi tu.

"Hivi ninyi mnacheza na akili yangu? Mmempeleka wapi huyu Nyambuda? Nawauliza ninyi hapo mbona mmenitumbulia mimacho, nataka majibu haraka." Mzee Malick alitoka macho yakiwa yamemtoka pima kama vile kapewa taarifa ya kurejea kwa duniani kwa mtu ambaye alifariki kitambo na hii ni baada ya kuingia kwenye chumba ambacho alihifadhiwa Catherine na kutomkuta zaidi ya dirisha kuvunjwa. Maneno yale ya mzee Malick yaliwatoa pale vijana wake na kuelekea mle ndani kuhakikisha kama kweli hakuwepo ndani.

"Buushiiiiit...... Kavunja dirisha na kutokomea, Haraka poteeni mkamtafute huyu Mbagdad kabla hajavuka msitu huu." Wayaki aliwaamrisha wenzake huku yeye akirejea kwa bosi wake ambaye muda huo alikuwa akienda mbele mara nyuma mara akae mara akune kichwa kwani ni tukio ambalo hakulitarajia ukizingatia mtu mwenyewe alikuwa kazimia hivyo hawakumtilia maanani sana zaidi ya wakina Jumbe.

"Enhh mmempata?" Alimuuliza Wayaki.

"Hapana bosi ndiyo wamekwenda kumsaka." Wayaki alimjibu.

"Unasemaje wewe? Eti wamekwenda kumchaka kumchakaaaa na wewe unafanya nini hapa?" Aliyarudia maneno ya Wayaki akiwa kaibana pua yake.

"Nakwenda bosi." Wayaki alimjibu na kuondoka.

"Mnanijua vizuri sana na ole wenu mrudi mikono mitupu mtanitambua." Mzee Malick aliongea akiwageukia wakina Jumbe waliokuwa wamepigika vilivyo pale mtini.


JE NI NINI KITATOKEA HUKO PORINI KATI YA CATHERINE NA MJOMBA WAKE?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


#SULTANUWEZO 

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post