MUUAJI MWENYE BARAKOA - 22
sultanuwezotz.blogspot.com
Walikaa mezani na kuanza kupanga namna watakavyoingia pale kwa tahadhari kubwa. Kitu kilichokuwa kikiwaumiza kichwa ni Hotel hiyo ina ulinzi gani. Hivyo walituliza akili kuhakikisha hawafanyi makosa ya kijinga kama yaliyotokea nyumbani kwa mzee huyu.
"Awadh unaonaje ukimpigia simu Seynabou atueleze wako kona gani ya mjengo huo?" Soud alitoa wazo.
"Kweli aise hebu mcheki kama anapatikana anaweza kutupa mwanga kidogo." Adoyee aliunga mkono hoja ya Soud. Kabla Awadh hajajibu chochote mara ujumbe uliingia kwenye simu ya Awadh iliyokuwa mezani na kumfanya kuufungua haraka ili ajue nini kimetumwa na Seynabou ambaye jina lake lilionekana.
" Mathew hafahamiki aliko ila mimi na Jumbe tumekutana kwenye chumba cha kuhifadhia vifaa mbalimbali, msaada tafadhali." Awadh aliwatazama wenzake kisha akawaeleza kilichoandikwa na Seynabou.
"Hebu ujibu huo ujumbe, muulize hicho chumba kiko upande gani wa Hotel ili tukifika tujue tunaelekea wapi." Adoyee alimwambia Awadh ambaye hakusubiri alifanya kama Adoyee alivyoshauri na ndani ya muda mfupi ujumbe ulijibiwa.
"Kinatazamana na vyoo vya nje vya Hotel, mkifika mtauona mpera ulipo sisi tuko ndani ya chumba hicho." Awadh aliusoma ujumbe ule kisha akampa simu kila mmoja ausome kwanza kisha wafanye maamuzi.
"Hakuna cha kusubiri tuchukueni zana tuelekee eneo la tukio upenyo umeshapatikana." Awadh aliongea akiwaangalia wenzake. Walichukua kila zana ambayo walihisi itakuwa msaada hasa ukizingatia begi la Catherine lilikuwa limesheheni kila kitu hivyo haikuwa tabu kwao.
" Si kila kitu kiko sawa?"Awadh aliuliza.
" Tuko sawa." Alijibu Adoyee. Walitoka na kuingia kwenye gari kisha wakaianza safari ya kuelekea TRAVIS MARK HOTEL tayari kwa kuwaokoa wenzao. Awadh katika kuonesha barabara za ndani ya jiji anazifahamu vilivyo aliingia za mtaani kitendo kilichowafanya wenzake kujiuliza maswali ambayo hayakuwa na majibu.
"Awadh barabara gani hizi za mitaani utagonga watu bwana na mwendo wako wa ajabu." Soud kama kawaida yake aliona aulize baada ya kuona wanapita barabara ambayo si rafiki kwa mwendo aliokuwa akienda Awadh. Lakini Awadh hakumjibu chochote badala yake alikuwa akitabasamu tu huku mikono ikipishana kwenye usukani.
Na baada ya kama dakika thelathini gari lilikuwa likiingia kwenye uchochoro uliokuwa na makazi chakavu ya watu ambayo yalionekana kukaliwa na watu wenye hali duni kwa namna walivyoonekana na hata namna majengo yalivyokuwa yamechoka huku milango michache ikiwa na milango huku mingine ikiwa ya imesitiriwa kwa vipande vya nguo na mikeka chakavu, hali ile iliwashangaza sana wakina Adoyee.
"Awadh vipi huku?" Adoyee alimuuliza Awadh aliyekuwa akishuka garini.
"Historia ya eneo hili nitawaeleza ndugu zangu ila kwa ufupi nimeona tupitie huku kwa usalama wetu sisi kwani watu wa huku ni wasiri sana ukichangia chochote." Awadh aliwaondoa hofu wenzake na wakati huo alikuwa akitoa ishara ya kumwita mzee mmoja aliyekuwa akiponda vyuma kando ya barabara chini ya mti wa mwembe.
" Ebwana ee kweli tembea uone." Soud alishangaa.
" Kijana wangu umekuja tena?" Mzee huyo alimwambia Awadh wakati akikumbatiana naye ilionesha wazi wanajuana.
"Ndiyo mzee wangu si unajua tena." Awadh alimjibu.
"Naona uko na sura mpya kwenye ardhi yetu umewatoa wapi?" Mzee huyo aliuliza.
"Hawa ni rafiki zangu huyu ni Adoyee na huyu huku ni Soud kwa umoja wetu ni timu mpya."
"Waoo bila shaka wataziba pengo la marafiki zako ambao mlishibana kupita maelezo." Mzee huyo ambaye alionekana ni maneno mengi aliongea akiwasalimu wakina Soud.
"Ni kweli mzee wangu, sasa mzee Jeremia tunaacha gari letu hapa tunaingia mtaa wa nyuma yako tunageuka sasa hivi." Awadh alimwambia mzee huyo.
"Mhh hebu ngoja kwanza, mtaa wa nyuma kuna nini usinifiche kitu huwezi jua Awadh naweza kuwa msaada wenu." Mzee Jeremia aliuliza.
"Kuna wenzetu wanashikiliwa ndani ya Hotel ya TRAVIS MARK."
"Malick kaanza mambo yake ya zamani?" Mzee Jeremia aliuliza.
"Tutaongea nikirudi mzee wangu huyo ndiyo mzee mwenzako bwana." Awadh alimjibu akimkabidhi funguo ya gari.
"Kuweni makini na hatua zenu Malick si mtu mzuri." Mzee Jeremia aliwapa tahadhari akirudi kwenye shughuli zake. Waliachana na mzee Jeremia wakaingia kwenye kinjia kilicho katikati ya nyumba mbili ambacho kiliwapeleka mpaka upande wa nyuma huko walipandisha kimuinuko kidogo mpaka eneo lililo la wazi ambalo hutumiwa kama uwanja wa mpira kutokana na magoli yaliyokuwa yamewekwa japo ni ya miti iliyopinda.
"Kweli huku uswahilini du!" Adoyee aliongea wakikatisha uwanjani hapo.
"Wewe ulifikiria nini ulipoambiwa Afrika ni moja?" Awadh alimuuliza.
"Kutokana na rangi yetu ya ngozi wala sikuwaza upande wa pili kama kuna maajabu kama haya." Adoyee alimjibu.
"Haya jamani Hotel yenyewe ndiyo ile pale chini." Awadh aliwaonesha jengo jeupe na ambalo lilikuwa refu kuliko mengine pale chini.
"Kumbe huyu mshenzi siyo mtu wa mchezo ee? Kumiliki mjengo kama ule lazima uwe na mkwanja wa kutosha eti." Soud aliongea baada ya kuliona jengo hilo.
"Ni hivi, nilitaka tutokee nyuma ambako kuna vyoo ili iwe rahisi kuingia nina uhakika macho na akili zao wataelekeza eneo la mbele zaidi huku wengine wakiwa bize kuwatafuta wakina Seynabou hivyo itakuwa rahisi kwetu kuingia ndani na kufanya kazi yetu." Awadh aliwaelekeza wenzake kile anachokijua kutoka kwenye jengo lile.
" Na wakati huo huo kumbukeni kuwa ile ni Hotel hivyo hawawezi kusimamisha shughuli nyingine kwa ajili ya hili, ni lazima watakuwa wanafanya hili kwa uficho kidogo." Awadh aliendelea kuwapa moyo wenzake ambao walikuwa wakimsikiliza yeye japo Adoyee alifika mahali hapo akiwa na wakina Catherine lakini siyo kwamba ni mwenyeji wa mazingira.
" Tumekuelewa Awadh tusipoteze muda wasije kuwaotea walipojificha." Soud alimjibu.
"Okay twendeni sasa hakikisha mkononi una zana ambayo wapita njia hawaioni."
"Wala usijali kiongozi." Adoyee alimjibu wakati wakishuka kimtetemko. Lakini hawakuvuta hata hatua saba mbele kulisikika milio ya risasi kutoka ndani ya Hotel kitu kilichowafanya wasambae kulia na kushoto tayari kwa mashambulizi.
***
Mchungaji Rodney aliendelea kutambulishwa kwenye makanisa yaliyo ndani na nje ya jiji la Mbeya na kazi hiyo ilikuwa ikifanywa na mwenyeji wake Daktari Sylvester Kitesa kwa ushirikiano mkubwa na timu maalum iliyokuwa chini ya Mchungaji Zebedayo Mwakanyasi. Na safari hii walikuwa wilayani Kyela katika eneo la Ipinda mahali ambapo ndiyo kuna kanisa lao lililo chini ya huduma ya Mchungaji Simon Mwaiduko ambaye ndiye Mchungaji kijana kuliko wote ndani ya Makanisa hayo ndani na nje ya Tanzania kitu ambacho kilimshangaza sana Mchungaji Rodney na kupelekea kutaka kumfahamu zaidi Mchungaji huyu.
"Mzee wangu huyu Mchungaji mbona bado mdogo sana ataweza kuhimili wishawishi kutoka kwa kondoo wake?" Mchungaji Rodney aliuliza wakati huo Mchungaji Simon Mwaiduko alikuwa akihubiri.
"Ni mwaka wa tatu toka tumkabidhi kijiti hiki ambacho kiliachwa na Mchungaji wetu mzee Abiud Taifa aliyefariki kwa ajali ya gari miaka mitano iliyopita na toka tumkabidhi pamoja umri wake mdogo lakini amekuwa Nembo ya Kanisa kwa Tanzania akiwa ndiye Mchungaji aliyeongeza idadi ya Waamini kwa asilimia Mia moja Sitini zaidi ya waliokuwepo awali hivyo ana sifa zote hayo mengine hatuombei yamtokee kijana wetu." Daktari Sylvester Kitesa alimjibu Mchungaji Rodney.
" Okay kumbe yuko vizuri sana na kama ulivyosema mzee kubwa ni kuelekeza maombi kwake kila wakati ili asimame mahali pake bila kuvutwa na Shetani ambaye ametuandama sana Watumishi wa BWANA."
" Hilo ndilo la kuomba kwa sasa." Daktari Sylvester Kitesa aliongea akiinua glasi ya maji.
Waliendelea kuyasikiliza Mahubiri ya Mchungaji Simon Mwaiduko ambaye alikuwa akishangiliwa kila wakati.
" Bwana Yesu asifiweee."
" Ameeeen." Waumini waliitikia huku wengine wakiinuka na kurukaruka juu kitu kilichoendekea kumshangaza sana Mchungaji Rodney.
"Najisikia furaha sana kuwa mbele ya Madhabahu hii ambayo kwangu imekuwa Baraka kubwa sana lakini zuri zaidi ni hili la kutembelewa na Kiongozi wetu mkuu Baba Kiongozi Daktari Sylvester Kitesa kutoka makao makuu Mbeya akiwa sambamba na Mchungaji Rodney Hauser kutoka nchini Senegal, hebu shangilia kwa bwana tafadhali."
Kanisa zima lilizizima kwa shangwe baada ya kusikia maneno hayo kutoka kwa Mchungaji wao kipenzi.
" Hivyo basi naomba nichukue fursa hii kumkaribisha baba kiongozi Daktari Sylvester Kitesa aweze kuwasalimu na kisha atamkarubisha Mchungaji Rodney Hauser kwa neno fupi, karibu baba." Mchungaji Simon Mwaiduko alimkaribisha Daktari Sylvester Kitesa.
" Mna Amaniii." Mzee Sylvester Kitesa alianza.
" Ndiyoooo."
" Basi nisikie kelele za shangwe na vifijo." Kilichotokea baada ya kusema hivyo yeye mwenyewe alibaki kushangaa kwani ilikuwa ni zaidi ya shangwe.
"Bwana Yesu asifiweee..." Daktari Sylvester Kitesa aliongea huku akirukaruka.
"Ameeeen..." Waliitikia.
"Hakika nimemuona bwana kwenye Madhabahu haya ya kijana wangu Simon Mwaiduko." Daktari Sylvester Kitesa aliongea akifuta kijasho kilichokuwa kikimtiririka usoni.
"Ameeeen...." Waliendelea kuitikia.
"Naweza kusema kijana wangu umekua sasa, nakuombea kwa Mungu uzidi kukua ili injili isonge mbele na Shetani azidi kuwa mtazamaji kupitia wewe. Na naomba niwaache kwa neno hili kutoka (Mithali 3 : 5-7) Maneno yanasema kuwa; 5 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe. 6 Katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyosha mapito yako. 7 Usiwe mwenye hekima machoni pako, mche Bwana ukajiepushe na uovu. Ameeeen." Daktari Sylvester Kitesa alimaliza.
" Ameeeen... " Waliitikia.
" Basi nichukue fursa hii kumkaribisha Mchungaji wetu mgeni kutoka nchi ya Senegal aweze kuwasalimia, karibu Mchungaji." Daktari Sylvester Kitesa alimkaribisha Mchungaji Rodney Hauser lakini cha ajabu alikuwa bize kwenye simu jasho likimtoka na kabla Daktari Sylvester Kitesa hajasema chochote Mchungaji Rodney Hauser alikwenda ndani na kuzimia. Kitendo kile kilipelekea taharuki ndani ya Kanisa huku kila mmoja akibaki kushangaa nini kilichomkuta Mchungaji Rodney Hauser. Haraka sana wazee wa Kanisa walimzunguka Mchungaji huku wengine wakiwarudisha kwenye viti waumini.
"Naombeni tutulie kwenye viti wakati wazee wetu wakiendelea kuliweka sawa hili lililotokea hapa, Bwana asifiweee...." Mchungaji Simon Mwaiduko aliwatuliza waumini wake huku Daktari Sylvester Kitesa kwa kushirikiana na viongozi wa Kanisa hilo kuhakikisha hali ya Mchungaji Rodney Hauser inakuwa sawa na pamoja na hilo lakini pia aliokota ile simu na kuangalia kilichomfanya apoteze fahamu.
"Ooh nooo!! Catherine yuko hai? Ina maana gani hii?" Daktari Sylvester Kitesa alijisemesha mwenyewe akipandisha ngazi kwenda chumba cha maombi cha Kanisa hilo.
JE NI NINI KITATOKEA KATIKA KITIMUTIMU HIKI?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
#SULTANUWEZO