NITAKUUA MWENYEWE - 16 (Mtunzi: Sultan Uwezo)



 NITAKUUA MWENYEWE - 16

sultanuwezotz.blogspot.com


Zoezi la kupita na gari ile kwenye tope liliweza kufanikiwa na safari iliweza kusonga mbele huku hofu ikitawala kwa kila mmoja kwani kwa muda huu walikuwa wakielekea Antonios pasipo kuwa na mwenyeji wa kuwaonesha baada ya dereva wa taxi ile kujidai mjuaji na kuambulia kifo. Lakini kwa kuwa tayari walikuwa wameyavulia nguo maji walijipa moyo na kuamini watasonga na kufika mwisho wa safari na hatimaye kupaa angani kuelekea Afrika salama kabisa.

"Hivi tutafika town bila kukutana na kikwazo njiani kweli?"

Robinson aliwauliza wenzake.

"Kwa maelezo ya yule dereva ni kwamba barabara hii huwa haifuatiliwi sana hivyo tunaweza kutoboa bila tatizo."

Jackline alimjibu huku gia zikiendelea kukanyagwa na Jasmine.

"Ila tunatakiwa kuwa na tahadhari." Robinson aliwatahadharisha wenzake.

"Ni kweli kabisa na ninafikiri hiki kigari tutakiacha mara baada ya kuingia tu mjini na uzuri itakuwa bado usiku itakuwa afueni kwetu."

Jackline alitoa wazo ambalo kila mmoja alilikubali.

Hivyo safari iliendelea na muda huu baridi nayo ilianza kuwa kali zaidi hali ambayo ilianza kuwatisha kwani kulikuwa na kila dalili ya mvua au ukungu na giza lilikuwa ni la saa tisa.

Mara wakiwa wameanza kuyaona mataa ya mji wa Antonios gari ilizima ghafla.

"Vipi mbona unasimamisha gari eneo hili?"

"Nahisi ni wese maana limekata moto lenyewe ghafla."

Jasmine aliwaeleza wenzake na hapo ndipo wakajua muda wa kudakwa umefika maana walipoangalia mbele waliweza kuona jiji la Antonios kwa mbali kiasi kwamba namna ya kulifikia ikawa ndiyo mtihani.

"Jamani ndiyo hivyo tena mafuta yamekwisha na hakuna ya ziada tunafanyaje hapa?"

Jackline aliwauliza wenzake juu ya kilichowakuta.

"Mimi nafikiri hakuna cha ziada zaidi ya kulitelekeza hili gari hapa hapa na tuanze mdogo mdogo mpaka tutakapofika mjini."

Jasmine aliwataka wenzake waianze safari pasipo kuangalia kuna umbali gani kutoka pale walipo.

"Najua tutachoka lakini hatuna jinsi jamani safari ianze au?"

Jessica aliona kama vile muda unachelewa akaona awatake safari ianze mara moja.

"Ni kweli jamani tunatakiwa kuanza safari maana mwenzenu nina hofu na hao jamaa wakitufuma hapa sijui itakuwaje?" Robinson alionesha hofu yake.

Safari ilianza na wakaona ili wafike salama inatakiwa wapite porini nje kidogo ya barabara kikubwa wasiiache barabara. Na msitu ulikuwa ni mnene kiasi kwamba kama ni muogaoga huwezi pita pori hilo.

"Mungu wangu hivi tutatoka salama kweli kwenye hili pori?"

Robinson aliuliza swali.

"Jamani tupunguze hofu kwanza ili tuweze kuvuka hili pori ila tukitanguliza hofu tu tutaishia humu."

Jasmine aliwataka wenzake waondoe hofu kwanza ili kuvuka msitu huo.

"Tukazeni buti jamani kwani hofu yangu mwenzenu ni juu ya maadui zetu."

Jessica aliona atoe lile linalomtia hofu katika safari yao.

Waliendelea na safari ya kupambana na msitu huo ambao walikuwa wakiangalia mbele ilikuwa ikiwatia moyo kutokana na mji wa Antonios kuonekana japo ilikuwa bado ni mbali kwa mguu. Wakiwa wanapita kwenye miti fulani ambayo ni mirefu sana karibu kabisa na barabara mara waliona gari likija nyuma yao, na hapo Jessica akatoa pendekezo la kulipiga mkono gari hilo walau liwasogeze kilometa kadhaa mbele.

"Gari hiyo inakuja mnaonaje tuisimamishe tuombe msaada wa kusogezwa walau umbali fulani."

"Tusijiingize kwenye mdomo wa Mamba hapa kumbukeni tunatafutwa kila kona na hofu yangu hata Santana atakuwa hajakata tamaa juu yetu hivyo umakini unatakiwa." Jackline alishauri wawe makini na maamuzi yao.

Lakini wakati wanaendelea kushauriana juu ya kuchukua tahadhari kwa kila wanaloamua. Ila waliposikiliza vizuri mlio wa hilo gari wakabaini kuwa halikuwa gari la kawaida bali lilikuwa ni gari kubwa.

" Jamani hilo ni gari kubwa la mizigo mnaonaje tulisimamishe?"

Robinson aliwauliza wenzake.

"Kama ni Lori tujitokezeni hilo ni salama ila lingekuwa ni gari dogo ingekuwa shida."

Jasmine aliunga mkono na hivyo walijivuta mpaka barabarani na kukaa kandokando wakisubiri hilo gari lifike waombe msaada.

"Hivi itakuwaje iwapo tutalisimamisha hilo Lori kumbe ni la Wanajeshi?"

Jackline aliwauliza wenzake japo ilikuwa kama utani hivi.

"Hivi Jackline mkono kwa sasa unauonaje?" Ilibidi Jasmine apotezee kwa swali maana aliamini kuacha swali hilo lijadiliwe lingeleta hofu kati yao na kupelekea kurudi porini wakati naye alikuwa anajikaza tu ila alikuwa kachoka.

"Kiukweli nashukuru Mungu naendelea vizuri tofauti na mwanzo ilivyokuwa."

"Jambo jema hilo na la kuangalia hapo ni kutokuugongesha na kuibua upya tatizo." Robinson alishauri.

Gari lilifika na Jessica aliibuka barabarani na kusimama katikati na kupunga mikono kuashiria kulisimamisha na lilipofika kama bahati lilisimama na ndipo Jessica alizunguka upande wa dereva ili kuongea naye.

" Habari yako kiongozi? "

"Salama binti mbona porini muda huu?"

"Sisi ni wanafunzi wa Chuo tulikuwa kwenye utalii katika mapango ya Nangiz na huko tukakutana na majinamizi yaliyopelekea kila mmoja kushika njia yake na sisi tuliokimbilia eneo moja ndiyo tunatokea barabarani muda huu."

"Poleni sana mko wangapi?"

"Tuko watu wanne tu."

"Okay hebu waite wenzako pandeni twende japo mimi sifiki mjini."

"Tutashukuru hata kwa hapo utakapotufikisha mzee wangu."

Hivyo Jessica aliwaita wenzake na kupanda nyuma kwenye magogo kwani mbele isingewezekana kutokana na gari hilo kuwa na siti ya dereva tu. Walipopanda dereva alishuka na kuja kuwaangalia kama tayari.

" Vipi tayari wote mmepanda?"

" Ndiyo mzee tayari." Jessica alijibu.

Na ndipo dereva huyo akiwa na sigara yake mdomoni alirudi kwenye usukani na kung'oa nanga.

"Kasema yeye hafiki mjini kuna sehemu atachepuka inaonekana kuna sehemu nje ya mji anajishughulisha na shughuli fulani hivi kutokana na magogo aliyobeba." Jessica alifungua mjadala kwa wenzake.

"Hapa tuwe makini sana na tena ikiwezekana kabla ya hajatushtukia inatakiwa turuke na kupotea zetu atakapokuja kuangalia hakuna watu."

Jackline aliwatahadharisha wenzake.

"Hiyo ni plani nzuri sana ila tatizo ni wapi anachepukia hatujui hivyo bado tu itakuwa ngumu kwenye mpango huo."

Jasmine alikubaliana nao lakini akaonesha hofu kutokana na kwamba si wenyeji na maeneo hayo na hawajui huyo mzee anachepukia wapi.

"Kwa hapo hatuna ujanja inatakiwa tuwe wapole tu liwalo na likawe kikubwa ni kujiandaa kukabiliana na lolote ndugu zangu." Jessica aliongea.

Baada ya umbali fulani hivi mwanga wa mashariki ulianza kuonekana kwa mbali kuashiria tayari jua linakaribia kutoka na kulitaka giza kuupisha mwanga nao uweze kutawala. Na hapo wakaona gari linapaki pembeni hali hiyo iliwapa hofu na kutaka kuruka na kukimbia lakini wakashauriana kutulia kwanza kujua kuna nini na walipochungulia chini walimuona dereva akipata haja ndogo na kisha akawa anakuja kule nyuma.

"Inawezekana kafika sehemu ya kuchepukia."

Jessica aliongea alipoona anakuja kule nyuma.

"Ngoja tumsikilize mwenyewe."

Robinson aliwauliza wenzake.

Na baada ya kufika pale nyuma dereva aliwataka washuke chini, na waliteremka na kumfuata alipokuwa. Aliwaangalia kwa muda kisha akageuka kuangalia pande zote kama vile ana hofu na kitu fulani hivi. Kitu kilichowapa hofu wakina Robinson kwamba kuna nini au mzee huyu amewatambua na anataka kuwakamatisha kwa maadui, hapo ikabidi Jackline ajitose kuuliza kabla mzee hajafanya lolote.

"Mzee vipi umefika sehemu ambayo unatakiwa kuchepukia?"

"Hapana bado kabisa."

"Kwa hiyo kuna nini mbona umetushusha na unatuangalia tu kama kuna kitu unasubiri hivi."

"Ni kweli kabisa binti nimefanya hivi baada ya kugundua utambulisho wenu kuwa ninyi si wanachuo bali ni watu hatari sana mnaotafutwa na jeshi la Ulinzi la Belem. Na muda si mrefu wametoka kuongeza zawadi kwa atakayefanikisha kuwatia nguvuni."

Maneno hayo ya mzee yaliingia vilivyo kwenye ngoma za masikio ya akina Jessica wakatazamana usoni kwamba nini kifanyike kwa mzee huyo na kabla hawajajua wamfanye nini dereva huyo, walikuwa wamechelewa kwani tayari alikuwa ameshamkata mtama mzee wa watu na kutua chini kama furushi la pamba.

"Mzee hujakosea kabisa sisi ni watu hatari sana na kwa kuwa umetufahamu lazima ufe."

Robinson aliongea naye akiwa ameshamtia kabali takatifu iliyomfanya mzee kutoa macho kama vile kamfumania mke wake.

"Lakini mzee bado una nafasi ya kutusikiliza kwanza inawezekana ukawa umepata taarifa zisizo sahihi juu yetu mzee hivyo ni wewe kutusikiliza yaliyotusibu kwanza kabla ya kutukabidhi kwa hawa wanaotutafuta au na sisi tukuue katika kujitetea mbele ya mkono wa sheria."

Jackline alikuwa kapiga magoti kumuelekea mzee pale alipokuwa kalazwa na Robinson.

" Naombeni mnisamehe bado napenda kuishi, kuna familia inanitegemea naombeni muongozane nami kwangu huko nadhani mtanieleza kila kitu kilichowakuta na ikiwezekana tutaangalia tunafanyaje maana hamuwezi kwenda kokote kule mnasakwa kama rupia wanangu."

"Tutakuamini vipi kwa haya uyasemayo?"

Jasmine alimuuliza.

"Niliwatambua toka mliposimamisha gari lakini niliamua kuwasaidia tu ila hapa nilitaka kujiridhisha kama ni ninyi kweli."

"Haya inuka utakuwa na mmoja wetu kule mbele japo hakuna siti atasimama."

Robinson aliongea kwa ujasiri mpaka Jackline alitabasamu kitu ambacho hakuamini kutokana na uoga aliokuwa akiuonesha siku za mwanzo.

"Nitakaa naye mimi ninyi pandeni, mzee twende."

Jackline aliona yeye ndiyo akakaye naye kule mbele ili akileta kujua aweze kumfundisha adabu. Walipanda na safari ikaanza tena baada ya kupata jamu isiyo rasmi.


Nini kitaendelea?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


      #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post