NITAKUUA MWENYEWE - 17 (Mtunzi:Sultan Uwezo)

 


NITAKUUA MWENYEWE - 17

sultanuwezotz.blogspot.com 


Baada ya masaa kadhaa waliwasili kwenye kambi moja ambayo ndani yake ilionekana kama kulikuwa na shughuli nyingi kama vile ni uzalishaji nguvu fulani au ni machimbo ya madini fulani hivi, kifupi lilikuwa ni eneo ambalo ni kama kambi fulani yenye kila aina ya mateso ndani yake. Lililowashangaza wakina Jackline ni wakati wakiingia ndani ndani ya Ngome watu wote waliacha shughuli zao na kukimbilia kwenye eneo ambalo lilionekana ni paredi hivi maana walijipanga kama vile wanajiandaa kuimba wimbo wa Taifa. Na mara gari liliposimama tu lile kundi lilipanga mstari mmoja kutoka kwenye gari lile na kuelekea ndani ya jengo fulani lililokuwa likitoa moshi kwa juu. 

"Mwanangu tumefika tayari ngomeni tushuke sasa." 

"Mbona kuko hivi na hawa watu mbona wamejipanga hapo chini?" 

"Ni tayari kwa ajili ya kushusha magogo hayo tuliyobeba." 

"Wote hawa ni wafanyakazi wako mzee?" 

"Ndiyo mwanangu na hao unaowaona ni wachache tu kwani wengine wako mashambani huko wakilima." 

"Unawalipaje wote hawa mzee mbona ni kundi kubwa sana?" 

Mzee yule alimpigapiga bega Jackline na kumwambia asiwe na haraka sana kwani kuna mambo mengi sana na ya kustaajabisha sana ambayo akitaka kuyajua yatachukua miaka kadhaa kupata ufafanuzi wake. Hivyo alimtaka washuke chini ili kutoa nafasi kwa wafanyakazi kushusha magogo kwani walikuwa wakisubiri oda yake. Walishuka chini na mzee aliwasalimu kwa kuinua kofia yake na kundi lote liliinamisha vichwa chini ikiwa ni ishara ya kutoa heshima kwa mkuu wao. 

Tendo lile kumbe hata wakina Jessica, Jasmine pamoja na mbabe wa vita Robinson liliwashangaza sana mpaka kuanza kuhisi kuwa walikuwa wamejipeleka wenyewe kwenye kambi ya mateso bila kujua. 

"Hali ya humu ndani mnaionaje wenzangu?" 

Jasmine aliwauliza wenzake baada ya kumuona Jackline akiwa sambamba na mzee yule kama kuna kitu anadadisi hivi. 

"Hapa sielewi chochote kile maana kama vile niko ndotoni labda tumsubiri Jackline atuambie kinachoendelea humu." 

Jessica alijibu huku akionekana kama kupata hofu hivi na hii ni kutokana na watu waliokuwa wakipita mbele yao na magogo mabegani afya zao zilikuwa zimedhoofu sana huku harufu mbaya ikitembea nao. Hapa walihisi hatari iliyokuwa mbele yao kwani hawakuona upenyo ambao unaweza kuwatoa mle ndani. Na mara alikuja kijana mmoja ambaye alikuwa kashiba sawa sawa akiwa na silaha begani ambayo ilifanana na old gun' maarufu kwa jina la Gobore. 

"Habari yenu wakubwa!!" 

"Kama utuonavyo." Alijibu Robinson. 

"Karibuni ngomeni." 

"Tumekaribia." Jasmine alimjibu kwa mkato. 

"Okay sawa, mkuu anawaita kule juu." Aliwajulisha kuwa wanaitwa na mkuu wao huku akionesha uelekeo aliko huyo mkuu wao lakini kilichowashangaza ilikuwa ni kule kule alikoelekea Jackline na yule mzee. Walitazamana wote kisha yule mlinzi na ndipo Jessica alipomjibu. 

" Okay tunashukuru, tunaelekea." 

Yule mlinzi aliondoka na kuwaacha wakiwa hawajui waanzie wapi kuliepuka eneo lile ambalo lilionekana si rafiki kwao. 

"Jamani hapa naanza kuihisi harufu ya ngome ya mateso kama ya Santana." 

Robinson aliendelea kuelezea hofu yake.

"Si wewe tu hata sisi ni hivyo hivyo kwani mazingira yanaongea yenyewe hayahitaji mwalimu wa kutoa ufafanuzi." 

Jasmine naye aliungana na Robinson. 

"Hebu twendeni kule juu tusionyeshe hali hii kiasi cha kuwafanya kutustukia mapema." 

Jessica aliwasihi wenzake kuwa wapande ngazi kuelekea kule juu ili kumsikiliza huyo mkuu wao ana jambo gani kwao. Na hivyo moja kwa moja waliongoza walikoelekezwa lakini cha ajabu wakiwa wanapandisha kule juu ambako ni ghorofa la miti na ni jengo ambalo liko juu kuliko majengo yote pale na yote yakiwa yamejengwa kwa miti na kukandikwa kwa udongo waliona kundi la walinzi wenye silaha kama yule wa mwanzo wakiwa nyuma yao na hapo wakajua yamewafika kooni. Walianza kupandisha ngazi kuelekea juu na hapo ndipo wale walinzi walibaki wamesimama hapo huku silaha zile zikiwa zimeelekezwa kwao. Walipandisha mpaka juu ambako walikutana na kama ofisi hivi kwani ilikuwa imesheheni kila kitu kinachotakiwa kwenye ofisi yoyote na kingine kilichowashangaza ilikuwa ni uzuri wa ofisi hiyo isiyofanana na muonekano wa nje ambako imekandikwa na matope tu lakini ndani ilikuwa imesakafiwa vizuri kwa saruji na kufuatiwa na rangi ya maziwa iliyong'aza zaidi ofisi hiyo ambayo ukitaka kujua uzuri wake unaweza kujaza maelfu ya karatasi. 

Na nyuma ya meza kulikuwa na mzee yule aliyekuwa akiendesha gari na waliyemfanyia vurugu. 

"Karibuni vijana wangu kwenye ngome ambayo kuingia kama hivi ni rahisi lakini kutoka ndiyo ngoma nzito." 

Hakuna aliyeitikia ukaribisho huo ulioonekana ni wa dharau kwao, hicho mzee yule alikiona na hivyo kuendelea na maelezo yake. 

"Nimewaita huku juu maalum kwa ajili ya kuwasikiliza kile ambacho mliniambia kuwa kiliwasibu huko mlikotoka mpaka kupelekea kufanya mauaji na kisha nitayachekecha kuona nawasaidiaje au ndo nawaripotisha ili nivute kiasi hicho cha mpunga (hela) ambacho kitasaidia katika kuukuza mradi wangu huu ambao ni maarufu hapa nchini."

Baada ya maelezo marefu ya mkuu huyo aliyetaka kujua kilichowasibu na ndipo aliposimama Jackline na kuanza kutoa historia ya safari yao mpaka pale alipowakuta. 

" Mzee kwanza kabisa tuko chini ya miguu yako kwa kitendo tulichokifanya kwako bila kujua wewe ni nani lakini ilikuwa ni moja ya hofu yetu tusamehe sana." 

Kisha aliinamisha kichwa kuashilia ombi lile linatoka moyoni mwake. 

"Lile lilipita mwanangu endelea na kipya nisichokijua kutoka kwenu." 

"Okey sawa, kifupi hapa tuko katika makundi mawili yaliyoungana ugenini namaanisha mimi na huyu hapa tumekuja hivi karibuni kutoka Tanzania na hawa wenzetu tumekutana nao huku huku lakini nao ni watanzania pia na ilikuwaje ikawa kama ilivyo ni kwamba mimi naitwa Jackline Joachim na huyu hapa ni Robinson Kaaya ambao tulikutana wilayani Chunya katika mji mdogo wa Lupa huko nilikwenda kumfuata baba mdogo aitwaye mzee Fikirini na hii ni baada ya kupoteza mawasiliano na rafiki wa marehemu baba yangu mzee Jonathan ambaye alifanya hivyo kwa makusudi baada ya kujua kuwa nilisha maliza masomo yangu ya chuo pale Soweto University cha Afrika ya Kusini ningechukua Mali za wazazi wangu ambazo alikabidhiwa na baba mdogo aziendeleze nafikiri ni kutokana na upeo mdogo wa elimu na yeye lengo lilikuwa ni kudhurumu na mpango wake ukiwa ni kutuangamiza na ndipo nilipoamua kukimbilia huku kwa ajili ya kuja kupata mafunzo ya kupambana ili nikiiva nirudi kupambana naye na kuzikomboa Mali zetu na ndipo nilipoongozana na huyu rafiki yangu Robinson."

"Na wazazi wako wako wapi mpaka Mali zenu ziwe kwa mtu mwingine ambaye ni rafiki tu."

Mkuu yule aliuliza swali baada ya kuonekana kuvutiwa na Simulizi ya Jackline.

"Wazazi wangu walifariki katika ajali mbaya gari wakiwa njiani kuelekea kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza nikiwa bado mdogo n...."

Alishindwa kujizuia akaanza kulia kutokana na kumbukumbu ya wazazi wake.

"Jack pole sana, nyamaza basi endelea na Simulizi yako."

Mkuu aliinuka kitini na kumfuata Jackline kumtuliza wakati akilia.

"Hivyo safari yetu ya kuja huku tuliunganishwa na mtu mmoja wa Afrika ya kusini aitwaye Simbozya kuwa kuna rafiki yake ambaye huwa ana chati naye mtandaoni akijitambulisha kama mwalimu wa mapigano na anamiliki shule nyingi za mapigano hivyo pasipo kufanya uchunguzi tukaunganisha safari na ndipo tukafikia katika mji wa Belem.. "

" Anaitwa nani huyo mwalimu pale Belem?"

Mkuu yule alimkatisha kwa swali.

" Anaitwa Santana."

"My God, my God ninyi watoto mna balaa hivi mnamfahamu Santana? Yule si mtu hapa Brazil ni nani asiyemfahamu, ni Zungu la Unga lile lina miliki kampuni lililoichukua kutoka kwa mzee Tuyilagezi Mrundi wa Afrika. Poleni sana na kwa ninavyomfahamu lazima hajatulia nina uhakika anawatafuta kila kona yule, eeh ikawaje sasa?"

" Baada ya kufika alitupokea yeye mwenyewe na kutupeleka kambini kwake na hapo ndipo alipoandaa mpango wa kutuangamiza lakini kama bahati hivi mchezo ule tuliusoma na kutoka kwenye chumba kile huku tukishuhudia wakiingia na kumimina risasi pale tulipokuwa tumelala na wakati tukihangaika ni wapi tupite ndipo tulipenya na kukuta kichumba ambacho ndani yake kulikuwa na hawa wenzetu na kutokana na walivyokuwa wamefungwa mle ilibidi kuwaokoa na kutoa huduma ya kwanza kwani hali zao zilikuwa sio nzuri na kisha ndipo tulipoongozwa na dada hapo aitwaye Jasmine na mdogo wake Jessica. Jasmine akiwa mke wa Santana na mdogo wake akiwa kaja kumtembelea na ndipo walipokutana na mateso baada ya Santana kuchukizwa na kitendo cha mke wake kukataa kumtoa mdogo wake Jessica kuuawa na kubeba madawa. Na wakati tunapambana kutoka tukipita kwenye njia za chini ambako tuliua walinzi wake na tulipotoka tuliomba lifti kwa mzee fulani ambaye alikataa na kutaka kupambana na sisi ndipo tulipomuua na kuondoka na gari lake na kulitelekeza mjini Belem na ndipo siri ya sisi kufanya mauaji hayo kubainika na mpaka sasa tunatafutwa mzee kwa ufupi iko hivyo tunaomba msaada wako tufanikishe zoezi letu na turejee Tanzania kulipa kisasi.. "

Jackline alianza kulia tena na tendo hilo lilipelekea wote kuanza kulia huku mzee akibaki kufuta machozi asijue afanye nini kutokana na historia ya vijana aliokuwa nao mle ndani kwani umri wao hauendani na makubwa waliyopitia na wanayoendelea kuyapitia.


Nini kitaendelea ndani ya Ngome ambayo bado hatujaifahamu jina lake?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


       #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post