NITAKUUA MWENYEWE - 18 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


NITAKUUA MWENYEWE - 18

sultanuwezotz.blogspot.com 


"Nimewaelewa vizuri sana na pia niwape pole kwa yote mliyopitia inawezekana ni mpango wa Mungu katika kuwafanya muweze kuwajua maadui zenu."

"Asante mzee tunamshukuru kwa kutuelewa." Jasmine alishukuru.

"Bila shaka, niwakaribishe katika Ngome yetu na pia nianze kwa kuwajulisha kuwa huu ni mgodi wa kuzalisha kokoto ni mgodi mkubwa sana ndani ya Brazil mengine mtaendelea kuyajua kwa muda mtakaokuwepo hapa. Na mimi ndiye msimamizi mkuu na miongoni mwa wamiliki wa Mgodi kwa majina naitwa Bruno Gautier.Karibuni sana."

"Asante mkuu, ila nilikuwa naomba kuuliza kidogo kama hutojali."

"Uliza tu binti."

"Tutakuwepo hapa kwa muda gani?"

Jessica aliuliza.

"Hapa mtakuwa nasi kwa kipindi hiki chote ambacho mnatafutwa mpaka pale hali utakapokuwa sawa mtaondoka tu."

"Hawawezi kubaini kama tuko ndani ya mgodi huu? Kama ulivyosema kuwa ni mgodi mkubwa." Robinson aliuliza swali jingine.

"Vijana wangu niwatoe hofu kuwa eneo hili huwa haliingiwi hovyo na watu wasiohusika kwani mgodi huu una eneo la kiwanda cha kuziboresha kokoto huko ndiko wateja wetu huishia." Alifafanua mzee huyo.

"Tutashukuru sana mzee na bila shaka tukiwa humu tutaweza kujifua zaidi na mazoezi ikiwa tutapata eneo."

"Hilo ni jambo dogo sana kwangu tegemeeni makubaliano kutoka kwangu."

Baada ya kikao hicho kisicho rasmi mzee Bruno aliwaacha ndani ya ofisi yake na yeye kushuka chini ambako alimwita mmoja wa walinzi wake na kuongea naye mambo fulani kisha yeye akaingia ndani ya Lori lake la kubebea magogo na kutoka zake na kitendo hicho kilionwa na Robinson aliyekuwa akichungulia kule chini kupitia dirishani na kupata wasiwasi kwanini aondoke na kuwaacha mle ofisini mwake?

"Mmhh jamani kuna sintofahamu hapa."

"Ipi hiyo Robinson?" Jasmine alimuuliza.

"Mzee Bruno kaondoka na mgari wake na pia kuna maelekezo alikuwa akimpa mmoja wa walinzi wake."

"Hakuna haja ya kupata hofu kwani mzee Bruno kama alivyosema ndiye mmiliki wa eneo hili na kiongozi pia hivyo hawezi kukaa tu humu ofisini ilhali kuna kazi zinatakiwa kuendelea." Jackline alimtoa wasiwasi mpenzi wake Robinson.

"Ni kweli kabisa Jackie lakini eneo hili bado nina mashaka nalo kutokana na namna mambo yanavyokwenda hatuwezi kusema ni salama hebu angalia kule chini namna wafanyakazi wanavyopata adhabu." Jasmine alionesha hofu yake ya wazi kwa mzee Bruno na Ngome yake.

" Ni kweli Jasmine hebu angalia kule namna yule mfanyakazi anavyokula mijeredi moja kwa moja hawa ni watumwa hawalipwi chochote kutokana na kazi wanazofanya humu ndani." Jessica alimuunga mkono dada yake.

"Kikubwa jamani tuwe makini hawa si ndugu zetu lolote linaweza kutokea."

Jackline aliwatahadharisha wenzake.

Wakiwa kwenye mjadala mle ofisini mara mlango ulifunguliwa na akaingia yule mlinzi aliyekuwa akipokea maagizo kutoka kwa mzee Bruno Gautier.

"Samahani naitwa James Martin ni mkuu wa kitengo cha ulinzi hapa GAUTIER MINING LTD."

Walitazamana wakina Jackline baada ya kusikia jina la mgodi huo hapo wakabaini kuwa asilimia mia moja mzee Bruno Gautier ndiye mmiliki mkuu.

"Okay asante ndugu." Robinson alijibu kwa ufupi.

"Hivyo basi kabla ya kuondoka kaniagiza niwachukue na kuwapeleka kwenye vyumba ambavyo mtakuwa mnakaa."

"Ok sawa brother hakuna tatizo tunaweza kwenda tu."

Jackline alijibu na kuwaonesha ishara ya shingo wenzake kuashiria kumfuata mlinzi.

Walishuka na kuongozana na mlinzi huyo mpaka kwenye vyumba vilivyoandaliwa kwa ajili yao. Na wakiwa njiani kuelekea huko walipishana na mmoja wa wafanyakazi aliyekuwa akiwaangalia huku akitikisa kichwa kuonesha ishara ya kuwasikitikia wageni hao. Hilo Jasmine alibahatika kuliona na hapo akajua si salama kwao. Walifika na mlinzi aliwaonesha makazi yao ila tu hofu iliongezeka pale walipoambiwa kuwa chumba kimoja kwa mtu mmoja.

"Brother sisi ni ndugu tunaweza kukaa chumba kimoja tu bila shaka yoyote." Robinson alimfuata mlinzi na kumuelekeza kwa sauti na ishara za mikono.

"Unaweza kuwa sawa lakini kulingana na kanuni zetu humu ndani ziko hivyo na hii ni kulingana na vitanda vyetu vilivyotengenezwa."

"Mbona hii mpya sasa." Jessica alijisemea huku akichungulia ndani ya chumba alichooneshwa kuwa kitatumiwa naye.

"Brother sasa mbona hata hivyo vitanda sivioni humo ndani?"

"Jamani mimi natekeleza maagizo ya mkuu na si vinginevyo na kama hamjaridhishwa basi mtaongea naye alirudi jioni."

"Jamani ee tuingieni tu humu tumejaa wenyewe hivyo hatuna jinsi."

 Jasmine alionekana kupaniki akaongea hayo na kuingia zake chumbani kwake. Kitendo hicho kilikuwa kama ni ishara kwa wenzake kwani nao ilibidi waingie vyumbani mwao. Na kilichowathibitishia kuwa wamedakwa ni baada ya wao kuingia tu milango ilipigwa lock.

Mle ndani kwa kuwa mlikandikwa kwa tope haikuwa tabu kwao kuendelea kuwasiliana kwa kuwa juu kwenye ukuta wa kutenganisha vyomba hivyo kulikuwa wazi hivyo sauti zao zilikuwa zikisafiri vizuri.

"Jamani ee hakuna kufanya chochote kile mpaka tuusome mchezo kisha tufanye yetu."

Jackline aliwatahadharisha wenzake.

"Ni kweli kabisa jamani kwani kufanyiwa hivi inawezekana ni kutokuwa na imani nasi na matukio tuliyotoka kuyafanya."

Jasmine akakubaliana na Jackline.

"Hatuna jinsi yoyote ila tu niwaombe simu zenu tafuteni sehemu ambayo ni salama ficheni hali inaweza kubadilika ukashangaa tunafanyiwa ukaguzi." Robinson alishauri wenzake.

"Brother umesomeka." Jessica alijibu.

"Robinson umetenganishwa na sukari yako itakuwaje sasa?" Jasmine alimtania Robinson.

"Ni mapito tu dada yangu yatakwisha na maisha mengine yataendelea."

"Kabisa mpenzi wangu." Jackline alimuunga mkono mpenzi wake.

Huku nje mlinzi yule aliyetambulisha kwa jina la James Martin na mkuu wa kitengo cha ulinzi alimpigia simu mkuu wake kumjulisha kuwa tayari kawabania vyumbani mwao.

"Mkuu kama ulivyoagiza ndivyo nilivyotekeleza."

"Vizuri sana sasa cha kufanya andaeni kile chumba cha mateso ili nikifika niwaoneshe mimi ni mtu wa namna gani."

"Kama ulivyoagiza bosi wangu."

"Hakikisha kila kona ya Ngome kuna ulinzi wa kutosha maana hao si watu wazuri hata kidogo James."

"Sawa bosi kila kitu kitakwenda vizuri."

"Okay, tunamalizia kupakia magogo na baada ya masaa kadhaa tutakuwa hapo."

"Sawa mkuu."

Bruno alikata simu na kumfanya mlinzi wake kuyapitia mageti yote kuimarisha ulinzi kisha akapenya mpaka kwenye kuta zote na chemba kuu ambayo ndiyo kokoto hupitishwa huko kwa njia ya viberenge kupeleka upande wa pili wa mgodi ambako kuna kiwanda cha kuziongeza thamani kokoto na kuzitenga kwenye madaraja huko kote alihakikisha ulinzi uko sawa.


***


"Haloo nani mwenzangu?"

Mke wa mzee Jonathan aliuliza baada ya kupokea simu ambayo alipigiwa na mtu asiyemfahamu.

"Samahani shemeji mzee Jonathan bado hajarudiwa na fahamu zake lakini jambo la kumshukuru Allah ni kwamba tumefanikiwa zoezi lake."

"Okay nashukuru sana kwa hilo vipi itamchukua muda gani mpaka kurejewa na fahamu?"

"Ondoa shaka hata dakika ishirini hazitafika atakuwa tayari kazinduka."

"Nawategemea sana ndugu zangu katika hili."

"Ondoa shaka mama ila sasa samahani kuna kijana wetu atakuwa maeneo Bismarck Coffee Table maeneo ya Nyakato jitahidi uonane naye kuna maagizo atakupatia."

"Muda gani itakuwa ili na mimi nielekee huko?"

"Hata sasa unaweza kwenda kwani yeye muda mrefu yuko huko tayari."

"Okay basi ngoja niende nikaonane naye."

"Sawa mama."

Simu ilikatwa na mama Jonathan haraka aliinuka kutoka pale alipokuwa akiandaa chakula na kuweka mchele pembeni na kuingia chumbani ambako alifanya maandalizi ya kuoga haraka katika kuondoa jasho la jikoni na kisha kupigilia viwalo vyake kisha akaliwasha gari lake na kuelekea alikoelekezwa.

"Hivi hawezi kunishtukia kweli kumbukeni yule ni mke wangu?"

Mzee Jonathan alionyesha hofu.

"Mzee huu ni mtihani iwapo atakutambua basi tunaanza upya maana yake kila mmoja huko mtaani atakutambua."

"Okay ngoja tusubiri basi tuone itakuwaje."

Mzee Jonathan aliendelea kutojiamini katika zoezi hilo.

"Mzee kikubwa fanya kama tulivyokueleza na si vinginevyo."

"Sawa sawa kijana wangu."

Wakiwa wanaendelea kuwekana sawa mara kuna gari lilikuwa linaingia pale Bismarck Coffee Table na hapo wenzake wakaondoka na kumuacha pale mzee Jonathan akutane na mke wake.

Mke wake baada ya kuteremka kwenye gari 

aliongoza moja kwa moja mpaka ndani na kuanza kuangalia huku na kule kuona kama anaweza kumuona mwenyeji wake na mara aliweza kumuona baada ya kuona mtu kwenye kona moja akimpungia mkono kumuonesha kuwa ni yeye mwenyeji wake.

"Habari yako Anti naitwa Ras Migo nimeagizwa na kijana mmoja anayeitwa Nyashiko kaniambia nikupe hii bahasha."

"Okay asante sana."

"Basi Anti naomba uniruhusu niweze kuondoka maana nilikuwa nakusubiri wewe tu."

"Upate hata kinywaji tu kijana wangu ndipo uende."

"Nashukuru sana siku nyingine nitakunywa."

Wakati wakiendelea na mazungumzo yao mara simu ya mke wa Jonathan iliita akaipokea.

"Ndiyo kijana wangu mzigo nimeupata tayari."

"Sawa mama hiyo bahasha utaihifadhi ndani ni documents za mtambo ambao mzee ameununua hivi karibuni."

Kisha simu ilikatwa na mke Jonathan aliiweka kwenye pochi yake na alipogeuka kumtazama mwenyeji wake hakuona kitu zaidi ya kiti. Aliangaza huku na kule hakuona mtu.

Kwa zoezi hili iliwapa matumaini kuwa muonekano mpya wa mzee Jonathan utawapa wakati mgumu sana maadui kumtambua.


JE NINI KITAENDELEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


       #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post