NITAKUUA MWENYEWE - 19 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


NITAKUUA MWENYEWE - 19

sultanuwezotz.blogspot.com 


"Ninyi ni hatari aise yaani mke wangu mimi anayenifahamu mpaka alama iliyo kwenye utumbo leo hii hajanitambua? Maskini weee Dorothy wangu."

Mzee Jonathan aliwamwagia sifa vijana waliobadili muonekano wake uliopelekea mpaka mke wake kumsahau baada ya kukutana pale Bismarck Coffee Table.

" Nilikwambia mzee hutaamini kazi ikikamilika hivyo basi kilichobakia hapa ni kuanza safari ukiongozana na vijana wangu wawili ambao watakusaidia mambo yako huko ukirudi na ushindi unatupa chetu." Aliongea kiongozi yule ambaye ndiye aliyefanya kazi ile ya kisanaa.

" Nashukuru sana kijana wangu naamini kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa maana sipate usingizi kabisa juu ya ile familia."

"Wale ni sawa na kuku walio ndani ya banda unaamua tu umkamate yupi na kwa staili gani mzee hawana ujanja waleeee." Alisisitiza kiongozi.

"Basi sawa nadhani mimi sasa nielekee nyumbani kwanza nikafanye maandalizi ya safari ili ifikapo saa nane mchana tuanze safari yetu."

"Bila shaka mzee."

Mzee Jonathan aliondoka pale kupitia uchochoro wa nyuma wa kingome kile na kutokea eneo moja hivi la wazi huko aliikuta gari yake ikiwa inamsubiri, ilimshtua kidogo kwani alipoikuta ni tofauti na pale alipoiacha lakini hakutaka kuonesha hofu hiyo mbele ya kijana aliyemsindikiza pale. Waliagana kisha mzee Jonathan akaondoka zake na baada ya dakika kadhaa alikuwa getini kwake akipiga honi. Geti lilifunguliwa na gari ilijaa ndani na mzee Jonathan alishuka garini, akiwa anafunga mlango wa gari mke wake aliyekuwa akitoka pale getini akashtuka kumuona tena yule mtu waliyekutana na kisha kupotea kule Bismarck.

"Vipi tena? Wewe si ulinikimbia bila kuagana?"

"Naomba unisamehe Anti kulitokea dharura na nimeona nije nikuombe radhi."

"Okay limekwisha hilo nambie lakini?"

"Naitwa Jonathan Ubao mumeo halali kabisaaa."

Baada ya utambulisho huo mke wake hakuamini macho yake na hapo hapo alidondosha machozi ambayo alijua mwenyewe kama ni ya furaha au ya mshangao.

"Mume wangu umebadilika hivyo?"

"Ndicho nilichokuwa nakihitaji hiki mke wangu nimekuja mara moja kufanya maandalizi ya safari nategemea mchana kuanza safari."

"Kwa muonekano huo kila apitaye mbele yako ni risasi tu."

Mke wake alimtania.

Waliingia ndani na mke wake alimuandalia maji ya kuoga na kisha wakapata chakula. Na kila kitu kilipokuwa tayari waliagana na kisha Kulga iliwashwa na kuondoka.

"Waambie wakina Black nawapitia wajiandae."

"Wajiandae nini tena mzee hawa kama Wajeda wako tayari muda wote wewe njoo muondoke."

"Okay sawa kiongozi."

Alifika pale na kuwakuta vijana wale wakimsubiri hivyo aliisimamisha gari na kisha wakapanda na gari ikang'oa nanga na nyuma ya usukani akiwa ni Black na huku mzee Jonathan akiwa pembeni yake.


***


Mzee Bruno aliingia ndani ya Ngome yake na kupaki gari lake lililokuwa limejaa magogo tena na kama ilivyokawaida kundi lile la watumwa walifika pale kwa mstari na kuanza kushusha huku mzee yeye akiwa sambamba na James kuelekea walikofungiwa wageni wake.

"Vipi wanasemaje hawa paka?"

"Hawana usemi ila tu walilalamikia kitendo cha kufunga mlango na kuwatenganisha vyumba."

"Wanatuletea sheria zao hapa ni kwangu lazima wafuate sheria zangu, kwanza niletee na vifaa vya kutolea wenge ili niwakaribishe rasmi ndani ya Ngome kuu."

"Kama ulivyoagiza mkuu."

Mlinzi yule aliondoka na kwenda kuleta vitendea kazi na kumuacha mzee Bruno akiliendea jengo lile walilofungiwa wakina Robinson. Baada ya kufika alikwenda moja kwa moja kwenye eneo la wazi ambalo ni ghala fulani likiwa na baadhi ya magunia kadhaa ya nafaka. Alikagua kagua magunia yale na mara kamanda wake James aliingia na kuweka chini vifaa vile ambavyo vilikuwa ni beseni la moto na baadhi ya vyuma pamoja na maji yaliyokuwa ndani ya kontena lenye barafu.

"Kawafungulie na uwalete hapa."

"Sawa mkuu."

Aliondoka na kwenda kuwafungulia wakina wakina Jackline ambao mpaka muda huo walikuwa gizani hawajui ni nini lengo la kufungiwa mle vyumbani tena kila mmoja na chake.

"Vipi mzee karudi?"

Robinson aliuliza baada ya kufunguliwa.

"Ndiyo na ndiye aliyeniagiza niwafungulie.Yuko kule mwisho kwenye lile jengo lenye mlango mkubwa anawahitaji."

Bila wasiwasi wowote waliongoza kule walikoelekezwa na hapo hapo James akawaamuru walinzi zaidi ya kumi na tano kuwafuata nyuma.

" Karibuni sana vijana wangu kwenye jengo hili ambalo mara nyingi watu huwa hawatoki salama."

"Mzee kwani kosa letu ni lipi kwako?"

Jasmine aliuliza.

"Wala hamjanikosea lolote ila tu sina imani na ninyi kwani kwa namna Ngome ya Santana ilivyo na ulinzi mkali lakini ninyi mkatoka na kumchanganya Santana hivyo ni mjinga gani ambaye awaamini kirahisi rahisi uongo wenu? Ila hapa ni sehemu pekee ambapo wenye roho ngumu huweza kulainika."

"Ina maana mzee hujatuamini kwa tulichokuelezea?"

"Ndiyo na sitaki niwaamini kirahisi ila kupitia eneo hili najua mtanieleza ninyi ni wakina nani na mmefuata nini Brazil na mmetokea wapi na ni nani aliye nyuma yenu."

"Mzee si...."

Kabla hajamaliza kuongea Robinson alikutana na ngumi nzito kutoka kwa mzee Bruno.

"Halafu wewe dogo unaongea sana, nafikiri sasa ni muda wenu wa kuongea."

"Hatuna tunalolijua jingine."

Jackline alijibu.

"James waite vitasa wafanye kazi yao mara moja."

Alimtaka James awaite vijana ambao hufanya kazi chumba cha mateso. Na muda mfupi baadaye waliingia vijana wenye miraba minne wakiwa na minyororo mikononi na miguuni na kisha walifunguliwa ile minyororo na kisha waliwafuata wakina Jackline.

" Anzeni kazi yenu mpaka walainike hao si mnaona walivyo strong' hao."

Hapo hapo walikamatwa wakina Robinson na kufungwa minyororo na kisha yale majitu yalianza kuwashushia vichapo.

Hali ya mle ndani ilibadilika kwani sakafu ilianza kutapakaa damu ikiwa ni dalili vijana walianza kuiva.


NIKUOMBE USIKAE MBALI NA SEHEMU YA ISHIRINI KUJUA NINI KITAENDELEA NDANI YA NGOME.


        #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post