NITAKUUA MWENYEWE - 21 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


NITAKUUA MWENYEWE - 21

sultanuwezotz.blogspot.com


"Ndiyo hivyo mzee sijui kaelekea wapi?"

"Ninyi tuondokeni eneo nahisi harufu ya damu mwenzenu."

Masanja aliwataka waondoke baada ya kijana waliyekuwa naye kutoweka.

"Hili picha mbona silielewi hivi?"

Mzee Jonathan aliuliza huku wakiondoka eneo hilo kurudi walikoacha gari.

"Au amekutambua nini mzee Jonathan?"

Black alimuuliza mzee Jonathan.

"Siyo rahisi nadhani ni ushamba wake tu si uliona hata mle kwenye gari alivyokuwa akitetemeka?" Ajibu mzee Jonathan.

"Hee oneni kule!!"

Masanja aliwashtua baada ya kuona kitu.

"Wapi dogo Masanja?"

Black aliuliza baada ya kuona Masanja kama kapigwa butwaa.

"Kule kwenye gari kuna nini?"

"Mungu wangu tumejulikana tayari, tufanye nini sasa?"

Mzee Jonathan alipigwa butwaa.

"Hatuna jeuri ya kufanya chochote lile kundi ni kubwa na hatujui wamejipangaje?"

Masanja aliwasihi wenzake kutofanya chochote.

"Jamani ee hapa ni kuangalia usalama wetu kwanza."

Mzee Jonathan alianza kutimua mbio huku akiwaambia wenzake waokoe roho zao.

"Au tuwashambulie nini kwani huko tuendako hatukujui mwisho wa siku tutakamatwa tu."

Black alitoa wazo baada ya kuona hakuna uwezekano wa kutoka eneo hilo. 

Wananchi waliokuwa wamelizunguka gari walisogea ndani ya yale makaburi na wengine kusalia pale kwenye gari hii ni mara baada ya kuona hawatokei washukiwa wao. 

" Vijana wangu muwe makini maana hao jamaa hatuwajui vizuri."

Mwenyekiti wa ulinzi na usalama wa kijiji cha Lupa mzee Kaaya na ambaye ndiye baba mzazi wa Robinson aliwasihi vijana wake kuchukua tahadhari. 

"Bila shaka mzee usiwe na mashaka." Alijibu kijana mmoja ambaye alikuwa karibu yake. 

"Jamani njooni muone viatu vyao vimepita huku." Aliwaita yule kijana ambaye aliwakimbia wakina mzee Jonathan. 

Wote walielekea kule kuangalia zile alama za viatu ili kujua zimeelekea wapi na baada ya kuziangalia wakajua hawa watu wako ndani ya makaburi yale au nje kimsitu kinachoelekea mtoni. 

" Kwenye gari msiondoke wote wengine wabakie." Mzee Kaaya alitoa tahadhari baada ya kuona wote wanakimbilia kwenye zile alama. 

Vijana walisambaa kwenye maeneo yale kuhakikisha wanawatia mikononi wahusika. Makaburi na msitu huo ulivamiwa na kundi hilo ambalo lilikuwa na zaidi ya watu mia moja.

" Wameelekea huku jamani nyayo zao zinaenda huku."

Mmoja aliwaita wenzake baada ya kuziona zikielekea eneo la mto Lupa.

"Jamani hivi tutatoka salama kweli?" Mzee Jonathan alionesha hofu yake baada ya kuona kundi lile likija nyuma yao.

"Tutatoka tu mzee kikubwa uwe na pumzi ya kutosha ya kukimbia."

Masanja alimtia moyo mzee Jonathan.

"Inaonekana hawa watu walishajipanga kuwakamata watu wote watakaogusia familia ya mzee Fikirini kutokana na kutambua azma ya yule kijana Surambaya ambaye aliuwawa kwa kuchomwa moto na jeshi la polisi kisha kutoa taarifa zangu kama mtuhumiwa namba moja."

Mzee Jonathan aliongea hayo baada ya kukutana na ukinzani ambao hakuutarajia kabisa.

" Mzee huu si muda wa kujilaumu tupambane kuhakikisha tunatoka eneo hili."

"Ni sawa usemayo Masanja lakini huku tuendako unakufahamu?"

"Sikufahamu ndiyo lakini hatuna jinsi kwani gari limetekwa hivyo tutafute njia mbadala kutoka."

Masanja aliendelea kufafanua.

"Oya ee tupiteni njia hii nimeifuatilia mpaka kule mbele inatoka nje."

Black aliingilia maongezi yao.

"Vizuri tuwahini kabla hatujatiwa mikononi jamani na tukitoka salama sitaki tena kuendelea na zoezi hili ni kurudi nyumbani nikajue la kufanya."

"Mzee Jonathan ulianzaje mambo haya ilhali unakiroho cha chipsi yao?"

Masanja alimcheka wakati akimkongoja kwa kumshika mkono.

"Weee usicheze na uhai hujui siku zote huwa tunapanga mipango kwa kuangalia upande mmoja tu bila kujua upande wa pili umejiandaaje."

"Ni kweli kabisa mzee Jonathan."

"Acheni stori nyinyi nitawaacha ohooo."

Black aliwatishia baada ya kuona wenzake mwendo hauridhishi.

"Tunajitahidi sana sema tu basi." Masanja alijitetea.

Baada ya kuona wanazidi kusonga tu mbele bila mafanikio waliamua kugawanyika na wengine kurudi tena mpaka barabarani ambako waliamua kuweka vizuizi uelekeo wa Mbeya na ule wa Tabora kuhakikisha wanawatia nguvuni na zoezi hilo likikabidhiwa kwa Jilanga ambaye ndiye aliwakimbia na kwamba amewakariri muonekano wao.


***


Wakiwa wamejipumzisha mara mlango ulifunguliwa na kuingizwa chombo ambacho kilikuwa na chakula. Na kisha mlango ulifungwa tena, waliinuka na kukichukua chakula na muda huu hawakuwa na minyororo tena. Ila tu mawazo yalikuwa bado kwa mwenzao Jackline ambaye fahamu zilikuwa hazijamrudia.

"Tuwaite tuwajulishe kuwa mwenzetu hajaamka bado watupe msaada." Jessica alishauri.

"Haiwezekani hiyo Jessica kumbuka wao ndiyo wamesababisha hayo na huyu huyu ndiye aliyewatia huzuni kwa kuwaua wenzao halafu tuwaambie kuwa tunaomba msaada wa tiba si watakwenda kumuulia mbali?"

Robinson aliweka upinzani kwenye hilo.

"Ni kweli lakini itakuwa ngumu hapa tukomae nae tu mpaka asubuhi muujiza utakuwa umetokea." Jasmine aliunga mkono.

Hivyo walijongea kwenye chakula, katika kufunua funua vyombo vilivyokuwa vimeletwa pale walikutana na kikaratasi kilichokuwa na maandishi.

"HILO BIRIKA LINA DAWA MNYWESHENI MGONJWA NA NYINGINE MKANDENI MAENEO YENYE VIDONDA."

"Jamani oneni maajabu sijui ni nani aliyefanya haya."

"Tuweni makini isije kuwa ni sumu akanywa ikawa ndiyo kwa heri."

Jessica alionesha wasiwasi juu ya dawa hiyo.

"Hapana ngoja tufanye kama ilivyo huoni watu ambavyo walimkubali pale nje hivyo nadhani kuna mtu kaonesha kuguswa na majeraha yake jamani." Robinson alipinga wazo la Jessica.

Jasmine alichukua ile dawa na kuanza kumfanyia tiba Jackline na nyingine wakimnywesha. Na walipo hakikisha kila kitu kiko sawa walichukua mihogo kiasi wakamuwekea pembeni akizinduka ale na mingine walikula wao.

" Jackline akiamka tu tunaanza mchakato wa kupanga namna kutoka humu nimeguswa na moyo wake inatakiwa tuungane naye."

Jasmine aliwaambia wenzake juu ya kuguswa kwake na Jackline.

"Hilo neno ndugu zangu na kwanza mpaka hapa naona kuna kila dalili ya kupata msaada." Aliongeza Jessica.

Wakiwa wanaendelea na mazungumzo yao mara walisikia kama ukuta unagongwa hivi.

"Nini hicho?" Jasmine aliuliza.

"Sijui ni nini?" Jessica alijibu.

"Hebu tulieni kwanza."

Robinson alinong'ona huku akiinuka na kusogea pale ambapo palikuwa panasikika kugongwa ili kuchungulia ni nini.

Kabla hata hajajua kipi kinaendelea mara aliona kijikaratasi kikipenyezwa kupitia kijitundu kilichotobolewa. Robinson alikivuta na kukifungua.

"MGONJWA AKIPATA NAFUU MSIFANYE CHOCHOTE JIFANYENI WAJINGA ILI MKUU AJIONE MSHINDI AKIONA HIVYO ATAJUA MUMEINGIWA UOGA HIVYO ATAWAPA KAZI ZA NJE KAMA SISI NA HAPO NDIPO TUTAWAUNGA MKONO KWENYE MPANGO WA KUTOKA HUMU KUNA NJIA RAHISI YA KUPITA HATA SISI TUMEUMISS UHURU."

Baada ya kukisoma alimpatia Jasmine ambaye naye alipokisoma alitikisa kichwa kama kukubaliana na kilichoandikwa.

" Kuna sababu hapa Robinson, hebu tufanye kama kimemo kinavyosema then tutajua cha kufanya kwa kushirikiana na huyu mtuma vimemo ambaye hatujamfahamu mpaka sasa."

"Uko sawa kabisa, hebu tutulie ili tuyasome mazingira ambayo yatatuonesha njia ya kutoka au kubaki."

Robinson aliunga mkono hoja ya Jasmine.

"Jamani mpaka hapa naiona njia ya kutoka tayari lakini pia msisahau kuwa kuna watu wanakuja nyuma yetu kututafuta."

Jessica aliunga mkono lakini pia aliwakumbusha jambo wenzake.


Nini kitatokea?


USIKOSE KUSOMA SEHEMU INAYOFUATA KUJUA KILICHOENDELEA.


     #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post