NITAKUUA MWENYEWE - 29 (Mtunzi: Sultan Uwezo)


 NITAKUUA MWENYEWE - 29

sultanuwezotz.blogspot.com


Rashid aliingia kwenye duka la vinywaji kununua vinywaji kwa ajili ya mzee Jonathan na vijana wake ambapo mara baada ya kumuona Black alibaini kitu kutokana na midomo yake kuonesha kukosa chakula kwa muda fulani maana midomo ilikuwa imemkauka sana hivyo alijiongeza, baada ya kununua alitoka na kuelekea kwenye kibanda cha kuuza vyakula lakini akiwa mdogo mdogo mara aliliona gari la polisi almaarufu kama Tenga likifika stendi na kutia breki zilizosababisha vumbi jingi kutimka kitendo kile kilimshtua sana Rashid lakini kwa kuwa alijiamini kama raia safi asiye na tatizo lolote na mtu yeyote aliendelea na mwendo wake. Lakini ni kama kuna kitu kilimsukuma kuangalia nyuma yake huko aliweza kuwaona askari polisi wakiruka kwenye Tenga hilo na kusambaa eneo lote huku mkuu wa kikosi kile akitoa tangazo kupitia kipaza sauti kilichokuwa kwenye gari.

"Ndugu wana Bitimanyanga nina wataarifu kuwa tuko eneo hili kwenye oparesheni maalum ya kuwasaka wahalifu ambao wako eneo hili, unachoombwa ni kutoa ushirikiano kwa jeshi lako la polisi kwa kutoa taarifa za watu hao ambao picha zao ndiyo zinabandikwa na askari wangu. Sura hizo ukiziona toa taarifa kwetu na kama kuna yeyote aliyewahifadhi kwa kujua au kutokujua ajisalimishe mwenyewe kwetu."

Wakati mkuu wa kikosi huyo akiendelea kutoa tangazo ilibidi Rashid asitishe zoezi lake la kuelekea kwenye banda la vyakula na kuongoza kwenye picha mojawapo iliyokuwa imebandikwa karibu na alipokuwa.

" Hee nini tena? Huyu aliye hapa mbona ni yule brother niliyemuacha kwenye gari? Na hawa wengine ni wakina nani?"

Rashid hakutaka kupoteza muda wake haraka sana aligeuza na kuongoza kwenye gari akamuangalie aliyemuacha ndani ya gari.

"Kijana hapo hapo simama mbona mbio mbio kwenye gari mara baada ya kuliona tangazo lenye picha za wahalifu wetu?"

Sauti hiyo iliyotoka nyuma ya Rashid ilimshtua kwani ilikuwa imeshirikiana na mdomo wa bunduki iliyokuwa tayari kwenye kisogo chake.

"Usijaribu kuvuta hata robo hatua nitausambaza ubongo wako."

Askari huyo aliunganisha maelezo kabla hata ya Rashid kujitetea.

"Afande ngoja tu niwe muwazi kwenye hili."

"Ehee ukweli gani huo? Eleza haraka kabla ubongo wako sijautawanya."

"Mimi nimefika hapa dakika chache kutoka Tabora na...."

"Tabora? Na hapa umefuata nini mbona una hofu?"

"Hofu lazima niwe nayo Afande kwa sababu mimi safari yangu ilikuwa inaishia Kambikatoto kununua asali lakini nikaambiwa huku pia inapatikana ikabidi nije lakini hali ikawa tofauti nikakuta bei iko juu ikabidi niondoke lakini nilipofika pale gari lilipo nikasimamishwa na kijana mmoja ambaye akaniomba lifti na nilipomhoji akasema katokea huko sijui Isangawana kwenye tumbaku na kule alishindwa kuvumilia manyanyaso ya bosi wake hivyo akatoroka na baada ya kufika hapa akawa kachoka sana na ndipo alipoona aombe lift mpaka Sikonge ambako ndiyo kwao basi nikaona nimchukue kama ilivyo kwetu watanzania tumejaaliwa huruma na ndipo nikaona nifuate vocha na hivi vinywaji kisha safari iendelee lakini kilichonishtua mpaka kutembea haraka hivi ni baada ya kumuwahi kwani kwenye ile picha mmoja wao ni yeye hivyo nilikuwa nakimbia kumuwahi."

"Afande Nyigo tufuate haraka.

Simama na wewe hapa kule usiende kwani tayari ni hatari tuachie sisi mchezo huu."

Pale pale Rashid alitoa simu yake mfukoni akaishika kisha akaifungua na kutoa betri kisha laini baada ya hapo aliiweka chini na kuifukia kwa mchanga kwa kutumia raba yake, laini na betri alivirusha pembeni baada ya kuhakikisha hakuna anayemuangalia kisha akasogea pembeni kidogo kutoka pale na hii ilikuwa ni baada ya kubaini kuwa kuna kila dalili ya kutiwa mbaroni kwani alihisi mzee Jonathan hayupo maeneo yale ila tu aliyekuwa garini ni mtu wake na inawezekana ndiye aliyemfuata.

"Kwanini mzee Jonathan na mke wake wanifanyie hivi?"

Rashid alijiuliza swali hilo pasipo kujua miongoni mwa wanaotafutwa na walio kwenye ile picha ni yeye lakini ule muonekano mpya ulimchanganya Rashid.

"We dogo mbona hakuna mtu humu unatuchezea sisi siyo?"

Yule afande alimgeukia Rashid baada ya kukuta gari jeupe halina mtu.

Ilibidi Rashid asogee akajiridhisha mwenyewe kwani ni mtu ambaye alimuacha ndani ya gari wakati akielekea dukani.

"Basi ametoka mbona nilimuacha humu ndani Afande?"

"Kijana usicheze na sisi kumbuka tumechoma mafuta yetu kuwafuata wao?"

Wakati afande huyo akiendelea kumuwakia, Rashid ilibidi ainame chini ya gari na kuchungulia kama anaweza kumuona lakini hakuweza kumuona ila kuna kitu alikiona.

"Afande angalia hapa hii ni alama ya viatu vyake."

Wakati ameshuka alikanyaga pale kwenye mchanga ikabidi yule afande na mwenzake Nyigo kuanza kufuatilia zile kanyagio za Black. Huku nyuma Rashid alibaki ameegemea gari asijue la kufanya.

Lakini akiwa pale kundi la pili la askari lilimpita kuelekea walikoenda wenzao na ndipo Rashid akapata wazo la kutoroka na kuliacha gari kwani alihisi kuwa wakirudi huko walikokwenda wakiwa hawajampata lazima adakwe yeye kwa kulisaidia jeshi la polisi.

Aliacha kila kitu na kuanza kutembea kidogo kidogo kama vile yupo huku anaangalia nyuma na akiwa hatua kadhaa kutoka kwenye gari aliliona pikipiki ikija nyuma yake ambayo aliisimamisha na kuombwa kukimbizwa Rungwa.

"Brother mimi sifiki huko naelekea shambani kupeleka chakula kwa vijana wangu."

"Nikimbize kaka wenzangu wananisubiri wasije niacha huku ni mgeni nitakulipa mara mbili ya nauli ya kawaida ya bodaboda."

"Utaiweza ndugu yangu?"

"Kwani ni shilingi ngapi mpaka nishindwe?"

"Nauli ya kawaida ni shilingi elfu kumi na tano na kwa ulivyosema itakuwa nyekundu tatu."

"Hiyo tu?"

"Ndiyo ni hiyo tu."

"Twende zetu basi ila jitahidi mwendo rafiki yangu."

"Kuhusu mwendo usijali shikilia tu nisijefika peke yangu."

"Poa poa."

Alipanda na pikipiki ilianza kulamba vumbi kwa kasi ya sifa kama alivyoomba Rashid.


****


"Kweli nimepatwa au nimezeeka sana? Yaani vile vitoto vinaniendesha hivi? Lakini nitavifundisha adabu si vinaniona boya fulani hivi ee kwanza havina shukrani hata chembe nimevihifadhi hapa lakini havijaona sijui niwataarifu askari wa jeshi la Ulinzi kutoka kambi ya Milton Camp kwa rafiki yangu Afande Felnando? Lakini hapana mimi mwenyewe nawamudu wale."

Mzee Bruno Gautier alikuwa akiongea peke yake huku akijiuliza na kujijibu mwenyewe ni baada ya kuambiwa anatakiwa kwenda mbele ya wakina Jackline.

" Mkuu fanya maamuzi kabla hawajataifisha mali zako."

Jamie alimkumbusha baada ya kuona anajizungusha tu.

"Jamie usinifanye kichwa cha panzi kumbuka mimi ni kamanda mstaafu wa jeshi la maji hapa Brazil hivyo nina mbinu za kila aina za kumkabili adui natakiwa kupanga ni namna gani niwakabili wale Bweha siendi kichwa kichwa tu kama ninyi."

Alijikanyaga kanyaga pale huku akiwaangalia walinzi wake kwa zamu na mate yakiwa hayamkauki mdomoni, alikichukua kiko chake na kukipeleka mdomoni kisha akawasha na kuanza kuvuta huku walinzi wakiendelea kumshangaa tu kwani si kawaida yake anapoletewa habari mbaya huchukua hatua mara moja, sasa kwanini hili la leo limemchukua muda mrefu kufanya maamuzi?

Na mzee Bruno Gautier ni kama aliyasoma mawazo ya walinzi wake kwani aliwaangalia kisha akawaacha na kupanda zake ngazi kuelekea ofisini kwake na sijui ilikuwa ni kwenda kuchukua nini na alipofika ndani aliufunga mlango na kwenda kujitupa kitini kwake na kutulia huku akikigongagonga kiko chake kwenye meno yake ambayo yalikosa ushirikiano. Lakini ghafla mlango uligongwa na haukugongwa kwa utaratibu aliouzoea kitendo hicho kikamshtua mzee Gautier na kujikuta akianza kujipapasa kuikagua bastola yake kama ipo alipohakikisha kuwa ipo mahali pake alisimama na kukivuta kiti kwa nyuma ili kumpa nafasi ya kuufuata mlango.

"Nani anayegonga mlango bila utaratibu?"

Aliuliza mzee Bruno lakini hakupata jibu lolote kutoka nje hapo akajua si salama akaichomoa bastola yake kisha akausogelea mlango karibu zaidi.

"Nani yuko hapo nje mbona hakuna anayejibu?"

Ajabu badala ya kujibiwa mlango uliendelea kugongwa na safari uligongwa kwa chini hali ambayo iliendelea kumchanganya mzee Bruno Gautier akiwa na bastola yake mkononi.

"Mmhh ni nani huyu anayegonga kwa nguvu kiasi hiki na hataki kujibu? Maana wangekuwa vijana wangu ningeujua ugongaji wao kwa vyovyote vile huyu si miongoni mwao, lakini ngoja kwanza."

Mzee Bruno Gautier alijiuliza maswali yasiyokuwa na majibu na wakati mwingine alikuwa akijijibu mwenyewe. Lakini mwisho alipata wazo ambalo lingemsaidia.

Aliiendea swichi ya taa na kuizima ili kama likitokea la kutokea aweze kujinusuru na baada ya kuzima alipeleka mkono kwenye kitasa cha mlango akakinyonga kikajibu lakini kwa kasi ya ajabu akaubana tena mlango kwa nguvu na kuulock kisha akauegemea huku akihema kwa nguvu. Aligeuka na kujaribu kuangalia nje kupitia nasi zilizo kwenye mlango kuona kama anaweza kuona chochote lakini hakuona kitu bila shaka nafasi haikuwa rafiki kuweza kuona nje. Aliinuka na kujitengeneza vizuri magwanda yake na kisha akaamua kufungua mlango ili liwalo na liwe tu mlango ulikubali sheria na kufunguka na katika hali ya kujiweka salama alijiviringisha kama gurudumu mpaka upande wa pili wa mlango ule na kusimama bastola mkononi. Lakini katika hali ya kushangaza hakuweza kuona kitu chochote zaidi ya mtu aliyekuwa kalala pembeni kidogo ya mlango, alimsogelea na kumuangalia.

Hakuamini macho yake baada ya kukutana na mlinzi wake ambaye alikuwa kachomwa visu vya maana muda mrefu na kuungana na mauti huku pembeni yake kukiwa na kikaratasi chenye damu damu alikiokota na kukifungua maana kilikuwa kimefinyangwa sana.

"MZEE BRUNO GAUTIER MTU USIYE NA HURUMA NA BINADAMU WENZAKO WATOTO WA WANAWAKE WENZAKE NA MAMA YAKO ALIKUZAA WEWE HESHIMA KWAKO, TUMEAMUA KUJISALIMISHA WENYEWE TUKO HAPA CHINI TUNASUBIRI HUKUMU YAKO."

Hakutaka kusubiri asome mpaka mwisho moja kwa moja akajua ni wakina Jackline tu hivyo haraka sana akazivamia ngazi na kushuka kwa kasi kwenda kukutana nao ili awadhihirishie kuwa yeye si mtu wa kawaida hata kidogo.

Alipofika kule chini hakuweza kuona chochote kama ujumbe ulivyoeleza na hapo ndipo alipopandwa na hasira zaidi na kuanza kuzungukazunguka huku akijipigapiga kichwa chake kwa bastola yake.

"Washenzi sana ninyi si mjitokeze sasa kama miamba ya vita."

Aliongea kwa sauti ambayo bila shaka hakujua kama amepayuka kwa nguvu lakini akiwa anataka kurudi kule juu mara alisikia sauti ya mtu akihema kwa tabu sana ndipo alipogeuka na kuifuata sauti ile.

" Buuuu shiiiiit......! Nitaua mtu mimi haki ya Mungu tena naapa."

Aliongea hayo akienda chini kwa hasira si kwamba alipigwa hapana bali alichokiona ndicho kilimfanya aende chini na kujipigiza kichwa ardhini.


ALIONA NINI MZEE BRUNO GAUTIER?


USIKOSE KUSOMA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII KUPATA MAJIBU.


           #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post