IMETOSHA MAMA MKWE - 28 (Mtunzi:Sultan Uwezo)

 


IMETOSHA MAMA MKWE - 28

sultanuwezotz.blogspot.com 


Rachel alikanyaga mafuta ya gari lake mpaka sehemu moja hivi iitwayo Mswisi, katika kitu ambacho sikukitarajia ni eneo hili la Mswisi. Ukipita tu barabarani unaweza kudharau lakini kumbe kuna vitu vya kuburudisha macho aisee, safari yetu iliishia ndani ya kiwanda cha kuzalisha kokoto ambacho kiko kilomita chache kutoka barabarani kwani hata ukitupa macho yako upande wa kulia unaelekea Mbeya au kushoto kwako ukiwa unaelekea Dar utakutana na mitambo mikubwa chini ya kijimlima kinachoelekea ukingoni kutokana na kubebwa kwa malighafi zinazotumika. Ndani ya kiwanda kile tulipokelewa na Husna Nyakya ambaye ni rafiki mkubwa wa Rachel kwa maelezo yao ni kwamba wamesoma pamoja sekondari na baada ya hapo walipotezana mpaka pale mitandao ya kijamii ilipowakutanisha tena wakiwa ni waajiliwa kwenye viwanda tofauti lakini ndani ya mkoa mmoja wa Mbeya.

"Rachel ndiyo sasa umenifanyia?" Husna alimuuliza Rachel tukiwa mlangoni kwake.

"Ha ha ha niliamua kukushtukiza rafiki yangu na ndiyo maana sikukupigia simu." Rachel alimjibu akicheka.

"Okay sawa mshindi wewe bwana, mgeni karibu ndani achana naye huyu nimemzoea mwenyewe." Husna alinikaribisha.

"Nashukuru dada." Nilimjibu.

"Tuko mazoezini mwili wake haujakaa sawa na ndiyo maana nimemshikilia hivi." Rachel alimjulisha Husna akiwa kanishikilia kiunoni kama sapoti nisije dondoka.

"Kafanyaje tena?" Husna aliuliza. 

"We acha tu ndugu yangu lakini tunachoshukuru Mungu ni kuwa amepata tiba kwa kwa mzee wetu Nyaswa hakuwa hivi unavyomuona siku tatu nyuma." Rachel alimjibu.

"Mzee Nyaswa! kuna watu wanamuamini sana kwenye tiba zake hasa wa mbali lakini mimi sioni chochote anachokifanya zaidi ya utapeli tu." Husna aliongelea suala la tiba za mzee Mbogo.

"Lakini kwenye hilo inategemea inawezekana huoni mchango wake kwako kutokana na huduma ambayo ulikuwa unaihitaji yeye si mtaalamu nayo." Niliona nichangie na mimi juu ya hilo kutokana na ninavyojua. Tulikuwa tukizungumza hayo tukiwa sebuleni kwake Husna, sebule ambayo ilikuwa imepambwa vilivyo kama ya Rachel tu utofauti ni ukubwa tu hii ya Husna ni ndogo.

" Usemacho Tina ni kweli kabisa, huyu rafiki yangu alikwenda kutafuta dawa ya kupendwa na wakubwa wake kazini akawa kasahau kuwa yule mzee ni Mtaalamu wa magonjwa tu." Rachel aliungana nami.

"Sawaa sasa kama yeye hakuwa na utaalamu huo kwanini alikubali kunifanyia dawa?" Husna aliuliza.

"Inategemea ulikwenda kipindi gani? Kama ujuavyo hela inapendwa na kila mmoja hivyo ingekuwa ngumu yeye kusema hawezi kukutibu wakati ana shida na hela kwa wakati huo." Rachel alimjibu Husna.

"Hebu tuachane na hayo kwanza yalishapita tayari mgeni unatumia kinywaji gani?" Aliniuliza.

"Naomba tu maji kama yapo." Nilimjibu. Aliinuka na kabla hajaondoka alimgeukia Rachel akamtazama kwa muda.

"Wewe tunajuana hivyo kuwa mpole." Aliongea na kuelekea lilipokuwa friji alilifungua na kutoa kopo dogo la maji pamoja na glasi akaniletea.

"Karibu Tina."

"Asante." Nilimjibu na kuipokea glasi pamoja na maji ambayo niliyafungua na kuyamimina kwenye glasi na kuanza kunywa.

"Wala usijihangaishe huko naomba tu glasi nyingine nitakunywa tu maji na dada Tina." Rachel alimwambia Husna baada ya kumuona akiwa na kikapu akiwa anataka kutoka.

"Au umeokoka mwenzangu?" Husna alimuuliza Rachel baada ya kurudi na kuketi.

"Naomba kwanza glasi ndiyo hayo maswali mengine yafuate bwana." Alimjibu.

"Glasi zile pale kwenye kabati kachukue mwenyewe umeshanikata stimu mimi." Husna alimgomea Rachel na hivyo aliinuka mwenyewe na kuifuata.

"Unajua nini Husna si kila gari unaloliona barabarani limetengenezwa na mzungu." Rachel alimwambia Husna baada ya kurejea.

"Kumbe?" Alimuuliza.

"Mengine yametengenezwa na Waafrika." Alimjibu.

"Unamaanisha nini kusema hivyo?" Husna ni kama hakumuelewa Rachel akamtupia swali jingine.

"Unakariri sana rafiki yangu, mimi Pombe nilishaacha niliona zinanipeleka kubaya." Alimjibu.

"Makubwa!! Wewe si ulikuwa ukinicheka kipindi kile?"

"Ndiyo, sikujua nini kitanitokea mbele ya safari." Rachel alimjibu huku akiitazama simu yake ambayo ilikuwa ikiita.

"Ni babu huyu anapiga atakuwa ameshafika kwa mzee Mbogo." Kabla ya kuipokea aliniambia mpigaji ni nani kisha akaipokea.

"Sawa babu tupe kama dakika kadhaa tutakuwa hapo." Aliijibu hivyo tu na kisha kuikata.

"Rafiki yangu ee tunatakiwa kuondoka babu keshafika kwa mzee Mbogo hivyo tutakuja wakati mwingine." Aliongea Rachel akinishika mkono.

"Ndiyo nini sasa si mngebaki huko huko kuliko kuja kunionjesha tu kisha kuondoka." Alilalamika Husna.

"Siyo sisi wewe mwenyewe umeona kilichotokea hapa." Rachel alijitetea kwa rafiki yake huku tukiwa tunalikaribia gari.

"Tina umeshapafahamu kwangu wakati mwingine karibu bila hata kumngojea chizi wangu huyo." Alinikaribisha Husna wakati mwingine.

"Bila shaka ndugu yangu kwanza nimefurahi kukufahamu." Nilimjibu huku Rachel akimpa ishara ya sikio akimaanisha kuwa watachekiana kwenye simu kisha akaondoka gari. Ndani ya muda fulani tukawa ndani ya Inyara na moja kwa moja tukaiacha barabara kuu na kuingia barabara ya vumbi ambayo ilitupeleka mpaka nyumbani kwa mzee Mbogo na kuwakuta wakiwa wanachambua majani fulani sijui zilikuwa ni mboga au nini, Rachel alipaki gari na kushuka kisha akaja upande wangu na kunipa sapoti ya kushuka.

"Taratibu dada." Alinisihi.

"Sawa." Nilimjibu.

"Wajukuu zangu mlikwenda wapi tena?" Mzee Mbogo alituuliza.

"Tulitoka kidogo babu lakini hatukuwa mbali sana." Alimjibu.

"Sawa Rachel lakini kumbuka kuwa haya si mazingira salama kwenu." Mzee Mbogo alitoa tahadhari.

"Tusamehe babu." Aliomba radhi Rachel.

"Limeisha hilo Rachel." Babu alimjibu kwa kifupi kisha akainuka kutoka pale ambapo ameketi na kuingia ndani.

"Rachel mlete mwenzako huku ndani." Alituita.

"Sawa babu." Tuliinuka na kuingia ndani na huku mzee Nyaswa akiwa bado bize na majani yake pale chini.

Baada ya kuingia ndani tulimkuta mzee Mbogo ameshika mkoba wangu mkononi.

"Mjukuu wangu hebu kagua vitu vyako kama vipo vyote maana nimekabidhiwa tu na Bi Kiziwa bila hata kukagua. Ningekagua nini wakati sifahamu kilichomo ndani." Babu aliongea huku akinikabidhi ule mkoba wangu. Na baada ya kuukagua nilikutana na kila kitu kilicho cha kwangu kisha nilimtazama babu usoni.

" Nakushukuru sana babu yangu kwa kila ulilolifanya juu yangu sina cha kukupa ila Mungu ndiye ambaye atakulipa."

"Wala usijali wewe ni mjukuu wangu kama alivyo Rachel hivyo kukusaidia ilikuwa jukumu langu hivyo mnaweza kuendelea na mambo yenu kama kila kitu umekiona." Alinijibu mzee Mbogo. Baada ya mzee Mbogo kutoka nje na kutuacha peke yetu ndani niliomba simu ya Rachel na kuipiga namba ya mama na safari hii iliita kitendo hicho kilinifurahisha sana na dakika chache mama aliipokea.

"Nani mwenzangu?" Mama aliuliza baada ya kuipokea simu.

"Mama shikamoo!!" Nilianza kwa kumsalimu.

"Marhaba lakini sijakufahamu ni nani?" Alijibu lakini bado akawa hajanifahamu.

"Mama bwana, mimi mwanao." Nilimjibu.

"Mwanangu? Wa wapi?" Aliendelea kuniuliza.

"Kwani wewe una watoto wa kike wangapi?" Nilimuuliza.

"Kwamba wewe ni Christina?" Aliniuliza swali kwa sauti ya chini kidogo.

"Ndiyo mama." Nilimjibu.

"Hivi umepatwa na nini wewe kiasi cha kutopatikana hewani hujasema kama umefanikiwa kupata nafasi badala yake hata kwenye simu ukapotea hewani umepatwa na nini?" Ni swali ambalo nililitegemea.

"Ni kweli mama yangu lakini kila kitu kiko sawa isipokuwa tu niliibiwa simu yangu hii yenyewe nimeiazima kwa rafiki yangu japo siku ya kesho nitairudisha laini yangu." Niliona nimdanganye tu sikuwa na jinsi.

"Sawa, kamilisha mambo yako haraka urejee nyumbani ili tuanze maandalizi kwa ajili yako." Mama alisisitiza.

"Sawa mama yangu." Nilimjibu mama kisha nikaikata na kumrejeshea Rachel simu yake na baada ya hapo tulitoka nje mpaka kwenye gari tukapanda na kutegua viti na kujilaza na muda huu hata maumivu ya mwili yalishapungua kwa kiasi fulani.

"Rachel kwanini usiongee na babu aongee na mzee Nyaswa turudi mjini ili kesho nikafanye mchakato wa chuo."

"Ngoja wamalize mambo yao ya dawa kwanza kisha nitazumgumza naye na si unajua tena chuma chetu hiki hata usiku wa manane tutachomoka tu, unahofu katika hilo?" Alinijibu na kisha akamalizia na swali.

"Sina hofu kabisa kwa sababu nikiwa na wewe najiona mshindi Rachel." Nilimtania.

"Acha kunijaza dada Tina." Aliiona hivyo akaipangua. Tuliendelea na mazungumzo mle ndani ya gari mpaka tulipoitwa na mzee Nyaswa ambaye alitueleza kuwa kaongea na mzee Mbogo juu yetu hivyo tutatakiwa kuondoka jioni kurudi mjini na kwa kuwa babu alikuwa chooni aliporejea naye alithibitisha hilo na kututaka tufanye maandalizi ya safari wakati wao walitoka kwenda kwa mzee mmoja anayeishi nyumba ya nyuma kama mita mia mbili hivi kwa ajili ya kupata ulanzi, maana inasemekana mzee huyo ni muuzaji wa muda mrefu wa kinywaji hicho chenye asili ya mkoa wa Iringa.


JE SAFARI YA CHRISTINA JUU YA KUTAFUTA NAFASI YA CHUO ITAFANIKIWA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUPATE KUJUA.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post