IMETOSHA MAMA MKWE - 29 (Mtunzi: Sultan Uwezo)


 IMETOSHA MAMA MKWE - 29

sultanuwezotz.blogspot.com 


Hatukuwa na la ziada zaidi ya kuianza safari ya kurudi mjini tukiwa na babu mzee Mbogo, tulitembea kwa takribani saa moja hivi na hii ilitokana na msongamano wa malori eneo la Mlimanyoka kuelekea Uyole hivyo ilitufanya tufike nyumbani mida ya saa mbili na vidakika kadhaa.

"Kweli nyakati zinakwenda sana yaani binti mdogo kama wewe unapishana na magari kiasi hicho wakati enzi zetu mabinti wa umri wako walikuwa wakibakia majumbani wakifanya kazi za nyumbani jamani." Mzee Mbogo alimwambia mjukuu wake Rachel wakati akilipaki gari ndani ya nyumba yake.

" Babu elewa kwamba zamani imebakia kuwa historia kama ambavyo hata haya yatasalia kuwa historia huko mbeleni." Rachel alimjibu babu yake.

" Babu bwana kwa hiyo umewazaa kwa anachokifanya Rachel kiasi cha kukufikisha mbali."

"Wee acha tu mjukuu wangu." Mzee Mbogo alinijibu.

Sikuamini kama tumefika salama mjini kutoka huko kijijini ambako bila kuugua sidhani kama ningefika lakini ndiyo hivyo ikawa imetokea, niliingia chumbani na kitu cha kwanza ikawa ni kuliangalia lile eneo ambalo lilisababisha kukutana na sura ya kutisha ya Bi Kiziwa nililiangalia kwa muda lakini lakini hakuna ambacho kilitokea nikajivuta mpaka kitandani ambako nilijilaza kwanza maana nilichoka kiasi.

"Dada Tina!! Dada Tina!!" Rachel aliniita.

"Abee!!"

"Hebu njoo usiniambie kama umelala." Aliniambia.

Niliamka na kwenda kuufungua mlango na kumkuta akiwa bado hajaondoka.

"Kama umeota vile kiusingizi kilianza kunichukua."

"Umelala sana dada Tina ni muda wa kula."

"Chakula? Umepika saa ngapi?" Nilimuuliza.

"Aahh hebu twende bwana kupika ndiyo mtaa gani nilitoka na kwenda kununua hapo mtaa wa nyuma kama ni masuala ya kupika tutafanya hivyo kesho."

Tuliongozana mpaka sebuleni ambako ni kweli chakula kilikuwa tayari.

"Mbona babu haji?" Niliuliza mara baada ya kuona kimya.

"Utamuweza babu yangu dada keshaondoka, kasema ana majukumu mengi ya kufanya usiku wa leo hivyo sikuwa jeuri ya kupingana naye maana huwa akisema hivyo harudigi nyuma yule mzee." Rachel alijibu.

"Mhh kweli babu yuko bize ni kazi gani hizo ambazo masaa yote ni kiguu na njia?"

"Achana naye uzuri ana kwake atajua mwenyewe sisi tule zetu mengine yafuate." Tulipakua chakula na kuanza kula na kwa kuwa siku kadhaa nilikuwa naumwa sikupata hamu ya chakula hivyo siku ya leo ilikuwa kama ndiyo nakionja kwa mara ya kwanza hali ile ilimshtua mpaka Rachel.

" Dada Tina!" Aliita.

"Nambie mdogo wangu."

"Kwenye friji kuna maziwa ya mgando kama hutojali." Alinijibu.

"Maziwa na baridi yote hii hapana labda kesho kwanza hapa nimeshatosheka."

"Enhh nimekumbuka dada Tina."

"Umekumbuka nini tena?" Nilimuuliza.

"Pale juu ya kabati nimeikuta simu yako, kumbe niliiweka ile siku."

"Iko pale pale?" Nilimuuliza.

"Yaa iko pale pale." Alinijibu.

Huwezi amini ni kiasi gani nilifurahi baada ya kusikia hivyo niliinuka haraka na kwenda kuichukua na baada ya kuichukua kitu cha kwanza ilikuwa ni kuiwasha kuona kama nilitafutwa na watu wangu wa karibu.

"Christina mpenzi wangu naomba unisamehe kwa yote niliyokufanyia kiasi cha kunichukia. Nimelijua kosa langu na kamwe siwezi kulirudia tena. Christina kumbuka kuwa ulishanitambulisha kwa mzazi wako na anahitaji kuniona unafikiri atahisi nini iwapo atajua tumefarakana kwa sababu zisizo na mashiko? Nipe nafasi ya mwisho mpenzi uone kama nitakukwaza. Kingine mpenzi ni kwamba nimeshapata nafasi tayari kilichobaki ni maandalizi tu... " Ilikuwa ni ujumbe kutoka kwa Jofrey ambao niliusoma mara mbili mbili baada ya kuingia kwani pamoja na mafarakano yetu kiukweli nilishindwa kumtoa akilini na moyoni Jofrey.

" Mshenzi wewe unayafanya haya yote kwa sababu unajua kuwa nakupenda.. " Nikiwa nimezama kwenye lindi la mawazo kumbe Rachel alikuwa akinichora tu.

"Tina kuna nini mbona unatabasamu mara unakunja sura umepatwa na nini?" Aliniuliza na ndipo nilipobaini kuwa nauza ramani mbele ya Rachel hivyo nikainuka na kumuaga pasipo kujibu swali lake.

"Naomba nikutakie usiku mwema mdogo wangu."

"Okay sawa, lakini kama kuna chochote ambacho kitakutatiza usisite kunijulisha si unajua mimi ndiyo Kamanda wako kwa sasa."

"Katika hilo wala usijali mdogo wangu nakuaminia kwa asilimia zote." Nilimjibu na kuondoka kuelekea chumbani huku nikimuacha akiendelea kuchezea simu yake. Nilipoingia chumbani niliubana vizuri mlango kisha nikavalia vazi langu la kulalia na kujongea kitandani na kuichukua simu yangu ili kuendelea kuupitia upya upuuzi wa Jofrey ambao ulianza kuniingia.

"Mama mbona hurudi nyumbani au ndiyo tayari umetususa huku nyumbani?" Ulikuwa ni ujumbe ulioingia muda mfupi kutoka kwa mwanangu Thobias akiitumia simu ya mama. Moyo ulipiga paaa mara baada ya kuuona ujumbe wa mwanangu kipenzi hapo hapo nikaona nisipoteze muda nikapiga ile namba ya mama.

" Mwanangu?" Mama aliita.

" Abee mama." Niliitika.

"Kwema huko uliko?"

"Ni kwema tu mama yangu kungekuwa na tatizo ningekujulisheni." Nilimjibu japo ni kwa uongo kwa sababu sikutaka kuwapandisha presha wazazi wangu hivyo ilikuwa lazima nifanye hivyo.

"Sawa mwanangu, baba yako kasafiri kuelekea jijini Arusha kuna semina sijui ya nini anatarajia kurejea keshokutwa."

"Nashukuru kwa taarifa mama yangu na mimi mambo yakienda kama nilivyoyapanga nategemea kurejea nyumbani keshokutwa maana kuna vitu vichache sijavikamilisha natarajia kuvikamilisha kesho. Na vipi mwanangu anaendeleaje maana kuna ujumbe aliutuma."

"Aliutuma kwako?" Aliniuliza mama kwa mshangao kidogo.

"Ndiyo, mbona kama unashangaa hivi wakati alitumia simu yako ina maana hukumpa?" Nilimuuliza.

"Bwana yangu namfahamu vizuri kwa vyovyote vile aliivizia kwenye chaji akakutumia huo ujumbe mimi sikumpa simu." Alinijibu.

"Makubwa, yuko wapi sasa?"

"Kalala kitambo sana kajichokea hovyo hovyo walikuwa kwenye mpira sasa sijui litimu lake limefungwa? Maana kafika hapa kala chakula na kuaga anakwenda kulala." Alinijibu.

"Basi utamwambia kesho tuwasiliane kabla sijaanza pilika zangu."

"Haina shida mwanangu, nikutakie usiku mwema na kingine usisahau kuja na mkwe wangu."

"Mama nawe hausahau tu? Basi sawa." Nilimjibu na kisha nikaikata simu na muda huo huo nikaiangalia ile namba ya Jofrey mara mbili mbili huku kidole kikitamani kuibonyeza. Na baada ya kutafakari kwa muda nikaamua kumpigia.

"Hey love." Yalikuwa ni maneno yake ya kwanza mara baada ya kupokea simu.

"Habari yako Jofrey?"

"Usinifanyie hivyo mpenzi yaani leo hii umeamua kulitaja jina langu kabisa kumaanisha kuwa huna mapenzi na mimi tena." Aliongea mara baada ya kulisikia jina lake kutoka kinywani kwangu.

"Naomba unisikilize vizuri Jofrey achana na ngonjera zako mimi ndiye niliyekupigia hivyo tega sikio lako vizuri."

"Kuna nini Tina? Niko tayari hata kulamba nyayo za miguu yako ilmradi tu unisamehe makosa yangu nakosa usingizi kwa ajili yako."

Jofrey aliendelea kuniomba msamaha.

"Sihitaji kuyasikia maneno yako Jofrey kitu kimoja tu ni wewe siku ya kesho kuonana na mimi Sky Hotel mida ya saa nne asubuhi tofauti na hapo usinitafute tena, umenielewa?" Nilijitahidi kumchimba mkwara mbuzi.

"Nimekuelewa Tina nitafanya hivyo." Alinijibu kisha mimi nikaikata simu. Nilifurahi sana kuisikia sauti yake mpenzi wangu Jofrey kwani pamoja na yote yaliyotokea lakini bado namhitaji japo sikutaka kumuonesha wazi hilo. Baada ya kuhakikisha kila kitu kiko tayari niliizima simu na kulala.

"Waoo Tina wangu ulikuwa wapi siku zote hizi? Yaani huwezi amini hata kidogo sikuweza kupata usingizi nikifikiria mazingira ambayo tuliachana. Na kwa kukudhihirishia kuwa nimekuja kukuomba msamaha wa dhati nimeona nije na mama yangu mzazi." Jofrey alifunguka.

"Mama yako? Noooooo... Jofrey haiwezekani hata kidogo." Nilipiga kelele mara baada ya kuota Jofrey akinitambulisha kwa mama yake mzazi ambaye ni Bi Kiziwa. Hakika nilijikuta nimeloa mwili mzima kwa jasho wakati kulikuwa na baridi la kutosha.

"Dada Tina kuna nini tena?" Rachel alifika mlangoni na kuugonga.

"Ni ndoto tu Rachel wala hakuna jingine." Nilimjibu.

"Hapana hebu fungua mlango mara moja." Hakuwa tayari kuyakubali maneno yangu.

"Nielewe mdogo wangu nimeota ndoto ya kutisha tu na si kitu kingine naomba unielewe kwa hili."

"Mmh haya bwana usiku mwema." Ilibidi tu akubali hata kwa shingo upande. Na hapo ndiyo nilipitiwa na usingizi mzito ambao ulinipeleka mpaka asubuhi.

"Umejihimu kiasi hicho?" Nilimuuliza Rachel baada ya kumkuta akimwagilia maua.

"Nimeona niamke mapema ili nijiandae kwenda kazini si unajua niliomba ruhusa ya wiki moja?"

"Ndiyo sasa imeisha?" Nilimuuliza.

"Hapana nimepigiwa simu kazini wakinitaka nifike leo kuna kikao cha kimkakati ambacho ni cha muhimu sana kwa kampuni." Alinijibu.

"Okay vizuri kumbe wacha tujiandae pamoja ili unapoelekea kazini na mimi nielekee chuoni nikafuatilie nafasi kama vile nilivyokueleza."

"Hakuna tatizo kumbe tufanye maandalizi ya kifungua kinywa kwanza kisha mengine yafuate." Alinijibu hivyo nilimuacha na kuelekea ndani kuandaa chai. Nikiwa jikoni naandaa chai simu yangu iliita sebuleni hivyo ikabidi nitoke kuipokea.


JE NI NINI KINAKWENDA KUTOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII YA KUSISIMUA.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post