IMETOSHA MAMA MKWE - 30 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


IMETOSHA MAMA MKWE - 30

sultanuwezotz.blogspot.com 


Niliipokea simu ile ambayo iliingia kwa namba ngeni ambayo sikuitambua.

"Nani mwenzangu tafadhali." Niliuliza baada ya kupokea.

"Habari yako Christina." Alinisalimu.

"Nzuri sijui naongea na nani?" Niliuliza tena.

"Shikamoo mama!" Alinisalimu.

"Marhaba, Ni nani huyu?" Nilimuuliza.

"Mama mimi ni Thobias nimeazima simu ya rafiki yangu." Alijitambulisha mwanangu kipenzi.

"Jamani habari ya huko mwanangu? Mama yako naendelea vizuri na muda si mrefu nitarejea nyumbani kuungana nanyi." Nilimuondoa wasiwasi hata kabla ya kueleza shida yake ninamfahamu vizuri Thobias.

"Sawa mama nimekupigia baada ya kuona kimya wakati sisi huku tumekukumbuka sana, pia unaporudi usisahau kuja na mananasi nasikia ni mazuri sana ya huko."

"Wala usijali mwanangu nitakuletea zawadi nyingi sana ambazo utashindwa mwenyewe kuzikabili."

"Nitashukuru mama."

"Haya utamsalimu bibi yako."

"Sawa mama." Alinijibu na kukata simu, nilirudi ndani nikamalizia maandalizi ya jikoni kisha tukapata kifungua kinywa na baada ya hapo tukajiandaa na kuondoka huku Rachel akielekea kazini kwake, hivyo alinichukua na kuniacha Mwanjelwa ambapo mimi niliingia kwenye bodaboda kuelekea Sky Hotel na kumuacha Rachel akigeuza gari lake na kuishika barabara ya kuelekea kiwandani kwao. Usafiri wa bodaboda haukuchukua dakika nyingi nikawa Sky Hotel iliyo eneo la Soweto.

"Bila shaka ni hapa dada yangu." Aliniambia dereva bodaboda.

"Ndiyo penyewe kaka." Nilimjibu akasimama na mimi nikashuka nikampa ujira wake kisha nikaachana naye moja kwa moja nikaongoza mpaka ndani ya Hotel. Lakini nikiwa napanda ngazi kuelekea mapokezi mara simu yangu iliita.

"Niko hapa nje." Alikuwa ni Jofrey.

"Umeniona?" Nilimuuliza.

"Nimekuona ndiyo si uko hapo ngazini, sasa geuka na urudi nyuma kisha angalia upande uliko mwamvuli wa safari lager utaniona." Alinielekeza na hivyo nilirudi nyuma na kuutafuta huo mwamvuli, kama bahati niliuona. Niliufuata na chini yake aliketi Jofrey akiwa na mtu mwingine ambaye sikumtambua.

" Karibu Christina." Jofrey alinikaribisha akinionesha kiti kilichokuwa tupu.

" Asante nashukuru." Nilimjibu nikikivuta kiti. Niliketi na kuwasabahi wote wawili.

"Tina huyu ni rafiki yangu anaitwa Gembe." Kisha alimgeukia Gembe.

"Gembe huyu anaitwa Christina habari zake unazo si unakumbuka nilikusimulia ee." Alimwambia.

"Shemeji karibu sana jijini Mbeya kama alivyosema Jay mimi ni rafiki yake na kwa bahati nzuri tutakuwa chuo kimoja mimi na yeye maana mimi niko mwaka wa kwanza na mwakani nitakuwa wa pili kwa majaliwa yake Allah ninyi mtakuwa mwaka wa kwanza." Alijieleza kama kalipwa vile.

" Nashukuru Gembe, lakini unatakiwa kurekebisha kauli yako siyo shemeji yako na pia unajuaje kama nitakuwa kwenye chuo unachosoma?" Nilimuuliza nikiwa nimemkazia macho kama afisa upelelezi.

" Mmhh siyo kesi Tina naomba unisamehe ilikuwa ni utani tu." Aliniomba msamaha na kitendo kile kilimfanya Jofrey kuinamisha kichwa chini kwani alijua kaumbuka tayari kwa yale aliyomweleza Gembe.

" Wala usijali Gembe limepita hilo, mmhh sorry naomba nimtoe kidogo rafiki yako nina mazungumzo naye mafupi tu." Nilimuomba Gembe.

"Wala usijali mnaweza kutumia hapa hapa mimi kuna kijisehemu naelekea nitapita hapa baada ya dakika kadhaa hivi." Alinijibu akimkonyeza Jofrey.

"Lakini mimi sijakufukuza Gembe!"

"Wala si hivyo Tina." Alinijibu akiinuka.

"Sasa mwana kama kawaida usichelewe sana." Jofrey alimwambia Gembe akiishia getini.

"Wala usijali dakika chache nitakuwa hapa." Alimjibu akitoka nje.

"Samahani dada naomba nikuhudumie tafadhali." Alikuja mhudumu na kuniuliza.

"Niletee maji madogo yanatosha." Nilimjibu.

"Hee kwanini usiagize kifungua kinywa cha nguvu?" Jofrey aliingilia kati.

"Una maanisha nini?" Nilimuuliza.

"Yaani kwanini usiagize hata chai au supu?" Alinijibu.

"Dada kaniletee maji tu." Nilimtoa yule mhudumu.

"Chai nilishakunywa tayari nyumbani niko fiti kabisa." Nilimjibu.

"Nyumbani wapi tena wakati wewe hapa ni mgeni?" Aliniuliza.

"Wewe ndiyo unasema hivyo hujiulizi siku zote hizi nilikuwa wapi? Lakini hayo hebu tuachane kwani siyo yaliyonileta hapa." Nilimjibu.

"Ina maana hujaja kunisikiliza?" Aliniuliza.

" Kukusikiliza nini Jofrey hivi kati yako na mimi ni nani alimpigia mwenzake?" Nilimuuliza.

" Wewe ndiye uliyenipigia."

" Sasa iweje nije kukusikiliza?"Nilimuuliza.

" Oohh naomba unisamehe."

" Nilishakusamehe ila kilichonileta hapa ni kitu kimoja tu ambacho ni kukuambia kuwa mimi na wewe tulitaka kuwa wanandoa lakini kwa mambo yako ya kijinga yamesimamisha mchakato hivyo kwa sasa nitaomba uniache kwanza kuna vitu navifuatilia kwanza na kwa kipindi hiki usinisumbue hata chembe kwani unaweza kunikosa kabisa."

"Aaaagh Christina usinifanyie hivyo kumbuka kuwa nimeyajua makosa yangu yote na kufikia hatua ya kukutafuta usiku na mchana ili nikuombe msamaha mpenzi wangu kwa hilo sikufanikiwa kwani hewani ulikuwa hupatikani mpenzi." Aliongea hayo huku akipiga magoti pasipo kujali kama kuna watu wanaomtazama.

" Ndiyo unafanya nini hapa hebu niondolee uchulo wako hapa bwana." Nilimsukuma na kuinuka pale nilipokuwa nimeketi na kuondoka.

" Anti, anti.... " Niliitwa na mhudumu wa ile hoteli.

"Unasemaje?" Nilimuuliza.

"Hujalipia maji." Alinijibu.

"Oohh sorry njoo uchukue." Nilimjibu na kutoa shilingi elfu moja na kuiweka kwenye meza iliyokuwa pembeni yangu na kuondoka.

"Tina hebu punguza hasira basi, mimi ni binadamu kama binadamu wengine kuteleza ni moja ya safari katika maisha ya ndoa hivyo usiponisamehe unafikiri itakuwaje unataka nife kwa ugonjwa wa penzi lako Tina? Please naomba tuyaongee haya mpenzi niko tayari kuongea kila kitu kilichopelekea tukafarakana." Aliendelea kuniomba msamaha huku akiwa kapiga magoti nje ya geti huku waliokuwa wakipita barabarani wakitukodolea macho kitu ambacho kilinifanya nione aibu kwani yaliyokuwa yakitokea sijawahi kukutana nayo kabisa. Mwisho wa siku nikajikuta nikifanya maamuzi magumu.

"Hebu inuka bwana." Nilimuinua na wakati huo huo nikiipa ishara Bajaj ilikuwa imepaki ng'ambo ya Hotel. Tuliingia haraka na kumtaka mwenye Bajaj atukimbize maeneo ya nane nane kilipo chuo cha ualimu cha st. Aggrey.

"Mtanipa shilingi elfu tano." Alituambia tukiwa njiani.

"Acha hizo au unafikiri sisi ni wa kuja hapa mjini? Utapata shilingi elfu tatu tu." Nilimjibu.

"Dada yangu lakini mafuta yamepanda sana bei hivyo ongeza kidogo."

"Unafikiri hata nikikupa shilingi elfu ishirini hapa itatosha kwenye mafuta? Msiwe hivyo bwana kuweni na huruma hata kidogo kwa abiria wenu."

"Yaishe dada yangu utanipa hiyo hiyo." Alinijibu hivyo baada ya kuona nimemkomalia na wakati huo Jofrey alikuwa kajiinamia tu macho yakiwa nje sijui ilikuwa ni aibu sijui hilo. Tuliendelea na safari mpaka pale ambapo tulifika nje ya geti la chuo tukashuka.

" Niwasuburi? "Dereva Bajaj aliuliza huku akipokea hela yake.

" Kwa bei zako hapana unaweza kwenda tu tutapanda daladala na hata hivyo tutachukua muda mrefu kidogo hivyo sidhani kama tutakutendea haki." Nilimweleza.

" Basi sista wacha mimi niwaache." Alinijibu huku akigeuza Bajaj na kuondoka huku sisi tukiingia ndani ya chuo. Tuliongoza mpaka kwenye jengo la Utawala ambako huko niliingia mwenyewe huku Jofrey yeye akisalia nje. Huko nilikamilisha kila kitu kilichotakiwa kwa wakati huo.

" Binti una bahati sana maana leo ndiyo siku ya mwisho ya kupokea maombi, hivyo mshukuru Mungu." Alinieleza msajili ambaye muda wote alikuwa kajaa tabasamu kitu ambacho kilinifanya kujiona huru ikiwa ni pamoja na kuuliza maswali ambayo yalinitatiza.

"Nikushukuru mama yangu kwa kunisaidia katika kulifanikisha hili, niseme asante sana." Nilimjibu nikiagana naye.

"Haya lakini jitahidi muhula utakapokuwa unaanza nawe uwe umefika ili usije achwa kimasomo." Alinisihi.

"Nitajitahidi mama yangu." Nilimjibu kisha nikamuaga na kutoka nje ambako nilimkuta Jofrey akiwa ananisubiri kwenye kiti cha wageni.

"Vipi wamesemaje?" Jofrey aliniuliza.

"Kila kitu kimekwenda sawa tunaweza kuondoka." Nilimjibu huku nikitoa simu yangu kutoka kwenye mkoba.

"Ashukuriwe Mola katika hili." Alinyoosha mikono juu kushukuru kwa alichokisikia japo mimi niliona ni kama ananifanyia maigizo tu hivyo sikumjali nikaitafuta namba ya mama na kumpigia.

"Ndiyo mwanangu hujambo!" Aliitika baada ya kupokea.

"Mama kesho niko barabarani huku kila kitu kimekwenda vizuri na kuanzia sasa mimi ni mwanachuo mtarajiwa mama yangu." Nilimweleza kila kitu.

" Asante Mungu kwa kumuona mwanangu katika hili, asante sana. Mwanangu ukifika itabidi twende kanisani tukatoe sadaka ya shukrani." Alifurahi sana mama yangu.

" Wala usijali mama yangu tutafanya hilo mara tu nikifika."

" Siamini itakuwaje baba yako akipata hizi taarifa. Enhh na vipi kuhusu mama yako mlezi mama Fabiana?" Mama aliniuliza.

" Nitamtembelea lakini ni baada ya kurudi kwanza nyumbani." Nilimjibu.

"Hilo linabaki mikononi mwako mimi hapa ni burudani tu mwanangu." Alinijibu na kisha nikaikata simu na kuiweka mkobani kisha nikamgeukia Jofrey.

"Enhh niambie." Nilimuanza Jofrey makusudi tu nimsikie anasemaje.

"Unafikiri nitasema nini mimi kwa sasa ni mnyonge wako nakusikiliza wewe tu utakalolisema kwangu ni tiki tu." Alinijibu huku akiutaka mkoba wangu anisaidie.

"Unataka kufanya nini?" Nilimuuliza.

"Nipe nikusaidie au hupendi." Alinijibu.

"Unajua nini Jofrey usifanye kwa sababu tu kuna kosa umefanya iwe kama njia ya kujisafisha, kuwa kawaida tu maigizo hayafai yasije amsha mengine." Nilimtahadharisha.

"Mmh haya bwana uelekeo ni wapi?" Aliniuliza tukiwa tumefika barabarani.

"Hapa tunaelekea Uyole tutakuwa kwenye Hotel yoyote ile yenye utulivu." Nilimjibu.

"Okay basi hoteli yenye utulivu ni Twitange Restaurant ambayo iko nje kidogo ya mji nafikiri itatufaa zaidi."

"Tuelekee hapo na sidhani kama utanificha kitu kitu chochote leo kwa kile kilichotokea." Nilimwambia hayo Jofrey huku tukiisimamisha daladala iliyokuwa ikija.

"Wala usijali nikufiche ili nini kitokee?" Aliniuliza.

"Sijui mwenyewe." Nilimjibu tukiingia kwenye daladala na safari ya kuelekea Uyole ilianza.


JE NI NINI KINAKWENDA KUTOKEA HUKO?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA KIGONGO HIKI.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post