IMETOSHA MAMA MKWE - 31 (Mtunzi:Sultan Uwezo)

 


IMETOSHA MAMA MKWE - 31

sultanuwezotz.blogspot.com 


Daladala tuliyopanda ilikuwa ikielekea Igawilo hivyo sisi tulishuka stendi ndogo ya mabasi yanayoelekea Tukuyu, Kyela na Makete hapo tuliifuata barabara inayoingia ndani ya soko na kisha tulilizunguka na kisha tulikifuata kiuchochoro kilichotupeleka mpaka upenuni mwa Restaurant ya Twitange.

"Ndiyo nini kunipitisha uchochoroni wakati kuna barabara nzuri kabisa ya kuja hapa?" Nilimuuliza Jofrey baada ya kuona tumepita uchochoroni wakati kuna barabara ambayo ni ya vumbi lakini usafiri wa aina yoyote unapita.

"Nisamehe bure kama umekwazika kupita kwenye kinjia hicho lakini nimefanya hivyo kwa kuwa ndiyo njia ambayo nilipitishwa na rafiki yangu na hivyo ndiyo niliishika haraka." Masikini Jofrey wangu alijieleza huyo vile anaomba kura kwa mwananchi.

"Kinachonishangaza pembezoni kote huku mlifuata nini?Usikute ndiyo ile siku ulikuwa unaona kama vile nakuchelewesha kwenye vinyapu vyako."

"Tina naomba tuingie kwanza mengine tutaongea huko ukinilaumu hapa utakuwa unanionea tu." Aliona anisihi tuingie ndani kwani alijua nakwenda kumpokonyoka kwa mara nyingine.

Nilitulia kama alivyotaka tukaingia ndani ya hii Restaurant ambayo ukiiangalia kwa nje unaweza kuidharau kutokana na makuti yaliyotumika lakini ndani ilikuwa na muonekano wa kipekee,kulikuwa na watu wachache wakipata vinywaji na vyakula mbalimbali na kilichonishangaza ni baada ya kuwaona na watu wa mataifa ya nje wakiwa mle ndani. Kingine ilikuwa ni mirindimo ya muziki uliokuwa ukigonga mle ndani haukusika nje wala sauti yake haikuwa ya juu kama ilivyo maeneo mengine hapa unaongea na jirani yako na mnaelewana vizuri kabisa. Ilinivutia sana na kujikuta nikibaki nimeganda kama masanamu ya yaliyojazana kwenye maduka ya nguo utafikiri misukule inayoita wateja.

"Tina mbona umeduwaa kiasi hicho?" Jofrey aliniuliza baada ya kuona sivuti hatua kwenda mbele wala kurudi nyuma.

"Hapana Jofrey ni mazingira tu ya humu ndani sikuyatarajia hata kidogo." Nilimjibu.

"Hebu twende tukaketi pale karibu na wale weupe labda tunaweza kunukia kikwaokwao." Aliniambia huku akinishika mkono, tulifika na kuchukua nafasi kwenye moja ya viti vilivyokuwa tupu karibu kabisa na wale wazungu.

"Karibuni, naitwa Fasha ni mmoja wa wafanyakazi wa Twitange Restaurant naomba kuwahudumia." Alifika huyu mhudumu akiwa kapambwa na tabasamu pana usoni kwake nafikiri ni mbinu ya kuwavutia wateja.

"Naomba uniletee samaki mmoja pamoja na soda ya baridi." Nilimwambia baada ya kuiangalia ile orodha iliyosheheni hudumu zinazotolewa hapo.

"Sorry dada yangu soda gani?" Aliniuliza tena.

"Itapendeza zaidi kama itakuwa pespi ya chupa." Nilimjibu kisha akamgeukia Jofrey ambaye alikuwa bado akiipitia ile orodha.

"Kaka yangu na wewe?" Alimuuliza.

"Kama ulivyoagizwa na mimi ni hivyo hivyo." Alimjibu huku akiniangalia mimi.

"Mbona macho kwangu?" Nilimuuliza.

"Wala sikuangalii wewe naangalia wale jamaa wanaopiga picha pale." Ilibidi nigeuke kuangalia hao anaowasema kama ni kweli au la, Ni kweli kulikuwa na kundi la watu waliokuwa wakipiga picha bila shaka ilikuwa ni tukio fulani.

"Kweli hili eneo ni la kipekee sana daa." Nilijikuta nikitokwa na maneno.

"Unaambiwa hapa ni sehemu pekee ambayo watu hupapenda hasa wasafiri waendao Makete pamoja na Rungwe, hao unaowaona wenye rangi nyeupe ni watalii wanaotembelea maeneo mbalimbali ndani ya mkoa wa Mbeya hasa hasa katika bustani ya Dunia ambayo imejaaliwa maua ya aina tofauti tofauti ambayo huwezi kuyaona popote pale duniani."

"Bustani gani hiyo?" Nilimuuliza baada ya kuona anaanza kunidanganya.

"Unapoelekea Makete kuna Kivutio kinachoitwa Kitulo hapo kuna maajabu mengi sana ikiwa ni pamoja na kukutana na ndege ambao husafiri kutoka mataifa ya ulaya na kuja kubarizi eneo hilo lenye maua mbalimbali ya kupendeza." Alinijibu.

"Kwa hiyo unataka kuniambia hawa Wazungu wanaelekea huko?" Nilimuuliza utafikiri na yeye ni miongoni mwa wafanyakazi wa hii Restaurant.

"Hapo kuna mawili aidha wanaelekea huko au wamerejea kutoka huko." Alinijibu.

"Karibuni." Alifika yule dada na kutukaribisha kwa vile ambavyo tuliagiza.

"Asante dada yangu tunashukuru." Jofrey alimshukuru. Nilimtazama mwanaume huyu na kubaini kuwa ni mtu ambaye siwezi kumuacha aende zake kirahisi japo kuna mtu mmoja bado simuelewi na sijui anauhusiano gani na Jofrey hilo niliamua kukaa kimya kwanza ili kupisha maisha mengine yaendelee.

"Samaki huyu ni mzuri sana." Nilichomekea tukiwa tumeanza kula.

"Sana sana ni mtamu kupita maelezo." Alinijibu.

"Unakumbuka nini unapokula huyo samaki?" Nilimchokonoa.

"Ni mengi Tina lakini naomba hilo tuliache kwanza tule kisha maongezi yaendelee mbele lakini yote kwa yote nakupenda sana hata wewe mwenyewe unalijua hilo." Alinijibu.

"Siyo mbaya tunaweza kula lakini mazungumzo yakichukua nafasi yake." Niliona anataka kukata kona nikamzuia kabla hajafanya hivyo.

"Kwa kuwa umesema mwenyewe basi tunaweza kuendelea." Alinijibu huku akiipeleka mdomoni chupa ya pespi.

"Ni uwanja wako sasa kunieleza kila kitu kilichotokea."

"Tina, kiukweli niseme tu kuwa naomba unisamehe kwa sababu mama yangu ndiye aliyenichanganya." Alianza kwa kunijibu.

"Unamaanisha nini unaposema mama yako alikuchanganya?" Nilitaka kujua katika hilo.

"Unajua tukiwa pale stendi alinitumia ujumbe na kuniambia kuwa nimeacha kufanya kilichonileta Mbeya lakini nimejiingiza kwenye masuala yasiyokuwa na tija kwa wakati huu ambao natakiwa kuijenga kesho yangu. Hilo ndilo ambalo lilinichanganya na kunifanya kuwaza sana ni nani aliyemfikishia habari hizi wakati mimi sikufanya hivyo ilifikia hatua nikamfikiria rafiki yangu Gembe labda ndiye aliyemwambia lakini alikataa. Kifupi hilo ndilo ambalo lilinichanganya sana mpenzi wangu." Alinieleza kwa kirefu.

" Kwa hiyo unataka kuniambia kuwa wewe una mtu mwingine tofauti na mimi? Kwanini mama aseme hayo wakati uliwahi kuniambia kuwa mama yako kafurahi sana baada ya wewe kumueleza juu ya uhusiano wetu." Niliona nimkumbushe.

" Unajua nini Tina? Mama yangu bado hujamfahamu vizuri nafikiri siku utakapokutana naye ndiyo utachambua mwenyewe." Alinijibu.

" Oohh kwa hiyo unataka kuniambia kuwa mama yako kabla hata hajaniona tayari kanichukia. Na siku akiniona itakuwaje?" Nilimuuliza huku nikimuita mhudumu aje kuchukua haki yake.

" Naomba hilo nisimsemee mama lakini kiukweli ni mtu wa kipekee sana na anatamani sana kupata mkwe pamoja na wajukuu na inawezekana aliongea hayo akijua kuwa labda kukaa Mbeya muda mrefu naweza kukupoteza wewe." Alinijibu huku akitoa waleti yake ambayo aliifungua na kutoa noti mbili za shilingi elfu kumi na kumkabidhi mhudumu.

" Umefikiria weee umeona unijaze siyo?" Nilimuuliza.

" Hapana huo ndiyo ukweli wangu kataa amini." Alinijibu.

" Okay nimekuelewa Jofrey na niseme kuwa nimekusamehe na sitegemei kama kilichotokea kinaweza kujirudia tena."

"Wala haitokuja kutokea kwa hilo naomba uniamini." Alinijibu.

Wakati tukiwa tunaendelea na mazungumzo mara ujumbe wa Rachel uliingia.

"Dada Tina mimi nimeshatoka kazini sijui tunakutana wapi ili safari ya nyumbani tuianze pamoja." Niliusoma kwa muda ujumbe ule kisha nikamtazama Jofrey usoni.

"Vipi mbona unanitazama hivyo usoni kuna baya limeingia kwenye simu yako?" Aliniuliza.

"Noo hakuna baya lolote lile bali ni ujumbe wa rafiki yangu umeingia akinitaarifu kuwa keshatoka kazini na ananisubiri mimi tu." Nilimjibu nikiuweka sawa mkoba wangu.

"Rafiki yako? Yupi huyo?" Aliniuliza.

"Jofrey unajua nini mgogoro wetu ndiyo ulionikutanisha na rafiki huyu aitwaye Rachel ni rafiki bora sana kwangu unajua ni mangapi nimepitia kipindi tumefarakana?" Nilimuuliza.

"Hapana sijui Tina labda ndiyo uniambie wewe."

"Kesho nitakueleza kila kitu na ikiwezekana Rachel ndiye atakayekueleza kwa muda huu naomba tuondoke hapa ili nimuwahi." Nilimwambia huku nikiipiga namba ya Rachel.

"Bwana ee fanya fasta tufanye manunuzi kidogo kabla ya kwenda nyumbani." Aliniambia hivyo baada ya kuipokea simu yangu.

"Okay sawa mdogo wangu niko njiani nakuja tukutane hapo Mwanjelwa." Nilimjibu.

"Kwa hiyo tutakutana saa ngapi?" Aliniuliza.

"Nitakujulisha hiyo kwa sasa naomba nikuache ili nimuwahi Rachel." Nilimjibu tukiwa kasi kidogo kuelekea kituo cha daladala.

"Tuachane kivipi? Kwani mimi naishi huku si hata mimi naishi Block T."

"Ningejuaje sasa? Uliniambia?" Nilimuuliza.

"Ni kweli mambo yalikuwa mengi nisamehe tu." Alinijibu.

"Hebu twende zetu bwana Rachel namfahamu mimi nikichelewa tu kinawaka." Nilimjibu tukiingia ndani ya daladala.

Tuliingia ndani ya daladala na kuketi huku tukisubiri muda wa gari kuondoka na wakati huo huo macho yakiwa hayaachi kuitazama simu yangu kuuchungulia muda.


JE NI NINI KITATOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post