IMETOSHA MAMA MKWE - 33 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


IMETOSHA MAMA MKWE - 33

sultanuwezotz.blogspot.com 


Nilimkuta Rachel akiitoa simu kwenye boksi lake na kwa namna simu ilivyo kali sijui itakuwaje huko mtaani hasa nitakaporudi nyumbani maana itakuwa ni mwendo wa 'selfie' tu kwa kwenda mbele.

"Pole sana Zainabu Matata ulijiona mjanja na kisimu chako cha kuzimia moto mtaa mzima joto kali tena lenye harufu ya kinyesi cha popo, sasa nakwambiaje Zai!! Umekwisha..." Niliwaza hayo mpaka kicheko kikanishika kilichopelekea Rachel kushtuka.

"Dada Tina umepatwa na nini mpaka uliachie cheko lote hilo?"

"Mdogo wangu acha tu nipunguze sumu mwilini." Nilimjibu.

"Unamaanisha nini?" Aliniuliza.

"Unajua nini mdogo, kuna kichaa mmoja mtaani kwetu aliachiwa kisimu cha urithi na marehemu babu yake saaasa tumepata taabu wakina siye wala mlo mmoja kwa siku tena tukiwa chini ya uvungu lakini wewe umejua kuninyoosha mdogo wangu na mimi kwa bakora hiyo hiyo nakwenda kuwaadhibu mtaani kwangu hasa huyo Zainabu Matata."Nilimjibu Rachel nikigonga naye.

" Mtajuana wenyewe huko huko kikubwa naomba laini yako naona simu imeshajaa tayari ili uanze kupyatika mwenyewe." Kusikia hivyo haraka sana nilichukua kirimoti changu na kutoa laini zote na kumkabidhi Rachel. Aliziweka kwenye simu yangu mpya kisha akaanza kunielekeza vitu vya muhimu si unajua tena mashikolo mageni hivyo nilikuwa makini kuhakikisha siachi hata kitu kimoja kwenye hili darasa, na kwa namna alivyokuwa akinielekeza nilishangaa kwanini Rachel hakuwa mwalimu maana alikuwa taratibu tena kwa utulivu kabisa na akifika mwisho wa maelezo ni lazima aniulize kama nimeelewa na kisha alinikabidhi nirudie kila kitu alichonielekeza mwanzo mpaka mwisho.

"Waooo umeweza dada yangu na mpaka hapo hiyo ni yako lakini kama nilivyokueleza hapo awali kuwa ili simu yako idumu muda mrefu hakikisha unaichaji wakati imemaliza kabisa moto uliomo." Alinisisitiza Rachel.

"Nitakuwa makini sana kwenye hilo." Nilimjibu.

"Sasa sogea hapa na simu yako nikuingize kwenye Ulimwengu wa kidigitali kwa kuunganisha kwenye mitandao ya kijamii."

"Na hicho ndicho nilichokuwa nikikisubiri kwa hamu mdogo wangu." Nilimjibu.

"Na ndiyo maana mdogo wako niko hapa kila kitu kitakuwa sawa." Basi alianza na mtandao wa kijamii wa Facebook ambapo aliniunganisha nao huku profile yangu ikipambwa na picha ambayo alinipiga nikiwa nateremka kwenye gari lake ilikuwa bonge la picha na baada ya kukamilisha tukaingia kwenye mtandao chochezi wa Instagram huko nako aliniunganisha.

"Tutumie picha gani Instagram?" Aliniuliza ikabidi tuanze kuzipitia picha zote ambazo alinipiga usiku ule na baada ya kuzipitia zote macho yangu yalinasa kwenye picha ambayo alinipiga siku mbili nyuma nikiwa nachezea laptop yake sebuleni kwa kutumia simu yake.

" Ila dogo wewe kiboko hii simu ulinipigaje bila mimi kujua?" Nilimuuliza.

"Ndiyo utanijua mimi ni nani? Lakini unaionaje hii itafaa?" Aliniuliza.

"Unauliza majibu hiyo ni ya kijanja zaidi itafaa hapo hauoni niko kama mnyamwezi." Nilimjibu nikimpiga begani.

Basi aliihamisha ile picha pamoja na picha nyingine zilizoko kwenye simu yake na kuzileta kwenye simu yangu kisha akaiweka kwenye profile yangu ya Instagram na baada ya kukamilisha aliingia kwenye app ya whatsApp ambako alimalizia kunisajili na ilipokamilika haraka sana nilimtafuta Jofrey kama yupo whatsApp na kama zali alikuwa online na hapo hapo sikufanya kosa nikamtumia ujumbe wa kichokozi.

"Dogo hujalala tu unataka nikunyonye damu?" Kisha nikautuma.

Haikuchukua muda ujumbe wangu ulipata majibu.

"Nani mwenzangu?" Aliniuliza. Jibu lile lilinifanya nishangae.

"Rachel mbona ananiuliza mimi ni nani? Ina maana namba yangu kaifuta au yuko na kidemu kingine huko."

"Hapana dada wala si hivyo elewa kuwa hajawahi kukuona kwenye masuala ya kimtandao hivyo lazima aulize wala usimuelewe vibaya." Rachel alinielewesha vizuri nikawa nimemuelewa. Na hapo hapo nikamjibu Jofrey.

"Tina hapa." Huku nikiambatanisha na moja ya picha yangu maridadi.

"Waoo karibu duniani kipenzi."

"Asante mpenzi." Nilimjibu.

"Ndiyo kusema kidigitali zaidi ee?" Aliniuliza Jofrey.

"Majibu mdomoni mwako hapa mwendo wa kuteleza tu."

"Basi sawa nikutakie usiku mwema tuko jikoni tunaliandaa zege."

"Na kwako pia." Nilimjibu kisha nikazima data na kumfuata Rachel jikoni ambako alikuwa akimalizia kuandaa chakula.

"Imekukifu tayari?" Aliniuliza baada ya kuniona pale jikoni.

"Hapana sitaki inizoee sana nahitaji kuiongoza mimi siyo yenyewe iniongoze mimi." Nilimjibu.

"Unasema tu bado hujakutana na vichaa wa mtandaoni hasa Facebook na Instagram."

"Hata kama itabidi nijitahidi kuithibiti hali hiyo kabla haijanizoea." Nilimjibu kisha nikamsaidia kupeleka chakula sebuleni na baada ya kila kitu kuwa sawa tuliketi mezani kula chakula lakini mara mlango uligongwa.

"Ni nani?" Niliuliza nikimuangalia Rachel.

"Sijui atakuwa ni nani?" Alijibu akiinuka kuufuata mlango huo. Na baada ya kuufungua tu.

"Umefanya nini sasa?" Lilikuwa swali kutoka kwa mgeni aliyefika kwetu mara tu baada ya mlango kufunguliwa.

"Kuhusu nini?" Rachel alimuuliza.

"Si nilikwambia kuwa tukutane leo kwangu kuna ndugu zangu nataka wakakufahamu?" Alilalamika mtu huyo ambaye ni kama mtu wake kutokana na malalamiko yake. 

"Othman inaonekana hukunielewa vizuri muda ule naomba nirudie tena kauli yangu 'ni mapema sana kuanza kutambulishana kwa ndugu na jamaa lakini maneno yangu si sheria ya kukuzuia wewe kufanya maamuzi' bila shaka umenielewa." Rachel alimjibu mkono mmoja kiunoni na mwingine mlangoni kama vile hataki mgeni apite. 

" Maamuzi gani hayo? " Othman alimuuliza Rachel. 

" Ya kumtambulisha mtu mwingine ambaye yuko tayari kupelekwapelekwa lakini kwa upande wangu bado."Alimjibu na kisha kuufunga mlango. 

" Na wakati mwingine usije hapa bila taarifa." Alimsindikizia maneno hayo na kugeuka kuja mezani. 

" Mdogo wangu ni nani kakuvuruga?" Nilimuuliza. 

" Achana naye huyo mjinga mmoja kisa kimilioni chake ambacho alinipa huko nyuma kashanigeuza mchumba wake nafikiri hanijui mtoto wa mjini, ni kweli nampenda lakini siyo anigeuzegeuze kama mtoto mdogo." Alinijibu huku akiachana na meza na kuinuka kuelekea chumbani kwake. 

" Ndiyo kusema umeshiba?" Nilimuuliza. 

" Nakuja nafuata simu mara moja." Aliingia chumbani kwake na baada ya dakika kama moja hivi alirejea sebuleni na kujilaza kwenye sofa ndefu na kuanza kuchezea simu yake bila shaka alishavurugwa na mimi baada ya kuiona hali hiyo nikaona niachane naye nikaondoa vyombo nikavipeleka jikoni kisha nikarudi na kumuaga Rachel.

"Sasa nikuache ngoja mimi nikautafute usingizi."

"Na mimi sitakuwa na muda mrefu sana hapa kuna taarifa naitafuta hapa basi usiku mwema dada." Basi niliondoka na kuingia chumbani kwangu ambako sikuhangaika na chochote zaidi ya kuingia bafuni kuoga kisha kulala.

Niliamshwa na simu ambayo iliita sana na bila shaka ni kutokana na mlio wa muziki ambao sikuuzoea hivyo nikaichukua na kupokea.

"Haloo."

"Mwanangu bado umelala?" Alikuwa ni mama aliyeuliza 

"Hapana nilikuwa naoga mama." Ilibidi nidanganye kwani baada ya kuangalia ya kuangalia saa ilikuwa ni saa mbili kasoro.

"Sasa utakapokuwa unakuja usisahau kuja na mchele wa Kyela pamoja na maharage gazeti ya mbeya wenyewe hapo wameyapa jina la maji mara moja."

"Sawa mama nitafanya hivyo." Nilimjibu na kisha alikata simu na mimi ikabidi nijiinue pale kitandani na kutoka nje na moja kwa moja nikaelekea chumbani kwa Rachel maana si kawaida yake kulala kiasi kile na baada ya kuufungua mlango wa chumbani kwa Rachel nilipokelewa na kitanda kilichokuwa kimetandikwa vizuri kama vile hakijalaliwa na mtu hali hiyo ilinishangaza sana nikatoka na kwenda sebuleni ambako nilikutana na kituko cha mwaka kilichonifanya nianze kucheka.

"Rachel, Rachel, wee Rachel hebu amka bwana." Niliona nimuamshe.

"Dada kumekucha?" Aliniuliza.

"Usiniambie kuwa umelala hapa hapa?" Nilimuuliza.

"Kweli usingizi hauna adabu." Alinijibu na kuamka kisha akaongoza chumbani kwake na mimi nikifungua mlango kutoka nje. Huko nilikutana na kituko kingine ambacho si cha kawaida haraka sana nilirudi ndani na kumfuata Rachel chumbani kwake. Nilimweleza kile nilichokiona hivyo haraka sana tukatoka kuelekea nje tena.

"Whaaaaaat???" Lilikuwa ni swali ambalo Rachel aliuliza baada ya kujionea kilichotokea.


JE NI KITU GANI AMBACHO KIMEMUACHA MDOMO WAZI RACHEL?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post