IMETOSHA MAMA MKWE - 34 (Mtunzi:Sultan Uwezo)

 


IMETOSHA MAMA MKWE - 34

sultanuwezotz.blogspot.com 


"Haiwezekani Othman ni wewe tu, nasema ni wewe hakuna mtu mwingine mwanahizaya mkubwa." Rachel alijikuta akitokwa na maneno makali hayo baada ya kuliona gari lake limeatamia ardhi tairi zake zote zikiwa hazina upepo na hii ni kumaanisha kuwa kuna mtu alifika na kuyafanyia mchezo mchafu wa aina hiyo. Hakika nilimuonea huruma mdogo wangu Rachel kwa kilichotokea kwenye gari lake ghafla akarudi ndani na kutoka tena akiwa na funguo mkononi na moja kwa moja akafungua mlango wa gari akaingia ndani na huko haikuchukua muda alitoka akiwa kashika kichwa chake akizunguka huku mara kule hali hiyo sikutaka inipite mbali nilimfuata na kumuuliza kulikoni lakini hakunijibu zaidi ya kunionesha kwa ishara kuwa nichungulie, nikasogea mpaka ulipo mlango wa gari na kuangalia.

"Rachel niambie basi nini kimetokea ndani ya gari! Unanipa ishara tu wakati unajua fika sisi wengine kwenye upande wagari ni zero." Nilimuuliza ili anipe jibu lakini badala ya kunijibu alianza kulia akielekea ndani. Na mimi bila ajizi nilimfuata nyuma.

"Nasema labda nisiwe mimi lakini kama ni mimi Rachel Othman atanitambua yaani afikie hatua ya kung'oa redio ya gari na pia kuharibu matairi? Nasema siwezi kulifumbia macho suala kama hili." Rachel aliongea maneno hayo kwa uchungu mkubwa na katika hili wacha nikiri kwamba aliyefanya tukio hili aweza kusema Othman anahusika au la japo mdogo wangu Rachel alihisi ni yeye kwa asilimia zote.

" Unacheza na akili zangu siyo? " Lilikuwa ni swali baada ya simu kupokelewa upande wa pili.

Sijui alijibiwa nini lakini kilichofuata ni Rachel kuitupa simu kitini na kuingia chumbani kwake ambako hakukaa muda mrefu akarudi na kuichukua simu yake tena akapiga namba fulani alizokuwa akizisoma kutoka kwenye kadi fulani nyeupe.

"Kaka Muhidini tafadhali nakuomba hapa nyumbani kwangu muda huu." Kisha alikata na kunigeukia mimi.

"Dada nisamehe kichwa changu hakiko sawa lakini nitakuwa poa tu nimeshaongea na Fundi aje aliangalie kisha alifanyie Service lakini huyu Othman ajiandae simuachi salama hata kidogo."

"Kwanza kabisa nikupe pole mdogo wangu kwa kitendo hiki cha kinyama kilichofanywa kwenye gari lako lakini nashindwa kukubaliana na akili yangu inayoniambia kuwa Othman si mhusika wa tukio hili, uchunguzi ukifanywa tutamdaka mhusika tu." Nilimjibu Rachel.

"Hivi dada unachokiongea kinatoka mdomoni kwako kweli? Yaani mtu aje hapa asubuhi yatokee haya halafu nimhisi nani?" Aliniuliza swali.

"Siyo kwamba napingana na wewe lakini ninachotaka kusema mdogo wangu tusimhukumu moja kwa moja huyo Othman.." Lakini kabla sijamaliza kuongea mara mlango uligongwa na kwa kuwa haukufungwa Othman aliingia ndani moja kwa moja.

"Hivi wewe mwanamke unanitakia nini mimi asubuhi yote hii?" Aliingia na swali.

"Unauliza nini kwani hujui ulichokifanya? Au unataka kunifanya boya mimi."

"Kwa hiyo una uhakika mimi ndiye niliyefanya hicho unacholaumu?"

"Ndiyo ni wewe kwani hujui?" Rachel alimjibu bila hata wasiwasi kama vile alimuona.

"Okay vizuri Rachel si nimekuwa mbaya kiasi hicho wacha nikubali lakini najua utaupata ukweli tu na sihangaiki kukueleza kama ni mhusika au la lakini nitalifanyia ukarabati." Othman alimjibu akitoka nje.

"Unasemaje wewe bwege? Nani kaomba hisani kwako? Yaani uliharibu halafu uje kujidai utalitengeneza unaumwa nini?"  Rachel alimwambia Othman maneno ambayo hata mimi nilipatwa na woga.

"Hebu punguza ukali wa maneno mdogo wangu." Nilimwambia.

"Achana naye huyo hana jipya." Alinijibu akiufuata mlango ili aurudishe mara baada ya Othman kutoka, lakini alipofika usawa wa dirisha alitulia kwa muda macho yakiwa nje ikabidi na mimi nimfuate nione kuna nini.. Mmhh huwezi kuamini alikuwa ni Othman akiwa watu kadhaa wakilifanyia ukarabati gari la Rachel.

"Huyu kichaa anafanya nini pale?" Aliuliza akifungua mlango ili atoke lakini akiwa anatoka nje Othman naye na vijana wake walikuwa wanaondoka.

"Othman, Othman hebu nisubiri kwanza." Rachel alimwita Othman ambaye ni kama hakusikia chochote alitoweka. Nilirudi chumbani kuchukua simu yangu ambayo nilikuwa nimeizima toka usiku.

"Niko maeneo ya Rift Valley Hotel hapa." Ulikuwa ni ujumbe kutoka kwa Jofrey. Ikabidi nimpigie kwani ulitumwa muda mrefu tu zaidi ya saa moja.

" Uko wapi kwa sasa?" Nilimuuliza.

" Nimeona kimya nimetoka naelekea Isanga." Alinijibu.

" Simu yangu ilikuwa imezima ndiyo naiwasha sasa na kukutana na ujumbe wako, hivyo rudi mpaka ulipokuwa tukutane hapo na mimi ndiyo natoka nyumbani."

"Okay sawa kipenzi." Alinijibu kisha nikakata simu. Nilirudi na kuipachika chaji kisha nikajiandaa na baada ya hapo nikamwambia Rachel.

"Jofrey yuko Rift Valley ananisubiri ngoja nimfuate."

"Sawa unajua nini dada Tina? Nenda kwanza halafu nitakueleza kilichotokea." Alinijibu.

"Ni salama lakini?"

"Ni mshangao tu, wewe muwahi kwanza Jofrey tutaongea." Alinijibu na mimi bila kusubiri nikatoka na kuelekea Rift Valley nilipofika nje nikachukua Bajaj na baada ya kufika nikamkuta kafika tayari.

"Twenzetu." Nilimwambia baada ya kumsogelea alipokuwa akapanda.

"Uliponichukua tafadhali." Nilimwambia dereva Bajaj.

"Sawa dada." Alinijibu.

"Niambie." Nilimwambia Jofrey.

"Nikuambie nini zaidi ya kukukumbuka tu mtu wangu." Alinijibu.

"Kunikumbuka huko kwiyooo...si jana tulikuwa pamoja?" Nilimuuliza.

"Ndiyo lakini wajua ninachomaanisha Tina."

"Si ndiyo hapa sister?" Aliniuliza dereva Bajaj.

"Asante mdogo wangu." Nilimjibu nikimkabidhi ujira wake.

"Ndiyo hapa?" Jofrey aliuliza baada ya kumuona Rachel akiwa kando ya gari akiswaki.

"Yes ndiyo hapa." Nilimjibu.

"Daa ninyi ni wanyama aisee." Jofrey alijikuta akitokwa maneno.

"Acha hizo bwana hebu twenzetu." Nilimwambia.

"Shemeji lake hilo karibu kwa wagumu." Rachel alimkaribisha.

"Asante shem wagumu gani ninyi makazi tu ni Classic huo ugumu umetoka wapi?" Alimuuliza Rachel.

"Kwa hiyo unabisha?"

"Nabisha leo, nabisha kesho na nitabisha milele ninyi ni mayai kabisa." Jofrey alimjibu.

"Haya bwana kwa kuwa umesema na kukataa mwenyewe nani akubishie, lakini karibu ndani shemeji." Alimkaribisha.

"Asante sana nimekaribia." Tuliingia ndani.

"Najua ni mapema sana lakini karibu maziwa." Rachel alimkaribisha Jofrey glasi ya maziwa fresh kisha akaniita na tukaingia chumbani kwake.

"Unajua nini dada, gari limetengenezwa kama unavyoliona hapo nje lakini cha ajabu nimetumiwa clip ikiwaonesha wakina Othman wakiwa kwenye Ukumbi wa Mkapa kwenye tamasha la 'Mama Nijali' ambalo hufanyika kila mwaka na sijui kwanini jana nilisahau."

"Kwa hiyo unataka kuniambia nini?" Nilimuuliza.

"Nahisi Othman hahusiki na inawezekana alivyokuja hapa jana labda alitaka kunieleza hilo pia." Alinijibu.

"Si nilikwambia mdogo wangu." Nilimjibu.

"We acha tu dada yaani nimeishiwa pozi kama lote lakini pamoja na hayo najiuliza ni nani aliyefanya hili?"

"Vuta kumbukumbu vizuri kwenye mapito yako hakuna uliyewahi kukosana naye?" Nilimjibu.

"Hebu tuyaache kwanza haya kumbuka tuna mgeni." Aliniambia tukatoka sebuleni na kuungana na Jofrey.

"Shemeji samahani tulikuzilia sebuleni." Rachel alimwambia Jofrey.

"Wala usijali shemeji." Alimjibu akiiweka mezani ile glasi yenye maziwa.

Tukiwa tunaendeleza maongezi mara simu ya Rachel iliita na baada ya kuiangalia alisimama na kuelekea chumbani kwake na kutuacha.

"Kwa hiyo inakuaje kuhusu safari yako na pili huyu Rachel mlifahamiana vipi ilhali wewe uliniambia ni mgeni hapa mjini?" Jofrey alianza maswali yake.

"Safari yangu iko pale pale leo naondoka na magari ya mchana ningeondoka asubuhi lakini imeshindikana kutokana na gari la Rachel kuharibiwa usiku wa kuamkia leo hivyo mpaka tumjue aliyefanya hivyo japo gari limeshafanyiwa service muda si mrefu..." Alinikatisha.

" Hebu hebu kwanini imekuwa hivyo wameharibu kitu gani?"

" Iling'olewa redio pamoja na matairi yote kutolewa upepo." Nilimjibu.

" Huyo ni mtu anayemfahamu vizuri wala hajatoka mbali."Jofrey alinijibu.

" Ndiyo hivyo lakini kwa upande wa kukutana na Rachel ni stori ndefu sana kwani kabla ya kukutana na huyu kuna mbibi ambaye nilifikia kwake huko ndiko kwenye kitendawili ambacho nitakueleza ilikuwaje wakati mwingine tukiwa eneo tulivu na si hapa." Nilimjibu.

" Lini sasa wakati leo unarudi Iringa?" Aliniuliza.

" Kwani hatuji kuonana tena? " Nilimuuliza.

" Tutaonana ndiyo lakini raha ya supu ya mbwa uinywe ikiwa bado ya moto kwani ikipoa si supu tena utaishia kuimwaga." Aliendelea kung'ang'ania.

" Nimesema nitakusimulia wakati mwingine umekazania nini kwanza hujui kuwa wewe ndiyo chanzo cha haya yote?" Nilimuuliza Jofrey.

" Yapi hayo tena jamani?" Rachel alifika na kuingilia kati.

" Shemeji hakuna kitu ni vimaongezi tulivyokuwa tunaongea hapa na chizi wangu." Jofrey alimjibu.

" Okey kumbe ni mambo ya wapenzi hayo, dada Tina babu kanipigia kasema anakuja muda si mrefu kulishughulikia suala la gari." Alinieleza Rachel.

"Itakuwa vizuri sana hiyo." Nilimjibu. Baada ya hapo tuliendelea na maongezi ya hapa na pale hasa Rachel alikuwa akihitaji kumfahamu vizuri Jofrey hivyo maswali mengi alikuwa akimuuliza na mimi kusalia msikilizaji tu mpaka pale mlango ulipogongwa.

"Ni nani huyo?" Niliuliza.

"Sijui." Rachel alinijibu.


JE NI NINI KITATOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA KIGONGO HIKI.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post