IMETOSHA MAMA MKWE - 35 (Mtunzi :Sultan Uwezo)

 


IMETOSHA MAMA MKWE - 35

sultanuwezotz.blogspot.com 


Basi Rachel aliuendea mlango ili kuangalia ni nani aliyegonga na baada ya kuufungua alikutana uso kwa uso na mzee Mbogo.

"Mjukuu wangu nimekuja kupambana na mtu aliyevamia makazi yako usiku wa jana na kufanya uharibifu wa usafiri wako." Alitamba mzee Mbogo akiingia ndani.

"Babu nawe umejuaje kama hili limetokea?" Rachel alimuuliza.

"Unauliza au umesahau kuwa nilishakuambia nimefunga mtambo wangu wa ulinzi, nilishasema sitakuwa tayari kuona ukionewa mjukuu wangu labda niwe marehemu." Alimjibu akiketi.

"Babu shikamoo!!" Nilimsalimu mzee Mbogo.

"Marhaba mjukuu wangu mwenyewe Tina, pole na majukumu."

"Majukumu wapi babu yangu zaidi ya kukata mitaa tu." Nilimjibu.

"Kukata mitaa nayo ni kazi pia." Aliongeza.

"Nashukuru babu." Nilimjibu.

"Shikamoo mzee wangu." Jofrey alimsalimu.

"Marhaba kijana, mbona katikati ya warembo?" Mzee Mbogo alimuuliza mara baada ya kumuangalia kwa muda Jofrey.

"Sijaelewa mzee wangu?" Jofrey aliuliza.

"Hujaelewa nini kijana, ulishaona lini swala kwenye simba?" Babu alizidi kumtandika maswali Jofrey kitu ambacho Rachel alikiona na kuamua kumuinua mzee Mbogo na kutoka naye nje.

"Huyu mzee anazungumza nini mbona simuelewi?" Jofrey aliniuliza.

"Achana naye mzee huyu muda wote yeye hupenda utani." Nilimjibu Jofrey ambaye alionesha hofu kiasi fulani.

"Utani gani huo anaongea kama vile ana hofu na mimi halafu wenyeji wangu mmetulia tu hata kunisemea chochote hakuna." Jofrey alilalamika.

"Unaongea nini wewee mbona unapenda kujilalamisha kiasi hicho? Rachel kafanya nini hapa?" Nilimuuliza na kabla hajajibu mara simu yake iliita ikabidi aitoe na kuangalia ni nani aliyempigia kisha akasimama na kutoka zake nje kuipokea. Nilibaki peke yangu na kuamua kufungua whatsApp yangu na kisha kumtumia ujumbe Fabiana.

" Hi my sister?"

" Who are you?" Aliniuliza badala ya kujibu salamu yangu.

"Huna macho?" Na mimi nilimuuliza.

"Macho kivipi?" Maswali yaliendelea baina yetu.

"Si uangalie picha hapo?"

"Kwanini niangalie picha wakati hapa naendelea kuchati si uniambie ni nani?" Aliniuliza tena.

"Ngoja nipokee simu hii iliyoingia hapa kisha nitakupandia hewani." Nilimtaarifu Fabiana.

"Utakavyoona mwenyewe." Alinijibu.

Na mimi sikujali majibu yake nikaamua kumuacha kwanza kisha nikaingia Facebook ambako nilianza kupitia posts mbalimbali za marafiki zangu na nilipopitia komenti zilizotolewa kwenye picha ambayo nilipost masaa kadhaa nyuma.

" Duu kama utani Njiwa wangu umeruka na kuelekea kusikojulikana sijui ni lini utaungana nami?" Niliusoma ujumbe huu mara mbili mbili kwani sikuutarajia kabisa hasa ukizingatia hata namba ya mtu huyu sikuwa nayo. Lakini sikuishia hapo nikaona niangalie chini yake kumeandikwa nini tena.

" Aahh mshikaji unazingua bwana unataka kusema nini hapo?" Ulikuwa ni ujumbe wa mdau mwingine tu.

"Nazingua kivipi? Unanijua mimi wewe?" Meshack alionekana kukerwa na komenti zilizotolewa na hawa sijui ni rafiki zake au la.

"Maamaaa umewaka Tina wewee au wamekuedit? Hebu nijibu fasta ukishindwa nifuate inbox tuchonge kidogo." Baada ya kuangalia mtoa komenti hiyo ni nani kwani picha yake ilikuwa ni ua tu halafu jina lilikuwa ni Queen Ney hivyo ikanibidi nimfuate inbox na kisha kumtumia ujumbe.

" Habari, Tina hapa."

" Mhh mwenzangu umekuwa jimama hivyo?" Alinijibu.

" Samahani ni nani mwenzangu?" Nilimuuliza.

"Makubwa! Yaani umenisahau?" Alinijibu.

"Nimekusahau? Queen Ney ni nani?" Nilimuuliza.

"Hee kumbe ni hivyo? Mimi si ni dada yako Noela." Alijitambulisha.

"Jamaaaaaani dada Noela za siku nyingi." Nilimsalimu huku mzee Mbogo na Rachel wakiingia ndani.

Ikabidi nisitishe kuchat na dada Noela mtu ambaye sikutarajia kukutana naye kwa kipindi hiki kwani ni muda mrefu sana toka tuachane mjini Makambako miaka kadhaa iliyopita.

"Natoka kidogo lakini narudi kuna wenyeji wangu wameingia hapa ngoja niwasikilize kwanza." Nilimjuza dada Noela.

"Usiende mazima mdogo wangu bado nina hamu ya kuendelea kuongea na wewe ukimalizana nao piga namba hiyo..." Aliitaja namba hiyo na mimi nikaisevu kisha nikaachana naye na kuwageukia wakina Rachel.

"Vipi mbona peke yako?" Rachel aliniuliza baada ya kuniona peke yangu.

"Yuko nje huko anaongea na simu." Nilimjibu.

"Anaongea na simu?" Aliniuliza.

"Ndiyo." Nilimjibu.

Lakini cha ajabu walitazamana na babu kwa muda kidogo kisha mzee Mbogo alinisogelea.

"Mjukuu wangu Christina, awali ya yote niombe msamaha kwa kile nilichokiongea kwa mgeni wako pasipo kujua alikuwa ni nani kwako. Naomba unisamehe sana sana." Aliniomba msamaha huku akiwa kanishika mikono yangu.

"Babu mbona hukusema baya lolote lile baya, lingekuwa baya iwapo ungekuwa umejua. Hivyo hakukuwa na sababu ya wewe kuniomba msamaha wowote." Nilimjibu mzee Mbogo aliyekuwa bado kaishikilia mikono yangu.

"Nimekuelewa mjukuu wangu lakini kama hutojali unaonaje ukimpigia simu mwenzako." Aliniomba.

"Hakuna haja atakuja tu iwapo atamaliza kuongea na simu." Nilimjibu.

"Dada Tina unajua ni kwanini babu anasema hivyo?" Rachel aliniuliza.

"Sijui labda kumtaka Jofrey aingie ndani." Nilimjibu.

"Jofrey hayupo nje kaondoka muda mrefu sana zaidi ya robo saa iliyopita." Maelezo ya Rachel yalinishtua na sikuamini kama ni kweli Jofrey kaondoka maana hajaongea chochote na kwanini kaondoka bila taarifa hivyo kwa kujihakikishia ikabidi nitoke nje kuhakiki kile nilichoambiwa na Rachel, ni kweli hakukuwa na hata unyayo wake nikabaki nimeduwaa.

"Hiyo ndiyo ilikuwa maana yangu ya kukutaka umpigie maana alipotoka tu alitoka nje na kuingia kwenye Bajaj iliyokuwa ikipita hapo barabarani." Mzee Mbogo akiwa ananieleza hayo mimi macho yangu yalikuwa kwenye simu kuitafuta namba ya Jofrey ili nimpigie, niliipata na kumpigia lakini cha ajabu hakupatikana hewani. Niliijaribu tena na tena lakini wapi haikuwa hewani.

" Kwanini kafanya hivi?" Nilijiuliza swali hilo huku nikiwa nimemgeukia mzee Mbogo aliyekuwa akiingia ndani.

"Atakuwa kaelekea wapi huyu Pimbi jambo dogo tu kuzira gunia zima na hapo hatujaoana bado tukioana itakuwaje?" Niliendelea kujiuliza maswali yasiyo na majibu huku nikirudi ndani lakini wakati huo huo simu ya baba iliingia na mimi bila kupepesa macho wala kope nikaipokea.

" Baba shikamoo." Nilianza kwa salamu baada ya kuipokea.

" Marhaba mwanangu unaendeleaje?" Alinijibu na kuniuliza. 

"Naendelea vizuri tu ninyi huko?" Nilimuuliza. 

"Hatujambo isipokuwa tu mwanao jana alivunja mguu akiwa mazoezini hivi tunavyoongea tuko hapa 'Tumaini Jipya Hospital' toka jana maana jana hakupata tiba ya maana kutokana na muda tuliofika hivyo leo ndiyo wanamshughulikia." Majibu ya baba yalinivuruga kabisa na kujikuta nikishindwa kuingia ndani na kujitupa chini kama furushi nikiwa nimeishiwa nguvu kabisa. 

" Baba sasa mbona hamkuniambia jana ile ile?" Nilimtwisha zigo la lawama mzee Thobias lakini hakuweza kukutana nalo kwani tayari alishaondoka hewani. 

"Wewe kuna nini mbona hivyo?" Rachel alikuja na kuniuliza. 

"Rachel naomba nijiandae kwa safari mwanangu Thobias kapata ajali akiwa mpirani hivyo nasikia kavunja mguu na tayari wako Hospitali toka jana." Nilimweleza Rachel aliyekuwa pembeni huku mimi nikiwa bado nimekaa chini. 

"Maskini dada yangu yamekuwa hayo tena? Pole sana dada Mungu akutie nguvu katika hili inuka twende ndani ukafanye maandalizi ya safari." Niliinuka kwa msaada wa Rachel na kuingia ndani ambako moja kwa moja niliongoza chumbani tayari kwa maandalizi huku nikimuacha Rachel sebuleni akiteta na mzee Mbogo. Sikuwa na muda wa kupoteza nilikusanya kila kilichokuwa changu na kisha nilitoka sebuleni. 

"Dada Tina si ungeoga kabisa au?" Rachel aliniuliza. 

"Wala usijali mdogo wangu nitaoga tu nikifika nyumbani maana sielewi ipi ni nyekundu na ipi ni blue." Nilimjibu nikiufuata mlango.

Mzee Mbogo alikuja nyuma yangu na kunishika mkono wangu.

"Mjukuu wangu elewa kwamba ili dhahabu ipate thamani ni lazima ipite kwenye moto hivyo na wewe haya yote unayoyapitia kwa sasa yanakuimarisha kiimani na kukufanya kuwa imara mara dufu na hata siku usije ukafikiri kuwa dunia hii imekuinamia peke yako la hasha isipokuwa kuna siri nyingi sana ndani ya vijumba vyetu na ndiyo maana ukiviangalia vijumba vyetu asilimia kubwa vimevimba kwa juu kwenye paa kuashiria kuwa vina siri nzito sana hivyo nakuomba uwe imara katika hili na mengine yote unayopitia, lakini pia mdogo wako nadhani atakusindikiza mpaka Makambako ili kukupunguzia safari." Mzee Mbogo aliniasa kwa kirefu sana kiasi cha kujiona mwepesi na mimi nilimshukuru kwa nasaha zake kisha tukatoka Rachel akiwa kaubeba mkoba wangu naye akiwa tayari kwa safari.

" Kama babu alivyokwambia nitakusindikiza mpaka Makambako kisha nitarudi si unajua mambo ya kazini tena ningekupeleka mpaka nyumbani."

"Rachel hujui tu ninajiona kwa kila jambo unalolifanya kwangu hivi unafikiri ni nani angethubutu kuacha kibarua chake kisa tu Tina? Nimshukuru sana mzee Mbogo kwa kutukutanisha mimi na wewe." Nilimshukuru kwa kile alichoamua kukifanya kwangu na hapo tulikuwa ndani ya gari huku mzee Mbogo akiwa kasimama mlangoni akitupungia mikono.


UNADHANI NINI KINAKWENDA KUTOKEA HUKO?


MAJIBU YA MASWALI HAYA NA MENGINE TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post