IMETOSHA MAMA MKWE - 36 (Mtunzi:Sultan Uwezo)


 IMETOSHA MAMA MKWE - 36

sultanuwezotz.blogspot.com 


Baada ya safari ndefu tuliwasili Makambako ambako moja kwa moja tuliingia mpaka stendi mpya na baada ya kuingia hapo tulimuita mmoja wa Maafisa Usafirishaji ndani ya stendi hii na kumuuliza iwapo kama kuna gari linaloelekea Iringa kwa muda huo kwani tayari ilikuwa ni saa saba mchana,kijana huyo alitueleza kuwa kuna gari linatoka Songea nusu saa baadaye litakuwa hapa.

"Samahani kaka hakuna gari jingine ambalo linaondoka muda huu?" Nilimuuliza.

"Mhh hebu ngoja kwanza nimcheki jamaa yangu pale Iringa road kama private yoyote." Alinijibu akiitoa simu yake mfukoni. Na baada ya kuongea na simu alirudi kwetu tena.

"Mshikaji kasema kuna Noa iko pale inaelekea Dar hivyo jamaa anahitaji abiria wanne tu kama hamtojali." Alinijibu.

Rachel hakutaka maneno mengi sana alichokifanya ni kumpa ishara kijana huyo aingie garini ili tuelekee huko, aliingia kwenye gari na Rachel aliondoa gari.

" Nauli anafanyaje? Maana hiyo ni private." Nilimuuliza ili kuwa na uhakika maana asije sema ni shilingi elfu sitini bure.

"Kikubwa safari na kufika hayo mengine yatafahamika tukifika hapo walipo." Rachel alijibu macho yakiwa nyuzi tisini mbele mikono ikiwa kwenye usukani. Ilibidi niwe mpole maana Rachel huwa hapendi kupingwa akiongea jambo. Na baada ya dakika kadhaa tuliwasili Iringa road na kuikuta hiyo Noa ikiwa inajiandaa kuondoka hivyo nilishuka haraka huku Rachel naye akiwa nyuma yangu.

"Nimeongea naye kasema anahitaji shilingi elfu tano tu." Kijana huyu aliongea baada ya kuongea na mwenye Noa hiyo.

"Tunashukuru sana kijana Mungu akubariki." Rachel alimshukuru kijana huyo akimkabidhi shilingi elfu kumi kitu ambacho kilimshangaza sana kiasi cha kushindwa kuongea chochote. Niliingia kwenye gari kisha Rachel alimfuata dereva ili aongee naye.

"Habari yako." Alimsalimu.

"Salama sister kwema."

"Mhh kumbe ni wewe?" Rachel aliuliza.

"Rachel umefuata nini Makambako?" Dereva huyo alimuuliza Rachel.

"Norbert swali gani hilo tena? Nimekuja kuwasalimu ndugu zangu hapa." Alimjibu.

"Oohh kumbe, mimi naelekea Dar mara moja si unajua biashara zetu?"

"Yes najua na kwa kuwa tumekutana ghafla hapa naomba usiisahau perfume yangu mzee wa vipodozi si unaikumbuka?" Rachel alimuuliza Norbert.

"Nasahau vipi mteja wangu mwenyewe?" Alimuuliza.

"Okay vizuri, fanya hivyo bwana na siyo umdai nauli dada yangu huyo." Rachel alimtania.

"Rachel bwana wacha sisi tuianze safari mengine atakwambia mwenyewe." Norbert alimjibu Rachel akiliondoa gari huku Rachel akinipungia mkono kuagana.

Safari ilianza tukipitia kituo cha mafuta ambako aliijaza na kisha tukaanza safari.

"Rachel ni mdogo wako kweli?" Norbert aliuliza akikirekebisha kioo kilicho juu yake bila shaka ili aweze kuniona vizuri.

"Kwanini unauliza hivyo?" Nilimuuliza.

"Hapana nauliza tu maana Rachel mjanja mjanja sana yule." Alinijibu.

"Ni mdogo wangu kwa maana ya kifamilia si kwa kuzaliwa pamoja." Nilimjibu.

"Habari ya muda Tina." Ujumbe uliingia kwenye simu yangu na nilipouangalia ulitoka kwa Jofrey, niliupotezea. Lakini kabla sijakaa sawa simu iliita na hakuwa mwingine alikuwa ni Jofrey mwenyewe nilitaka kuipotezea lakini nikaona niipokee tu nimsikie anasemaje.

" Mbona haujibu ujumbe wangu?" Aliniuliza.

"Ujumbe gani?" Nilimuuliza.

"Mbona swali ina maana hujauona?" Aliniuliza. Sikuona sababu ya kuendelea kupoteza muda kwa mtu ambaye haoni thamani yangu kwake nikakata simu.

Niliwasili Ilula salama kabisa na moja kwa moja nilielekea nyumbani kwanza kisha safari ya Hospitali ifuate. Kwa bahati nzuri nilikutana na baba akiwa anajiandaa kutoka.

"Aahh mwanangu umefika?" Alishangaa kuniona.

"Ndiyo baba shikamoo!" Nilimjibu.

"Marhaba pole na safari."

"Nashukuru Mungu nimesafiri na kufika salama baba yangu." Nilimjibu.

"Hilo ndilo la kushukuru zaidi, kama bahati mwanangu hivi unavyoiona nilikuwa ndiyo nataka kuwasha pikipiki nielekee Hospitali kumuona wajina wangu." Alinieleza.

"Kumbe!! Inabidi twende wote." Nilimwambia nikiurushia sebuleni mkoba wangu.

"Si ungepumzika kwanza maana mwanao alishafanyiwa oparesheni tayari hivyo ungekwenda baadaye kidogo." Alinieleza baba akiwa anaiweka sawa kofia ngumu ya pikipiki.

"Nitapumzika tu baba lakini kitu cha kwanza nimuone mwanangu." Nilimjibu nikipanda kwenye pikipiki hivyo hakuwa na jinsi zaidi ya kuwasha pikipiki na kuondoka.

"Haya umeshinda." Alinijibu.

Tuliondoka taratibu kama ujuavyo wazee hawanaga mbwembwe nyingi wawapo barabarani kama vijana na tuliwasili salama Hospitali na baada ya kuingia kwenye wodi niliongoza kwenye kitanda alichokuwa kalazwa Thobias huku pembeni yake akiwa bibi yake ambaye baada ya kuniona alifurahi sana.

"Waooo mwanangu mwenyewe pole na kukimbia bila shaka lilikuchanganya sana hili. Pole sana kama unavyomuona hapo anaendelea vizuri kwa kweli." Mama Alinieleza kwa ufupi akiwa kanikumbatia.

"Mwanangu pole sana." Nilimpa pole mwanangu mara baada ya kuachana na mama wakati huo baba yeye alitoka kwenda kufuata maji dukani.

"Asante mama yangu."

"Unajisikiaje lakini?"

"Najisikia vizuri kwa sasa tofauti na nilivyoletwa." Alinijibu.

"Mungu atakusaidia mwanangu utapona tu kikubwa ni kufuata yale unayoshauriwa na wataalam hapa Hospitali sawa mwanangu?"

"Nimekusikia mama." Alinijibu.

"Nafurahi kusikia hivyo eenh ilikuwaje mpaka likakukuta hili?"

"Ilikuwa ni ajali tu mama maana wakati najiandaa kuupiga mpira karibu na eneo la goli alifika beki wa timu pinzani ambaye katika kuhakikisha kuwa hakutokei hatari golini kwao alinizoa mzima mzima na baada ya kuanguka ndipo nilipokutana na hili." Alinijibu.

" Pole sana mwanangu utapona tu hiyo naweza kuweza kusema ni bahati mbaya kwenye viwanja vya mpira hutokea."

"Ni kweli kabisa mama." Alinijibu.

"Haya hebu kula kwanza chakula kabla hakijapoa." Mama alikuja na kumtaka Thobias ale kwanza baada ya kuona stori zimezidi kati ya mama na mwanaye.

Kisha tulitoka nje na kumuacha Thobias akiendelea kula.

"Enhh mwanangu za huko?" Mama aliuliza.

"Huko kwema kabisa na kila kitu kimekwenda vizuri kabisa kama vile tulivyotarajia japo nilikutana na mtihani ambao matokeo yake yangekuwa mabaya kama si msaada wa wasamaria." Nilimjibu.

"Mbona unanitisha tena nini kilikukuta huko na vipi huyo mkwe mlikutana?" Mama alitaka kujua zaidi.

"Mama mbona una haraka hivyo utajua tu tukifika nyumbani." Nilimjibu nikiinuka kumpokea baba maji,niliingia nayo mpaka alipokuwa Thobias na kumkabidhi.

"Mbona huli?" Nilimuuliza.

"Nimeshiba mama." Alinijibu.

"Hapana umeshiba vipi wakati umekula kidogo?"

"Nimejilazimisha lakini wapi hakipiti shingoni." Alinijibu.

"Umeanza kudeka baada ya kuniona, unadekaje mtoto wa kiume?" Nilimuuliza.

"Nilazimishe ili nitapike hata hiki kidogo?" Aliniuliza.

"Okay kwa hiyo unataka chakula gani ambacho ni rafiki mkubwa wa koo lako?" Nilimuuliza swali ambalo lilimfanya atabasamu.

"Labda kipande cha kuku na vichips kwa mbali."

"Vichips kwa mbali...." Nilimjibu nikiwa nimeibana pua kurudia baadhi ya maneno aliyoyaongea Thobias.

"Si nimelijibu swali lako mama?" Aliniuliza.

"Haya ngoja nikakufuatie hapo mabandani." Nilimjibu na kutoka nje.

"Wapi tena mama Thobias?" Mama aliniuliza mara baada ya kuona nawapita pale walipokuwa wamekaa na baba.

"Si mumeo huyo kaniona tu usenu umeanza eti chakula hakipiti hivyo anataka nyama ya kuku na chips." Nilimjibu.

"Mhh haya kamnunulie."

"Sawa mama." Nilimjibu.

"Au niende mimi mwanangu?" Baba alinitupia swali.

"Muache aende mwenyewe." Mama alimjibu huku akinipa ishara ya kuendelea na swali.

Nilifika mpaka kwenye mabanda yachomayo chips na kuku kwa wingi nje ya jengo la hospitali na kisha kutoa oda. Na kwa kuwa kinjaa kilinishika ikabidi na mimi niagize mayai yangu mawili ya kuchemsha pamoja na juisi ya nanasi na hapo hapo nikatoa simu yangu na kumpigia Rachel.

"Enhh niambie dada yangu." Alianza mara baada ya kupokea.

"Nimeshafika mdogo wangu safari niliiona fupi sana kutokana na maneno ya rafiki yako." Nilimjibu.

"Hakutupa ndoano? Maana jamaa namuelewaga kwenye hizo mambo huwa hachezi mbali." Aliniuliza.

"Hakufanya hivyo labda ni kutokana na abiria wengine tuliokuwa nao kwenye gari."

"Weee nani huyo? Anajaligi yule sema jini lake la kutongoza lilikuwa limetoka kwenda kuzurura."

"Kwa hiyo ni noma eee?" Nilimuuliza.

"Usiombe kusimuliwa." Alinijibu.

"Duu kwa hiyo na kwako alifanya yake?" Nilimuuliza.

"Hebu achana na hizo mambo mgonjwa anaendeleaje?" Alipotezea.

"Kiukweli anaendelea vizuri nimetoka mara moja kumtafutia chakula si unajua tena mama kafika siyo kudeka kule."

"Hata ningekuwa ni mimi ningefanya hivyo hivyo." Alinijibu mara simu iliingia hivyo nikamuomba akate ili niipokee kwani ilikuwa ni namba ngeni kabisa.

"Naongea na nani tafadhali?" Niliuliza mara baada ya kupokea simu.

"Kwamba umenisahau Tina?" Upande wa pili uliuliza.

"Ni namba ngeni halafu nakutana na watu wengi hivyo ni ngumu kuwakumbuka wote." Nilimjibu.

"Unalikumbuka basi la Kibiki Express?" Aliniuliza mtu huyo.

"Kibiki Express?" Na mimi nilimuuliza.

"Ndiyo hilo hilo au hulikumbuki?" Aliniuliza.

"Kibiki, Kibiki Ex.... Aaa nimelikumbuka tayari na wewe ni nani kwenye hilo basi?" Nilimuuliza tena.

"Kumbuka vizuri siku hiyo ulikaa na nani kwenye siti ukiwa unaelekea Mbeya?" Alinijibu kwa swali.

"Aaaa nimekumbuka tayari....." Kabla sijamjibu alinikatisha.

"Kama umekumbuka mimi naitwa nani?"


JE NINI KITAENDELEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII YA KUSISIMUA ZAIDI.


 #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post