IMETOSHA MAMA MKWE - 53
sultanuwezotz.blogspot.com
Sikumjibu chochote Rachel nilichokifanya niliikata simu na kwenda kwenye sehemu ya kuandikia ujumbe nikaandika na kumtumia Salehe mwanaume ambaye kwa muda mrefu amekuwa hakati tamaa kulivizia penzi langu akiwa na matumaini tele ya kuninasa siku za usoni.
"Sorry kwa kuikata simu yako Salehe siko sehemu nzuri nikitulia nakucheki mtu wangu." Nikautuma.
"Vipi mbona umeikata au ni mbadala wa Jofrey nini?" Rachel aliniuliza baada ya kuona sijaipokea ile simu.
"Hapana ni mpuuzi mmoja hivi mara nyingi hunisumbua sana hivyo nimeona nimpuuzie tu."
"Hii dada yaani mpuuzi ndiyo umuwekee tabasamu pana kiasi hicho? Basi wewe ni mtu mbaya sana unaweza kumuua mtu huku unacheka." Alinijibu Rachel baada ya kutoridhishwa na majibu yangu.
"Wala usijali Tina nilitaka kukujulia hali tu wala si kingine but yote kwa yote baadaye...." Salehe aliujibu ujumbe wangu.
"Pamoja Salehe." Nilimjibu.
"Unajua nini mdogo wangu si kila adui lazima umnunie japo kuna wengine ni ngumu kuona hata rangi ya meno yako."
"Mfano Jofrey eti?"
"Pigia mstari mwenyewe." Nilimjibu.
Tukiwa maeneo ya Igawa nilimkumbusha Rachel vinywaji tulivyoviacha kwenye friji pale Ilembula Golden Star wakati huo tukihangaika kununua maji na juisi maana njaa ilitufanya mbaya.
"Yaani we acha tu tungejua tungebeba kidogo sasa angalia kinachotokea muda huu."
"Akili zote zilikuwa wilayani tungekumbuka vipi?"
"Ni kweli kabisa."
Tuliingia garini na kuelekea na safari baada ya kila kitu kuwa sawa. Safari hii mwendo haukuwa mkali sana kwa sababu tulikuwa tunakula katika kupunguza njaa. Na wakati huo huo simu ya mama iliingia.
"Abee mama..." Niliitika baada ya kuipokea.
"Tina mko wapi muda huu? Sisi ndiyo tunashuka hapa Inyara stendi."
"Mmewahi!! Basi msiondoke hapo baada ya dakika arobaini tutakuwa hapo au ngoja nimpigie simu mzee Nyaswa aje kuwafuata, sisi ndiyo tunaitafuta Chimala."
"Bora iwe hivyo lakini kuwasubiri watu ambao bado mko mbali hapana hebu mpigie huyo babu yenu." Mama aliona hakuna sababu ya kutusubiri hivyo aliunga mkono kufuatwa na mzee Nyaswa. Na wao walitangulia baada ya kukubaliana kuwa watatukuta stendi ya Inyara au tutawakuta maana kwa mizunguko yetu tuliona siyo vizuri kuambatana nao. Pasipo kusubiri Rachel alimpigia simu mzee Mbogo na kumjulisha kila kitu juu ya safari yetu ikiwa ni pamoja na kumjulisha kuwa barabarani kuna wageni wanawasubiri.
"Babu keshapona dada Tina." Alinigeukia na kuniambia baada ya kukata simu ya babu.
"Umejuaje?" Nilimuuliza.
"Si kasema ngoja awafuate yeye mwenyewe kwa sababu mzee Nyaswa kaelekea porini kutufuta viungo vya dawa zako." Rachel aliniambia na muda huu tulikuwa tunaitafuta Igurusi huku Chimala tukiwa tumeiacha kama dakika kumi zilizopita.
"Mungu mkubwa mdogo wangu mzee Mbogo hawezi kufa kizembe hivyo nakwambia."
"Haswaa na safari hii hao wajiitao wakina Jofele sijui wajiandae namfahamu babu yangu akiguswa kizembe." Rachel aliongea akitabasamu nyuma ya usukani.
"Natamani hata awasagesage tu vinyamkera hao na vile walivyonitoka acha tu."
"Yaani hapa dada natamani hata niruke si unajua ukifika ugenini halafu yule mwenyeji wako hujamkuta inavyokuwaga?" Rachel aliniambia.
"Ni kweli lakini kuwa makini ndugu yangu tutawakuta tu wenzetu wamefika tusije ishia kwenye jeneza bure." Nilimtahadharisha na mwendo wake.
"Abee mama.." Niliitika baada ya kuipokea simu ya mama.
"Nilitaka kukuambia kuwa tayari tumefika hapa kwa mzee wenu alifika mzee Mbogo kutufuata."
"Sawa mama na sisi hatuko mbali sana hivyo msijisikie upweke."
"Wala msijali wanangu uzuri mzee Mbogo ni mcheshi kama vile tumewahi kukutana hapo awali, anaongea huyo!!!"
"Na hapo mbona bado ni mcheshi sana mzee Mbogo na hapo hajafika mwenyewe.."
"Basi twawasubiri safari njema." Aliaga na kukata simu.
"Wamefika tayari?" Rachel aliuliza.
"Anamshangaa babu ambavyo ni mcheshi."
"Chezea babu nini na hapo kazeeka sijui kwenye ujana wake alikuwaje?" Rachel aliuliza wakiwa wanaiacha Mswisi.
"Mke wangu uko wapi? Inamaana hautaki kukutana nami kweli? Hebu jaribu kuwa na tone hata moja tu la huruma hata kama tumekosana isiwe sababu ya kunifanyia hivyo, rudi mke wangu tuyaweke sawa haya yanazungumzika mbona." Uliingia ujumbe kwenye simu ya Christina na baada ya kuusoma alicheka kwa sauti kitu kilichomfanya Rachel kumtolea macho dada yake.
" Dada Tina utanifanya niangushe gari mwenzako si unanijua mdogo wako ambavyo huwa sipendi kupitwa na umbea?"
" Huna lolote Rachel unanivuta ili nikwambie kinachonichekesha hapa na mimi sikwambii muda huu mpaka tukifika nyumbani." Nilimjibu.
"Mhh sawa dada nifanyie tu hivyo lakini kumbuka mimi ni ndugu yako."
"Najua mdogo wangu lakini elewa kuwa ubuyu wote umedondoka wacha nianze kuuokota najua mpaka kufika Inyara utakuwa tayari." Nilimjibu Rachel huku nikimuandikia ujumbe Jofrey.
"Nausubiri huo japo utakuwa umeanza kupoapoa."
"Usijali ongeza umakini kwenye usukani."
"Poa dada."
Niliendelea kuandika ujumbe ambao nilijua ukimfikia Jofrey lazima akereke kama siyo kuzimia kabisa.
"Leo ndiyo umegundua kuwa mimi ni mke wako? Na kama ndivyo ilivyo kwanini ulikuwa ukiwasiliana kwa kila kitu na familia yako ambao ndiyo wake zako kuanzia maandalizi ya safari kutoka Singida mpaka unafika Ilembula? Najua kilichokuleta kwangu wewe na ndugu zako uliowatoa huko walikotoka. Labda nikwambie kuwa mimi si yule uliyemdhania kufanikisha zoezi lenu la kishirikina, mimi ni mwingine kabisa ambaye maisha yangu yako mikononi mwa wanipendao. Kwa sasa achana na mimi ninachoweza kukushauri nikiwa kama aliyekuwa mkeo shughulika na afya ya mama yako ambayo imeteteleka wakati akiwa kuwanga. WACHAWI WAKUBWA NINYI na ninakupa siku nne tu muwe mmeihama nyumba yangu tofauti na hapo moto mtauona."
Nilipoituma tu niliamua kuizima kabisa simu na kuiweka mkobani. Lakini nikiwa bize na simu Rachel alikuwa akinichora tu huku ameshalipaki gari chini ya mti wa mwembe.
" Mbona umenitolea macho hivyo? Haa tumeshafika tayari."Nilijikuta nikiuliza swali na kulijibu mwenyewe.
" Wewe si uko bize na simu."Rachel aliniambia akishuka.
" Siyo hivyo mdogo wangu kuna kitu nilikuwa nakifanya nitakuonesha usijali." Nilimjibu Rachel.
" Mmepaa hewani?" Mama alikuja na kutuuliza akiwa haamini kile anachokiona maana aliongea macho yakiwa kwenye saa yake.
" Hapana mama ni mwendo wa kawaida kwani gari lenyewe linaruhusu mwendo wowote." Rachel alimjibu.
" Poleni na safari lakini." Nilimsalimu.
" Mungu ni mwema tumewasili salama japo mwendo ulikuwa ni roho mkononi."
"Shikamoo mama!" Rachel alimsalimu mama ambaye alikuwa akisimulia ya barabarani.
"Marhaba mwanangu bila shaka ni Rachel eehh!" Aliitikia na kumuuliza.
"Ni mimi mama." Alimjibu.
"Mwanangu nakuombea maisha marefu kwani wewe ni mkombozi wa Tina."
"Kwa maombi yenu mama maana maadui wametanua mbawa zao juu yetu na ndiyo maana babu chupuchupu kulalia jeneza."
"Waooo wanangu..." Baba naye mzee Thobias alitoka ndani na kuja kutulaki.
"Hamjambo wanangu? Poleni na yote yaliyowapata maana mzee Mbogo kanieleza kila kitu. Poleni sana na Mungu aendelee kuwatangulia kwa kila hatua yenu."
"Tunashukuru sana baba." Tuliitikia kwa pamoja.
"Mwanangu una mkosi gani wewe yaani makuzi yako yote hujawahi kuyafurahia maisha yako." Baba aliniambia akiwa kanikumbatia machozi yakinitoka maana maneno ya baba yaliuchoma moyo wangu.
"Kuna msemo usemao ILI DHAHABU IWE NA THAMANI LAZIMA IPITE KWENYE MOTO inawezekana ndiyo moto ninaoupitia baba naomba mzidi kuniombea tu."
"Kila siku ndiyo wimbo wetu huo kuanzia asubuhi mchana na jioni na ninakuhakikishia hakuna baya ambalo litakukuta kipenzi changu." Alinijibu akiniachia na kumfuata Rachel.
"Mwanangu hakika wewe ni mkombozi wa Tina na leo naomba nikwambie kuwa mimi ndiyo baba yako na utakuwa binti yangu wa pili ukiwa tayari lakini."
"Kwa nilivyozoeana na dada Tina niko tayari kuwa mwanao mzee Thobias." Maneno ya Rachel yalimvuta mama Tina kutoka alipokuwa kasimama na Tina na kumfuata Rachel aliyekuwa kakumbatiwa na mzee Thobias na kumvutia kwake.
"Rachel sisi tunajivunia kuwa na wewe kwenye familia yetu na Tunakuhakikishia kuwa tutafanya chochote juu ya maisha yenu."
Wakati huo huo mzee Nyaswa aliwasili akiwa na kimfuko chake begani huku mkononi akiwa na kajembe kadogo, alichokutana nacho uwanjani kwake kilimfanya apigwe na butwaa hivyo kumsogelea mzee Mbogo na kumuuliza kinachoendelea.
" Mzee mwenzangu mbona hivi?"
" Hawa ndiyo wazazi wa Tina hapa wanampongeza Rachel." Alimjibu mzee Mbogo.
"Kwa kweli hata mimi ninamshangaa huyu mtoto kwa roho yake hii ya kuamua kuomba likizo ya wiki mbili ilmradi tu kuhakikisha ndugu yake wa barabarani anarudi kwenye hali yake ya kawaida na angekuwa mwingine angeshamfukuza hasa baada ya wewe kukutana na kisanga cha Bi Kiziwa na chanzo akiwa ni Tina."
" Kweli kabisa ni moyo wa kipekee sana." Mzee Nyaswa sambamba na mzee Mbogo walisogea walipokuwa wamesimama wakina Rachel.
" Wageni karibuni sana, mwenyeji wenu sikuwepo japo mwenyeji mgeni kawakaribisha karibuni sana."
" Tunashukuru sana mzee wetu." Baba alimjibu.
" Tina naomba upeleke ndani hii mizigo." Mzee Nyaswa aliniambia. Nilichukua ule mfuko na kijembe kisha kuvipeleka ndani kama alivyonielekeza. Na baada ya makaribisho yale walisalimiana kisha wakaingia ndani bila shaka mzee Nyaswa hakutaka kupoteza muda aliona aanze shughuli yake.
JE NI NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII.
#SULTANUWEZO