MUUAJI MWENYE BARAKOA - 31 (Mtunzi:Sultan Uwezo)


 MUUAJI MWENYE BARAKOA - 31

sultanuwezotz.blogspot.com 


Catherine alijiuliza akiinua kichwa kumtazama vizuri mtu huyo. Akiwa haamini macho yake baada ya kuhakikisha ni mzee Malick gari aliloingia mzee huyo liliondoka mahali hapo kitu kilichomfanya na yeye Catherine aachane na zoezi la kuusaka usingizi na badala yake kuanza kulifukuzia gari lile.

"Sikubali uniponyoke mjomba tusameheane katika hili." Alijiambia akiwasha gari na kuondoka. Aliingia barabara kuu na kuanza kulifuatilia ambalo kwa wakati huo alikuwa akiliona kwa mbali sana lakini hakukata tamaa miguu ilikuwa ikipishana kwenye pedali za gia pale chini. Spidi ya gari la mzee Malick iliendelea kumshangaza zaidi Catherine ambaye pamoja na kutembea mwendo ambao aliuamini lakini bado alikuwa akimuona anazidi kupotea mbele ya upeo wa macho yake.

"Ile gari ni aina gani? Mbona inatembea vile?" Catherine alijiuliza. Alichukua simu yake na kumtumia ujumbe rafiki yake Uriah.

"Huyu mtu nimemuona tayari lakini kinachonishangaza ni mwendo wake si wa kawaida mdogo wangu sijui nitafanikiwa?" Ndani ya dakika mbili hivi simu iliita na ikabidi aipokee.

"Niambie mdogo wangu."

"Pole dada yangu." Uriah alimpa pole Catherine.

"Sijui nisemeje mdogo wangu maana nikisema asante sijafanikiwa hata kumkaribia ndiyo anazidi kupotea tu." Catherine alimjibu Uriah.

"Usijali dada yangu huyo huna haja ya kushindana naye barabara huwezi kujua mfumo wa gari lake hivyo wewe tembea mwendo wa kawaida tu na mimi wacha nimtafute kupitia ile namba yake kisha nitamfanyia kitu ambacho kitakuongoza." Uriah aliamua kumpa msaada Catherine kupitia mfumo wa intaneti.

"Utakuwa umenisaidia sana mdogo wangu, kumbe wewe shughulikia hilo wacha na mimi niendelee kumfukuzia hivyo hivyo." Alishukuru.

"Usijali dada yangu tuko pamoja." Uriah alimjibu na kuondoka hewani kumuacha Catherine aendelee kupambana na usukani. Hivyo Catherine alikaa vizuri kwenye siti yake na kuendelea kumfukuzia mzee Malick. Baada ya umbali wa kutosha Catherine hakuweza kuliona tena gari la mzee Malick hali hiyo haikumrudisha nyuma bali alizidi kusonga mbele mpaka pale Uriah alipomtumia ujumbe kuwa azidi kusonga mbele kwani gari la mzee Malick Bolenge haliko mbali na pale alipo yeye ujumbe huo ulizidi kumpa nguvu ya kusonga mbele. Kwa mbali aliliona gari lile likiwa limesimama kando kidogo ya barabara na hali hiyo ikamfanya Catherine apunguze mwendo kuchukua tahadhari katika hilo. Akiwa anapunguza mwendo aliinua simu na kumpigia Uriah ili kumuuliza kitu kabla ya kumfikia adui yake.

"Ndiyo dada." Uriah aliitika baada ya kupokea simu.

"Mdogo wangu niangalizie umbali uliopo kati yangu na wa mzee Malick."

"Kuna nini tena dada?" Uriah alimuuliza.

"Nitakwambia wewe fanyia kazi hilo kwanza." Catherine alimjibu akifungua mlango wa gari ili ashuke.

"Sawa dada." Uriah alimjibu.

"Asijekuwa kanitegea mtego maana hii mizee inakuwaga na machale sana." Aliongea peke yake akishuka chini huku macho yake yakiwa nyuma kuona kama kuna usalama wowote kisha akavuka upande wa pili wa barabara ambako alikwenda kuketi kwenye kichuguu ambacho alikiona akiwa anasimamisha gari, aliketi na kuendelea kuiangalia simu yake akiwa anategemea kupata taarifa yoyote kutoka kwa Uriah.

"Kuna kama kilometa kumi hivi mbele." Ujumbe mfupi uliingia na baada ya kuinua kichwa na kuangalia mbele aliweza kuliona lile gari pale pale lilipokuwa.

"Kwa hiyo ina maana hili siyo gari la mzee Malick? Hii ina maana gani kwangu?" Catherine alijiuliza akiinuka pale alipokuwa amekaa na kuanza kulifuata lile gari ili akajiridhishe. Baada ya kulifikia alisogea na kuchungulia ndani kupitia kioo cha mbele kuona kama anaweza kupata chochote kutoka kwenye hilo gari lakini hakuona kitu, ikabidi agonge kioo kuona kama anaweza kujibiwa lakini haikuwa hivyo.

"Kwa hiyo hili gari ni la nani?" Alijiuliza.

Akajaribu kuutekenya mlango kuona kama anaweza kuufungua lakini haukufunguka. Alitulia kwa muda kisha akaangaza huku na kule lakini hakuona mtu akaona aondoke tu eneo hilo lakini kabla hajavuta hatua kadhaa mbele alimsikia mtu akikohoa nyuma yake hivyo ikabidi ageuke kumuangalia mtu huyo.

"Ninaweza kukusaidia chochote mjukuu wangu?" Sauti nzito sana ilipenya masikioni mwa Catherine na kwenda kutua kwenye ngoma, kilichomshangaza Catherine ni sauti hiyo ambayo ilitoka kwa mzee ambaye si wa makamo sana mwili mwembamba hivi lakini sauti nzito.

"Unasemaje babu?" Ilibidi Catherine aulize kama vile hakusikia alichoulizwa.

"Nasema hivi kuna chochote naweza kukusaidia?" Alirudia swali akizidi kumsogelea.

"Samahani sikusikia vizuri mzee wangu, kwanza heshima yako." Alimjibu.

"Kivipi?" Yule mzee alimuuliza.

"Shikamoo babuu...!" Catherine aliona amsalimu kwa uwazi.

"Hewala mjukuu wangu hiyo ndiyo salamu sasa siyo unaanza tu heshima yako imefanya nini unafikiri... Marahaba mjukuu wangu kuna tatizo?" Alimuuliza.

"Hapana babu nilipoliona gari lako nikawa nimelifananisha na la ndugu yangu mmoja ambaye tuko safari moja lakini yeye alikuwa mbele yangu." Catherine alimjibu.

"Ooh pole sana." Mzee huyo alimpa pole huku akiikagua gari lake kwa nyuma kisha akamgeukia Catherine kwa macho yenye udadisi.

"Yanafanana? Unataka kuniambia hilo gari la ndugu yako hujashika namba yake? Au hata kuuliza kwa njia ya simu kujua yuko wapi?" Yalikuwa maswali mfululizo kutoka kwa mzee huyo ambaye hakujulikana jina lake mara moja.

"Akili haikuweza kufikiria hilo mzee wangu lakini kwa upande wa mawasiliano kwa sasa hapatikani hewani." Catherine alimjibu huku akikuna kichwa chake.

"Jitahidi unapokuwa barabarani usiwe na mawazo mengi kwani hatari sana." Alimshauri Catherine.

"Nakushukuru mzee wangu kwa ushauri wako nitaufanyia kazi." Alimjibu.

"Nitafurahi kama itakuwa hivyo mjukuu wangu kwani barabarani kuna mengi." Aliongeza mzee huyu ambaye alikuwa akitoa kamasi kwa kileso chake kilichochoka.

"Sawa mzee wangu, lakini naomba nikuulize swali kama hutojali."

"Uliza tu mjukuu wangu."

"Ukiwa hapa hakuna gari lolote kama hili lililopita hapa?" Catherine alimuuliza.

"Kiukweli hakuna gari lililopita hapa toka nimesimama." Alimjibu.

"Na wewe una tatizo gani?" Catherine alimuuliza.

"Mimi ninasubiri niletewe mafuta yamenikatikia hapa." Mzee huyu alimjibu.

"Pole sana babu ningekuwa na ya akiba ningekupa lakini ndiyo hivyo sina hata tone."

"Usijali mjukuu wangu kuna kijana nimemuagiza anitelee." Alimjibu.

"Sawa wacha mimi nikuache babu yangu tutakamatana mjini."

"Sawa mama yangu." Mzee huyu alimjibu akiwa kamtumbulia macho Catherine eneo la kifuani kutokana na kivesti alichokuwa kakivaa na Kuliacha eneo la kifua wazi na ilitokana na joto lililokuwa eneo hili ambalo lilimfanya Catherine avue koti lake huku kichwani akiwa kavaa 'cap' ya rangi blue.

"Ubaki salama mzee." Catherine alimuaga na kurudi kwenye gari lake huku akiwa anaendelea kumuangalia mzee huyu na baada ya kuingia kwenye gari alimpigia tena simu Uriah.

"Vipi umempata?" Uriah alimuuliza baada ya kupokea simu.

"Bado Uriah kuna kitu sikielewi hapa unajua." Alimjibu.

"Kivipi dada?" Uriah alimuuliza tena.

"Hebu mcheki tena nipate kujua umbali uliopo kati yetu maana najihisi kuchoka hivi." Alimuomba tena.

"Nipe dakika sifuri hivi." Uriah alimjibu na kukata simu.

"Hapa kuna mchezo nauona nachezewa." Catherine alijiambia mwenyewe akiegema kitini huku simu akiitupa pembeni yake.

Na baada ya dakika kadhaa simu yake iliita na kuipokea haraka.

"Nipe ripoti mdogo wangu." Alianza baada ya kuipokea.

"Kwa sasa kuna kilometa arobaini hivi kati yenu." Alimwambia.

"Makubwa haya..." Catherine aliongea baada ya kupata taarifa ile.

"Kwani ikoje dada?" Uriah alimuuliza tena.

"Yaani huwezi kuamini ndogo wangu nimekutana na gari hapa porini linafanana vile vile na la mzee Malick sasa unavyonitajia huo umbali nashangaa." Alimjibu.

"Kweli dada?" Uriah alimuuliza.

"Ndiyo hivyo mdogo wangu yaani hapa kichwa kinauma hatari maana ni kama mazingaombwe hivi mbele ya macho yangu." Catherine alimjibu.

"Nisikilize dada yangu vizuri kama ni kuachwa umeshaachwa tayari hivyo ninachokiona mimi hapo wewe ondoka kasi ili kumuhadaa huyo mwenye hilo gari kisha ukifika mbele ingiza gari porini kama hakufuatilii kisha kupitia porini huko huko rudi nyuma kumfuatilia unaweza kupata kitu ambacho kitakusaidia maana nahisi hapo kuna kitu wamekifanya baada ya kuhisi wanafuatiliwa kupitia simu yao." Uriah alimshauri Catherine ambaye muda huo alikuwa kaweka simu sikioni na kuibana kwa bega huku akichomoa biskuti moja baada ya nyingine.

" Kwa hiyo umehisi mchezo gani?" Alimuuliza.

" Nahisi wao wako hapo hapo ila simu ndiyo imesafirishwa huo umbali ili kukupoteza boya." Uriah alimjibu.

"Mhhh yaaaap! Ndiyo maana nilikupigia jembe langu. Sasa nitakupigia." Catherine aliinuka na kuitupa pembeni simu huku kiboksi cha biskuti akiwa hana mpango nacho pale kitini, akafunga mkanda vizuri akimuangalia yule mzee kwenye lile gari aliyekuwa bize na simu kisha aliwasha gari na kuondoka na kumpita kasi mzee huyu akiwa kashusha kioo cha upande wake na kumpungia mkono mzee huyo ambaye na yeye alimpungia vile vile. Alikwenda kwa umbali kama wa kilometa tano hivi na baada ya kuuona upenyo ambao ulikuwa wazi akalipachika gari lake na kabla ya kushuka alipandisha kioo na baada ya kuhakikisha kila kitu kiko sawa alishuka na macho yake aliyazungusha huku na kule kuona kama kuna mtu eneo lile kisha akaipachika bastola yake kiunoni na kuanza kupandisha alikotoka.

"Ole wao nibaini kitu cha kuichezea akili yangu nitawaonesha kazi hasa haka kazee." Catherine alikuwa akiongea peke yake huku akiendelea kusonga mbele, pamoja na kutembea lakini masikio yake alikuwa kayategesha kuhakikisha ananasa mawimbi ya sauti yaliyo mbali na pale alipo na hii ikiwa ni njia mojawapo ya kujilinda. Baada ya kutembea kwa umbali fulani alianza kusikia harufu kama nyama ambayo inachomwa hivi hivyo akaona abadili mfumo wa ufuatiliaji na hivyo akaanza kuitumia pua yake.

"Bosi tuleni haraka tuianze safari yetu tambueni kuwa bado tuna safari ndefu ambayo hovyo hovyo tutaingia mji wa Dosso usiku wa manane na hofu yangu ni namna ya kuupita msitu huu wa mpakani ambao una kambi nyingi za wahalifu." Sauti ya yule mzee ilipenya masikioni mwa Catherine kitu ambacho hakukitarajia hata kidogo kukisikia kwa wakati ule hivyo ikabidi atulie aweze kuyanasa maongezi yao zaidi.

"Mzee Gongo mbona unazidi kunichanganya kwani kati ya mji wa Niamey na huo wa Dosso ni upi unatangulia? Kumbuka kuwa safari yetu ni ndani ya mji mkuu wa Niger." Malick Bolenge alimuuliza swali mzee Gongo ambaye dakika kadhaa nyuma katoka kuongea na Catherine.

" Iko hivi Bosi, tutaanza na Dosso ambao hauko mbali sana kutoka mpakani na baada ya hapo ndiyo tutaanza kuutafuta huo mji wa Niamey ambao uko kilometa chache kutoka mto Niger hivyo si safari nyepesi kwetu." Kijana mwingine aliingilia kati mazungumzo hayo ambayo yalizidi kumuingia Catherine aliyekuwa kajificha. Mazungumzo yao yalizidi kunoga hasa huyu mzee Gongo alitamba namna alivyomhadaa Catherine kiasi cha kuamua kuondoka akijua kuwa wako mbele kumbe yeye ndiyo katangulizwa hilo lilimpandisha hasira zaidi Catherine ambaye alitamani kuinuka akamvae mzima mzima lakini alijizuia, alichokifanya aliikagua vizuri bastola yake kama iko tayari kwa kazi kisha akaizima simu ili isimuumbue pale alipo. Na baada ya kumaliza alianza kunyata kusogea karibu zaidi na walipokuwa wakina Malick Bolenge.


AAAH IBAKIZE HIYO HAMU YA KUTAKA KUJUA NINI KINAKWENDA KUTOKEA HAPO PORINI.


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUPATE KUJUA ALIFANIKIWA KUWATIA MIKONONI MWAKE AU YEYE NDIYO ALIGEUZWA KISUSIO.


#SULTANUWEZO 

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post