MUUAJI MWENYE BARAKOA - 32 (Mtunzi:Sultan Uwezo)

 


MUUAJI MWENYE BARAKOA - 32

sultanuwezotz.blogspot.com 


***

Baada ya kurudi kwenye hali yake ya kawaida Mchungaji Rodney Hauser aliangaza macho yake kuwaangalia wote waliokuwa mle ndani na hii inawezekana alikuwa anazisoma sura zile ili kuona anaweza kuokota kitu kwenye sura zao, lakini kubwa zaidi alikuwa anajaribu kuvuta kumbukumbu ya kilichotokea kabla lakini hakuweza kubaini chochote. Akiwa bado kwenye tafakari zito kuna wazo liligonga kichwa chake haraka sana akapapasa mifuko ya suruali yake na ghafla alitulia kama anawaza kitu.

"Bwana Yesu asifiwe Mchungaji." Alishtuliwa na salamu ya Mchungaji Simon Mwaiduko ambaye hakuwamo mle chumbani.

"Amina Mchungaji nini kilisababisha kuwa kwenye hali hii?" Mchungaji Rodney Hauser alimuuliza baada ya kuitikia salamu.

"Kiukweli sifahamu chochote maana tulipigwa na butwaa baada ya wewe kupoteza fahamu lakini baba Askofu kasema anataka kuongea na wewe." Mchungaji Simon Mwaiduko alimjibu. Majibu hayo yalimshtua kidogo Mchungaji Rodney japo hakuuonesha wazi mbele ya Mchungaji Simon.

" Kwani yuko wapi?" Alipotezea kwa kumuuliza.

" Bila shaka atakuwa koridoni hapo nje wacha tumsubiri." Mchungaji Simon alimjibu lakini wakati huo huo mlango ulifunguliwa na Daktari Sylvester Kitesa aliingia na kumkuta Mchungaji Rodney akiwa kaketi kitandani.

" Karibu mzee wangu." Mchungaji Rodney alimkaribisha huku akijiweka sawa na wakati huo huo Mchungaji Simon Mwaiduko alitoka nje na kuwaacha wenyewe mle ndani.

"Unajisikiaje Mchungaji?" Daktari Sylvester Kitesa alimuuliza akiketi pale kitandani.

"Mungu ni mwema baba yangu najisikia vizuri kiukweli." Mchungaji Rodney alimjibu.

"Ni jambo la kukushukuru Mwenyezi Mungu kwa kujibu maombi yetu kwa sababu muda wote watumishi wako hawakulala wakikuomba umponye Mtumishi wako ambaye kwa uweza wako kaketi akiwa salama na hii ni udhihirisho wa ukuu wako, jina lako Lihimidiwe Jehova." Alimaliza kumshukuru Mungu Daktari Sylvester Kitesa.

" Ameeen." Mchungaji Rodney aliitikia.

" Pole sana kwa kilichokutokea siku ile na kupelekea kupoteza fahamu."

"Asante sana mzee wangu."

"Vipi unaweza kukumbuka ni nini kilitokea kabla?"

"Kiukweli mpaka sasa sikumbuki chochote kile japo kinachoniijia kichwani ni kushika simu kwa mara ya mwisho ambayo hata sijui iko wapi." Mchungaji Rodney alimjibu mzee Kitesa ambaye alitoa simu na kumkabidhi.

"Kuna Mtumishi mmoja aliiokota pale ulipokuwa umeidondosha." Daktari Sylvester Kitesa alimwambia baada ya kuona ni kama ana wasiwasi.

"Afadhali maana nilichanganyikiwa mpaka basi."

"Hakuna haja ya kuwa na mashaka yoyote Mchungaji Rodney hapa vijana wangu ni watiifu sana." Alimjibu.

"Shukrani sana." aliongeza kushukuru akiwa anaikagua programu moja baada ya nyingine.

"Sasa unatakiwa ujiandae upate chakula kisha tuelekee Hospitali kwa uchunguzi zaidi wa afya yako." Daktari Sylvester Kitesa alimwambia akiinuka.

"Hospitali tena?" Mchungaji Rodney aliuliza kwa mshangao kidogo.

"Mbona unashangaa Mchungaji hilo si jambo la kawaida tu katika kujiridhisha kuona kama uko timamu kiafya?" Alimuuliza.

"Nimekuelewa mzee wangu." Alimjibu akiinuka pale kitandani wakati huo Daktari Sylvester Kitesa akitoka kumpa nafasi ya kufanya maandalizi.

"Simu alikuwa nayo Baba Askofu ina maana hajaikagua kweli? Na waleti itakuwa wapi isije kuwa nayo anaishikilia mhh sijui itakuwaje akiwa kaziona zile dawa." Mchungaji Rodney Hauser alijiuliza akiwa anaupitia tena ujumbe ambao alitumiwa.

"Mke wangu yuko hai inakaaje hii? Na huyu ambaye alimteka alimpeleka wapi na kama yule anayenifuatilia mimi ndiye alimshikilia mbona hajaongea chochote cha ajabu kunitishia? Na toka nipate hii taarifa mbona mke wangu hanitafuti?" Alizidi kujiuliza maswali ambayo hayakuwa na majibu ya moja kwa moja akiwa anachana nywele zake. Lakini kuna kumbukumbu iliyokuwa ikimuijia na kutoka kichwani kwake.

Akijaribu kuiweka sawa kumbukumbu hiyo lakini hakuweza ikabidi atoke haraka mpaka kwenye nyumba ambayo alifikia Daktari Sylvester Kitesa na kumgongea mlango.

"Ooh Mchungaji wangu karibu ndani." Alikaribishwa.

"Asante mzee."

"Nakuona kama kuna kitu kinakutatiza Mtumishi ni kipi hicho?" Daktari Sylvester Kitesa alimuuliza baada ya kumuona akitokwa na kijasho chenye mchanganyiko wa hofu.

"Kuna kitu kinanitatiza hapa mzee wangu."

"Kipi hicho Mtumishi?"

"Najua nilizimia baada ya kupokea ujumbe ambao ulinishtua sana kwani siku zote niliamini mke wangu alishauawa na adui yangu."

"Ndiyo."

"Sasa kuna maswali lukuki kichwani kwangu yanayonitatiza baba Askofu."

"Yapi hayo?"

"Kwanza ninachojiuliza mzee wangu kama ni kweli mbona hajawahi kunitafuta? Na pili alitekwa na nani? Na tatu kuna kitu kinaniijia hapa ni kama niliongea na mtu hivi karibuni lakini hii kumbukumbu haikai vizuri sana unaweza kunisaidia?" Mchungaji Rodney alimuomba Daktari Sylvester Kitesa.

" Maswali yako ya awali sina majibu yake hebu tuyape muda kwanza hayo lakini hili la mwisho ni kweli kabisa uliongea na mtu ambaye ni mkeo ndiyo lakini vitu ambavyo alikuwa akiongea na wewe bila shaka tunapata majibu ya kwanini hataki kukutafuta." Daktari Sylvester Kitesa alimwambia.

" Kivipi Baba Askofu mbona sikumbuki niliongea naye vipi?"

" Kuna simu ilipigwa tena kwa namba ngeni lakini maelezo ya awali nilihisi ni mtu wako wa karibu hivyo nilikuletea simu uongee naye japo fahamu hazikuwa zimekurejea vizuri na mwisho wa ile simu hamkuelewana vizuri sijui tatizo lilikuwa nini?" Daktari Sylvester Kitesa aliendelea kumsimulia.

" Kivipi mbona sielewi? " Aliuliza.

" Unachojiuliza wewe hata mimi nilijiuliza sana lakini sikupata majibu na ndiyo maana nilikwambia jiandae tuelekee Hospitali wakakufanyie 'checkup' ya kiafya kabla hatujaanza kikao chetu cha ndani kati yangu mimi na wewe kuna vitu vingi sana nahitaji kujua kutoka kwako." Daktari Sylvester Kitesa alimjibu.

" Kiukweli mimi sina tatizo lolote kiafya, niko vizuri na timamu hivyo hakuna sababu ya kwenda huko niamini mimi." Mchungaji Rodney Hauser aliona amueleze ukweli Bosi wake.

" Una uhakika kwa unachokiongea Mchungaji?" Daktari Sylvester Kitesa alimuuliza.

"Asilimia mia moja baba yangu."

"Kwa kuwa umeongea wewe mwenyewe mimi ni nani nikulazimishe ilhali afya ni ya kwako."

"Naomba uniamini." Mchungaji Rodney Hauser alisisitiza.

"Nimekuelewa Mtumishi hivyo wacha tupate chakula kisha tutaingia kwenye kikao chetu." Daktari Sylvester Kitesa alimwambia.

"Bila shaka baba." Mchungaji Rodney alimjibu na wakati huo huo aliingia mama mmoja ambaye alipewa jukumu la kuwahudumia kwa kipindi chote ambacho wako pale Ipinda.

"Karibu mama Grace, nikikuonaga tu wewe tumbo huanza kutabasamu." Daktari Sylvester Kitesa alimkaribisha mama huyo na kumtania.

"Wala hujakosea baba Askofu meza yetu iko tayari naomba mkaribie." Mama Grace alimjibu kama alivyotegemea.

"Tunashukuru sana." Alimjibu

"Karibuni sana." Aliongea na kutoka kisha Daktari alimgeukia Mchungaji Rodney Hauser na kumwambia waelekee mezani japo Mchungaji Rodney alionekana mwenye mawazo sana.

"Kijana wangu unatakiwa upunguze mawazo hujui kuwa huo nao ni ugonjwa?"

"Mhh nilikuwa bado nafikiria ni kitu gani mke wangu alikiongea mpaka kufikia hatua ya kutoelewana."

"Usijali ukipata muda mtalimaliza hilo." Daktari Sylvester Kitesa alimjibu wakitoka kuelekea sehemu ambayo iliandaliwa kwa chakula. Walifika na kuikuta meza imependeza huku Mchungaji Simon Mwaiduko akiwa pale anawasubiri.

"Kijana wangu maeneo haya huwa huchezi nayo mbali." Alimtania wakati akivuta kiti akae.

"Mzee wangu kuna maeneo ya kucheza nayo mbali lakini kwa hapa hapana naogopa sana vidonda vya tumbo." Mchungaji Simon Mwaiduko alimjibu.

"Uko sahihi sana mdogo wangu." Mchungaji Rodney alikubaliana na maneno ya Simon Mwaiduko.

Wakiwa wanapata chakula Mchungaji Rodney alikuwa akiendelea kucheza na simu yake ndipo alipokiona kibahasha cha ujumbe ambao haukusomwa na alipouangalia vizuri akagundua ni wa muda kidogo hivyo akapata shauku ya kuusoma.

"Bwana Yesu asifiwe baba Mchungaji, huku mambo yanaendelea kuwa magumu huwezi kuamini mzee Lukosa hatunaye. Wakiwa kwenye kikao cha kazi kilichofanyika kwenye moja ya Majengo ya Kanisa alivamiwa akiwa chooni na mtu ambaye alificha sura yake huku jina langu likiwa kwenye orodha yake." Ujumbe huo ulimfanya Mchungaji Rodney Hauser adondoshe kijiko chenye chakula kitendo kilichomfanya kila mmoja pale mezani amkodolee macho.

" Daktari Brown Lutasya anamaanisha au anataka kunirusha roho tu?" Alijiuliza huku akiwa haelewi kama kijiko kiko chini Mchungaji Simon Mwaiduko aliinuka na kwenda kumletea kijiko kingine.

" Kuna nini tena kijana wangu?" Daktari Sylvester Kitesa alimuuliza baada ya kuona yuko mbali kimawazo.

" Naam!"

" Kuna nini?"

" Hakuna kitu baba nadhani mwili unajikunjua kuwa sawa." Jibu lake lilimfanya Daktari Sylvester Kitesa kucheka.

"Una taaluma ya Udaktari eehh?"

"Hapana sina bali nahisi tu."

"Nikuombe hiyo simu uiweke chini kwanza ili ushibe na baada ya hapo utaendelea ukiwa umetulia mwenyewe." Daktari Sylvester Kitesa alimshauri.

"Sawa baba." Alimjibu akipokea kijiko kutoka kwa Mchungaji Simon Mwaiduko.

"Nashukuru sana mdogo wangu na samahani kwa kukusumbua." Alimshukuru Mchungaji Simon Mwaiduko.

Chakula kiliendelea na baada ya kutosheka Mchungaji Rodney alishukuru na kuwaacha wenzake wakiendelea kula yeye akarudi sebule kubwa na kuketi lakini akainuka na kutoka mlango wa pili akazunguka nyuma ya jengo hilo na kumtafuta Daktari Brown Lutasya ambaye kama bahati alimpata hewani na ndani ya dakika kadhaa aliipokea simu yake.

"Habari yako Mtumishi wangu." Alianza baada ya kupokea simu.

"Namshukuru Mungu naendelea vizuri lakini ujumbe wako umenishtua sana."

"Ujumbe?"

"Ndiyo ujumbe au umeusahau?"

"Sikumbuki kama nimekutumia ujumbe leo mimi au umechanganya habari?"

"Hapana mzee kuna ujumbe huu unaohusu tukio la kuvamiwa kwenu."

"Unausema huo ambao tulishasahau kitambo na nilijua hujaujibu kwanini." Daktari Brown alimjibu.

"Sikumaanisha hivyo mzee wangu kwani hata kama nilikuwa kwenye kutoelewana naye lakini siyo kwamba akipatwa na tatizo nisijali?" Mchungaji Rodney alijitetea.

"Na kwa taarifa yako huku taarifa zilizoenea juu ya kifo chake mzee Lukosa zinasema wewe ndiye uliyehusika kutokana na ugomvi wenu na inavyoonekana alikuwa na siri zako ambazo alitaka kuziweka hadharani na wewe haukuwa tayari kuona hilo linatokea hivyo ukaona umfanyie unyama ulioufanya. Kama ni kweli umelifanya hili Mungu anakuona na siku zako zinakuja."Baada ya kusema hivyo tu Daktari Brown Lutasya alimkatia simu wakati yeye alikuwa bado anataka kuendelea kuongea naye na alipotaka kupiga hakuweza kumpata hewani na wakati anahangaika kumtafuta mara alishangaa kukutana uso kwa uso na Daktari Sylvester Kitesa baada ya kugeuka na kumuona akiwa kasimama mlangoni. Hilo lilimfanya Mchungaji Rodney Hauser kuishiwa pozi kwani hakutarajia kumuona Daktari Sylvester Kitesa mahali pale kwani ile kwake ilikuwa ni faragha.

"Samahani Mchungaji nakuomba tuingie kwenye mazungumzo yetu." Daktari Sylvester Kitesa alimwambia na kisha yeye alitangulia ndani na kumuacha Mchungaji Rodney akiwa anajitengeneza shati lake kulifanya likae vizuri.

"Huko ndani kuna nini mbona huyu mzee kaniganda hivi au kashtukia mambo yangu huyu?" Mchungaji Rodney alijiuliza swali akianza kupanda ngazi kuelekea ndani.

"Kasema msubiri hapa kwanza kuna mtu anaongea naye kwanza." Mchungaji Simon Mwaiduko aliyekuwa kaketi pale 'waiting room'.

"Anaongea na nani huko?"

"Mhh ni mama mmoja kaingia na mtoto wake ambaye ni miongoni mwa wale ambao Kanisa letu linawasomesha hivyo kila wanaporejea hufika hapa kwa ajili ya kujua maendeleo yao pamoja na changamoto nyingine wanazopitia wawapo huko shuleni." Mchungaji Simon alimjibu.

" Safi sana hii nimeipenda hata sisi kule tuna hii programu ambayo imekuwa msaada kwa watoto wengi hasa wale waishio kwenye mazingira magumu." Mchungaji Rodney alipongeza hilo. Na wakiwa wanaendelea na mazungumzo yao mara mama yule na binti yake walitoka ofisini na kuwapa nafasi na wao kuingia.


UNAFIKIRI DAKTARI SYLVESTER KITESA ANATAKA KUONGEA NINI NA MCHUNGAJI RODNEY HAUSER AMBAYE TAYARI KAANZA KUWA NA MASHAKA?


USIJALI TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUPATE KUJUA KUNA BOMU GANI HUKO OFISINI NA MENGINE MENGI HASA HILI LA KUHUSISHWA NA KIFO CHA MZEE LUKOSA.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post