MUUAJI MWENYE BARAKOA - 33 (Mtunzi:Sultan Uwezo)

 


MUUAJI MWENYE BARAKOA - 33

sultanuwezotz.blogspot.com 


Waliingia na kumkuta Daktari Sylvester Kitesa akiwa analifunga kabati na baada ya kuwaona aligeuka na kuwapa ishara ya kuketi kisha naye aliketi kwenye kiti chake na kuwatazama kwa zamu Mchungaji Rodney Hauser pamoja na Mchungaji Simon Mwaiduko.

"Mchungaji Rodney unajisikiaje kwa sasa?" Alianza kwa kumtupia swali.

"Kwa sasa namshukuru Mungu niko sawa kabisa."

"Vizuri vijana wangu na mimi nafurahi kusikia hivyo pia niendelee kukushukuru Mchungaji Simon Mwaiduko kwa kuuchukua muda wako ambao ungeutumia kufanya masuala yako mengine na kuhakikisha kuwa tunalala vizuri, tunakula vizuri kwa hilo sina budi kukushukuru." Daktari Sylvester Kitesa alimshukuru Mchungaji Simon Mwaiduko.

" Ni moja ya majukumu yangu baba Askofu hivyo naona faraja kukuhudumieni mkiwa wageni wangu." Mchungaji Simon aliongea.

" Okay sawa kijana wangu nimekuelewa wacha turudi kwenye agenda iliyo mezani, ndugu yangu Rodney kuna kitu nahitaji kujua kutoka kwako." Daktari Sylvester Kitesa alianza.

" Kitu gani baba Askofu?" Mchungaji Rodney aliuliza akikaa vizuri kwenye kiti.

"Kuna vitu sivielewi kutoka kwako toka tumewasili hapa Ipinda Kyela na elewa kuwa nilikutaka uje huku baada ya kunieleza maswaibu yaliyotokea kule Senegal lakini kila kukicha nakuona una vitu vya siri ambavyo hutaki watu wajue, na katika hili nimemuita na kijana wangu Simon ili tusaidiane kulijadili hili suala."

"Baba Askofu kwanini umeamua kuniweka kikao tawini tena mbele ya mdogo wangu Simon wakati mambo kama haya unafahamu yanatakiwa yajadiliwe wapi na kingine nikikuangalia nakuona umepanga jambo juu yangu na ndiyo maana unanifuatilia kila kona kiasi cha kushindwa kupumua, nimechokaaaaa...!! " Mchungaji Rodney alimuijia juu kiongozi wake.

" Nakuona unavyochomoza pembe kijana wangu, kuna baya gani nililokufanyia hapa?" Daktari Sylvester Kitesa alimuuliza baada ya kumuona akibadilika.

" Kaka mbona sijaona baya lolote hapa na ukizingatia baba Askofu kaona tulizungumzie kama familia ili lisije kufika huko unakotaka liende linaweza kukuletea shida." Mchungaji Simon Mwaiduko alimwambia Mchungaji Rodney Hauser ambaye muda huo alikuwa akikitembeza kitambaa usoni kwake kulipunguza jasho ambalo lilikuwa na linamtiririka kama chemchem.

" Simon ndugu yangu wewe bado mdogo sana kwenye huduma hii mwenzako nina miaka zaidi ya kumi na tisa na kitu kingine ambacho hukijui ni kwamba unapozungumzia kukua kwa kanisa letu la 'JESUS OUR KING' ndani na nje ya Afrika huwezi kuacha kulitaja jina langu hivyo unapoongea na mimi jitahidi kupangilia maneno yako vizuri isije kukuletea matatizo." Mchungaji Rodney bila kupepesa macho aliongea jambo lililomchanganya Daktari Sylvester Kitesa.

" Unasemaje Mchungaji Rodney? Unataka kusema wewe ni mkubwa kuliko mimi siyo?" Daktari Sylvester Kitesa alimuuliza.

" Hayo unayaongea wewe na si mimi ila tu nilikuwa najaribu kumwambia ukweli wa mambo ulivyo na aweze kujua namaanisha nini ninaposema hii siyo sehemu sahihi ya kulizungumzia jambo langu na hata kama umedhamiria kunisimamisha kazi mimi sijali sababu umeshapanga iwe hivyo." Daktari Sylvester Kitesa alimtazama Mchungaji Rodney Hauser aliyekuwa akibwabwaja maneno yake bila breki bila kumjibu chochote na alichokifanya alivuta droo ya meza na kuvitoa vitu vilivyokuwa ndani yake na kuviweka mezani.

" Naomba ukague kimoja baada ya kingine ili kujiridhisha kama vipo vyote."

Baada ya kuyatupa mezani na kuviona vitu vyake vya siri ambavyo hakuwahi kuvianika mbele ya macho ya watu wengine isipokuwa yeye tu.

"Na...na...na..hi..hiki kilikuwa kwenye wale...waleti yangu ba...ba...baba Askofu?" Alijikuta akiuliza kwa kukatakata maneno. Lakini Daktari Sylvester Kitesa hakumjibu chochote zaidi ya kumpa ishara Mchungaji Simon Mwaiduko kutoka nje kisha naye akatoka na kumuacha Mchungaji Rodney Hauser akiwa ameitolea macho meza iliyokuwa na vitu vyake.

"Mwaiduko naomba kaendelee na majukumu yako wacha mimi nipumzike kidogo." Daktari Sylvester Kitesa alimwambia Mchungaji Simon ampishe apumzike kidogo.

"Sawa baba Askofu lakini umeyachukuliaje maneno ya Mchungaji Rodney?" Mchungaji Simon Mwaiduko alimuuliza Daktari Sylvester Kitesa ambaye alikuwa akiliangalia paa la kanisa.

"Usijali Mchungaji hilo nitalimaliza tu kwa sasa wacha nipumzishe akili kwanza." Alijibu kisha akatoa simu yake na kusogea mbele kidogo na baada ya kumuona Mchungaji Simon Mwaiduko kaondoka pale alipokuwa alirudi akiirejesha simu mfukoni bila ilikuwa ni njia ya kumuondoa Mchungaji Simon Mwaiduko. Baada ya kuona kabaki peke yake aliondoka na kuelekea kiliko chumba chake ambako aliingia na kuufunga mlango.


***


"Kaka Martin hali yangu kwa sasa iko kama unavyoiona." Adoyee aliongea akijikagua ubavu wake uliofungwa tambaa jeupe wenyewe wanaliita bandeji.

"Hata mimi naona hilo Adoyee lakini umebakiwa na kitu kimoja tu ambacho ukikitimiza hicho nitajua umepona." Martin alimjibu.

"Umeanza mambo yako brother ni kitu gani hicho?" Adoyee aliuliza.

"Si kingine ni upande wa chakula tu."

"Ona sasa chakula kitu gani kaka leta hapa hata debe nikuoneshe ni kwa kiasi gani niko bambam." Alimjibu akijaribu kuinuka pale alipokuwa amekaa.

"Debe kitu gani bwana wakati kila siku huo ndiyo umekuwa wimbo wa nyumba." Martin aliongea akiitoa simu yake mfukoni ambayo ilikuwa ikiita.

"Uko wapi Seynabou?" Aliuliza baada ya kupokea simu.

"Niko huku porini nafanya mazoezi."

"Mazoezi gani hayo Seynabou ilhali bado hujapona vizuri huo mguu wako."

"Huamini au? Njoo ujionee mwenyewe kama huamini maneno yangu." Seynabou alimjibu.

"Mmh haya nimekuelewa hata kama si kwa asilimia mia." Martin ilibidi akubaliane tu na kile alichoambiwa.

"Ni nani huyo, Seynabou nini?" Adoyee alimuuliza akiwa anaunyosha mguu wake wa kushoto aliouweka juu ya kiti.

"Seynabou na mambo yake eti yuko kufanya mazoezi porini, hivi unakubaliana na hilo?" Martin alimuuliza Adoyee.

"Seynabou huwa hatabiriki inaweza kuwa kweli na kwa sasa hakuna kitu kingine kinachomuuma kama kubaki hapa wakati wakina Jumbe wako mzigoni." Adoyee alimjibu huko majibu hayo yakidakwa na Seynabou moja kwa moja kutokana na kutokatwa simu. Na baada ya kuiangalia akagundua kuwa hakuikata hivyo akaikata.

" Umeuza nyuzi?" Adoyee alimuuliza baada ya kumuona anavyohangaika na simu.

" Sijui kama amesikia nilisahau kuikata." Alimjibu.

"Lakini Seynabou ni Mzungu hanaga shida yule hivyo usiwe na presha." Adoyee alimpa tumaini Martin.

"Ngoja nimfuate huko huko nikaongee naye maana simuelewi vizuri." Martin alimwambia Adoyee. Na wakati akiondoka simu yake ilikuwa ikiita.

"Dada mkubwa anataka kusema nini tena?" Martin aliuliza baada ya kuiona namba ya Catherine ikicheza kwenye kioo cha simu yake.

"Anataka kukupa taarifa nzuri si unajua hashindwagi yule akiliamulia jambo." Adoyee alimjibu.

"Uko sahihi sana Adoyee yaani kwenye shughuli zangu ningekuwa na kile kichwa mbona wangenijua vizuri ila ndiyo hivyo yeye ni mama visasi."Martin aliongea akipokea simu hiyo na kuiweka sikioni.

" Nipe ripoti jembe langu." Martin alimwambia baada ya kupokea simu.

" Ni majanga tu mtu wangu." Alimjibu kwa sauti ya chini.

" Una maanisha nini kusema hivyo?" Martin alimuuliza.

" Banyamlenge kaniotea aisee yaani huwezi amini ilikuwa sekunde tu nifanye yangu lakini kijiti kikavu kikaniharibia."

"Kwa hiyo unataka kusema kuwa...." Kabla hajamalizia kuuliza swali lake Catherine alimkatisha.

"Jamaa wamenishuti risasi ya bega na kukimbia."

"Dada mkubwa eee hebu nieleze vizuri imekuwaje mpaka umepigwa risasi?" Martin alitaka kujua zaidi.

"Unanichosha bwana iko hivi, wakati nawavizia walipokuwa wamejificha ghafla nikakanyaga kimti kikavu ambacho kilipiga kelele wakati kikikatika na kuwafanya jamaa kuanza kushambulia upande wangu bila hata kuangalia kwanza na wakati huo nilikuwa nachukua tahadhari lakini nilichelewa kwani risasi ilitua vilivyo begani na kunifanya kubadili mkono na kuishikia wa kushoto nikaendelea kuwashambulia japo sikuwa imara sana lakini jamaa waliamua kutimua mbio sikujua nini kilipelekea wao kufanya hivyo." Catherine alimfafanulia Martin ambaye alijikuta akikaa chini kutokana na taarifa hiyo.

" Kwa unavyoona kuna uwezekano wa kujiokoa hapo ulipo? Na ni eneo gani hilo?" Martin alimuuliza.

" Niko taratibu kulifuata gari lakini hata hivyo nimeshampigia simu rafiki yangu Uriah aje anipe kampani na hivi tunavyoongea alishaianza safari na hapa nilipo ni ndani ya msitu mmoja hivi ambao sijaujua jina lake lakini upo karibu na mpaka wa kuingia nchi ya Niger."

" Mmh yaani wewe ni hatari uko huko? Yaani ungejuaga ungeondoka na sapoti ya wakina Jumbe."

" Kwa hiyo unanilaumu sasa? " Catherine alimuuliza.

" Sina maana hiyo dada mkubwa naongea hivyo kwa sababu huo msitu naufahamu vizuri sana una matukio ya ajabu ajabu hivi lakini siyo kukulaumu." Martin alimfafanulia Catherine ambaye tayari alishakata simu.

" Kafanyaje?" Adoyee alimuuliza Martin ambaye alikuwa kaduwaa baada ya Catherine kuondoka hewani.

" Nini?" Alimgeukia Adoyee na kumuuliza.

" Nasema kafanyaje Bosi?" Adoyee aliuliza tena.

" Yaani sijui dada mkubwa anakuwaga namna gani hatujamaliza anakata simu." Badala ya kujibu swali aliloulizwa yeye akaongea jingine ambalo lilimfanya Adoyee kumfuata pale pale alipo.

"Kaka ina maana hujalisikia swali langu?" Adoyee alimuuliza akimgusa mgongo.

"Oyaaa vipi mbona tunatingana hivyo si umpigie kama mwili unakuwasha kutaka kujua kilichomkuta." Alimjibu na kuondoka akimuacha pale pale Adoyee.

Wakati Adoyee akiwa ameduwaa kwa kilichofanywa na Martin mara Seynabou alitokea akiwa anaendesha baiskeli na kwenda moja kwa moja mpaka alipokuwa Adoyee.

" Vipi kaka mbona umeduwaa hivyo au umepokea taarifa mbaya kutoka nyumbani nini?" Seynabou alimuuliza akishuka kwenye baiskeli.

"Ni kweli nimepokea taarifa mbaya lakini siyo kutoka nyumbani bali ni kutoka kwa Bosi."

"Bosi gani tena?" Seynabou alimuuliza.

"Na wewe kwani tuna mabosi wangapi hapa?" Adoyee alimuuliza.

"Sasa si ndiyo unijibu swali langu?"

"Namaanisha Bosi Catherine."

"Enhh?"

"Ndiyo hivyo lakini sijui niseme nini maana mwenye taarifa kamili mwenyewe anaringa kama nini kakataa kunieleza kaelekea ndani." Adoyee alimjibu akiinuka.

"Au kafa?" Seynabou aliuliza.

"Unasemaje?"

" Najiuliza tu simaanishi hivyo." Seynabou alimjibu.

"Shauri yako."

"Wacha nimfuate huko huko ndani akaniekeze kwanini anaikalia taarifa muhimu kama hii." Seynabou alimwambia Adoyee na kuelekea ndani aliko Martin.

"Umerudi tayari?" Martin alimuuliza.

"Kutoka wapi? Hivi unakuwa na maana gani kukaa kimya na taarifa kama hiyo?" Seynabou alimuuliza swali badala ya kumjibu swali aliloulizwa.

"Mbona mapovu mdogo wangu?"

"Mapovu eee kwa hiyo mimi nimekuwa sabuni siyo?" Seynabou alimuuliza akimsogelea karibu zaidi.

"Hebu keti kwanza hapa maneno mengi ya nini Seynabou?" Martin alimtaka atulie kwanza ili aweze kumpa taarifa ilivyo.

"Kaka siyo vizuri hivyo ujue." Seynabou alimwambia akiliendea friji la maji huku Martin akiwa kashikilia simu yake ambayo ni kama alikuwa akimtafuta mtu hivi bila mafanikio.


JE NI NINI KITATOKEA KATIKA KITIMUTIMU HIKI?


USIJALI TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUPATE KUJUA MBIVU NA MBICHI.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post