MUUAJI MWENYE BARAKOA - 34 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


MUUAJI MWENYE BARAKOA - 34

sultanuwezotz.blogspot.com 


"Unajua nini Seynabou? siyo kwamba sitaki kuwaambia chochote kutoka kwa bosi wenu la hasha ila tu mwili umepata ganzi kwa nilichoambiwa na Madam Catherine." Martin alimjibu Seynabou.

"Basi tuambie kilichomsibu ili mioyo yetu ipate kutulia." Seynabou aliendelea kusisitiza na wakati huo Adoyee akiwa na wakina Soud ambao walitumwa mjini na Martin waliingia ndani.

"Kwa mujibu wake ni kwamba kashambuliwa na watu wa mzee Malick Bolenge na hivi ninavyoongea nanyi bado yuko msituni akimsubiri rafiki yake." Martin alitoa ufafanuzi.

"Kama sijasikia hivi kiongozi unasema big mama kafanyaje?" Soud aliuliza akiweka mizigo mezani.

"Ina maana masikio yako yana nta? Hujamsikia kasema bosi kashambuliwa?" Adoyee alimjibu Soud huku Martin akiipiga tena namba ya Catherine.

"Dada mkubwa niambie, ameshafika huyo rafiki yako au tukufuate wenyewe?" Alimuuliza mara baada ya kupokea simu.

"Msiwe na wasiwasi juu yangu ndugu zangu sijaumia kihivyo na rafiki yangu ameshafika tayari." Catherine alimjibu Martin.

"Kwa hiyo mnarudi au mnasonga mbele?" Martin alimuuliza.

"Turudi wapi tena? Oparesheni ndiyo kwanza imeanza, nisikilize kwanza; wao mpaka sasa watajua wameniweza hivyo wataendelea kutanua wakiamini wameshinda na ndiyo hapo nitawamaliza kwenye 'angle' ambayo hawataitarajia hivyo kuhusu kurudi nitawaambia." Catherine alimjibu Martin kwa kujiamini kama vile hajapatwa na tatizo lolote.

" Ukipanga ni nani wa kukupinga 'big mama' kikubwa muwe makini huko ugenini." Martin alikubaliana na Catherine japo kwa shingo upande. Na kisha alikata simu na kuwageukia wenzake waliokuwa wametanua masikio kutaka kujua kulikoni huko.

"Anarudi eee?" Seynabou alimuuliza.

"Anarudi wapi si unamjua dada yako ukimuona anarudi nyuma ujue kapata anachokitaka na si vinginevyo hivyo kasema anasonga mbele." Martin alimjibu.

"Ooooshh...." Seynabou alishusha pumzi ndefu baada ya kusikia hayo mikono kichwani.

"Yaani sijui yatakwisha lini haya?" Seynabou alijikuta akijiuliza kwa sauti.

"Usijali Seynabou nayo yatapita tu." Soud alimjibu.

"Mpaka lini sasa?" Seynabou aliendelea kuuliza kama vile kavurugwa hivi.

"Unauliza nini wewee kuwa muelewa hata kwa sekunde tu." Adoyee aliamua kumuwakia Seynabou ambaye alihisi kama vile anawachanganya.

"Acheni mikelele yenu bwana mnabishana nini sasa hebu kuweni eboo." Martin aliwaka akitoka nje baada ya kuona wakina Seynabou wanamchanganya.


***


Baada ya kufika lilipo gari lake aliona kazi kuingia ndani yake badala yake aliufuata mti uliokuwa pembeni ya gari hilo na kujilaza. Na akiwa hajalala vizuri kuna gari lilifika na kusimama na alipoinua kichwa kuangalia ni nani aliyekuja alijikuta akitabasamu japo kwa maumivu.

"Waoo Uriah nilishakata tamaa nikajua unanitia moyo tu." Catherine alimwambia Uriah akikumbatiana baada ya kushuka garini.

"Kwanini nikudanganye dada yangu kwani hujui tulikotoka?" Uriah alimuuliza Catherine.

"Tuache hayo mdogo wangu hebu tufanye utaratibu wa kuondoka eneo hili si unajua hakuna usalama." Catherine aliamua kukatisha mazungumzo maana ndugu yake ni maneno mengi sana.

"Okay sawa dada wacha nimalizane na kaka wa gari kisha tuendelee na yetu." Aliinuka na kumfuata mwenye gari ambaye alimkabidhi kilicho chake na kisha alirudi alipo Catherine akampa msaada wa kuingia garini kisha safari ya kuelekea Niger ikaanza.

"Kwanza pole kwa yaliyokukuta dada yangu maana uliponiambia kuwa umeshambuliwa kwa risasi mwili wangu wote ulipigwa ganzi si unajua toka nizaliwe risasi huwa naziona za kuchonga kwenye video." Uriah alimwambia Catherine akiwa nyuma ya usukani.

"Kawaida sana mdogo wangu, nilishazoea kupishana na milio ya risasi na risasi zenyewe na huu mwili uuonao una makovu ya kutosha ya risasi, visu nk hivyo usijali kikubwa tuwahi kufika Niger nipate matibabu." Catherine alimjibu akitabasamu.

"Kwa hiyo unataka kuniambia hiyo risasi bado iko begani?" Uriah alimuuliza.

"Bado ipo itatoka vipi mdogo?" Catherine alimjibu akifungua kopo la juisi ya Pera aliyoletewa na Uriah.

"Usijali dada yangu itatoka tu kikubwa Mungu bado anakupenda. Unaionaje juisi?"

"Ni tamu sana aisee wala sikutarajia itakuwa hivi mimi nilizoea juisi ya nanasi na embe pia parachichi hii sikuwahi iwazia maana hata hilo pera lenyewe sijawahi kula sembuse juisi yake?"

" Ndiyo hiyo sasa itakubidi na tunda lake uanze kula sasa."

" Naweza kujaribu lakini si kwa asilimia mia moja." Catherine alimjibu akiangalia nje kulikokuwa na bango kubwa lililokuwa likisomeka 'UNAINGIA NCHI YA NIGER USIMUAMINI MTU USIYEMFAHAMU' na lilimfanya kumuonesha Uriah aliyekuwa bize na usukani.

" Umeyasoma maandishi yake lakini? "

" Mabango yamejaa jumbe kama kanga tu hivyo sioni umuhimu wake bwana kikubwa kama umesoma wewe inatosha." Uriah alimjibu akisimamisha gari pembeni baada ya kusimamishwa na Maafisa Uhamiaji na baada ya kuonesha nyaraka zote muhimu na wao walitimiza na majukumu yao kwa kuwaambia waelekee kwenye banda lililokuwa upande wa pili ambako kulikuwa na taratibu nyingine. Walifanya kama walivyoelekezwa huku Catherine akijikaza ili asishtukiwe na hawa Maafisa.

"Huyu wa nyuma ni kama mwenyewe." Ni maneno ambayo yalipenya masikioni mwa Catherine akiwa mbele ya hawa Maafisa na hapa ndipo alipoanza kupata hofu hivyo alivuta hatua mpaka kwa Uriah na kumvuta koti akiwaangalia wale Maafisa.

"Kuna nini dada?" Uriah alimuuliza baada ya kuona anavutwa lakini haongei chochote.

"Tumechomewa utambi hapa."

"Kivipi?"

"Nimewasikia hao askari wakiulizana juu yangu."

"Mmh atakuwa ni huyo Malick?"

"Unafikiri atakuwa nani mwingine." Wakati huo walikuwa wakisogea kwenye dirisha ambalo walikabidhi nyaraka zao na baada ya kupitiwa ziligongwa mihuri na kisha taratibu nyingine zilifanyika kisha walikabidhiwa na kuanza kurejea garini.

"Cheki wanavyotuangalia." Catherine aliendelea kuonesha hofu yake.

"Achana nao hao."

"Sasa mbona wako wawili na wao walisema kuwa yuko peke yake?" Mmoja alisikika akimuuliza mwenzake.

"Na hata jina mbona si lenyewe inawezekana si yeye wacha tusubiri lazima mhusika atapita tu hapa." Walitiana moyo huku wakina Catherine wakiingia kwenye gari na kuondoka. Na safari hii Catherine aliukalia usukani bila shaka alitaka kutembea mwendo wake ambao Uriah hakuufikia hata kidogo.

" Dada hujionei huruma na hiyo risasi? " Uriah alimuuliza akifunga mkanda lakini Catherine hakumjibu kitu zaidi ya kumuonesha ishara ya kumpigia 'lock' ya mkanda wake huku macho yakiwa mbele kuhakikisha hakuna hatari anayoisababisha. Ndani ya saa moja walikuwa ndani ya msitu ambayo unasemekana ni hatari sana kwa matukio ya kiharifu na hata wanyama wakali.

"Kwa maelezo ya yule mzee ambaye yuko na mzee Malick bila shaka tunakaribia kuingia mji wa Dosso ambao hapo ndiyo itabidi nifanyiwe matibabu." Catherine alifunguka na kumwambia Uriah ambaye alikuwa muda wote macho yako kwa Catherine ambaye mkono mmoja ndiyo uliifanya kazi ya kucheza na usukani.

" Kwa hiyo mji wa kwanza ni Dosso?" Alimuuliza.

" Ndiyo na kisha tutaanza kukutana na vimiji vidogo dogo mpaka tunaingia Niamey ambao ndiyo mji mkuu wa nchi ya Niger."

"Itakuwa poa sana maana nakuonea huruma sana dada yangu naona kama vile mimi ndiyo nina hilo lirisasi."

"Usijali kuhusu mimi Uriah kama nilivyokuambia awali, ila wale machizi walinitia presha ya pua? Na nikajua safari yetu imeishia pale pale." Catherine alimwambia Uriah.

"Kwa hiyo haya yote uliyajua ndiyo maana ukatengeneza kitambulisho hewa?" Uriah alimuuliza.

"Si kimoja kwa kuwa bado uko na mimi utakutana na maajabu mengi kunihusu." Catherine alimjibu Uriah ambaye alimtumbulia macho huku kagiza nako kakianza kuchukua nafasi yake.

"Hapo naanza kuamini kuwa wewe si mtu wa kawaida dada."

"Hapana ukisema hivyo utakuwa unakosea mdogo wangu, mimi ni wa kawaida sana ila huwa nabadilika kwa mtu anayekwenda kinyume nami."

"Hee kwa hiyo unaweza kunifanyia hata mimi?" Uriah alimuuliza.

"Ikiwa namsaka mpaka mume wangu Uriah unahisi nini kitatokea kwako iwapo utakwenda kinyume nami?" Catherine alimuuliza Uriah akinywa maji.

"Mhh sina jibu dada yangu wewe pambana na usukani tuwahi kufika." Uriah alimjibu akiegemea kiti bila shaka alitaka kulala kidogo.

Kwa mbali mataa yalianza kuonekana na hii ikawa ni ishara ya wao kuufikia mji wa Dosso, Uriah baada ya kuyaona yale mataa aliinama na kuanza kusali ikiwa ni kumshukuru Mungu kwa kuwasaidia kufika salama bila tatizo lolote tofauti na lile la awali alilokutana nalo Catherine.

"Nakuona mdogo wangu kumbe na wewe ni mtu wa ibada ee?" Catherine alimuuliza Uriah ambaye alikuwa bado anaendelea kusali hivyo hakuweza kumjibu chochote mpaka alipomaliza kusali ndipo alimgeukia Catherine na kumjibu.

"Dada Catherine, toka nilipovamiwa mwaka jana na Majambazi na kunusurika kifo kwa kuchomwa kile kisu cha tumbo huku vitu vyangu vyote vikiibwa niliamua kumkabidhi Mungu maisha yangu awe jibu la kila tatizo langu." Uriah alimjibu Catherine ambaye hakuamini kile alichokisikia maana Uriah wa awali anamfahamu vizuri sana lakini huyu wa sasa hakuwa akimjua vizuri.

" Kwanza nikupongeze kwa hilo mdogo wangu unajua wewe uliyekuwa miaka kadhaa si huyu wa sasa na ndiyo maana nikabaki nakushangaa tu." Catherine alimjibu akiiacha barabara kuu na kuingia inayoelekea ilipo Hotel ya HILLADIA ambayo kibao chake kiko pale barabarani.

" Mbona tunaacha barabara kuu?"

" Tunaingia Hotelini mdogo wangu." Catherine alimjibu.

" Usiingie tu kwenye Hotel ambayo huijui vizuri eti tu umekiona kibao chake kwanini tusiangalie Hotel za mbele?" Uriah alimuuliza Catherine ambaye alikuwa kaamua kuingia kwenye hiyo Hotel.

" Usiwe na wasiwasi Uriah uko na dada yako jasiri hivyo jiamini." Catherine alimjibu akiliingiza gari ndani ya HILLADIA HOTEL.

" Karibuni wageni wetu ndani ya Hotel ya nyota tano na inayopendwa na kila mgeni anayeingia nchini kwetu." Mlinzi wa Hotel hiyo aliwakaribisha wakina Catherine waliokuwa wakishuka garini.

" Asante kaka." Uriah alimjibu mlinzi huyo aliyeonekana mchangamfu sana kiasi cha kumfanya Catherine kutabasamu.

" Mimi nimefurahishwa na uchangamfu wako tu hata kama mtu alitaka kuahirisha kupata huduma zenu lazima abadili mtazamo wake tu, Hongera kwa hilo." Catherine alimpongeza mlinzi huyo.

"Asante dada kwa mara ya kwanza napokea pongezi kutoka kwa wateja wetu haki ya Mungu tena sijawahi kupokea hapo awali." Mlinzi huyo aliendelea kumvunja mbavu Catherine kwa lugha ya alama iliyoenda sambamba na mazungumzo yake.

"Basi mshukuru Mungu kwa hilo." Uriah alimwambia mlinzi huyo wakiachana naye na kuelekea uliko mlango wa kuingia ndani ya hoteli hiyo. Walimkuta mhudumu wa hoteli hiyo na kuhitaji huduma.

"Karibuni sana ndugu zangu kwa huduma." Mhudumu huyo aliwakaribisha.

"Tunashukuru dada tunahitaji vyumba ambavyo vimekaribiana au kama 'suit rooms' zipo itakuwa vizuri sana." Catherine alimjulisha mhudumu ambaye aliwaambia vyumba vya kila aina vinapatikana hotelini hapo.

"Basi tunahitaji hicho cha 'suit' dada yetu." Catherine alimjibu.

"Twendani nikawaoneshe kisha nanyi mtachagua cha kuwafaa." Aliwajibu kisha walielekea viliko vyumba hivyo. Walikagua vyumba vyumba vyote lakini Uriah alikipenda kile kilichokuwa na jina la 'WINNERS' kitu ambacho hata Catherine hakuwa na pingamizi lolote kwenye hilo hivyo waliingia humo huku Catherine akiomba kuletewa mashine ya malipo lakini alishangazwa na majibu ya mhudumu.

"Kila mlango una mashine yake ya malipo dada yangu."Alimjibu akimuonesha ilipo hiyo mashine ambayo sehemu ilipo huwezi kujua kama ni mashine ya malipo kwani imekaa kama kitasa hivi cha dharura upande kushoto wa mlango.

" Kweli teknolojia inakuwa aisee." Uriah hakusita kuyatoa ya moyoni wakati Catherine akifanya malipo.

"Karibuni sana kama kuna hitaji lolote simu yetu iko masaa ishirini na manne." Mhudumu aliwaambia hayo baada ya Catherine kukamilisha malipo.

"Asante dada tutafanya hivyo." Uriah alimjibu akiufungua mlango wa 'WINNERS'

"Hii kweli ni Hotel ya nyota Tano dada hebu cheki inavyovutia utafikiri tuko peponi?" Uriah alimwambia Catherine akivikagua vyumba ambavyo idadi yake ni viwili na sebule kubwa ikiwa na kila kitu kuanzia meza ya kujisomea, friji, na vikorombwezo kede kede ambavyo ni vutivu kwa mteja kiasi cha kumfanya mteja kutojutia fedha alizotoa.


UNAFIKIRI NI NINI KITATOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUPATE KUJUA KINACHOKWENDA KUTOKEA NDANI YA NIGER.


#SULTANUWEZO 

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post