MUUAJI MWENYE BARAKOA - 36
sultanuwezotz.blogspot.com
Walitazamana kwa muda kidogo kabla ya Catherine kuuendea mlango uliogongwa kujua ni nani aliyegonga na kwa sababu gani na ukizingatia ni usiku mkubwa.
"Dada subiri kwanza usifanye haraka unamjua ni nani anayegonga?" Uriah alimshika mkono kumzuia asiende kufungua mlango huo.
"Wacha niufungue tu mdogo wangu vyovyote itakavyokuwa."
"Okay basi acha mimi ndiyo niufungue na wewe chukua tahadhari nyuma yangu." Maneno ya Uriah yalimuingia Catherine ambaye aliifuata bastola yake kisha alirejea na kujificha upande wa pili wa mlango na kumpa ishara ya kuufungua na Uriah bila ajizi aliutekenya mlango ambao ulikubali na kufunguka.
" Aaah m...m...mko po...u...waaa?" Kwa sauti ya kilevi Juliette aliongea huku akitaka kuingia ndani.
"Unakwenda wapi wewe?" Uriah alimuuliza huku akimsukuma arudi nje.
"Ni...ni...nia...niacheeee!" Alimjibu akienda chini na kwa bahati mbaya alijipigiza sakafuni na kuanza kutokwa damu.
"Mungu wangu hii ni nini dada?" Uriah alimwambia Catherine akijaribu kumgeuza Juliette pale chini.
"Huu ni mchezo Uriah hebu subiri kwanza." Catherine alimwambia Uriah huku akimkagua Juliette aliyekuwa akitokwa na damu puani pamoja na kichwani.
"Mchezo kivipi dada?" Uriah aliuliza akipiga magoti pale chini.
"Hebu angalia hapa Uriah?" Catherine alimuonesha eneo la mgongoni ambalo lilikuwa likitoa damu kwa wingi.
"Kwa inavyoonesha kapigwa risasi huyu au?" Uriah alimuuliza akiliangalia lile donda lililokuwa likitoa damu.
"Hii siyo risasi bali ni kisu, kwa inavyoonekana kuna mtu alimchoma kisu."
"Kisu?"
"Mmh nimekumbuka Uriah inawezekana nilipopishana naye kule chooni akipepesuka alikuwa ameshapata shambulio." Catherine alivuta kumbukumbu ya tukio la muda mfupi uliopita akiwa anaingia chooni.
"Tunafanyaje sasa?" Uriah alimuuliza Catherine.
"Kuna nini hapo?" Kabla Catherine hajajibu swali la Uriah alitokea mhudumu wa Hotel ambaye hushughulikia usalama wa ndani na kuuliza baada ya kuuona mwili wa mfanyakazi mwenzake akiwa chini huku kazungukwa na wakina Catherine.
"Hatujui chochote kumhusu kagonga mlango wetu na tulipotoka alikuwa chini tayari tumejaribu kumkagua tumemkuta na majeraha ya kuchomwa kisu ubavuni na kichwani ni baada ya kujipigiza alipoanguka." Uriah alijaribu kumuelewesha yule mhudumu.
"Inawezekana vipi ilhali nimemkuta mikononi mwenu?" Yule mhudumu aliuliza akiiangalia simu yake.
"Kuwa muelewa basi, unataka kufanya nini kwenye simu?" Catherine aliinuka na kumkaba shingoni yule mhudumu ambaye inawezekana hakuwajua hawa viumbe.
"Unaogopa eee kwa sababu mnajua mlilomfanyia mwenzetu siyo?" Akiwa amejaa ukaidi aliendelea kumkera Catherine.
"Ningekuona wa maana kama ungefanya jitihada za kumfikisha Hospitali mgonjwa ambaye mpaka sasa hatujui kama yu hai au la lakini wewe unataka kutuvisha kesi isiyotuhusu na ninavyokuona unahusika kwenye hili mshenzi wewe." Catherine aliongea hayo na kisha kumsukumia nyuma na kwenda chini kisha alimfuata na kumkamata kichwa na kuanza kumgongesha chini mpaka pale alipojiridhisha kuwa kakata pumzi ya mwisho.
" Dada umeshaua hujui umeongeza tatizo juu yetu? " Uriah aliuliza akiangalia juu kuona kama kuna Kamera za Ulinzi.
"Nalijua hili mdogo wangu hebu kamata huko." Alimjibu akimtaka asaidie kumshika Juliette miguu wamuingize chumbani mwao na wakafanya hivyo kisha wakamchukua na yule mhudumu mwingine kisha wakarudisha mlango.
"Kuna jambo tunatakiwa kulifanya muda huu kabla ya jogoo la asubuhi kuwika." Catherine alimwambia Uriah huku akiiangalia bastola yake.
"Dada umeshaniingiza kwenye majanga mimi, sijawahi kuua mtu lakini sasa naiona jela kwa kesi ya mauaji..." Uriah hakutaka kusikiliza kilichosemwa na Catherine badala yake alijutia kilichotokea na kuanza kulia.
"Unaongea nini wewe? Hebu nisikilize kwanza, unaanza kuleta miuchuro yako hapa hujui huu ni mchezo na kama ni mchezo lazima ujue kuna mtu karibu yetu sasa wewe endelea kulialia hapa." Catherine aliongea huku akiwa anatembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine macho yakiwa kwenye ile miili miwili.
"Unafikiri tunaweza kunasuka hapa?" Aliuliza akiyafuta machozi yake.
"Iwezekane isiwekane lazima tutoke humu ndani tukiwa salama, hebu kusanya kila kilicho chetu tuondoke."
Catherine alimjibu.
Na Uriah pasipo kuongea chochote aliondoka na kuelekea chumbani kwake ambako hakuchukua muda alirudi akiwa na mkoba wake.
"Niko tayari dada."
"Utakuwa nyuma yangu na kwa yeyote tunayekutana usiongee chochote hiyo kazi nitaifanya mimi."
"Sawa." Walitoka na kuelekea kwenye mlango wa kutokea nje lakini wakiwa pale mlangoni mara kuna mtu alitokea nyuma yao.
"Vipi mbona na mabegi usiku huu?"
"Kuna dharura imejitokeza tunaomba ufungue mlango tafadhali." Catherine alimjibu akimtupia jicho Uriah.
"Dharura? Utaratibu wa Hotel yetu huwezi kuondoka mpaka tupokee taarifa ya kiusalama kutoka 'control room' hivyo mnatakiwa kutulia kwanza." Mzee huyu aliongea akiwaonesha sehemu ya kukaa.
"Tumekuelewa lakini mzee unaonaje tukielekea kiliko hicho chumba tukakague huko huko ili kuokoa muda maana tuna haraka sana."
"Hilo halina tatizo tunaweza kwenda lakini siyo wote mmoja atabaki hapa."
"Mdogo wangu nikukute." Catherine alimwambia Uriah na kuondoka na yule mzee, waliongozana mpaka kiliko kile chumba ambacho ni cha siri sana na moja ya kosa alilolifanya yule mzee ni kumuingiza mtu asiyemfahamu.
"Kijana wangu hebu pitia chumba cha 'WINNERS' tupate kujua usalama wake laki......" Kabla hajamalizia neno lake alisita baada ya kuona tukio ambalo hata yule kijana wa mle chumbani alipigwa butwaa.
"Haa huyu si Juliette a...." Hakumalizia neno lake alikutana na kisu cha tumbo kilichompeleka chini huku huyu kijana akiwa katoa macho haamini anachokiona.
"Mimi nililala dada yangu sikufanya chochote kile ndiyo naona muda huu."
"Kaa kimya wewe unaongea nini? Una kazi moja tu ya kuupigania uhai wako,Sawa?" Yule kijana wa 'control room' aliitikia kwa kichwa kuwa yuko tayari.
"Nahitaji hizo video zote kisha uchafu mwingine wote upige deki haraka kabla sijausambaratisha ubongo wako lakini akiwa anampa vitisho yule kijana huyu mzee akijitahidi kutaka kumkamata mguu Catherine.
" Kawasalimu kuzimu mwanaharamu wewe." Catherine alimwambia mzee wa watu akimshindilia risasi mbili za kichwa kwa kuitumia bastola yake ambayo ni ya kiwambo cha sauti.
"Na wewe fanya haraka kabla sijachafukwa zaidi." Alimgeukia yule kijana aliyekuwa akitetemeka.
"Hii hapa dada." Kijana huyu alimkabidhi ile flash yenye video zenye matukio yake.
"Kila kitu tayari?"
"Ndiyo."
"Futa hizo zote haraka."
Alimwambia azifute huku ile flash akiiweka vizuri kwenye mfuko wa jaketi lake.
Na baada ya kuhakikisha kila kitu kiko vizuri alimgeukia yule kijana.
"Kwa heri kijana wangu." Catherine alimuaga akimshindilia risasi ya kichwa kisha akatoka na kuondoka zake kuelekea aliko Uriah lakini hakuweza kumkuta pale.
"Huyu naye kaenda wapi tena?" Catherine alijiuliza akiitoa simu yake ili ampigie lakini alikutana na mdomo wa bunduki nyuma ya kisogo chake akajikuta anakuwa mpole kama kondoo.
"Utafuata maelezo yetu kuanzia sasa." Sauti hiyo iliongea kutoka nyuma yake, lakini Catherine hakuongea kitu alibaki kimya akitafakari nini cha kufanya.
"Geuka nyuma haraka na mikono yako ielekee juu." Amri ilitolewa na Catherine ikabidi aifuate.
"Mdogo wangu kuna nini?" Catherine alimuuliza Uriah baada ya kumuona akiwa nyuma ya mlinzi wa Hotel akishuhudia kinachoendelea.
"Nisamehe bure dada yangu nilikwambia toka mwanzo mimi kwa sasa nimemrudia Mola wangu hivyo siwezi kushiriki Ushetani wa aina yoyote ile na ukumbuke kuwa nilikufuata kwa ajili ya kukurudisha nyumbani kutokana na ulichofanyiwa na si kushirikiana kwenye oparesheni yako isiyo na kibali." Uriah alimpa majibu ambayo yalimfanya Catherine kuuma meno yake kwa hasira.
" Kwa hiyo umeniuza siyo?" Catherine alimuuliza akiwa kamtolea macho huku jasho lenye wingi wa hasira likimtoka.
" Sina jibu dada yangu ila kwa sasa acha haki ichukue mkondo wake na mimi nitakuwa shahidi mbele ya mahakama..." Uriah akiwa amejiachia kumjibu Catherine alishuhudia yule mlinzi akianguka mbele yake na alipojaribu kumuangalia Catherine usoni kutaka kujua nini kimetokea alijikuta akisalimiana na bastola ya Catherine ambayo huwa haimuachi salama adui yake.
" Huyu ndiyo dada yangu ninayemfahamu chezea wewe." Uriah aliongea akitetemeka huku akirudi nyuma kujaribu kutafuta upenyo.
"Unafikiri unaweza kuikwepa hii?"
"Naomba unisikilize dada yangu huyu mlinzi alinikuta hapa hivyo nikamhadaa kwa kumwambia kuwa uliniteka lakini uliniacha hapa na kwenda kutafuta ufunguo akaniambia nimuoneshe uliko tukiwa tunakutafuta ndipo tukakukuta hapa ambapo kikatokea kilichotokea na si kingine." Uriah alijitetea na muda huu akiwa kakabwa shingo na bastola ikiwa kwenye paji lake la uso.
" Umekosea sana mdogo wangu kucheza huu mchezo wako kwa mtu kama mimi, ulidhani mtafanikiwa eee na labda nikwambie kitu ambacho hukijui mdogo wangu toka uliposema kuwa umeokoka nilijiongeza nikajua wewe siyo mlokole kwa maana ya kusali nilijua wewe ni 'undercover' ambaye ulipewa jukumu la kunifuatilia kutoka Senegal kwa kigezo cha urafiki wetu wa zamani." Catherine alifunguka.
" Siyo kweli dada hiyo kazi mimi sijawahi kuifanya."Uriah alimbishia Catherine ambaye alikuwa akimvutia kwenye vyumba ambavyo walifikia.
" Uriah mimi huwa sibahatishi mambo yangu hebu ingia humo ndani tukaongee vizuri." Alimwambia akimsukumia ndani baada ya kuufungua mlango. Na baada ya kuingia ndani huku bastola ikiwa bado imemuelekea Uriah alitoa kitambulisho ambacho alikikuta kwenye suruali ya Juliette na kumkabidhi.
" Huyo ni nani? "
" Huyu ni...ni...ni Scolastica Naruto." Uriah alimjibu akikisoma kile kitambulisho.
"Alijitambulisha vipi kwetu?"
"Juliette."
"Hukujiuliza kwanini yule mhudumu wa Mapokezi humuoni?"
"Naomba msamaha dada yangu."
"Na huyo ni nani?" Catherine alimuuliza akimrushia kitambulisho kingine.
"Haaa umekitoa wapi kitambulisho changu Mwanaharamu wewe?" Uriah aliuliza baada ya kukutana na kitambulisho chake ambacho alikuwa nacho yeye lakini hakujua ni muda gani alikichukua bila hata kushtukia.
"Unauliza?"
"Hata ukiniua utakamatwa tu kabla ya jua la kesho kutoka."
"Uko sahihi mdogo wangu labda nikwambie kitu ambacho ulikuwa hukijui, vinasa sauti vyako, GPS pamoja na vifaa vingine vyote vya Kiusalama nilivibadili mfumo wake na kuvifanya vipeleke taarifa kwa watu wangu badala ya watu wako na kama huamini ikague simu yako ya kazi."
" Mshenzi mkubwa wewe na ulaaniwe mpaka siku ambayo utaingia kaburini."
"Kawasalimu rafiki zako waambie mimi ndiyo chuma kisichoguswa kwa namna yoyote ile Uriah lakini kingine ambacho nitaumia ni kukupoteza rafiki yangu ambaye uliniingiza mkenge kwa adui yangu ambaye hakujua niko wapi dakika za mwisho mpaka pale nilipokujuza naelekea wapi nyambaaaaaf...... " Alimmiminia risasi mbili za kichwani na kuchukua begi lake na kutoka nje ambako aliongoza mpaka kwenye gari lake.
" Madam unaelekea wapi?" Catherine badala ya kujibu aligeuka na kumuangalia mlinzi aliyemuuliza kisha akamrushia kitita cha hela.
" Kayaanze maisha yako mapya kuendelea kuwepo hapa wataanza na wewe."
"Sawa madam lakini unapoondoka hapa elekea kaskazini tofauti na hapo unaweza kukutana na vipingamizi barabarani." Mlinzi huyu ambaye alinunuliwa na Catherine mara tu baada ya kuingia ndani ya HILLADIA HOTEL kwa kumtumia Daktari wa NIGERFRIENDS HOSPITALI alitoa maelezo akiwa amekitolea macho kitita alichorushiwa na Catherine. Alitoka na kupotelea gizani na kuiacha Hotel iliyojaa harufu za damu ndani yake huku video za matukio yote zikiwa mikononi mwake.
UNAFIKIRI NI NINI KITATOKEA KATIKA KITIMUTIMU HIKI?
NI WEWE KUENDELEA KUWA KARIBU YANGU KWA KUWEKA BANDO LA KUTOSHA UPATE KUFAHAMU MENGI YATAKAYOENDELEA KWENYE HADITHI HII.
#SULTANUWEZO