MUUAJI MWENYE BARAKOA - 37
sultanuwezotz.blogspot.com
Pamoja na ugeni ndani ya mji Dosso lakini Catherine aliweza kuumudu usiku akiwa nyuma ya usukani taratibu huku macho yake yakicheza kulia na kushoto kwenye 'site mirror' kuona kama kuna mtu anacheza na njia zake na wakati huo huo alikuwa akiikagua baadhi ya mitaa iliyokuwa kulia kwake na kushoto, alifika kwenye mtaa mmoja uliokuwa umetulia sana kukiwa hakuna mpishano mkubwa wa vyombo vya moto na watu pia hii ikamfanya Catherine kuingia mtaa huu akiamini kuwa atakuwa salama na kama bahati vile macho yake yalikutana na bango kubwa lenye maandishi 'EGESHO LA MAGARI AINA ZOTE' ambalo lilimvuta na kuamua kuufuata mshale ulioelekeza eneo hilo liliko na alipofika alisimamisha gari na kushuka.
"Samahani kaka habari." Alimsalimu kijana mmoja aliyemkuta ameketi karibu na geti la kuingia kwenye EGESHO hilo.
"Bila samahani bidada nikusaidie nini?" Kijana huyo aliuliza kwa sauti ya kilevi.
"Wahusika wa hapa nawapata wapi?" Aliuliza baada ya kuliona geti hilo likiwa limefungwa kwa makufuli zaidi ya matatu.
"Unawataka wa nini weweee mbona unaingiza mbu kichwani kwangu?"
"Hapana siyo hivyo, wakati napita nimeona bango linaloonesha kuwa kuna huduma ya kuegesha magari lakini sioni dalili yoyote hapa zaidi ya makufuli."
"Ukiona hivyo ujue walisahau kung'oa hilo bango hivyo unaweza kuwasaidia." Kijana alimpa jibu ambalo lilimfanya Catherine abaini kuwa anaongea na mtu ambaye ni 'zero calculation' akaamua kuondoka na kuachana naye, aliingia kwenye gari akaligeuza na kurudi ambako alitokea kisha akasonga mbele.
" Watu wengine sijui wanakuaje saa sita hii jitu limekaa tu halijitambui au ndiyo kapiga pombe za ofa nini?" Catherine aliongea peke yake huku akiwa anaumaliza mtaa na kuibukia upande wa pili na kuikamata barabara ya vumbi ambayo sidhani alijua inaendelea wapi.
" Mmh mbona eneo hili lina miti iliyopandwa kiustadi hivi inaelekea wapi?" Alijiuliza akizidi kukanyaga mafuta lakini mazingira ya hili eneo yalimfanya aingiwe na wasiwasi kwani hakuweza kuona hata mbwa aliyekatisha mbele yake. Hili lilimfanya asimamishe gari pembeni ili afanye uchunguzi wake kwanza asije jiingiza mdomoni mwa mamba bure. Alishuka na kufunga mlango vizuri bastola mkononi na kuanza kutembea lengo lake likiwa kutafuta kibao kinachoonesha pale alipo ni wapi hilo alifanikiwa aliporudi nyuma kama hatua hamsini hivi aliweza kukiona alikisogelea na kukisoma 'KAMBI YA JESHI LA ULINZI NIGER' moyo ulimlipuka baada ya kuifikia nukta ya kibao hicho, hivyo hakutaka kupoteza muda alirudi nyuma na kuanza kukimbia kurudi liliko gari lake lakini hakufika mbali alisikia mlio wa bunduki ambao hakujua umetokea wapi akapunguza spidi kusikilizia kwanza ni upande gani huo akiiweka sawa bastola yake.
"Silaha chini na mikono yako juu." Ilisikika sauti nzito kutokea pembeni mwa barabara huku mwanga mkali ukiwa umemmulika Catherine usoni.
"Sijaeleweka au?" Mtu huyo aliuliza baada ya kuona Catherine hajatii amri yake.
"Nahitaji kukujua kwanza, wewe ni nani?" Catherine alimjibu mtu huyo ambaye alizidi kumchanganya kwa tochi yake kitu kilichomfanya ashuke chini kuweka silaha yake kisha alipiga magoti na kunyoosha mikono juu kuashiria amesalimu amri. Mtu huyo alimsogelea akiwa kammulika usoni kwa tochi yake na kisha aliichukua ile bastola.
"Ni nani huyo?" Aliuliza mtu mwingine ambaye alikuwa anakuja sehemu hiyo.
"Ni mrembo lakini sijui kafuata nini machinjioni?" Alimjibu mwenzake huku akimfunga pingu Catherine kwa nyuma.
"Ndiye yeye aliyepiga hiyo risasi?"
" Hapana ni mimi baada ya kuona analeta jeuri."
"Mrembo inakuaje uwe mbishi kwenye makazi ya watu?" Catherine hakujibu kitu zaidi ya kutulia kimya akipiga hesabu zake za kuwatoka watu hao ambao hakujua kama ni askari au la. Hawakujali walimchukua mpaka kambini kwao na kumuingiza kwenye moja ya chumba na kumfungia humo.
" Mfungue pingu bwana au umelewa?"
"Nilijisahau tu bosi." Aliufungua tena mlango na kumuita asogee mlangoni ili aweze kumtoa zile pingu.
Catherine alikuwa mpole utadhani siyo yule korofi, alisogea mpaka mlangoni akageuka kumruhusu aweze kuzifungua. Baada ya kuzifungua alimsukumia ndani kisha akaufunga mlango. Kwa Catherine huo ukawa ni mtihani mwingine ambao ulimuumiza kichwa. Ndani ya kile chumba ambacho hakikuwa na mwanga zaidi ya giza Catherine alijizungusha akijaribu kushika hapa na pale kuona kama anaweza kuchomoka lakini hakupata ufumbuzi ikabidi akae kwenye moja ya kona kuisubiri hatma yake iliyokuwa mikononi mwa watu hao ambao hakuwa na asilimia zote kama kweli ni askari.
***
Daktari Sylvester Kitesa alirudi jijini Mbeya bila hata kumtaarifu Mchungaji Rodney Hauser ambaye alimkwaza isipokuwa alimuaga Mchungaji Simon Mwaiduko ambaye alikuwa mwenyeji wao kwa kipindi chote hicho cha huduma wilayani Kyela. Na baada ya kufika mjini aliitisha kikao kumjadili Mchungaji Rodney Hauser ambaye mwanzo hakuweza kumjua vizuri kutokana na vile alivyomweleza japo utata ulikuja baada ya kukutana na vitu vya ajabu kutoka kwenye simu ya Mchungaji huyo pamoja na kwenye mifuko yake ya suruali, hapa ndipo palipozua tafurani na kupelekea kutoelewena baina yao.
"Ndugu zangu naomba niwashukuru kwa kufika kwenye kikao hiki cha dharura, pasipo kupoteza muda naomba mzee Ulio utuongoze kwa sara kisha tuanze." Daktari Sylvester Kitesa alifungua na kisha mzee Ulio alisimama kwa sara ambayo ilichukua takribani dakika nne kisha akarejesha kijiti kwa kiongozi wao Daktari Sylvester Kitesa ambaye aliingia moja kwa moja kwenye agenda iliyowakusanya ukumbini pale.
" Ndugu zanguni awali ya yote tunatakiwa kujipongeza kwa hatua ambayo tumeifikia hakika huyu Mungu ni wa ajabu sana. Nadhani mnakumbuka miaka kadhaa nyuma namna tulivyoianza huduma yetu ya hii ambayo tuliipa jina la 'JESUS OUR KING' tukiwa pale Ilomba kwenye Kanisa letu la MATURUBAI, mnakumbuka lakini?" Daktari Sylvester Kitesa aliwauliza kabla ya kuendelea.
" Tunawezaje kuisahau kumbukumbu hii isiyopotea karne na karne?" Alimjibu mzee mmoja aliyekuwa ameketi karibu yake huku wengine wakiitikia kwa vichwa.
" Nafurahi kusikia hivyo ndugu zangu basi ngoja niendelee, mnakumbuka tulivyolipambania Kanisa letu kiasi cha kupelekea ndoa zetu kupata misukosuko lakini hatukurudi nyuma mpaka wenyewe walituelewa kwa msaada wake Mwenyezi Mungu. Kitu kimoja nakumbuka niliwahi kuwaeleza ndugu zangu kuwa Kanisa letu limekuwa maarufu sana kiasi cha kufikia kufungua matawi katika kila mkoa hapa nyumbani Tanzania, Umaarufu ulivuka mipaka kabla hata ya vurugu za mitandao ya kijamii kuanza mpaka nchi za wenyewe hili lilianza kunipa hofu."
" Kiongozi, tuliwahi kukwaruzana baada ya kupata Wahisani kutoka nchi za Ulaya pale marehemu mzee Mahenje alipokataa kabisa kusikia hawa watu na akasisitiza kuwa kuwakubali ni kuukaribisha ukoloni ambao historia inasema watangulizi waliwahi kupitia kwenye madhehebu pia hivyo alitutaka tulitafakari hili lakini tulimuona Zipompapomba mpaka akaamua kuhama na kuelekea kwa wenzetu wasioyumbishwa kirahisi na upepo wa kiangazi nini kilitokea baada ya hapo?" Mzee mwingine alidakia na kuongea yake.
" Ulichokiongea mzee Yohana hujakosea uko sahihi sana tuliweka pamba masikioni kwenye hili na ndiyo sababu ya kuwaita hapa, mnajua nini ndugu zangu matokeo ya kuwakubali hao Wahisani ni kuingia mikononi mwa shetani." Daktari Sylvester Kitesa aliendelea.
"Kivipi baba Kiongozi?" Mmoja wa wazee wa baraza aliuliza.
"Kuna siku mtakuja kujua wazee wangu lakini kwa leo naomba kuwataarifu kuwa kwenye kikao kijacho cha kazi tutapitia maendeleo ya kila Kanisa hasa yale ya Magharibi." Daktari Sylvester Kitesa alihitimisha.
"Mbona anafichaficha kuna nini?" Mzee mmoja aliuliza wakati Daktari Sylvester Kitesa akitoka nje ya ukumbi.
"Yakiwashinda siku zote ndivyo walivyo wanaanza kutafuta sababu na ukiona hivi ujue kuna jambo, wacha tusubiri." Mwingine aliongeza wakati nao wakitoka nje. "Naomba Mchungaji ujiandae kwa safari ya kuelekea nchini Senegal kuna kazi nahitaji ukaifanye lakini usimwambie mtu yeyote hata huyo Mchungaji Rodney Hauser asijue hizi taarifa." Ulikuwa ni ujumbe wa Daktari Sylvester Kitesa kwa Mchungaji Simon Mwaiduko wa Kanisa la JESUS OUR KING Ipinda Kyela.
***
Mlango ulifunguliwa akaingia Askari mmoja akiwa pleti za chakula na kukiweka sakafuni kisha akamfuata Catherine ambaye alikuwa katulia konani amejikunyata.
"Mrembo mwenyeweee, unataka nitumie nguvu eee?" Askari huyu alimuuuliza akimshika kidevu.
"Unataka nini kutoka kwangu?" Catherine alimuuliza askari huyu akimtoa mkono wake.
"Ooooh kumbe mbabe siyo?" Askari huyu alionekana kukereka, aliinuka na kuanza kuvua mkanda wake.
"Mbona unavua mkanda unataka kufanya nini?" Catherine alimuuliza akiinuka.
"Utajua maana yake mrembo." Alimjibu.
"Kama wewe ni Kamanda kweli kwanini uanze kutafuta sapoti jiamini." Catherine alianza kumpandisha hasira.
"Unasemaje? Unafikiri mimi ni kiroba eee?"
"Umeongea wewe na si mimi." Catherine alimjibu akirudi nyuma, lakini alichelewa kwani yule Askari alishambetua mtama na kuanguka chini kama furushi. Akajaribu kuinuka lakini bahati haikuwa kwake kwani yule Askari alimfuata na kumtandika teke la tumbo lililomfanya Catherine kwenda chini mkono ukiwa tumboni.
"Vipi tunaweza kuendelea na mchezo? Unaonekana unauweza sana mkono twende kazi." Askari yule alizidi kumshindilia maneno ya kuchoma ambayo yalimfanya Catherine aume meno na kutamani kumrukia lakini maumivu ya tumbo yalimfanya awe mpole.
"Nakuona unavyotamani kupambana, hebu kula chakula kwanza kisha usiku nitakuja tena kukupa huduma ya kwanza utaifurahia mwenyewe 'I love you bebeeee...'" Aliongea akitoka nje na kumuacha Catherine akiugulia maumivu.
"Yaani ndiyo nakufa hivi hivi bila hata kufanikisha malengo yangu? Noooooo......" Alijikuta akipiga kelele ambazo ziliwafikia baadhi ya Askari waliokuwa Lindo na kuja kumchungulia.
"Sister mbona makelele kuna nini?" Mmoja alimuuliza akiwa mlangoni.
"Tu....tu....tu...tumbo ni...ni...nime....nimepigwa na mwen...mwenzenu." Alimjibu kwa shida.
"Dada yangu kitakacho kuua wewe ni jeuri yako kwanini usimwambie kilichokuleta kwenye hii kambi? Hata kama ni Gaidi wewe waeleze tu ama sivyo utakufa tu." Askari huyu aliyekuwa na silaha mkononi aliona amwambie ukweli na kuondoka zake. Maneno yale yalimuingia Catherine vizuri na hapo akajua kuwa asipochukua tahadhari anakwenda kufa.
Ilipofika usiku wa manane Catherine alianza kupiga kelele za kuomba msaada.
"Nakufa jamani naombeni msaada wenu tumbo languuuuu......"
"Dada hebu acha kutupigia makelele yako bwana mbona mgumu kuelewa?" Yule Askari wa mchana alirudi tena na kumuuliza.
"Makelele kivipi wakati tumbo linaniuma sana mpaka nashindwa kuvuta pumzi vizuri." Alimjibu.
"Unafikiri ukipiga hayo makelele utapata msaada? Kumbuka hapa ni kambini na wewe ni mhalifu uliyetaka kuvamia kambi yetu hivyo hakuna hata mmoja anayeweza kukuhurumia hivyo kuwa mpole."
"Basi nikuombe kitu kimoja kaka yangu."
"Kitu gani hicho?" Askari huyo aliuliza.
"Kwenye gari langu kuna taarifa zangu ambazo zitawafanya kujua kama mimi ni gaidi au mtu wa aina gani, hivyo nikuombe ukanichukulie tafadhali."
"Gari? Gari gani leo ni siku ya tatu toka liwe majivu."
"Majivu? Unataka kusema gari langu mmelichoma moto?" Catherine aliuliza.
"Unauliza majibu."
"What?" Catherine aliuliza akianguka chini.
JE, MWISHO WA CATHERINE UMEFIKA? NA MCHUNGAJI RODNEY YUKO WAPI?
SEHEMU IJAYO INAKUHUSU JIANDAE.
#SULTANUWEZO