MUUAJI MWENYE BARAKOA - 38
sultanuwezotz.blogspot.com
Alikuja kuzinduka amefungwa kamba mikono yake na kuning'inizwa katikati ya milingoti miwili ya chuma na chini yake kukiwa kumewekwa takataka zilizomwagiwa petroli zikisubiriwa kupigwa kiberiti. Askari waliokuwa wamepewa jukumu la kumuangamiza kwa moto mahali pale baada ya kuona amezinduka walisitisha zoezi lao na kisha kumtaarifu mkubwa wao juu ya kuzinduka kwake.
"Kwa hiyo kama amezinduka mimi nifanye nini?" Kiongozi wao alihoji baada ya kuuulizwa kwenye simu.
"Tulitaka kujua maana ulisema kuwa tumuue kabla hajazinduka na yeye kuzinduka kabla ya kuuawa."
"Kijana mbona ni king'ang'anizi kiasi hicho okay sasa mleteni anihudumie mchana wa leo wote kisha usiku asindikizwe ahera huko najua ulitaka kusikia hili juu ya mtoto mzuri si ndiyo." Alikata simu na kumuacha askari huyu kaitolea macho simu akidhani labda ni mtandao tu lakini haikuwa hivyo akairudisha simu mfukoni kisha akawapa ishara wenzake wamfungue.
" Mbona umenitolea mimacho yako hivyo au umenipenda nini?" Aliongea mmoja wa askari waliokuwa wakishusha kutoka pale chini, maneno yale yalimfikia askari kiongozi aliyepewa jukumu la kuhakikisha kuwa Catherine anafika kwa mkubwa wao hivyo alimsogelea na kumtandika teke la mgongo.
" Unaongeaje hivyo na chakula cha kiongozi wako, hujipendi siyo?" Alimuuliza akiwa kamkaba kwa buti.
"Nisamehe nilikuwa natania tu Afande haikuwa namaanisha." Alijitetea.
"Mshenzi mkubwa wewe haraka inuka mfungueni hayo makamba mikononi kisha mpelekeni akapate maji kabla ya kuonana na 'Big Boss' tumeelewana?"
"Nimekuelewa mkuu." Alijibu akiinuka na kuungana na wenzake waliokuwa wakimalizia kumfungua kamba Catherine.
"Najua nilikosea kukanyaga eneo hili lakini ndiyo niadhibiwe namna hii kweli? Na kwanini mlilichoma gari langu lililokuwa na nyaraka zote za utambulisho wangu?" Catherine alimuuliza huyu Askari aliyeonekana kuwa kiongozi.
"Unafikiri huo uongo wako ni nani atausadiki mrembo, kwa hiyo kusikia tu kuwa gari limechomwa moto umeona upite humo humo siyo? Huna jipya wewe jipange kumburudisha Boss wetu na kwa jinsi ulivyo mtamu itakuwa siku nzuri sana kwake na baada ya hapo utakwenda kutoa huduma kama hiyo Kuzimu, mpelekeni akaoge hawezi kwenda kwa Bosi na miharufu yake hiyo." Maneno ya Askari huyu yalimfanya Catherine amuangalie kwa muda kisha alitoa tabasamu akipitishwa karibu yake japo maana ya lile tabasamu hakuna aliyelijua.
" Unamchekea nani Malaya wewe? Hebu nenda huko."
" Kwani na wewe hautaki nikupe vitu adimu ninavyokwenda kumpa mkubwa wako?" Catherine aligeuka na kumuuliza.
"Umpe nani wewe?" Askari huyu alijibu huku akiwafuata nyuma.
"Naombeni dakika moja niongee naye kiongozi wenu." Catherine aliomba kuongea na huyu Askari na hawa askari hawakumzuia walimpa nafasi hiyo.
"Nisikilize wewe Askari mtanashati, acha kuvunga kwa kukuangalia tu naona umekufa juu yangu usiukoseshe raaaha ya ma...ma..penzi moyo wako." Catherine alimwambia akilishika tumbo lake.
"Nini tena?" Yule Askari alimfuata na kumuuliza.
"Tumbo limeanza kuniuma tena naombeni msaada wenu ndugu zangu." Catherine alimjibu na kuanza kulia.
"Mnashangaa nini hebu mshikeni huko akapatiwe tiba, na wewe Abdul kimbia kamwite Daktari Benadetha haraka." Alitoa amri hivyo ya kumkimbiza kupata tiba.
"Lakini hali yake pia si nzuri unaonaje angekwenda kuoga kwanza kabla ya yote?" Askari mwingine alitoa pendekezo lake ambalo halikupingwa na yeyote pale hivyo hatua ya kwanza walimpeleka kwenye mabafu ya kambi yaliyo upande wa Magharibi ya kambi na kumuingiza kwenye moja ya bafu na kisha kuurudisha mlango na muda huo huo Daktari Benadetha alifika.
"Daktari ingia kampe msaada wa usafi mtuhumiwa wetu kisha mfanyie vipimo analalamika tumbo." Alipewa na maagizo ambayo aliyaitikia kwa kichwa na kuingia mle bafuni ambamo alimkuta Catherine kafungulia maji na kuingia kuoga akiwa na nguo bila kuzivua, alimtazama kwa muda kisha aliifuata koki na kuyafunga maji.
" Vipi mbona umeikatisha starehe yangu, una wivu eee?" Catherine alimuuliza Daktari huyo ambaye alikuwa akikunja mikono ya koti lake tayari kwa kazi aliyoambiwa.
"Starehe gani ya kuoga na minguo hivyo hivyo?" Alimuuliza.
"Sikuweza kuvua kutokana na maumivu ya tumbo na mikono." Catherine alimjibu.
"Pole sana binti, sogea hapa basi nikupe msaada wa kukuvua."
"Itakuwa vizuri sana dada." Catherine alimsogelea Daktari na kumziba mdomo kisha akampa ishara ya kutulia.
"Ukienda tofauti na mimi nakunyonga humu humu sawa?" Alimwambia akiwa kamtolea macho kama vile anakufa muda si mrefu. Daktari hakuwa na jinsi zaidi ya kuitikia kwa kichwa.
"Unachotakiwa kufanya muda huu ni kunisikiliza mimi ni nini nakihitaji tofauti yake ni kifo ambacho utakuwa umekitaka mwenyewe mimi sina kawaida ya kumuua mwanamke mwenzangu ila akileta jeuri huwa sifanyi kosa kazi kwako." Alipomaliza kuongea hayo alimuachia mdomo wake na kumkandamiza ukutani ili asilete jeuri yoyote.
" Niko tayari kwa lolote utakalo tafadhali lakini usiniue."
"Utapiga kelele ya kuomba msaada kuashiria mimi nimezidiwa watataka kuingia wote na wewe utamchagua huyo kiongozi wenu na hii ni baada ya kufungua mlango. Okay?"
"Sawa nimekuelewa." Alimjibu.
"Nikihesabu mpaka tatu unaanza zoezi."
"Sawa."
Catherine alihesabu mpaka tatu yule Daktari akafanya kama alivyotaka na muda huo huo mlango uligongwa na Askari wote walikuja kutaka kujua kulikoni.
"Mgonjwa wenu hali ni tete hivyo nakuomba Afande tusaisiane ninyi wengine subirini kwanza." Daktari alitoa maelezo akiwa katoa kichwa tu huku ndani Catherine kamkamata mkono wake.
"Sawa." Askari huyo alijibu na kuingia mtegoni mzima mzima kabla hajakaa sawa Catherine alimkaribisha kwa kumsukumia ndani na kisha kuufunga mlango na yule Askari alipotaka kumpiga risasi alichelewa kwani alishainyakua ile bastola yake na kuwaweka chini ya ulinzi wote wawili na Daktari wake.
"Naitwa Catherine pia najulikana kwa kama mama Mchungaji huwa naichezesha msondo akili yangu nipendavyo ni muda wenu kulipia mliyoyafanya kwangu...." Catherine alitamba akimfuata yule Askari alikuwa kakodoa macho kama kafumaniwa vile.
"Tafadhali dada yangu usifanye hivyo mimi niko tayari kufanya ukitakacho."
"Vizuri sana toa simu yako mpigie huyo bosi wenu mpenda vizuri aje humu humu bafuni mwambie hali yangu ni mbaya hivyo aje mara moja." Yule Askari alitoa simu na kufanya kama alivyotaka Catherine na ndani ya dakika kadhaa yule mzee mwenye mwili uliokosa nyama kama mnywa gongo asiyezingatia ratiba ya chakula alikuwa mlangoni.
" Fungueni mlango."
Catherine alimpa ishara Daktari afungue huku bastola ikizunguka kama feni kuhakikisha hakuna janja janja.
"Kuliko......." Kabla hajamalizia kuongea Catherine alishaongea naye kwa kumtandika risasi kwenye mkono uliokamata silaha ambayo ilikwenda chini huku naye akipiga mayowe ya maumivu, Catherine aliinama kuikota kisha akainuka kwa tahadhari kubwa.
"Naomba mnisikilize ninyi Kenge, nilikuwa nawachora tu lakini hakuna hata mmoja wenu anayeweza kuucheza muziki wangu kama hamuamini jaribuni." Wakati Catherine akitamba mbele yao mkuu wa kambi ile alimpa ishara kijana wake amdake mguu Catherine ili akianguka tu chini wamvamie, lakini alichokutana nacho kilimfanya yule mzee na Daktari wake kuinua mikono juu kukubali yaishe kwani Catherine alimsambaratisha ubongo kisha aliwataka wafungue mlango kuongoza nje huku akimtaka mkuu wa kambi kuwaambia vijana wake warudi nyuma hatua mia tatu tofauti.
"Nimeeleweka wewe kizee?"
"Umeeleweka." Alimjibu.
"Haya haraka." Aliwaamrisha akiufungua mlango, lakini badala ya kufanya kama alivyoagizwa mkuu wa Kambi alichokiona chepesi ni kutimua mbio ambazo hazikumfikisha popote kwani alikutana na risasi ya paja huku Daktari akienda chini na kuanza kuwapigia kelele wale askari wengine kutofanya chochote na wakati huo Catherine alikuwa kamfikia yule mzee.
"Unafikiri mimi nikiamua jambo huwa linashindikana mzee? Haya waamuru vijana wako waweke silaha zao chini kabla sijafanya kitu kibaya hapa." Catherine alimwambia huyu mzee ambaye muda huu alikuwa akilia kama mtoto.
"Mwanaharamu mkubwa wewe unadhani utatoka salama kwenye hii kambi?" Alimjibu lakini muda huo alikuwa akiwapa ishara vijana wake waweke silaha chini lakini wakati silaha zikiwekwa chini na wale Askari kuna mwanga fulani ulimmulika Catherine usawa wa paji la uso na kumfanya kuhisi kitu hivyo kwa kasi ya ajabu iliyowashangaza wale Askari aliruka juu akiwa kajinyonga na kuanza kuachia risasi hovyo upande ulikotokea ule mwanga na dakika sifuri majibishano ya risasi kutoka juu yalianza huku hawa wengine waliinama kuokota za kwao lakini Catherine alikuwa mwepesi sana kwani aliweza kukimbia na kuruka fensi kwa nyuma na kuanza kukimbia. Ndani ya kambi filimbi na ving'ora vilipigwa kuashiria kuwa kambi imechafuka. Catherine akiwa anatimua mbio aliweza kusikia kelele za filimbi na ving'ora akajua mwisho wake umefika kwani alijua akikamatwa safari hii watamla nyama hivyo alijipa moyo na kuendelea na mbio zake mpaka alipovuka barabara na kwenda upande wa pili ambako kulikuwa na Hifadhi ya wanyama ya Dosso lakini hakujali hilo aliona ni bora akapambane na wanyama kuliko Askari waliovurugwa tena hawajui wanahusika na nini.
"Ooouugh...." Alipumua kwa nguvu baada ya kujificha kwenye kichaka katikati ya hifadhi.
"Atakuwa kaenda huku huyu twendeni." Aliwasikia wakiambiana karibu zaidi na alipojificha yeye.
"Mungu wangu nitapona kweli?" Catherine alijiuliza wakati akijaribu kutoka ndani ya lile chaka.
"Unaponaje mrembo kwenye hifadhi kama hii, naomba ujisalimishe wewe mwenyewe kabla sijapiga filimbi." Iliongea sauti kutoka nyuma yake, kumbe akiwa anatoka mle kichakani kuna Askari alijificha karibu baada ya kulishtukia lile chaka.
"Acha kujidanganya wewe huwezi kufanya lolote lile wewe tii amri yangu tu hapa." Aliendelea kumtisha lakini muda huo Catherine alikuwa anajiuliza amkabili vipi Askari huyu kwani akimpiga risasi itakuwa ndiyo kawaita askari wengine, alikuwa kwenye mtihani.
"Nimfanyaje huyu mtu?" Alijiuliza akiwa anainama kuiweka silaha chini kwa kasi alijigeuza na kummiminia risasi kama zote yule Askari na alipoona ya kwake imeishiwa risasi alikwenda kuichukua SMG ya yule Askari aliyekuwa maiti muda mrefu akaivaa na kuigeuzia mgongoni na kulikimbia eneo hilo. Risasi zile ziliwarudisha nyuma askari waliokuwa wamepita pale na kuanza kumsaka Catherine eneo lile.
"Ameua, ameua, ameua jamani tawanyikeni yuko eneo hili hili hajatoka lazima atiwe nguvuni." Kiongozi wao wa oparesheni alipiga kelele hizo baada ya kuuona mwili wa mwenzao ukiwa chini. Yeye alibaki pale ulipo mwili wa mwenzao.
"Mmh huyu mwanamke si mtu wa kawaida hata kidogo." Alijisemesha akiulaza vizuri pale chini. Alipoinua macho yake hakuamini macho yake baada ya kukutana na sura ya Catherine iliyotapakaa damu akiwa haongei chochote.
"Umejileta mwenyewe siyo ngoja nikuoneshe kazi mwanahizaya wewe." Yule Askari aliinuka kama Mbogo na kumfuata Catherine ambaye alisimama akiwa anamtazama tu akija mzima mzima.
"Lazima ufe we....." Kabla hajamalizia sentensi yake alikutana na risasi moja ya kifua iliyomtupa chini na Catherine alimfuata na kumkagua mifukoni ambamo alikutana na simu ndogo aina ya Galaxy aliiangalia kisha akaitupa pale pale akainuka na kutimua mbio mpaka barabarani ambako kama bahati vile alikutana na gari ndogo aina Toyota Stout akaipiga mkono ikasimama.
"Umepatwa na nini binti yangu?" Mzee aliyekuwa nyuma ya usukani alimuuliza Catherine aliposogea mlangoni.
"Unaelekea wapi babu?"
"Safari ya Niamey binti yangu."
"Naomba msaada wako na mimi naelekea huko huko." Kabla mzee wa watu hajajibu kama ni ndiyo au hapana Catherine alishaingia ndani na kuketi.
"Ondoa gari mzee ili eneo siyo salama hata kidogo." Catherine alimwambia baada ya kuona anamshangaa tu.
"Wewe ni Jangili siyo? Na unataka uniingize na mimi kwenye janga lako?" Mzee aliendelea kuwa kaidi.
"Unaondoa gari huondoi?" Alimuuliza akiwa kamnyooshea silaha yake, mzee kuonana vile akaanza kujichekesha mwenyewe.
"Hutaniwi binti yangu, huu ulikuwa ni utani tu mbona mambo kama hayo ni kawaida hata mimi kabla ya kuanza biashara ya ndizi nilianzia huko huko." Catherine alikuwa kamtolea macho tu akimuangalia anavyojieleza bila kuulizwa.
"Nani kakuuliza hayo ongeza mwendo mzee."
"Aaahh kuhusu hilo wala usijali wewe shusha hiyo bunduki uone spidi yangu lakini ikiwa imeelekezwa kwangu namna hiyo tunaweza kupata ajali babu yako nina mzio na vitu hivyo tafadhali shusha." Catherine alianza kucheka.
MAMBO YAMEPAMBA MOTO JE CATHERINE AMEOKOKA KWELI?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA TUPATE KUJUA.
#SULTANUWEZO