MUUAJI MWENYE BARAKOA - 39
sultanuwezotz.blogspot.com
Wakiwa wanaendelea na safari huku mzee wa watu akijitahidi kupiga gia kama alivyoamriwa na Catherine, kupitia kioo kinachoonesha mandhari ya nyuma cha upande wake analiona gari likija kasi, kwa namna linavyokuja na rangi yake ilivyo inampa mashaka Catherine na kuihisi hatari kichwani kwake, anamtazama dereva wake kwa muda kama vile kuna kitu anataka kumweleza lakini anatulia na kuvuta pumzi kwanza. Lakini lile tukio linaonwa na yule mzee ambaye anashindwa kujizuia na kuamua kumuuliza.
"Mwanangu mbona unaniangalia kwa jicho kali namna hiyo au hujapendezwa na mwendo wangu?"
"Siwezi kukulaumu mzee wangu inaonekana ndiyo mwisho wa spidi ya gari lako hivyo jitahidi tu." Catherine alimjibu huku bado akiendelea kulifuatilia lile gari ambalo lilianza kuwakaribia, hakuwa na njia nyingine zaidi ya kufanya maamuzi magumu ambayo hakujua kama itakuwa ni salama kwake au la lakini hakuwa na chaguo jingine.
" Mzee tukiifikia ile kona utapunguza mwendo kisha mimi nitaruka na wewe utaendelea na safari kama una huruma utanisubiri mbele."
"Kwanini ufanye hivyo binti?" Mzee alimuuliza.
"Wewe fanya kama nilivyokuambia mzee wangu, sawa?" Catherine alimjibu akiweka silaha sawa tayari kwa kuruka.
"Mhh kwa kuwa umeamua mwenyewe haina shida." Mzee alimjibu na baada ya kufika kwenye kona alipunguza mwendo na Catherine aliviringika kama gurudumu na kuishia porini huku yule mzee akiwa haamini anachokiona kwani alizoea kuona vitu kama vile kwenye filamu pamoja na kwenye maonesho ya Jeshi la nchi hiyo kama kuna maadhimisho fulani lakini kwa uraiani hakuwahi hata mara moja pamoja na umri wake alionao ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Catherine.
"Huyu siyo kiumbe wa kawaida hata kidogo, kapona huko alikofikia?" Mzee wa watu alibaki kujisemesha mwenyewe huku akiendelea kukanyaga mafuta. Lakini akiwa bado anamfikiria Catherine mara aliliona gari nyuma yake likija kwa kasi sana.
"Mhh kulikoni tena hawa wanyama?" Alijiuliza baada ya kuliona gari aina ya Tata ambalo analijua vizuri kuwa ni la jeshi.
Haikuchukua muda mrefu sana lilimpita na kwenda kusimama mbele kwa kuikatisha barabara akiwa haelewi kinachoendelea aliwashuhudia Askari waliokuwa ndani ya gari lile wakiruka na kulizunguka gari lake baada ya kusimama bunduki zikiwa zimemuelekea yeye.
"Mzee Mahmoud habari yako?" Kamanda wa kikosi kile alimsogelea na kumsabahi.
"Si nzuri Afande zitakuwaje nzuri wakati mmenizuia mbele huku mibunduki ikielekea kwangu kama vile mimi ni Jambazi." Alimjibu.
"Hatuna ubaya na wewe mzee Mahmoud lakini nitawaruhusu vijana wangu kulifanyia upekuzi gari lako na kama hatutakuta tunachokitafuta utaruhusiwa kuendelea na safari mzee wangu." Kamanda huyo aliyekuwa kachafuka mabega yake alimwambia mzee yule kilichokuwa kimewafanya wamzuie.
" Ina maana siaminiki kwa sasa Kamanda mpaka mnifanyie upekuzi na itakuwaje kwa muda mtakaokuwa mmenipotezea na mimi?"
" Mzee wangu unakuwa kama ni mgeni wa shughuli zetu wewe tulia tufanye yetu utaendelea na safari tu bila shaka yoyote ila wacha tufanye kilichotuleta huku."Alimjibu na kuwapa ishara vijana wake ya kuanza upekuzi.
" Kamanda wangu ninyi ndiyo wenye nchi wenyewe fanyeni tu kazi yenu bwana." Mzee yule aliona hakuna haja ya kubishana nao alifungua mlango na kushuka lakini wakati huo tayari maaskari walikuwa ndani ya gari nyuma wakipekuapekua.
"Unakwenda wapi mzee wangu isiwe ndiyo taratibu unataka kutukimbia?"
"Hivi na uzee wangu huu nitafika wapi si nitakufa kwa kuishiwa nguvu na hewa?"
"Kimuonekano mko hivyo lakini kwenye uhalisia mnatoka baruti ninyi...!" Yule Kamanda aliongea huku akicheka wakati huo akimuangalia mzee huyu anataka kufanya nini.
"Hakuna ukweli wowote kwenye hilo, halafu ni bora mngenishirikisha mnachokitafuta labda ningewasaidia lakini kwa upekuzi wa aina hiyo ndugu zangu tunatiana hasara hapa daa." Mzee Mahmoud aliongea kwa hasira kidogo baada ya kuona vifurushi vyake vingine vikiwa vimetupwatupwa chini tendo lile hata Kamanda wa kikosi hakulifurahia na hivyo aliwageukia vijana wake.
" Ndiyo mnafanya nini sasa? Kwani hamuwezi kuhamisha viroba humo humo kwenye gari mpaka mvitupe chini? Kuweni wastaarabu hata kidogo basi."
Alimgeukia mzee Mahmoud na kumuomba radhi kwa tendo lile lakini ikabidi amwambie kusudi lao lilikuwa ni lipi baada ya vijana wake kutoona chochote.
" Mzee wangu awali ya yote tusamehe kwa kila kitu kilichotokea kuanzia kukuchukulia muda wako, kusambaza hovyo mazao yako ni mambo ya kazi tu. Lakini kilichotufikisha huku ni binti mmoja hivi kavalia kadeti la kaki na kitisheti cheusi tunamsaka hujamuona ukiwa barabarani?"
" Unaona sasa Kamanda wangu, kama mngeniambia tangia awali msingenifanyia hata hivyo mlivyofanya huyo msichana mnayemsema si anaminywele mirefu hivi na michafu?"
" Yes, huyo huyo mzee wangu umemuona wapi?" Yule Kamanda alimuuliza kwa shauku kubwa sana mzee Mahmoud.
" Mhh mimi nilimpita kule juu kabisa unapoiacha tu hifadhi nilipomuona kwa alivyokuwa mchafu huku akikimbia kando ya barabara nilijua ni mwehu fulani hivi ila kilichonishtua ni ile silaha yake." Kamanda aliona kama mzee Mahmoud anamchelewesha kwa maelezo yake marefu akamuamuru dereva aligeuze gari lao haraka.
" Safari njema mzee wetu.. " Alimuaga akirukia kwenye gari huku wakimuacha mzee Mahmoud akilivuta turubai vizuri baada ya kufinyangwafinyangwa na wale Askari.
"Yuko hivi sijui nini ili iweje? (akiwa kabana pua) kwanza hamna adabu na pili ni nani asiyewajua Wakatili wakubwa ninyi?" Aliongea akiingia kwenye gari huku macho yakiwa kwenye pori kuona kama anaweza kumuona Catherine, aliamua kusitisha kuingia kwenye gari na kuvuka barabara ili kumtafuta binti huyo ambaye hamjui vizuri undani wake. Alizunguka kwa muda mrefu bila mafanikio akaamua kurejea kwenye gari lake ili aendelee na safari yake. Mzee Mahmoud alitokwa na jasho kwenye eneo la mwili wake baada ya kumkuta Catherine akiwa kakaa kwenye kiti akimsubiri yeye.
"Mzee wangu unashangaa nini sasa ingia uendeshe gari au nikusaidie mzee wangu?" Catherine alimuuliza akiwa anatabasamu.
"We binti naomba ushuke kwenye gari langu kabla sijakufanya kitu mbaya."
"Unanitisha mzee wangu? Na kama unataka nishuke ulifuata nini kule porini?"
"Ndivyo unavyojidanganya hivyo ee kule nilikuwa najisaidia na wala si kitu kingine."
"Mimi sishuki hata iweje na zaidi ninaweza kukuacha hapa hapa na funguo yako mkononi." Maneno ya Catherine yalimfanya mzee Mahmoud aanze kutafuta funguo mifukoni.
"Wewe endelea kuitafuta ukiipata utanifuata." Catherine alimwambia akihamia upande wa dereva na kumuonesha ufunguo.
"Weeeee subiri kwanza unataka kufanya nini?" Mzee Mahmoud aliuliza baada ya kuona Catherine akiwa na funguo yake huku akitaka kuliwasha.
"Unauliza au unajibu?" Alimuuliza mzee Mahmoud ambaye muda huo alikuwa akigombana na mlango ili apande.
"Utaumia bure mzee wangu panda taratibu." Catherine alimwambia mzee Mahmoud akimsaidia kuufungua.
"Ila wewe mtoto utanitoa roho yangu mimi ujue?" Mzee Mahmoud alimwambia Catherine akijitupa kwenye kiti cha abiria na kumuacha aendeshe.
"Vuta pumzi mzee safari ndiyo inaanza upya hivyo." Catherine alimjibu na kuondoa gari. Baada ya muda kidogo mzee Mahmoud alimgeukia Catherine aliyekuwa hana hata chembe ya wasiwasi nyuma ya usukani na kufungua kinywa chake.
"Samahani binti wewe ni nani na kwanini unatafutwa na kikosi maalum cha jeshi? Umewafanyia nini huko?"
"Mimi mwenyewe sielewi mzee wangu na kama ukitaka kunijua omba Mungu tufike salama tuendako kwa sasa naomba sana usiniulize maswali mengine niache niongee na gari lako." Catherine alimjibu akikaa sawa.
"Okay sawa lakini utaliweza?" Mzee Mahmoud alimtupia swali jingine akiukunjua uso wake.
"Mzee wangu nimeendesha magari mpaka yasiyo na breki sembuse hili jipya kabisa au unanionaje?" Catherine alimuuliza.
"Nakuona kama vile mtoto wa mboga saba aliyeamua kufanya maigizo katikati ya familia za kifukara."
"Macho yako yanakudanganya lakini kiuhalisia mimi wala siko hivyo mzee wangu. Kwanza nikuulize swali mzee wangu, wale maaskari uliwaambia nini mpaka wakaamua kurudi?"
"Nimewaambia kuwa nilikutana na wewe kule hifadhini ukikimbia kama kichaa sina ninachokijua zaidi hivyo wakaamua kuondoka haraka." Mzee Mahmoud alimjibu Catherine akiivua kofia yake ambayo alihisi kama vile inafanya asione mbele.
"Ila wewe ni kiboko aisee kwanini uliamua kudanganya?" Alimuuliza.
" Majibu unayo mwenyewe ni kwanini nimedanganya."
" Mhh haya mzee wangu wacha nikuoneshe umahiri wangu kwenye usukani wewe si ulikuwa unalitetea."
" Litashindwaje kukutii mwanamke mdogo lakini mpaka Jeshi linakuogopa."
"Tuache hizo stori mzee." Catherine aliona amkatishe mzee Mahmoud na kuendelea na usukani ambao ulionekana unataka nguvu kidogo kunyoosha na ndani ya masaa kadhaa walianza kuliona jiji la Niamey kwa kuanza kuona Maghorofa yaliyotokeza juu na urefu tofauti tofauti na kulifanya kupendeza kwa muonekano wake.
"Mzee wangu ile ndiyo Niamey?" Catherine aliona aulize.
"Kweli wewe ni dereva yaani mara hii tunakaribia kufika?" Mzee Mahmoud aliuliza akishtuka kwani alikuwa kalala.
"Unalalaje wakati umebebwa na mtu usiyemuamini wala humjui?"
"Nani huyo?"
"Si mimi hapa." Catherine alimjibu.
"Kitendo cha kukutoa mikononi mwa wale washenzi tayari nimekuamini na ndiyo maana hata wewe baada ya kuruka hukwenda mbali na baadaye ulirudi tena wakati ukijua kuwa wale Wanajeshi walinisimamisha." Mzee Mahmoud alimjibu akiivaa kofia yake.
"Ni kweli kabisa mzee wangu kwanza nikushukuru sana kwa msaada wako na bila wewe muda huu ningekuwa nateseka kwa baridi mle msituni,hivyo Nakushukuru sana mzee wangu."
" Kwa hilo usijali unajua nini binti?"
" Sijui."
"Okay, pale uliporuka kwenye gari nilipatwa na hofu sana juu ya usalama wako na pale kuna sauti ilinijia na kuniambia kuwa msaidie huyo msichana na ndiyo maana nikafanya nilichofanya." Mzee Mahmoud alimwambia Catherine aliyekuwa akipunguza mwendo kusubiri maelekezo.
" Nashukuru sana mzee wangu, sijui naendelea wapi?" Catherine alimuuliza.
" Hapo mbele simama ili huku mbele niendeshe mwenyewe maana natakiwa kuingia sokoni kutua huu mzigo." Catherine hakujibu chochote zaidi ya kulipeleka gari pembeni na kulisimamisha. Kisha wakabadilishana viti na safari ikaendelea lakini wakati huo huo Catherine alivuta egemeo la kiti na kuipachika bunduki yake.
" Umefanya la maana sana ungepelekea watu kupigwa na taharuki."
"Ila kilichobaki ni huu muonekano tu." Catherine alimjibu akijitazama kwenye kioo cha juu mbele ya gari.
"Kuna sehemu nakwenda kukuacha nitakupitia baada ya kushusha mzigo."
"Sehemu gani hiyo?"
CATHERINE ALIMUULIZA MZEE MAHMOUD AMBAYE ALIKUWA AKIIKATA MITAA.
JE CATHERINE YUKO SALAMA? TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA
#SULTANUWEZO