MUUAJI MWENYE BARAKOA - 56 (Mtunzi: Sultan Uwezo)

 


MUUAJI MWENYE BARAKOA - 56 (Final)

sultanuwezotz.blogspot.com 


Walipofika kwenye mkokoteni walishangaa kukutana na sura za wakina mzee Malick Bolenge pamoja na Mchungaji Rodney Hauser wakiwa wametapakaa damu miili yao yote. Awadh alipanda kwenye mkokoteni kuwaangalia huku Frank na Tamia wakiwa wanamfuatilia.

"Mungu mkubwa nilijua wamekufa kumbe bado wanapumua." Aliongea Tamia baada ya kumsikia Mchungaji Rodney akipiga chafya na hii ni baada ya Awadh kumuwekea dawa fulani hivi puani. Catherine kusikia hivyo alikuja mbio kuhakikisha kama ni kweli kwa alichokisikia.

" Wazima?" Catherine aliuliza.

" Kumbe bado unampenda huyu mpuuzi?" Mzee Nyeye alimuuliza Catherine akimfuata nyuma.

"Kwanini unasema hivyo?" Catherine alimuuliza akiukaribia mkokoteni.

"Kwanini uliduwaa baada ya kuiona miili yao kwenye gari hili la ng'ombe?" Mzee Nyeye alimtwanga swali jingine.

Alimpotezea mzee Nyeye baada ya kufika kwenye mkokoteni alipanda na kuanza kuwakagua mapigo ya moyo ili kuthibitisha alichokisikia japo alimkuta Mchungaji Rodney akiwa macho kwake yeye alihisi ni mfu aliyetoa macho kama paka.

"Madam ni wazima ila wanahitaji muda tu." Awadh alimwambia.

"Kazi mnayoifanya mmeidandia kwa mbele sisi ndiyo tuliianza na siyo kwamba hatukujua tulichokifanya la hasha tulijua. Baada ya kuwakuta wakiwa mbio tukajua kuna jambo hivyo moja kwa moja tukaona tufanye jambo ndipo binti yangu alipowarushia sindano za sumu ambazo ziliwapata shingoni na kuishiwa nguvu.." Mzee Nyeye alieleza.

" Na vipi kuhusu hizi damu?" Frank aliuliza akiwa kamtolea macho Tamia.

" Hizo siyo damu kijana hiyo ni dawa ambayo usipokuwa makini unaweza kudhani ni damu na hiyo huwa tunaitumia kumchanganya adui aliyezima akizinduka na kujikuta ana damu mwilini lazima awe mpole, na hiki ndicho kilichotokea kwao." Majibu ya mzee Nyeye yalimvunja mbavu Catherine ambaye mpaka muda huo alikuwa mpole sana akidhani wamekufa.

" Ila umeniweza mzee, kiukweli niliishiwa nguvu sana yaani wafe kabla ya mimi kuwashikisha adabu weee." Catherine aliongea akicheka.

" Nilijua, na ndiyo maana nilikuwa nacheka tu. Maana sura ambayo niliiona kwako sijawahi kuiona toka nikutane na wewe siku ya kwanza." Mzee Nyeye alimjibu.

" Nasikia kiu jamani." Mzee Malick aliongea kwa taabu sana. Lakini Catherine alikataa kumpa maji badala yake walipelekwa mpaka kwenye yale maghala ambayo kwa muda waliyafanya kama makazi yao. Kisha waliwachukua na kuwaingiza kwenye gari. 

"Ndugu zangu hawa watu sihitaji kuwaua huku ugenini nataka kuwafanyia kitu ambacho hawataamini, hivyo mzee wangu na mdogo wangu Tamia Mungu aendelee kuwapa moyo huo huo na kwa wengine mwisho kabisa mkamwambie Maria kuwa ninampenda sana nitarudi tena Niger kwa ajili yake." Catherine aliongea maneno haya ambayo yalionekana kuwa machungu kwani machozi yalikuwa yanamtoka kama maji bila shaka ni kwa sababu alikuwa anakwenda kuachana na timu yake mpya aliyokutana nayo ugenini. 

" Sina la kusema mwanangu lakini niseme tu kwamba tutakukumbuka sana maana ndani ya muda mfupi tumeishi kama familia, nakuombea huko uendako ufike salama na pia usitusahau ndugu zako." Mzee Nyeye aliongea akimpa mkono Catherine. 

"Tamia mbona uko mbali?" Catherine alimuuliza. 

Lakini Tamia hakujibu chochote badala yake alijifunika kitenge usoni na kuanza kulia, hakika ilikuwa ni huzuni sana kwao kuachana walitamani waendelee kuishi pamoja. 

"Madam wanaweza kuja na kutukuta hapa si unaona kuna magari yao hapa?" Awadh alimwambia Catherine baada ya kuona kuagana hakuishi akaamua kukatisha wakati huo yeye alikuwa ameshapanda gari. 

"Frank tutawasiliana najua mwisho wa hii oparesheni ni mwanzo mpya wa sisi kufanya kazi pamoja." Catherine alimuaga Frank ambaye alikuwa msaada sana mkubwa sana kwenye shughuli yake. 

"Usijali dada Catherine muda wote na wakati wowote utakaonihitaji nipo." Frank alimjibu akimpa mkono. 

"Kaka Awadh ukifika tuwasiliane si unaikumbuka issue yetu haijakamilika?" Alimgeukia Awadh. 

"Naikumbuka vizuri sana hivyo tuombeane uzima tufike salama." 

"Nilitaka kusahau binti yangu kuna hii dawa mtawapaka hawa baada ya masaa sita ili kuondoa hayo madawa ya damu." Mzee Nyeye alimfuata Catherine dirishani na kumkabidhi kichupa chekundu

chenye dawa ambacho alikipokea na kumshukuru. Baada ya hapo Awadh aliwasha gari kuianza safari ya kuelekea nchini Senegal.


***


Ndani ya Ukumbi wa mikutano wa Kanisa la 'Jesus Our King'nchini Senegal kulikuwa na kikao cha moto sana kujadili mambo mbalimbali ya namna ya kulistawisha Kanisa lao ambalo limepata mtikisiko kidogo kutokana na Mauaji ambayo yalitokea huku chanzo kikielezwa kuwa ni Mchungaji Rodney Hauser ambaye mwanzo aliaminika na kila muumini lakini kadri siku zilivyokuwa zinasonga mbele kila mtu alimchukia sana Mchungaji Rodney. Ukumbi ulikuwa kimya kabisa kumsikiliza Mkuu wa Kanisa hilo lenye makao makuu yake nchini Tanzania katika mkoa wa Mbeya. Nadhani utashangaa ni kwanini hili Kanisa lianzie mkoani Mbeya? Kitakwimu huu ndiyo mkoa unaoongoza kwa kuwa na makanisa mengi nchini Tanzania hivyo hata hili lilianzia hapo. Na leo hii mkuu wa Kanisa hili Daktari Sylvester Kitesa alikuwa ndani ya mji wa Dakar sehemu lilipo kanisa hili akiongoza kikao hiki muhimu.

"Kama nilivyowaambia hapo awali Mchungaji Rodney Hauser ameondolewa rasmi kuwa Mchungaji wa Kanisa letu kutokana na mabalaa aliyotuletea nadhani hakuna asiyejua hili. Kwa upande wangu nilikuwa siamini hizi tetesi kumhusu mpaka pale niliposhuhudia mwenyewe kwa macho yangu tulipokuwa Kyela alipata tatizo ambalo lilipelekea kupoteza fahamu na hapo ndipo nilikutana na maajabu ya dunia kwa Mtumishi wa Mungu ambayo siwezi kuyaweka wazi lakini naomba mfahamu tu kuwa vilikuwa vitu ambavyo ni chukizo machoni pa bwana na pale alipobaini nimejua alitoroka nchini na mpaka sasa hatujui yuko wapi na hata Mchungaji Simon Mwaiduko analijua hili." Alimtaja Mchungaji Simon Mwaiduko ambaye alisimama na kuunga mkono yale yaliyosemwa na mkuu wake.

" Hivyo niwaombe ndugu zangu tuzike yale yote yaliyotokea huko nyuma najua inauma sana lakini bado hatuwezi kuwafufua wapendwa wetu na badala yake tumkabidhi Mwenyezi Mungu afanye maamuzi na sisi tubaki kuifanya kazi yake aliyotuagiza tu, mzee Isaya Daniel na kijana wangu Otago Mathew nayajua machungu yenu na mbaya zaidi nimepata taarifa kuwa mke wake ambaye ilisemekana kuwa alitekwa na kuuawa haikuwa kweli kwani alikwenda nchini Nigeria huko alimteka binti yetu Jennifer na hili linajidhihirisha kabisa ni namna gani familia hii ilivyokuwa ya Kishetani." Alipoingiza hili swala alikuwa kama ameuwasha moto kwani mikono ilikuwa juu kutaka nafasi ya kuongea chochote.

" Ndiyo Dkt Brown." Alimhurusu mzee Brown ambaye ni kiongozi wa Kanisa hilo kwa Senegal.

" Nashukuru kwa nafasi hii mkuu wangu, naomba nichangie katika hili, yule mama kufanya tukio lake la utekaji wa mtoto yule ilikuwa ni hasira tu kwani kwa maelezo ya mume wake na marehemu mama Jennifer bwana mdogo Otago alisema kuwa mtoto yule ni wa Mchungaji Rodney Hauser na hilo alilifahamu miezi kadhaa nyuma kabla ya umauti kumkuta. Na kwa inavyoonekana mhusika wa mauaji yale alikuwa ni Mchungaji mwenyewe katika kupoteza ushahidi."

" Otago Mathew hebu tuthibitishie hili." Daktari Sylvester Kitesa alimuinua mhusika.

"Mkuu wangu yuko sahihi kabisa na mbaya zaidi aliwahi kunitishia kuwa iwapo nitaongea kokote atanipeleka alikowapeleka wengine ambao walijidai ni mabingwa wa kufuatilia nyendo zake hivyo sikuwa na jinsi zaidi ya kukaa kimya..." Alishindwa kuendelea alikaa chini na kuanza kulia.

" Ndugu zanguni mnaona jinsi mambo haya yanavyochoma mioyo yetu? Na haya ndiyo yalinifanya nimtume kijana wangu kuja kufanya uchunguzi na mwisho nikaona nije kutafuta suluhu ambalo limeshapatikana na sidhani kama litajirudia tena. Mchungaji Simon Mwaiduko hebu sogea hapa mbele." Mchungaji Simon alisogea mbele kisha Daktari Sylvester akaendelea.

" Ndugu zangu huyu kwa sasa ndiye atakuwa Mchungaji wa Kanisa letu akiwa chini ya kiongozi wake Daktari Brown Lutasya naombeni mumpe ushirikiano wa kila aina na pale ambapo atakuwa anakwenda kinyume msisite kumuweka chini na kumkanya." Daktari Sylvester Kitesa alimalizia. Lakini wakiwa wanamalizia malizia kikao chao aliingia mtu ambaye hawakuwahi kumuona.

" Habarini wakuu wangu." Aliwasalimia.

" Unasemaje kijana? Halafu umepitaje mlangoni bila idhini yetu." Daktari Brown Lutasya alimuuliza kijana huyo aliyekuwa na bastola mkononi.

"Nimeingia mwenyewe na sijaja hapa kuomba msaada au kuwafanyia kibaya zaidi ya kuwaeleza kuwa kuna mtu msiyemtarajia anahitaji kuwaona."

"Kutuona sisi? Katokea wapi?" Daktari Sylvester Kitesa naye aliongeza swali baada ya kuona kijana huyo akiongea kwa kujiamini zaidi.

"Hiyo siyo kazi yangu mtamuuliza mwenyewe." Aliwajibu.

"Basi mwambie aingie." Daktari Brown alimruhusu. Aliingia mtu akiwa ameuficha mwili wake kwa mavazi maalum ambayo yaliacha macho tu. Kila mtu mle ndani alisimama kwa hofu kwani wengi wao walihisi ni magaidi wamelivamia kanisa lao. Wakiwa kwenye mshangao huo mtu huyo alilitoa lile vazi na kubakia na suruali yake jinsi, fulana nyeusi na chini alivalia safari buti la kike.

"Mama Mchungaji?" Daktari Brown alimuuliza kwa mshangao.

"Wala hujakosea mzee wangu mimi ndiye mwenyewe mama Mchungaji ambaye kwa sasa siyo mama Mchungaji niite tu Catherine niko hapa mbele yenu kuomba radhi pamoja na kukiri mbele za Mwenyezi Mungu kwa mengi niliyoyafanya ambayo ni kinyume na utaratibu. Baba Askofu Daktari Brown na wengine wote mlio humu ndani mimi ndiye niliyefanya matukio yote yaliyotokea miaka ya hapa karibuni, mimi ndiye muuaji ambaye sikutaka kuionesha sura yangu hadharani nilifanya haya kwa wale wote ambao walikuwa wakizuia jitihada zangu za kuwakamata na kuwaadhibu wale wote ambao walihusika kwenye Mauaji ya mama mzazi na wenzake waliokuwa wakitumiwa kama njia ya kuwavuta waumini kwa miujiza feki na baada ya kufanikisha hilo waliwaua na wahusika hao walikuwa ni Mchungaji Rodney Hauser na mzee Lusoka pamoja na wenzao hivyo Mauaji yote niliyefanya kwa wale ambao walinibaini mapema. Na ninavyoongea hivi hapo nje nimewaleta Mchungaji Rodney pamoja na mtu ambaye alimpeleka kwa wataalam mbalimbali wa kumng'arisha nyota yake wakati akijua ni kinyume na utume hivyo niko mbele yenu kutubu kwa nililolifanya najua nimekosea kwa njia niliyoitumia kuwakamata watu hawa lakini roho yangu imepata faraja." Wakati akiongea hayo Awadh alitoka nje na kuwaketa Mchungaji Rodney Hauser pamoja na mzee Malick na kuwapigisha magoti madhabahuni.

" Najua mkono wa sheria uko njiani kunikamata kwa niliyoyafanya na mimi siko tayari kwa hili ila wakifika waambieni kuwa chanzo cha haya yote ni hawa wawili hasa hasa huyu Mchungaji." Baada ya kuongea hayo aliwamiminia risasi za miguu wote wawili na kupelekea wale wote waliokuwa mle ndani kila mtu kutafuta ficho lake na wakati huo Awadh alitoka mbio baada ya kusikia ving'ora vya magari ya Polisi, Catherine hakuondoka pale alipokuwa kasimama badala yake alijichapa risasi ya kidevu ambayo ilimfumua sehemu ya chini ya mdomo ambayo ilipenya mpaka kwenye fuvu la kichwa na kudondoka chini. Polisi walipofika pale walikutana na pilika pilika za kujaribu kumnusuru Catherine pamoja na kuwafanyia huduma ya kwanza wakina Malick na Mchungaji Rodney Hauser. Polisi walisimuliwa kila kitu kilichotokea na kufanywa na Catherine kitu kilichowafanya wawachukue wakina Malick na pia kuubeba mwili wa Catherine ambaye alishakuwa marehemu. Waliwashukuru viongozi wa Kanisa hilo kwa ushirikiano wao katika tukio hilo na waliahidi kumtafuta Awadh na Washirika wao kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazowakabili kisha waliondoka na kuwaacha kujadili lililotokea.

Baada ya uchunguzi wa kina kufanywa na Jeshi la Polisi waliwakuta na makosa ambayo yalipelekea kifungo cha maisha kwa Mchungaji Rodney Hauser na kwa kuwa hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja ambao ulimfanya atiwe hatiani lakini pia sheria haikumuacha salama mzee Malick kwani alihukumiwa kifungo cha miaka kumi na sita jela. Na Kanisa la Jesus Our King lilifungwa kwa muda kupisha uchunguzi wa kufuatilia uhalali wake, kwani serikali ya Senegal ililihusisha na biashara za dawa za kulevya.


            *MWISHO*


FUNZO: Kwenye maisha yetu ya kila siku tuepuke kujichukulia sheria mikononi hata kama una vielelezo vyote vinavyokulinda lakini kila kitu kinafanywa kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Taifa husika. 

Catherine alikuwa sahihi kumtafuta muuaji wa mama yake lakini kujichukulia sheria mkononi lilikuwa ni kosa kubwa sana kwake, kwani mwenye mamlaka ya kutoa hukumu ni Mungu pekee na kwa upande wa serikali ni Mamlaka husika za kisheria. Maamuzi yake yalipelekea vifo vya watu wengi ambao wengine hawakuwa na makosa yoyote bali ni mihemko yake iliyosababishwa na hasira ambazo alishindwa kuzithibiti. 


NIWATAKIE  MAJUKUMU MEMA KWA MWAKA HUU MPYA WA 2021 lakini siwezi kuwaacha hivi WAPENDWA WANGU NITAWACHA NA UJUMBE WA MANENO KUTOKA KWENYE MAANDIKO MATAKATIFU ( zaburi 23:1-4),(zaburi 121:1-2),(zaburi 27:1-2), (efe 3:2) na (Amu 6:12)



#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post