NITAKUUA MWENYEWE - 37 (Mtunzi:Sultan Uwezo)



NITAKUUA MWENYEWE - 37

sultanuwezotz.blogspot.com 


Waliondoka mpaka kwenye helicopter yao kule porini na kujaa ndani ambako walimkuta Robinson akiwa kajikunja kwenye kona akiwa katoa macho baada ya kuwaona Santana na timu yake akajua mwisho wake umefika.

"Niko chini ya miguu yenu naombeni msiniue badala yake nirudisheni nyumbani au nipeni kazi yoyote ya kufanya maana wazazi wangu wananitegemea mimi hawana mtoto mwingine." Alianza kujitetea Robinson.

"Robinson, Robinson mbona unalialia hivyo kwani ni nani aliyekwambia tuna mpango wa kukuua?" Santana aliamua kumuweka sawa Robinson.

"Nimeamua kuwa nanyi na si kwingine."

"Hebu mfungueni hizo ringi." Santana aliamuru.

"Mpatieni chakula huyu najua atakuwa na njaa sana kijana wetu." Mzee Bruno Gautier aliagiza.

Aliletewa chakula pale ambacho kilikuwa ni mkate wa viazi mbatata ambao aliushambulia pamoja na juisi ya karoti. Na kwa ulaji ule walijua moja kwa moja alikuwa katingwa na njaa.

" Endelea kula tu Robinson chakula bado kipo cha kutosha na ukishiba tuna mvinyo wa kutosha."

Santana aliendelea kumsogeza karibu Robinson aliyeonekana kumuogopa yeye zaidi.

"Asanteni nimetosheka." Alishukuru Robinson.

Baada ya hapo ndipo alipomwita chumba maalum ambacho hicho mara nyingi hukitumia yeye tu Santana ndani ya ndege hiyo. Huku akimuagiza rubani kuzungusha panga za helicopter hiyo kuelekea Belem tayari kuangalia wanamuokoaje mke wa mzee Bruno ndani ya Rio Branco.

"Ni wakati wako sasa kunieleza chochote kinachokuhusu Robinson." Santana alimueleza Robinson.

"Mkuu mimi kama ninavyojulikana kwa jina la Robinson Kaaya ni mtoto wa pekee kwa wanandoa Mr&Mrs Kaaya. Wazazi wangu ni wakulima wadogo wa zao la tumbaku ambalo mpaka sasa ni kitendawili kutokana na mfumo wake wa uzalishaji nakichukia sana kilimo cha zao hilo la Tumbaku na ndiyo maana nilishawishiwa na Jackline kuja huku kumsaidia mambo yake lakini nilivyotulia nikajikuta natamani kuzifikia ndoto zangu za muda mrefu za kuwa na maisha mazuri na yenye furaha hivyo tu mkuu."

"Vizuri Robinson kumbe wewe ni kijana muelewa sana ee na ndiyo maana nikaona nikuajiri kusimamia kampuni yangu ya usambazaji wa vifaa vya michezo barani Afrika na makao makuu yakiwa hapa hapa Brazil hivyo jukumu lako ni kuhakikisha kuwa unafungua matawi ndani ya nchi za Tanzania, Afrika ya kusini, Misri, Kenya, Rwanda, na Zimbabwe."

"Kweli mkuu?"

"Kama ulivyosikia Robinson ndivyo ilivyo ila tu yote haya yatafanyika mara baada ya kuwatia nguvuni wale Mbwa Koko wasio na makazi na hilo si la leo wala kesho utalifanya kwa wakati wako mwenyewe."

"Niamini mkuu, katika hili wewe mwenyewe utajionea mbona kwangu wale nitawaminya kwa kutumia kwapa langu tu."

Robinson kwa namna ambavyo alitoa majibu ilipelekea Santana kusimama na kumfuata alipokuwa kakaa na kumkumbatia.

"Nimekukubali Robinson kwa namna ambavyo umejieleza nina uhakika tunakwenda kushinda hii vita."

"Kweli mkuu?"

"Niamini Robinson katika hili mimi ni mgumu sana kumuamini mtu lakini kwako naiona imani kubwa sana kikubwa usiniangushe kijana."

"Kijana wangu tumefika tayari maliza haraka mahojiano yako."

Mzee Bruno Gautier alimkumbusha Santana baada ya kuingilia maongezi yao.

"Okay mzee hata hivyo tumekamilisha tayari tunaweza kushuka." Alijibu Santana.

Wakiwa wanatelemka kutoka kwenye helicopter wakiwa ndani ya kambi ya Santana mzee Bruno Gautier alimuuliza inakuwaje juu ya suala la mke wake.

"Inakuwaje Santana kwenye suala la mke wangu ni masaa takribani mawili sasa na sijui ana hali gani?"

"Mzee punguza wenge yatakwisha tu hayo na muda si mrefu tutamrejesha akiwa salama."

"Tutafanyaje hapo?"

"Si walisema wanamhitaji Robinson?"

"Ndiyo ni moja ya mahitaji yao."

"Kinachotakiwa kufanyika hapo ni wewe mzee Bruno kuwapigia simu na kisha kuwauliza tunakutana nao sehemu gani kwani mtu wao tunaye mikononi mwetu."

"Hiyo itakuwa imekaa vyema Santana hebu ngoja niwapandie huko huko hewani." Aliongea hayo huku akiichukua simu yake mfukoni na akabonyeza namba ya mke wake na kuipiga hapo hapo mbele ya wenzake.

"Haloo halooo halooooo.....!"

Mzee Bruno Gautier aliita baada ya simu kupokelewa na upande wa pili kutoongea chochote.

"Haloo oo mhhh mbona kimya hawaongei chochote hawa?" Mzee Bruno Gautier alijiuliza swali.

"Vipi mbona unaongea peke yako mzee wangu kuna nini?"

Santana alimuuliza mzee Bruno wakati akiingia ndani mle na kumkuta akiongea peke yake.

"Wanapokea simu lakini hakuna wanachojibu au kuongea chochote." Mzee Bruno Gautier alieleza.

"Jaribu tena inawezekana mtandao haukuwa vizuri." Santana alimshauri mzee Bruno.

Kisha alipiga tena namba ya mke wake kwa mara nyingine tena.

"Mume wangu ni-na-ni.... nakufa niokoe kutoka kwa mbweha hawa si watu wazuri hata kidogo na laiti ungejua sehemu niliyofungiwa mume wangu usingekaa hata sekunde sifuri."

"Unasemaje mke wangu? Kwani wamekufungia sehemu gani?" Mzee Bruno Gautier aliuliza.

"Unataka kujua siyo?"

Huyu mzee mara baada ya kusikia tu swali hilo aliidondosha simu kwa pressure kwani sauti iliyouliza swali lile anaijua vizuri sana.

"Mzee mbona unaangusha simu au ni ya bei dezo?"

Robinson alimuuliza huku akiiokota simu na kumkabidhi mzee Bruno.

"Hapana Robinson imetokea tu."

Aliipokea na kuiweka sikioni kuona kama bado iko hewani au la.

"Halooo...." Mzee Bruno Gautier aliita.

"Mbona ulikuwa hauongei ni hivi mzee iwapo utachukua muda mrefu bila kumfuata mkeo tutakutumia kichwa cha mkeo kwani hatuna hasara yoyote." Jackline alimtisha. 

"Binti ndiyo tuko kukamilisha mipango ili twende sawa na kwa kuwahakikishia tu hata mwenzenu tunaye hapa."

"Mwenzetu gani mzee?"

"Si ni Robinson?"

"Robinson? Robinson gani huyo?" Jackline aliuliza.

"Kwani mlikuwa wangapi siku ile tulipokutana kule porini na mpaka kule mgodini kwangu?"

"Hatukumbuki kwani tulikuwa wangapi zaidi ya sisi wenyewe kama tulivyo hapa."

"Sasa mbona mnanichanganya maana hata kwenye vitu mnavyovihitaji ni pamoja na Robinson."

"Mzee masuala ya Robinson hatutaki kuyasikia hata kidogo huyo ni mwenzenu mnafikiri hatujui kilichomfanya akutoroshe?"

"Kitu gani hicho ambacho hata mimi sikijui?"

"Muda ukifika tu utajua mzee Bruno Gautier na huyo msaliti wako." Jackline alikazia maneno yake.

"Basi ongeeni naye mwenyewe huyu hapa yuko salama kabisa."

Aliongea maneno yale na kumkabidhi simu Robinson alikuwa pembeni yake muda wote akiwasikiliza.

"Haloo ni mimi Robinson niko vizuri kwa sasa na kuhusu kupotea kwangu ile siku nilitekwa na watu wa Santana."

"Huna chochote Robinson wewe ni msaliti na hilo ulilianza toka ile siku ulipokisikia kile kiasi cha fedha cha mzee Bruno."

Kisha alikata simu Jackline na kuwaachia maswali mzee Bruno na Robinson.


****


"Mkuu nakusikia."

Mkuu wa kituo Lupa aliitikia mara baada ya kupokea simu ya bosi wake kutoka Makongolosi.

"Vijana wangu hawajafika bado hapo?"

"Bado mkuu, niliwatafuta muda fulani hivi hawakupatikana ngoja niwapigie tena."

"Fanya hivyo kwani wanatakiwa kurudi hapa hata kama itakuwa ni usiku wa manane maana hapa kuna tukio jingine limetokea Saza Mining' kuna wafanyakazi wamefukiwa na kifusi walipokuwa shimoni huko na hapa hakuna gari jingine la kulitumia."

"Sawa mkuu wakifika tu sitawapa hata sikunde moja ya kukaa hapa."

Akiwa anaongea na mkuu wake wa kazi alisikia gari likipiga breki nje.

"Naona ndiyo wanaingia mkuu."

"Okay niwatakie majukumu mema."

"Sawa mkuu."

Alikata simu na kutoka nje ambako aliwakuta wakiwa tayari kwa kuwabeba wahalifu.

"Vipi mbona mmechelewa sana mpaka mkuu alipata hofu akapiga simu kutaka kujua nini kimewakuta."

"Tulikutana na tatizo kidogo la panja lakini mwisho wa siku tulilikabili na sasa tuko hapa."

"Okay basi subirini kidogo tuwaandae watu wenu maana sisi kazi yetu tushaimaliza Afande George."

"Bila tatizo mkuu."

Afande Mkonge aliingia ofisini kwake na kisha kumtumia ujumbe Afande Piliska.

"Njoo mara moja hapa ofisini kwangu."

Afande Piliska baada ya kuiona ile meseji alitoka na kuelekea kwa mkuu wake kuitikia wito.

"Mambo yameiva tayari utamfuata Afande Miraji aandaye lile faili la hao nyang'ao kisha amkabidhi Afande George pamoja na watuhumiwa."

"Kama ulivyoagiza mkuu."

Afande Piliska aliitikia na kutoka nje kumfuata Afande Miraji kumpa maelekezo ya mkuu.

"Mkuu kasema chukua faili la wale watuhumiwa wa Bitimanyanga na mkabidhi Afande George pamoja nao."

"Okay sawa."

Alitoka Afande Miraji na kufanya kama alivyoelekezwa na Afande Piliska akamkabidhi Afande George faili pamoja na wahusika.

"Mbona siwaelewi jamani? Kila kitu nilishamalizana na mkuu wa kituo juu ya kilichotokea kilichokuwa kikisubiriwa ilikuwa ni tamko kutoka kwake tu."

"Uko sawa kabisa na tamko alilolitoa ni ninyi kuhamishwa Kituo kutoka hapa na kwenda Kituo kikuu cha Makongolosi, umenielewa mzee Rasta?"

Afande Miraji alimkebehi mzee Jonathan kwa muonekano wake wa nywele.

Mzee Jonathan aliishiwa pozi lote na nguvu zilimwisha aligeuka tu nyuma kumtazama Masanja ambaye alikuwa kimya muda wote.

" Mzee Jonathan yako wapi sasa majigambo yako? "

Masanja aliongea hayo kwa sauti ya chini huku akimpita na kuliendea gari lililokuwa likiwasubiri.

"Yakwisha tu haya mimi ndiyo Jonathan Ubao mtu hatari zaidi ndani ya nchi."

Mzee Jonathan aliongea hayo kimoyo moyo huku akimpita Afande Piliska aliyekuwa akiwaangalia kwa jicho la huruma.


NINI KINAKWENDA KUTOKEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII.


          #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post