NITAKUUA MWENYEWE - 38

 


NITAKUUA MWENYEWE - 38

sultanuwezotz.blogspot.com


"Mzee Bruno Gautier hebu watafute hao Kenge waambie tuko njiani tunakutana wapi?" Santana alimuagiza mzee Bruno.

"Sawa kijana wangu ngoja niwaulize mara moja." Mzee Bruno Gautier alijibu.

"Fanya haraka sana maana siku ya leo nina mzuka hatari."

Mzee Bruno alimpigia simu mke wake kwani mara nyingi ndiyo namba wanayoitumia wakina Jackline pia. Baada ya kuipiga mara kadhaa haikupatikana kitu kilichomchanganya sana mzee Bruno.

"Wasije kuwa wameshamuua mke wangu?"

Mzee Bruno Gautier aliuliza swali huku akipiga piga kichwa kwa simu yake.

"Vipi kwanini unasema hivyo mzee?"

Santana alimuuliza mzee Bruno baada ya kuona hayuko sawa.

"Mhhh hakuna kitu." Mzee Bruno Gautier hakuwa sawa kabisa.

"Kwanza ngoja, umewapata hewani?"

Santana ilibidi aulize swali la msingi baada ya kuona mzee mzima kama kachanganyikiwa hivi kwa jinsi alivyokuwa akigongagonga bodi ya gari.

"Ndicho kinachonichanganya Santana hapatikani hewani kabisa nimepiga na kupiga lakini hakuna kitu na si kawaida yao au wamemuua mke wangu?"

"Sikiliza mzee usiwe kama boga wewe ni shujaa ninayekuamini kwenye mambo yangu mengi sana sasa nitakushangaa kuchanganyikiwa eti kisa mkeo hapatikani hewani, kwanza nimekwambia wapigie wale wanawake na si mkeo."

"Santana hata wewe hauko sawa hata kidogo nilikwambia wale hawana simu hivyo wanatumia ya mke wangu."

"Ni kweli kabisa simu hawana, sababu ni kwamba simu zetu tuliziacha ndani ya chumba ambacho tulifungiwa mgodini kwako mzee hivyo sina uhakika kama walikumbuka kwenda kuzifukua pale ambapo tulizichimbia." Robinson alifafanua.

"Si unaona Santana, nilikwambia hawana simu wale."

"Kwani nilikataa juu ya hilo? Mimi nilitaka wapatikane tu haijalishi ni kwa kutumia simu ya nani?"

Santana alipaza sauti ya juu baada ya kuona hawaelewani kila mmoja akiongea lake.

"Okay hebu tuyaache hayo Santana tujadili ni namna gani tunawapata."

Mzee Bruno Gautier ilibidi amrudishe Santana kwenye mstari kwanza ili mambo mengine yaendelee.

"Hebu niitieni rubani wa ndege mara moja." Santana aliagiza.

Baada ya kuja rubani wake alimwambia aikague ndege kama iko vizuri kuna safari wanatakiwa kwenda.

"Kamanda wangu wa anga ifanyie ukaguzi ndege kama iko poa."

"Sawa kiongozi wangu."

Rubani alitoka na kuelekea kwenye egesho la ndege.

Rubani alipotoka tu ofisini kwa Santana, simu yake iliingia ujumbe.

"NAISIKIA HARUFU YA DAMU YAKO SANTANA."

Baada ya kuisoma tu alijikuta jasho likimtoka mfululizo na kama hakuielewa hivi ile meseji akaisoma tena akiamini labda yalikuwa ni mawenge ya macho yake tu lakini alipoirudia kuisoma ilikuwa ni ile ile. Alihisi kichwa kinawaka moto.

" Ni nani aliyetuma ujumbe huu kwa kutumia namba ngeni?"

Aliinuka na kutoka nje ambako wenzake walikuwa wamekaa wakimsubiri yeye waianze safari yao.

"Vipi kijana wangu mbona macho juu kama jogoo anayeangalia muda wa kuwika."

Mzee Bruno Gautier alimuuliza Santana baada ya kumuona kafika pale haongei chochote zaidi kuangalia juu kama vile kulikuwa na kitu kipya angani ambacho hajawahi kiona.

"Nimepokea ujumbe wa kutisha kidogo si sana."

"Ujumbe wa kutisha? Kutoka wapi? Kwa nani?" Mzee Bruno Gautier aliuliza.

"Sijui uliko toka ila nahisi ni wale wanawake tu kwani namba ya mtumaji haionekani, nimeitafuta na kuitafuta lakini wapi."

"Inasemaje hiyo meseji mkuu?" Robinson alimuuliza Santana.

"NAISIKIA HARUFU YA DAMU YAKO SANTANA." Robinson aliusoma ujumbe ule baada ya kupewa simu na Santana.

"Kiongozi si wengine waliotuma huo ujumbe bali ni wakina Jackline tu, eleweni kuwa hawa ndiyo maadui zetu wakubwa kwa sasa na kwa namna nilivyowafahamu hawa wasichana kwa kipindi chote nilichokuwa nao huwa wakisema kitu lazima kiwe hivyo huo ujumbe msiubeze hata kidogo." Robinson aliwatahadharisha wakuu wake wapya.

" Unataka kututisha siyo au ndivyo ulivyoagizwa na hao mapunguani waliopoteza network' za maisha? "

Santana alimgeukia Robinson ambaye alijua anashauri zuri kumbe alikuwa ameharibu.

" Hapana kiongozi nilikuwa najaribu kukuelezeni nilivyowafahamu hawa viumbe na mfanyaje kuwakabili.. "

" Keleleeee.... Unaongea upuuzi gani kama wewe ni muhubiri mzuri si ungekuwa huko kwenye Masinagogi ukihubiri neno la Mungu kwa wanaolihitaji lakini siyo sisi kijana."

"Naombeni msamaha kama nimewakwaza wakubwa zangu." 

Robinson alipiga magoti kuomba msamaha baada ya kubaini kuwa amechafua hali ya hewa. 

"Santana haina haja ya kuendelea kulumbana hapa zaidi tuangalie mbele tunakutana nao vipi hao viumbe?" 

Mzee Bruno Gautier aliingilia kati baada ya kuona Santana hamuelewi Robinson. 

"Na wewe mzee elewa kuwa kama mkeo atakufa itakuwa ndiyo mwanzo wetu wa kukuwa kiuchumi hivyo sioni sababu ya kwenda kumkomboa mtu kama yule mzee wangu mbona sisi wengine hatuzungumzii Mahusiano ni wewe tu na huyo kenge wako ana kipi cha kuichanganya akili yako kiasi cha kuacha kufikiria namna ya kuuendeleza mgodi?"

" Hapo umenigusa pengine kijana wangu naona sasa heshima inashuka, mke wangu wa kwanza ulimuua na madawa yako na huyu tena unasema wa nini kwangu kweli Santana? "

Kabla Santana hajajibu chochote kwa mzee Bruno mara alifika rubani kutoa ripoti ya kile ambacho aliagizwa na mkuu wake. 

" Mkuu ndege iko tayari kwa safari."

"Okay vizuri kamanda wangu pakia lile boksi la vinywaji na wewe Mtanzania hapo ongozana na rubani kachukue maboksi ya vyakula pakieni haraka tuko nyuma ya wakati." 

"Nashukuru mkuu kwa kunisamehe." Robinson alishukuru lakini Santana hakumjibu kitu zaidi ya kuendelea kunywa mvinyo wake na macho yakiwa kwa mzee Bruno ambaye muda huo alikuwa katulia tu akitafakari maneno ya mbia mwenzake ya kumkashifu mke wake Bi Claudia. 

" Kila kitu kiko sawa mkuu tunaweza kuondoka sasa." Rubani alitoa taarifa. 

"Okay tuondokeni sasa." 

Santana aliongea na kuchukua koti lake huku akimuacha mzee Bruno Gautier akiwa bado katulia tu hajafanya maamuzi. 

"We mzee hauongozani nasi?" 

Santana alimuuliza mzee Bruno baada ya kugeuka na kumuona bado hajainuka zaidi ya kujiinamia tu. 

Aliyasikia maneno ya Santana lakini hakujibu chochote zaidi ya kusimama na kuongoza ndege ilikokuwa. 


***


Wakina Jackline baada ya kutoka hospitali kumuona mama yake Roberto Stanley ambaye wakina Jackline walimuahidi Roberto kumsaidia. Waliongoza mpaka kwa rafiki yake Jasmine aitwaye Melissa anayefanya kazi kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Brazil.

"Unajua bado najiuliza sana huku Rio Branco mmefuata nini ninyi Warembo?"

Aliuliza Melissa akiwa nyuma ya usukani akiwapeleka wageni wake kwake maeneo ya North Angle eneo ambalo hukaliwa sana na Waafrika kutokana na hali ya utulivu na hali ya hewa inayofanana na ya Afrika na hata shughuli za kilimo hufanyika kwa wingi eneo hili.

"Unajua nini Melissa? Kwa sasa tumekuwa kama digi digi hatuna makazi maalum hapa Brazil."

"Kivipi Jasmine na vipi kuhusu Santana wako maana nakumbuka kuna siku uliniambia kuna kitu kimetokea unataka kuniomba ushauri."

"Ni kweli kabisa lakini masaa chache nilitiwa pingu na watu wake nikiwa na mdogo wangu Jessica na kisha kushindiliwa madawa ya kulevya lengo likiwa ni kunikomoa kutokana na hatua yangu ya kumsaidia mdogo wangu ambaye alitaka kumtumia kusafirisha madawa yake na bora ingekuwa kwa makubaliano na mhusika lakini yeye alitaka amuue kisha asafirishe kama maiti."

"Mhh makubwa hayo, pole sana Jessica (alimgeukia Jessica) eeh sasa ikawaje mpaka leo mko nje ya mikono michafu ya Santana?"

"Acha tu yaani kama muvi vile walitokea hawa wenzetu nasema wenzetu sababu walikuwa wawili Jackline na mpenzi wake Robinson ambaye ametusaliti na kurudi upande wa pili kisa mkwanja, walituokoa baada ya wao pia kuokoka kutoka kwenye mikono hiyo hiyo ya Santana ambaye aliwaambia waje yeye ana chuo cha mafunzo ya mapigano kumbe tageti yake ilikuwa ni kuwanyofoa viungo vyao na kuvipeleka India lakini kabla hajafanikisha zoezi lake watanzania wenye chale zao wakaiona na kutoroka."

"Poleni sana ndugu zangu, mwenzenu huyu Jasmine nilimkanya sana juu ya Santana lakini masikioni aliweka pamba."

"Ni bora alifanya hivyo kwani angekubali ushauri wako inawezekana mpaka leo angejua wewe ndiye uliyemtenganisha na mpenzi wake."

"Ni kweli Jackline, jamani karibuni hapa ndipo ninapoishi kwa sasa." 

"Tunashukuru sana dada Melissa." Aliitikia Jessica ambaye muda wote alikuwa kimya akiwasikiliza tu.

" Dada hivi unamuamini tumemuamini vipi Roberto kumuachia Bi Claudia?"

Jessica aliuliza swali hilo kama vile naye hakuwepo wakati wanamkabidhi.

" Hebu achana na hizo mambo mdogo wangu itajulikana tu baada ya kutoka hapa." Jasmine alimjibu mdogo wake.

"Hebu mtishe tena Santana bwana ili ajue tuko siliasi."

"Nakujuaga ukisema hivyo tu tayari kichwani una jipya chukua simu hii hapa mfanyia jambo."

"Poa."

Aliipokea simu kutoka kwa Jasmine na kuuandika ujumbe mwingine ambao aliutuma tena kwa Santana nao ulisomeka hivi..

"KESHO ALFAJIRI KWENYE Ufukwe wa PRAIA DO FUTURO ulioko ndani ya mji wa FORTALEZA kuna zawadi yako na ukipuuza tu Utajuta kutufahamu."

Na baada ya kuukamilisha aliwaonesha wenzake ambao waliufurahia kisha alimtumia Santana.

"Nina uhakika baada ya kuusoma ujumbe huo lazima achanganyikiwe na pale atakapojaribu kututafuta hewani hawezi kutupatau." Jackline alichekelea.

"Sasa lengo lenu ni lipi kwenye mtego wenu huu?" Melissa aliuliza.

"Kikubwa ni kumfilisi Santana na mshirika wake mzee Bruno Gautier na kisha kumfunza adabu Robinson hata kama itakuwa miaka elfu mia moja wakati huo huo kuhakikisha Mali za marehemu wazazi wangu zinarudi kwangu na wakati huo tutakuwa na mabilioni ya dollars."

Jackline alitoa ufafanuzi zaidi kwa Melissa ambaye aliona kama na anashauku ya kutaka kujua hivi.

" WATU WAKO NINAO NYUMBANI KWANGU"

Melissa alimtumia ujumbe Santana baada ya kuwaacha wenyeji wake sebuleni na yeye kuingia chumbani kwake.

" WAMEFIKAJE KWAKO?" Santana aliuliza swali.

"WAMEFIKA TU SI UNAJUA MIAKA KADHAA NYUMA NILIKUWA MSIRI MKUBWA WA JASMINE KABLA HAMJAOANA."

"KWELI?"

"NDIYO, MASIKINI JASMINE NA MPAKA LEO ANAAMINI MIMI BADO NAFANYA KAZI UBALOZINI KWETU KUMBE NILIACHA KITAMBO BAADA YA KUUNGANA NA WEWE KWENYE BIASHARA YETU YA VIUNGO VYA BINADAMU."

"ENDELEA KUCHEZA NA AKILI ZAO NA SISI TUTAKUWA HAPO BAADA YA DAKIKA CHACHE KUWAONESHA MIMI NI NANI."

"POA JEMEDARI WANGU."

Alipomaliza kuchati na Santana alirudi pale sebuleni kwa wageni wake waliokuwa wanamsubiria.

"Niwaletee kinywaji gani wageni wangu?"

Aliwauliza huku akiwa na tabasamu pana la ushindi usoni.


UNAFIKIRI NINI KITAENDELEA?


TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.


#SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post