NITAKUUA MWENYEWE - 39 (Mtunzi: Sultan Uwezo)


NITAKUUA MWENYEWE - 39

sultanuwezotz.blogspot.com


Baada ya kutaja vinywaji wavihitajivyo Melissa aliiendea friji yake akachukua vinywaji vile na kuwaletea wageni wake kisha akachukua nafasi yake naye akaketi.

"Melissa hivi toka kipindi kile tumeachana ndipo ulipata kazi ubalozini au kabla kuna kona ambayo ulipita kwanza?" Jasmine alimuuliza Melissa wakiwa wanaendelea kupooza makoo yao.

"Kabla ya Ubalozini nilijiajiri kwanza hapa mjini nikiwa natembeza matunda ya maepo."

"Wee kwa nyodo zako wewe uliwezaje kufanya biashara hiyo ya maepo?"

"Biashara ya maepo kwa hapa bonge la dili kwani huuzwa kwa bei ya juu sana huenda mpaka dola tatu kwa epo moja."

"Lakini nasikia matunda haya yana uhusiano mkubwa sana na madawa ya kulevya sababu kule Afrika ya Kusini matunda hayo yalikuwa yakiuzwa mpaka dola ishirini kwa epo moja na mara baada ya serikali kuyafanyia uchunguzi wakabaini kuwa sura ilikuwa ni epo lakini mfumo wa burudani wa ndani ulikuwa ni madawa ya kulevya ambayo yalipachikwa kitaalam sana na maeneo yalikokuwa yakipelekwa na kuuzwa sana ilikuwa ni kwenye masaluni."

Jackline alichangia hoja hiyo kwa kuelezea namna ambavyo anaijua biashara hiyo.

" Kwa hiyo unataka kusema na mimi nilikuwa nafanya biashara hiyo ya madawa ya kulevya?

Melissa aliuliza kwa kumkazia macho Jackline kama vile aliotea uhalisia wa biashara yake hivyo ilikuwa kama vile kumkata fikra zake.

" Hapana sijamaanisha hivyo nimeelezea tu ninavyoifahamu biashara ya maepo kwa maeneo niliyokuwepo."

"Okay ila kwa upande wangu haikuwa hivyo mpendwa."

"Dada tuwashie muziki tuburudishe ngoma za masikio kwani tuna muda mrefu sana hatujawahi kusikia milio ya muziki zaidi ya milio ya risasi na mabomu."

Jessica aliona dalili hazikuwa nzuri kwa upande wa Jackline na mwenyeji wao Melissa.

"Kweli kabisa mdogo wangu umenena ni muda sana hebu Melissa tufanyie mambo tuzungushe viuno hapa visijekuwa vigumu kama vimeshikwa na kutu bure."

Jasmine aliongea hayo na kuwafanya wote kuachia vicheko huku Melissa akihangaika kutafuta flashi yenye ngoma tofauti tofauti kutoka kila bara.

Katika kuitafuta ndipo akaikuta na kuipachika kwenye Home Theater yake na kama zali vile si ngoma ya kwanza ikawa ni ile ya BEMBELEZA iliyoimbwa na Wanamuziki wa kizazi kipya kutoka Tanzania Quick Rocka akimshirikisha Joh Makini pale sebuleni nani alikaa? Kila mmoja akicheza kwa ustadi wake aliyecheza kwa kuzungusha kiuno haya, aliyecheza kwa kuchezesha tumbo twende kazi ila kituko kilikuwa kwa Melissa aliyecheza kiustadi zaidi kutokana na staili yake ya kuweka mguu wake mmoja juu ya kochi na kuanza kukisasambua kinyonga chake.

"Mmhh mwenzetu umetushinda kwa staili hiyo duu!"

Jackline aliongea baada ya kujikuta akiduwaa kumuangalia tu Melissa. Naye kama vile alifanya makusudi kwani alipoona anatazamwa sana ndipo akaongeza mbwembwe zaidi.

"Bwana eee umeshinda wewe sasa..." Jasmine naye akaona amkatishe kwa kumsukuma.

"Wivu wenu tu hamna lolote kama hamjui hamjui tu ninyi zenu ni silaha tu mambo hizi tuachieni siye."

Melissa akawazodoa na muda huo akaingia chumbani kwake huku akiwaacha wakina Jessica wakijisevia maji ya baridi baada ya kulinunua joto la ghafla.

"NDIYO TUNAINGIA KWAKO HAPO."

Meseji iliingia na ndipo Melissa akaona amtwangie tu Santana.

"Mnaingia na staili gani sasa?"

"Hakuna zaidi ya kuvamia tu na kisha kuwabeba wote kisha tutajua wewe tunakuachaje ."

"Sawa ila changu mapema maneno sitaki. "

"Kitambo sana akaunti yako inapumulia mipira kutokana na kuzidiwa na midola."

"Hayo ndiyo maneno vingine havinihusu ni kazi yenu kucheza na vipanya buku vilivyowashinda midume mizima na kunasa kwenye mtego wangu mdogo tu."

"Haya mama yake andaa mazingira jeshi langu limeshafika nje ya mjengo wako."

"Poa."

Melissa alikata simu na kurejea sebuleni na kuwakuta wenzake wakiwa wameacha kucheza na muda huu walikuwa wanaangalia katuni kupitia kwenye chaneli maarufu ya katuni ya hapo Brazil inayofahamika kama LIVE CARTOON. Aliwaangalia kisha alitikisa kichwa kwani alijua muda wa kunaswa umefika na yeye kuzidi kuchanua kiuchumi.

"Mtanisamehe sana Melissa hana undugu na binadamu mbele ya Mkwanja."

Wakiwa wametekwa na katuni pale sebuleni mara mlango uligongwa, walitazamana na kisha wakahamishia macho kwa mwenyeji wao ambaye alisimama na kwenda kuufungua. Aliusogelea na kuufungua na alipojaribu kuchungulia nje kuona ni nani aliyegonga alikutana na kitako cha bunduki kilichotua kichwani na kumpeleka chini kisha wagongaji wakiingia ndani wakimruka Melissa pale mlangoni.

Wakina Jackline wakiwa bado hawajui kinachoendelea mara waliingia watu watatu wakiwa na mitutu mikononi mwao na usoni wakiwa wamevalia maski.

Jackline akaona njia pekee ya kujinasua ni kuchomoa bastola yake iliyokuwa kiunoni mwake lakini alichelewa kwani walioingia hawakuwa na masihara hata kidogo kwani aliyekuwa katikati yao alifyatua risasi iliyomkosa na kupiga kabati la vyombo. Hapo Jackline akajua akileta za kuleta anakwenda kukutana na pembenne huku tani sita za udongo zikiwa juu yake.

Akalala chini kama wenza huku akiiachia bastola yake.

"Jackline usilete ujuaji kwenye mdomo wa bunduki utakufa mama yangu."

Robinson aliongea hayo huku akivua maski na kuchuchumaa pale alipo Jackline.

"Haaa Robinson ni wewe kweli usiniambie kama umetisaliti wenzako na mimi mpenzi wako?"

Jackline aliongea baada ya kuiona sura ya Robinson ikiwa ndani ya mavazi yale ya rangi ya kijani nyeusi ambayo huvaliwa na watu wa Santana.

"Jackline kwanza naomba unisamehe kwa kukutelekeza kabla ya kufikia lengo lako la kuokoa Mali zenu na pili nikuambie tu mpenzi wangu kuwa chini ya jua hakuna mtu yeyote ambaye ni mjanja mbele hela na ni hela hizo hizo zilikuleta huku Brazil kuzipambania nikaona mwenzangu tayari unazo, Jasmine na mdogo wake wanazo na mimi mtoto wa kapuku nina nini nikaona nifanye maamuzi ya kiume kama haya ikiwa ni kukukamateni na kuwapeleka machinjioni kwa mtu ambaye mmemkimbia weee mwisho wa siku mnarudishwa kwake."

"Keleleeeeee Robinson unaongea nini wewe?"

Jackline aliongea huku kajipindua na kumtandika teke la kisogo Robinson lililompeleka chini na kuachia bunduki ambayo Jackline aliirukia aichukue lakini alichelewa kwani Robinson alifanikiwa kuisukuma kwa teke na kumfikia mmoja wa wale aliokuja nao na wakaichukua. Ndipo Jackline akajipindua na kumvaa Robinson ambaye kwa wepesi wa hali ya juu alimkwepa na kumfanya Jackline atulie kwenye mkono wake ambao aliumia kwenye ajali ya pikipiki na hapo ndipo walimvaa wale wengine na kumpiga cheni. Upande wa Jasmine na Jessica wao ilibidi watulie kwanza kuusoma mchezo unakwendaje lakini wakaona wababe wao walikuwa kamili ikabidi watulie tu. Wote walipigwa cheni za mikono na miguu na hapo ndipo walipofanikiwa kuiona sura ya mtu wa pili kati ya wale walioongozana na Robinson kuwa alikuwa ni mzee Bruno Gautier.

"Jackline mrembo jasiri usiyeogopa kitu chochote kwa hilo nakupongeza sana lakini nikuhakikishie tu safari hii huruki geti aisee."

Mzee Bruno Gautier alipokuwa akiongea hayo mbele ya Jackline alishangaa akitemewa mate usoni na Jackline.

"Asante sana Jackline kwa kitendo hiki na ndiyo maana niliongea mwanzo kuwa wewe si wa kawaida lakini fanya yote unayohisi yatakusaidia kujinasua lakini angalia usije wahi kuzimu kabla ya muda wako.

" Tunawahakikishia kuwa tunakwenda kuibuka tena na kuwasambaratisha kwa mara nyingine tena." Jessica aliibuka na kuongea maneno ya kujitia moyo.

"Unajidanganya sana Jessica ni muda wenu sasa wa kutangulia kuzimu huku sisi tukibakia kula maisha milele."

"Robinson acha kujidanganya wewe na nikuhakikishie kuwa hata nife leo nitainuka tena na kukuua kwa mkono wangu." Jackline aliongea huku machozi yakimtoka.

"Shutup your mouth."

Robinson aliongea hayo na kumtandika ngumi ya shavu iliyompeleka chini na kuuangukia mkono ule ule na hapo uzalendo ulimshinda na kujikuta akianza kulia kwa sauti.

"Bibie usiniletee uchuro ndani ya jumba langu lenye bahati ya minoti subiri ukitoka hapa ndani ndiyo uendelee kulia sawa wewe nguchiro? Na wewe mwehu hapo ulijua mimi ni kama wewe eee mwenzako naitwa Melissa Madola upo nyonyoooo." Melissa aliongea mbele ya Jackline na Jasmine kisha aliwapita na kwenda kuongeza sauti ya muziki ambao muda huo ilikuwa ikipigwa ngoma ya BABA LAO ya Diamond Platinum kisha akaanza kucheza na hapo ndipo walipobaini kuwa Melissa ndiye mchawi wao aliyewauza.

"Nipe ripoti mzee Bruno Gautier."

"Kijana wangu tulia basi kila kitu kimekaa sawa chezea Robinson wewe utaugua ugonjwa wa Corona shauri yako."

"Ikoje mzee?"

"Tumewadaka kama nzige wale wadudu wasumbufu kule Kenya pamoja na mbwembwe zao zote lakini walikuwa wakidakwa kiulaini sana na ndivyo tulivyowadaka hawa vibwengo."

"Fanyeni haraka mniletee wakiwa hai ili niwatoe viungo vyao ambavyo kwa utatu wao tunakwenda kuingiza 'a lot of dollars' mzee wangu."

"Tutegemee kijana wangu ila kama utakuwa umekamilisha masuala yako ungana nasi basi kwani hatuwezi kuondoka hapa kabla sijajua mke wangu alipo japo uliniudhi kwa kauli zako juu ya mke wangu."

"Aaah mzee wangu yale yalikuwa ni madawa tu sikuwa mimi muda ule ila yote kwa yote wafanyieni chochote kile but' muwe makini na roho zao tu. Mimi siwezi kuungana nanyi hapo sababu bado namalizia kuingiza pesa kwenye akaunti ya Melissa na pia kwenye akaunti ya bwana mdogo Robinson walau aifurahie kazi mpya siyo kama hao Kenge waliokuwa wakimtumia dere."

"Vizuri kijana wangu basi wewe endelea na yako na sisi na yetu."

"Sawa sawa mzee."

Mzee Bruno Gautier alikata simu na kuwageukia wabaya wake ambao wameichanganya sana akili yake ndani ya muda mfupi kitu ambacho hakuwahi kutana nacho tokea aingie kwenye biashara ya machimbo ya kokoto.

Jackline muda wote alikuwa akimuangalia sana Robinson pamoja na Melissa ambaye bado alikuwa anacheza muziki ikiwa ni furaha baada ya kuingiza mkwanja mrefu ndani ya muda mfupi bila hata kutoa jasho.

Mara simu ya Jackline iliita na kwa kuwa ilikuwa mfukoni hakuweza kuhangaika nayo alitulia tu huku akiwa anaendelea kupiga hesabu zake za kujiokoa.

"Baby hiyo simu si inaita?" Robinson aliuliza.

"Kwa hiyo kama inaita inakuhusu?" Jackline alimjibu.

"Nilijua hujaisikia nilikuwa nakujulisha tu."

"Achana na mimi wewe Kinyago cha Kimakonde na tena usinizoee na nikuhakikishie tu kwa namna yoyote ile nikiwa nimekufa au nikiwa hai lazima nitakuua mwenyewe Robinson na lazima utayajutia maamuzi yako na wewe hapo mshenzi wa tabia." Akimuangalia Melissa.

"Jackline unajua unachekesha sana toka lini maiti isiyo na viungo vyote yaani yenye upungufu wa viungo ikaamka na kuua watu."

Robinson aliongea hao akiwa anauchezea mdomo wa Jessica ambaye muda wote alikuwa katulia tu hasemi chocolate lakini kwa kitendo kile cha kuchezewa na mtu kama Robinson alijikuta akimtwanga Robinson bonge la kichwa kilichomfanya ateme damu za kutosha.

"Paaaaa....." Ilikuwa ni mlio wa risasi.


NI NANI ALIYEIPIGA HIYO RISASI NA IMEKWENDA KWA NANI?


KAA MGUU SAWA KATIKA SEHEMU INAYOFUATA KUJUA ZAIDI.


          #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post