NITAKUUA MWENYEWE - 40 (Mtunzi: Sultan Uwezo)


 NITAKUUA MWENYEWE - 40

sultanuwezotz.blogspot.com


"Afande Bupe nawahitaji wale watuhumiwa walioletwa hapa kutoka Lupa."Mkuu wa kituo aliagiza.

"Kama ulivyoagiza mkuu."

Alijibu Afande Bupe na kisha kutoka ofisini kwa mkuu wake.

Alienda kuwachukua wakina mzee Jonathan na Masanja na kuwaleta mbele ya mkuu wake wa kazi.

"Kaeni bwana msinisimamie kama milingoti hapa."

Mkuu huyu alianza kwa kuwapiga biti walipoingia tu. Na Afande Bupe akafungua mlango ili kutoa nafasi kwa mkuu wake kuweza kuwahoji watuhumiwa hao.

"Unakwenda wapi Afande tulia hapa hapa."

"Sawa mkuu."

Alirudisha mlango na kurudi kuchukua nafasi kando ya watuhumiwa.

"Ehhh naomba kuwafahamu zaidi ya ninavyowafahamu waungwana." Alianza mkuu wa kituo.

"Sijakuelewa Afande." Mzee Jonathan alijibu.

"Hujanielewa eee, niambie basi nitumie lugha ipi ambayo utanielewa mzee mwenzangu."

"Hiyo ni juu yako mwenyewe si jukumu langu mimi, watu gani mnakuwa vigeugeu hapa."

Mzee Jonathan aliongea kwa jazba huku kamtolea macho mkuu wa kituo.

"Afande Bupe nitolee huyo kijana kwanza nianze na mzee mwenzangu labda tutaongea lugha moja."

"Sawa mkuu."

Afande Bupe aliondoka na Masanja na kumrudisha sero kisha akarejea tena.

"Sasa nafikiri tutaelewana si ndiyo?"

"Bado sikuelewi Afande." Alijibu mzee Jonathan.

"Ooohhh kumbe ni mgumu wa kuelewa siyo? Afande mfungue kufuri la uelewa mara."

Afande Bupe hakujibu lolote kwa mkuu wake zaidi ya kumzoa mzee Jonathan na kumsogeza pembeni kidogo ambapo alianza kumtandika viboko na fimbo ilivyokuwa ikitumika ilikuwa kama vile ngozi ya mnyama hivi kwa namna ambavyo ilikuwa ikimzunguka mzee Jonathan maana ilikuwa ikimchapa mgongoni inakwenda mpaka tumboni na kisha Afande huyu mwenye sura ya kazi alikuwa akiivuta na kupelekea makelele.

"Ahhh.. aghhhh inatosha Afande nitaongea kila kitu."

"Ha ha ha kumbe hii ni njia ya kukuelewesha mzee mwenzangu?"

"Afande naomba msaada wako tafadhali."

"Msaada gani huo unaouhitaji kutoka kwangu?"

"Fanya kila unaloweza niondoke hapa maana sijayazoea hata kidogo."

"Okay kwanza niambie haya niliyoyasoma kwenye faili lako ni ya kweli?"

"Inawezekana Afande."

"Kivipi?"

"Sijaona kilichoandikwa hata kimoja Afande sasa nitasemaje ni sawa?"

"Lakini wewe si ndiye uliyetoa maelezo?"

"Ndiyo Afande."

"Basi nataka kujua kutoka kwenye maelezo yako mwenyewe."

"Mimi kwa majina naitwa Jonathan Ubao ni mfanyabiashara nikiwa na biashara nyingi sana nyingine nazimiliki kihalali na nyingine nilifanya dhuluma na hizo ndizo zinanitesa mpaka sasa."

"Ulizidhulumu kutoka kwa nani?"

"Ni stori ndefu Afande lakini kifupi ni kutoka kwa familia ya rafiki yangu mkubwa sana na ambaye aliniinua pale nilipoanguka na hata baada ya kufikwa na umauti wao mzee Fikirini ambaye ni ndugu na hiyo familia alinikabidhi kusimamia Mali za marehemu ambazo ni Hotel Joachim iliyoko Morogoro, kampuni ya utalii iitwayo Joachim Safaris yenye makao yake jijini Arusha pamoja na shamba la mpunga kule Kilombero Morogoro bila kusahau kampuni ya usafirishaji mizigo ya Mzalendo Cargo ya jijini Dar nyingine nyingi."

"Hiyo familia hujaitaja hapo zaidi ya ndugu yake mzee Fikirini."

"Ni ya mzee Joachim Thomas ambaye alifariki pamoja na mke katika ajali ya gari maeneo ya Sekenke Singida na hapo alipona binti yao aitwaye Jackline."

"Okay ndiyo maana unaisaka kwa udi na uvumba ili uiteketeze siyo?"

"Ni kweli kabisa na kwa sasa kazi imebakia ndogo tu kwani mzee Fikirini na mkewe nao nasikia walishalamba lamba mchanga na wanaonisumbua ni Jackline pamoja na watoto wa mzee Fikirini ambao siwafahamu Kiukweli."

"Kwa hiyo pamoja na kukutia mikononi mwetu bado una hesabu za kuwaua?"

"Lazima iwe hivyo nikiwapata Afande kwani iwapo sitafanya hivyo itakuwa shida kwenye maisha yetu hasa huyu Jackline ambaye nimemsomesha mpaka nje ya nchi."

"Hizi picha unazikumbuka mzee Jonathan?"

Baada ya kuziangalia zile picha aliduwaa kidogo na kisha akakubali kuzitambua.

"Nazifahamu vizuri sana huyu ni kichaa wangu Surambaya, huyu mwingine ndiye mzee Fikirini na huyu binti ndiye Jackline anayekisumbua kichwa changu usiku kucha."

"Vizuri sana kwa hiyo unakiri kuwa wewe ndiye kila kitu kwenye matukio haya yote kuanzia ajali ya mzee Joachim mpaka utekaji kwenye lile basi?"

" Ni kweli kabisa Afande ile ajali ya rafiki yangu mzee Joachim m Thomas niliifungia safari mpaka ndani ya kisiwa cha Saa Nane Mwanza kwa mtaalam mmoja ili tu kuwapoteza ambapo niliamini mtoto wao nitamtunza kumbe nilijidanganya bora ningemmaliza tu kumbuka hata huu muonekano nimeutengeneza kwa gharama kubwa ili kujilinda na wabaya wangu lakini nahisi jinamizi la Mzee Joachim linaniandama."

"Aisee basi nikuhakikishie kuwa sisi kama serikali tumeamua kukubadilishia makazi."

"Kivipi Afande?"


***


Mzee Bruno Gautier baada ya kuona Robinson kapigwa vile na Jessica akaona njia pekee ya kumnusuru kijana wake ni kumtwanga tu risasi ya mguu Jessica.

"Maamaaaaa mguu wanguuuu..........."

Jessica alipiga kelele kiasi cha kuwashtua wenzake ikiwa ni pamoja na Melissa mwenyewe aliyewauza.

"Mzee Bruno Gautier umefanya nini sasa?"

Melissa alimpigia kelele mzee Bruno kwa kitendo kile.

Pamoja na kuwa kwenye cheni waliinuka na kumvaa mzee Bruno na kumzungusha ile cheni na kuanza kumnyonga mzee huyu lakini yule kijana mwingine aliyekuwa na wakina Robinson akaona muziki huo hauwezi na ukizingatia bosi wao anawataka wakiwa hai mabinti hao alichokifanya yeye ni kutoa Kopo fulani mfukoni na akalifungua na kulirusha hewani na kisha kumfuata Robinson kumvutia nje. Mle ndani hali ilibadilika kwani wakina Jackline walijikuta wakiishiwa nguvu na kujikuta wakimuachia mzee Bruno ambaye aliomba msaada kwa wenzake ambapo yule kijana alikuja na kumbeba lakini naye alipofika mlangoni alianguka na kumbwaga mzee Bruno pembeni.

Hali ikawa tete kwani kila aliyekuwa pale alipoteza fahamu, hali ile ilikwenda kwa masaa kadhaa kisha Robinson alikuwa mtu wa kwanza kupata fahamu kutokana na kupigwa na upepo pale nje lakini wengine wote mpaka Melissa naye alikuwa kapoteza fahamu. Aliamua kufanya maamuzi ya haraka ikiwa ni pamoja na kuwatoa nje wote ili wapigwe upepo hasa Melissa, mzee Bruno na yule mwenzao aliyesababisha hilo tukio la watu kupoteza fahamu lakini wengine ambao ni Jackline, Jasmine na Jessica akiwaacha humo humo ndani waendelee kumezwa na ile sumu. Akakaa nje ili akili ikae sawa kwanza wakati akiwasubiri wenzake wapate fahamu.

"Mkuu huyu mtu wako Tom kafanya yake hapa na kusababisha watu kupoteza fahamu."

"Kivipi wewe dogo?"

"Wakati kumetokea vurugu hapa ndani yeye akaona njia pekee ni kupuliza sumu aliyokuwanayo mfukoni."

"Mungu wangu hivi Tom ana akili zote kweli? Ile sumu si ya mchezo hata kidogo sisi huitumia kwenye biashara yetu ya madawa ya kulevya na Mazungu wenzetu na mbaya zaidi ukikosa hewa safi kwa dakika ishirini lazima upoteze maisha kabisa au uzinduke baada ya wiki kadhaa mbele."

"Kwa maelezo yako tu hayo ambao wanaweza kuinuka ndani ya masaa kadhaa yajayo labda mzee Bruno na yeye mwenyewe Tom kama sikosei na Melissa ila hawa wengine sina uhakika kwani mpaka sasa wako ndani ya sebule ambako lile kopo lipo na bado linatoa harufu ile."

"Kazi ishakuwa mbovu hiyo tena, okay hebu tuje na vifaa maalum vya kuvaa ili tuwatoe humo ndani."

"Sawa mkuu nimekupata."

Simu ilikatwa na kisha akarudi mlangoni kuiangalia kama kile kikopo kimeacha kutoa ile hewa ya moshi wenye sumu na baada ya kuangalia hali ilikuwa ni ile ile akarudi alipokuwa kakaa akiendelea kuangalia mdomo wake ambao ulikuwa umechwa sehemu ya chini na mtoto Jessica.

Mara helicopter ilikuwa juu ya anga ikitafuta sehemu nzuri ya kutua na ndipo Robinson alipoinuka na kupunga mkono juu kuwaonesha sehemu walipo na kisha kuongoza upande ambao ulikuwa na uwazi mkubwa na huko akamjulisha Santana kunafaa kwa kutua ndipo ndege ilielekea huko na kutua. Haraka sana hakukua na muda wa kupoteza walianza kuwapakia wakina Tom, mzee Bruno pamoja na Melissa kwenye ndege kisha Wakavalia maski maalum tofauti na zile za nguo ambazo walivaa wakina Robinson wakati wakivamia na kisha wakaingia ndani na kuwabeba wakina Jackline na wenzake wakina Jessica na Jasmine na kuwapakia ndegeni kisha Santana alirudi kwenye ile nyumba akakagua mazingira ya ile nyumba hasa pale sebuleni na kukutana na vilivyokuwa vimeharibiwa na chini kulikuwa na simu moja aliiangalia ile simu ambayo ilikuwa ikifunguliwa na password maalum akaona haina maana akaachana nayo na kisha kutoka na kufunga milango na kuzama kwenye ndege (helicopter) ikaondoka eneo hilo.

"Mnapokuwa kwenye oparesheni kama hizi mnatakiwa kuwa makini hasa kwenye vifaa vyenu msiende kinyume na maelekezo."

"Nimekupata bosi wakati mwingine hilo haliwezi jirudia."

"Na huo mdomo vipi?"

"Ndiyo sababu ya Tom kurusha lile kopo la sumu ni mara baada ya mimi kutaitiwa na huyu Jessica."

"Yaani hawa viumbe huwa hawakati tamaa mapema usije ukashangaa fahamu zikiwarejea tu wanalianzisha."

"Ni kweli kabisa tunatakiwa kuwa nao makini sana."

"Yaani pamoja na kuwa katika hali hiyo watatakiwa kuwa kwenye chumba maalum chini ya ardhi ambako hata Jasmine hajawahi fika na miguu na mikono yao ikiwa kwenye minyororo bab'kubwa na si hiyo."

"Sawa Sawa mkuu."

Baada ya dakika kadhaa hivi helicopter lilikuwa limeinamisha pua likinusa eneo lake la kujidai ndani ya Ngome ya mtu mzima Santana na kisha ilitua.

"Leteni gari ya gari hapa."

Santana aliagiza gari iletwe ili wawachukue wagonjwa na kuwapeleka kwenye vyumba maalum ambako wataanza matibabu.

"Hao kenge wapelekeni kwanza kwenye kile chumba cha barafu kwanza wakaipate freshi wanaweza kuwa wanazuga wamezirai kumbe wanatuchora tu na wakina Bruno kwenye zahanati yetu kwa matibabu."

"Bosi huyu Jessica anajeraha mguuni alilopigwa na mzee Bruno Gautier."

Robinson alimwambia Santana ambaye alionekana kuwa na furaha kidogo baada ya kuwanasa wabaya wake ambao aliamini watainuka ndani ya masaa kadhaa ili zoezi la kuwacharanga lianze mara moja.

" Si muhimu sana achana naye shida yangu si mguu mimi ninahitaji moyo, figo muhimu kwanza vingine ni kwa maelekezo ya mteja kama na Ngozi watahitaji au la."

Basi Robinson aliondoka baada ya kujibiwa vile na Santana akaelekea Kantini sehemu ambayo wafanyakazi wa Santana hupumzika kwa bata lao fulani baada ya kazi hasa ile ambayo huwa matokeo chanya.


JE, NINI KITAENDELEA?

TUKUTANE TENA KATIKA SEHEMU INAYOFUATA YA HADITHI HII.


      #SULTANUWEZO

Sultan Uwezo

In our hands you will find out Songs and Videos of Various Artists without forgetting News from Newspapers. Here you will also find Employment's Information from the Government and the Private Sectors.

Post a Comment

Previous Post Next Post