NITAKUUA MWENYEWE - 43
sultanuwezotz.blogspot.com
Baada ya kuhitimu kidato cha nne katika shule ya Sekondari Lupa Shamimu Fikirini alirejea nyumbani kwa mzee Kaaya kama ambavyo Jackline aliomba ndivyo ambavyo mzee Kaaya alifanya kwa mdogo wake, tokea waondoke kwenda nje ya nchi mzee Kaaya aliendelea kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha Shamimu anapata mahitaji yake yote ya msingi kama mwanafunzi na Mungu saidia mpaka anahitimu hakuacha deni shuleni kitendo ambacho mzee Kaaya alipongezwa na uongozi wa shule hiyo kwani kwa mwingine angeweza kutelekeza majukumu yake.
"Karibu nyumbani mwanetu Shamimu."
Mama Robinson alimkaribisha akiwa anampokea begi.
"Asante mama nimekaribia." Shamimu alijibu.
"Karibu sana."
"Asante mama nashukuru."
"Angalia chumba chako kama kiko vizuri si unajua tena na uzee huu nilikuwa sikihudumii kwa wakati."
"Usijali mama nitakifanyia usafi tu. Shamimu alijibu.
" Pumzika na mimi niko jikoni nikiendelea kuandaa chakula cha jioni."
"Mama bwana unapika chakula gani hicho mbona muda bado sana si ni saa kumi na mbili hii?"
"Ni kweli mwanangu nimeona niandae mapema ili muda ukifika iwe ni kula tu kwa utulivu si kuanza kutoa mijasho jikoni."
"Ni kweli kabisa mama sasa wewe kaa pembeni mwanao nimerudi hii kazi yangu."
"Hapana wewe kakiandae chumba chako usije lalia nyoka bure na kuhusu kupika wewe utaanza kesho au umesahau kama wewe ni mgeni leo?"
"Mama nawe mgeni wa wapi mimi? Basi wacha nikafanye usafi."
"Hayo ndiyo maneno mwanangu."
Shamimu aliingia chumbani kwake kufanya usafi huku akimuacha mama yake jikoni akiendelea kupika chakula kwa ajili ya jioni.
Alianza kufanya usafi wa chumba kile huku akiangalia kikae katika mkao gani ambao ataupenda.
Aliendelea kuumiza kichwa mpaka baadaye akaona atulie kwanza kitandani hapo ambapo alijilaza na kwa kuwa usingizi hauna adabu ulimchukua hapo hapo bila kumuacha amalizie shughuli yake ya usafi kwanza.
"Mambo shemeji yangu kipenzi." Robinson alimsalimu Shamimu.
Shamimu alikuwa kajiachia mwenyewe akiwa kama alivyozaliwa akisugua miguu yake kwenye jiwe huku sehemu za nyuma zikitikisika akijua yuko peke yake pale mtoni Lupa.
"Shemeji umefuata nini huku mtoni." Shamimu alijibu huku akiwa kajirushia kwenye maji ili ajisitiri.
"Aahhh shemeji Shamy ni swali kweli hilo?"
Robinson alisogea mpaka alipokuwa kaweka nguo zake Shamimu na kuketi.
"Hivi kwa mfano dada anatokea hapa unafikiri itakuwaje shemeji?"
"Na kwa kuwa ni mfano haiwezi kutokea shemeji yangu." Robinson alijibu huku akiziangalia nguo za Shamimu.
"Shemeji acha basi mambo yako sipendi naomba uondoke nivae nguo."
"Au nikuletee kabisa shemeji yangu kipenzi, unajua nini shemeji yangu nimeona nikufuate huku huku mtoni nije nikueleze hisia zangu juu yako mtoto mrembo kama wewe uliyeumbwa ukaumbika kwanini nisikufuate popote ulipo? Wewe ni sawa na pafyumu mpenzi."
Na muda huo alikuwa akiinusa kufuli ya Shamimu.
" Hivi unajua sikuelewi kabisa shemeji? "
" Kwa sasa huwezi kunielewa ila muda si mrefu utanielewa tu shemeji."
Aliweka chini ile kufuli ya Shamimu na kisha alisimama na kuanza kuvua nguo zake ambapo kitendo kile kilimfanya Shamimu afiche macho yake kwa mikono yake ili asione shemeji yake anataka kufanya nini. Alipomaliza kuvua nguo zote ndipo Shamimu akajua kuwa shemeji yake alikuwa kadhamiria kweli na hapo ikabidi apige mbizi kuelekea upande wa pili, lakini Robinson naye alianza kuogelea kumfuata kule kule, Shamimu alijitahidi kwa uwezo wake wote kuogelea kuhakikisha anamshinda shemeji yake huyo. Lakini ilikuwa kazi bure kwani alishtukia akidakwa miguu kwa nyuma.
"Shemeji niachie haraka kabla sijapiga kelele."
"Piga tu kama unafikiri itakusaidia shemeji."
Robinson alionekana kadhamiria kufanya jambo kwa shemeji Shamimu ambaye muda huo alianza kupiga kelele lakini ajabu ilikuwa pamoja na kupiga kelele hizo watu walikuwa wakiendelea na shughuli zao wanakuja wanachotaka maji na kuondoka zao kama hawajaona kitu vile.
"Si umeona eee ndiyo ujue hakuna mwenye shida na makelele yako hivyo ni bora utulie shemeji yako nile vyangu humu humu majini."
"Nimesema niachie huko sitakiiiiii...." Safari
hii Shamimu alifanikiwa kumsukuma Robinson kwa miguu yake ile ile na kumfanya aanguke chali na kumpa nafasi Shamimu ya kukimbia lakini alipaniwa kwani hakufika mbali kwani alipigwa bonge la mtama uliompeleka chini na kuangukia kwenye majani nje kidogo ya mto na kisha Robinson alimfuata kwa juu lakini akiwa anahangaika pale juu mara walisikia sauti ikiita.
"Shamimu, Shamimu, Shamimuuuuuuu." Ile kugeuka hawakuamini macho yao hakuwa mwingine alikuwa ni Jackline, nguvu zilimwisha Robinson akajivuta na kutoa nafasi kwa Shamimu kuweza kumsukuma pembeni.
"Shamimu, Shamimu........."
Alishtuka baada ya kuona anatikiswa mabegani mwake huku macho yakiwa yamemtoka.
"Maamaaaaa...." Aliita.
"Bee mwanangu,inaonekana ulikuwa umechoka sana maana si kwa usingizi huo nimeita na kuita wapiiiiii."
"Nisamehe mama inawezekana ni uchovu tu wa wiki mbili za mitihani."
"Amka sasa ukajimwagie maji ya baridi mwili upate nguvu na kwa kuwa usafi haujafanya itabidi ulale sebuleni ili kesho ndiyo uamkie usafi. Na baba yako kafika tayari."
"Sawa mama."
Mama yake mlezi ambaye ni mama yake Robinson aliondoka na kumuacha Shamimu akijinyooshanyoosha viungo vyake aliinuka na kujikagua vizuri kisha alikaa tena kitandani na kujishika mashavu.
"Hivi hii ndoto ina maanisha nini kwangu, yaani shemeji atake kuniingilia bila idhini yangu? Kuna nini huko waliko? Kuna usalama kweli?"
Shamimu alijiuliza huku akiinuka kutoka nje ya chumba kile.
"Mwanangu Shamimu umerudi mama?"
Mzee Kaaya aliuliza baada ya kumuona Shamimu akipita pale sebuleni.
"Ndiyo baba nimerudi tayari na hii ni baada ya kukamilisha kila kitu pale shule na kwa sababu ni jirani sikutaka kuendelea kuwepo pale shuleni."
"Umefanya jambo la maana sana Shamimu na bila shaka ungependa kujua kinachoendelea kule kituoni."
"Ni kwe..." Kabla hajamalizia neno lake mama aliingilia kati.
"Baba Robinson muache kwanza mtoto akaoge kisha hayo mengine yataendelea."
"Ohh basi sawa, kaoge kwanza mwanangu."
"Sawa baba."
Shamimu alitoka na kuelekea jikoni kuchukua maji kisha akaingia bafuni kuoga.
***
Wakiwa na furaha ya ajabu baada ya kufanikiwa kuwatupa majini wakina Jackline, wakina Robinson walirejea kambini wakiwa wanapiga kelele za shangwe.
"Kuna nini vijana wangu?"
Mzee Bruno Gautier aliuliza baada ya kuwasikia wakina Chude wakipiga makelele ya furaha.
"Kwanza kabisa pole sana Bruno kwa kurejewa na hali ya kawaida wewe na wenzako wakina Tom."
Chude alianza kwa kumpa pole mzee Bruno Gautier.
"Asante sana kijana wangu. Kumetokea nini huko mpaka mje na mikelele yenu hapa?"
"Mzee tumefanikiwa leo kukiteketeza kizazi jeuri, kizazi cha ajabu ambacho ndani ya muda mfupi kimepelekea hasara na mambo kwenda kombo ndani ya makampuni yetu ikiwa ni pamoja na kumteka mke wa bosi wetu." Chude aliendelea kufafanua.
"Weeeeee usiniletee mashairi yako yasiyo na kichwa wala miguu hapa unataka kunieleza nini nikuelewe maana unakoelekea usiniambie kuwa mmewaua wale mabinti."
"Ndiyo hivyo mzee unauliza tena juu ya hilo pigia mstari maana kwa muda huu nahisi misamaki itakuwa ndiyo inamalizia mifupa yao." Robinson naye aliongezea kwenye maelezo ya Chude.
"Na mke wangu je amepatikana?" Aliuliza mzee Bruno Gautier.
"Tumefikia hatua nzuri mzee Bruno kwani mpaka sasa simu iliyokuwa ikitumiwa na wakina Jackline tayari tunayo mikononi mwetu na kesho tutakuwa eneo alilofungiwa mkeo kwa msaada wa Melissa."
Santana aliingilia mazungumzo yale ya wakina Chude na mzee Bruno.
"Naweza kuipata hiyo simu ili nianze muda huu kuyatafuta mawasiliano hayo."
"Mbona una haraka mzee Bruno kila kitu kinakwenda kwa utaratibu mzee wangu, elewa kuwa baada ya kila kukamilika kifuatacho ni kushughulikia suala la mke wako." Santana aliendelea kufafanua zaidi.
Lakini mzee Bruno ni kama vile hakuridhishwa na namna mambo yalivyoendeshwa haraka vile hivyo kwa hasira aliamua kuondoka na kuingia ndani kulala.
" Hebu niambieni ina maana Jasmine, Jackline na Jessica mmefanikisha kuwaua?"
Melissa aliuliza swali hilo baada ya kusikia malumbano yale hivyo akaona amuulize Robinson.
"Ni kweli kabisa Melissa, inavyoonekana ile sumu iliwadhuru sana kiasi cha kutozinduka tena kama ninyi na hivyo bosi akaagiza tukawatupe ndani ya bahari kwani hakutaka kuona kitu chochote kitakachobakia kama ukumbusho wao kwake."
Robinson alimfafanulia Melissa kilichotokea siku leo na kabla.
" Aisee pole zao marafiki zangu najua huko waliko watakuwa wananichukia sana mimi ila tu naomba wanisamehe kwa kilichotokea na kupelekea kukatisha safari yao ya maisha hapa duniani kwani hata mimi mwenyewe najilaumu sana ila mbele ya mkwanja na maisha mazuri mtanisamehe sana na ninachoweza kuwaambia ni kwamba nakwenda kumteka rasmi Mr Santana kwa gharama yoyote ile ilmradi tu awe wangu."
Aliongea Melissa huku akimkodolea macho Robinson ambaye akinywa juisi.
" Ila na wewe ni mpuuzi wa tabia ndiyo nini kumsaliti mpenzi wako aliyekuonesha dunia ikoje?"
Melissa alimrushia swali Robinson ambalo hakulitegemea muda huo.
"Hata bila yeye bado hii dunia ningeifahamu tu kwani ndoto zangu zilikuwa kutoka nje ya Tanzania kutafuta maisha na kwa bahati akapita katikati ya ndoto yangu na kuwa kama ganda la ndizi vile."
"Kweli wewe una matatizo ya akili, hivi unafikiri kumtoa sadaka mpenzi wako kwa Santana utawini maisha? Hujamfahamu bado Santana wewe na endelea kumuomba Mungu asije pandwa na pepo la umwagaji damu."
"Vyovyote itakavyokuwa poa tu dada yangu."
"Okay sawa kidume mpambanaji."
Melissa alimjibu na kuelekea ndani kwenye ofisi ya Santana na kuwaacha wakina Robinson wakiendelea kuburudika.
NINI KITATOKEA?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
#SULTANUWEZO